Uzinduzi wa Muongozo wa Masomo ya Biblia sio Suluhisho la Kupambana na Ufisadi Nchini Kenya!

Mnamo Jumatano 26 Septemba 2018 Tume ya Maadili na Kupamba na Ufisadi (EACC) ikiongozwa na Mwenyekiti wake Eliud Wabukala (Mstaafu Kadinali Bishop wa Kanisa la Anglican) wakishirikiana na Sekta ya Muungano wa Dini Mseto walizindua Muongozo wa Masomo ya Biblia kwa jina ‘Uadilifu: Silaha Dhidi ya Ufisadi.’  Muongozo huo unatarajiwa kutumiwa na makundi au watu binafsi wanaohusika na masuala ya ufisadi. EACC ilisema “Muongozo wa Masomo ya Biblia unatarajiwa kuwasaidia Wakenya kuweza kutangamana na Biblia na kugundua msimamo wa Mwenyezi Mungu juu ya ufisadi na muelekeo wa kuishi maisha yasiyokuwa na ufisadi. Licha ya cheo chako katika jamii, unaweza kuleta mabadiliko. Muongozo huu unatupa motisha kutenda na kuamini kuwa nchi yetu inaweza kuachana na ufisadi. Vita dhidi ya ufisadi vitashindwa lakini lazima kila mmoja ajifunge kuishi maisha yanayokuza uadilifu, haki uzalendo na mapenzi kati yetu.” (The Star, 26/09/2018)

Eliud Wabukala aliingia kwenye tume ya EACC mamlakani mnamo 23 Julai 2017 kuhudumu kama  Mwenyekiti wa Tatu baada ya kujiuzulu kwa Philip Kinisu –Agosti 2016 na kabla yake alijiuzulu Mumo Matemo – Mei 2015.Wote walijiuzulu kwa tuhuma za kuhusika na ufisadi kwa njia moja au nyingine! EACC tangu kubuniwa kwake imekuwa kama shimo lililoko kizani kiasi kwamba kila Mwenyekiti na Makamishna wake hudondoka humo ndani kwa tuhuma za ufisadi. Hivyo hatua hii ya uzinduzi wa Muongozo ni dhihirisho kuwa EACC imeshindwa kupambana na ufisadi na hivyo imefikia kileleni na imekata tamaa. Ili kufahamu hilo zingatia nukta zifuatazo:

Kwanza: Kenya ni nchi ya kisekula (serikali imetanganishwa na dini / dini haina mchango katika serikali.  Mfumo wake ni urasilimali uliomakinishwa juu ya usekula. Nidhamu ya kiuchumi ya kirasilimali ndiyo inayoathiri uendeshwaji wa serikali kiasi kwamba warasilimali (wanaomiliki mitaji) ndiyo wenye usemi. Hivyo basi taifa la Kenya kama yalivyo mataifa mengine ulimwengu wanajitungia sheria ikiwemo katiba kutumia akili zao finyu ili kupangilia namna ya kuendesha maisha jumla. Sheria hizo zimejikita katika kudhamini uhuru aina nne: Uhuru wa Kuabudu, Uhuru wa Maoni, Uhuru wa Kumiliki na Uhuru wa Kibinafsi. Kutokana na uhuru hizo nne ndiyo twapata nidhamu ya kiutawala ya demokrasia, ambayo huumpa mwanadamu ubwana wa kuendesha mambo ikiwemo kutunga sheria n.k.

Pili: Kwa mtizamo wa itikadi ya usekula urasilimali maisha yamefungwa juu ya Uhuru wa Kibinafsi au kwa maana nyingine fanya unavyotaka wakati wowote pasi na kujali yeyote bora tu isiwe kwamba wamvunjia mwenzako Uhuru wake wa kibianfsi. Lengo la maisha ni kumiliki mali kwa kiwango cha juu kwa kadri ya uwezo wako na furaha/ustawi ni kukishibisha/kukistarehesha kiwiliwili chako kwa kiwango cha juu uwezavyo. Hivyo basi, wanadamu daima wanakwenda mbiyo kuchuma mali kwa njia yoyote na kuitumia kwa njia yoyote wapendayo!

Tatu: Mahusiano baina ya watu yamekitwa katika kushindana katika kumiliki mali na kwamba kipimo cha kufaulu kwa mtu ni wingi wa mali aliyokuwa nayo na hivyo usemi na ubora/mchango wake katika jamii unategemea na mali aliyokuwa nayo. Hivyo basi kipimo cha vitendo kimekitwa juu ya maslahi/manufaa/madhara!

Nukta hizo zinaashiria kwa asilimia 100 kuwa asili ya ufisadi umeanza na itikadi ya usekula na mfumo wake wa urasilimali na kwamba kuwepo na kutekelezwa kwake ndiyo mzizi wa ufisadi. Tume hiyo na Taasisi zote nchini na Ulimwenguni zimeasisiwa juu ya ufisadi huo. Licha ya Kenya kuwa ni nchi yenye Wakristo wengi lakini dini ya Ukristo haina nafasi katika uendeshaji wa serikali. Hata kama dini ya ukristo ingepewa nafasi isingeliweza kusimamia watu/taifa kwa sababu ni dini iliyoegemea upande wa kiroho tu na haina mtizamo wa kimfumo (suluhisho kwa matatizo yote yanayomkumba mwanadamu ya kisiasa, kiuchumi, kijamii n.k). Ndiyo maana pia wako wasiokuwa na dini mfano Muungano wa Wasioamini Kenya (AIK) nao pia wanatambuliwa na kupewa nafasi katika jamii.

Suluhisho la msingi lipo katika mfumo wa Uislamu ulioasisiwa juu ya itikadi ya ‘Hapana Mola Apasaye Kuabudiwa kwa Haki na Muhammad ni mtume wa Mwenyezi Mungu’. Itikadi hii haina nafasi ya Uhuru na kwamba mwanadamu ni ‘mtumwa kwa Mwenyezi Mungu.’Hivyo basi mwanadamu lazima ajifunge kikamilifu na maamrisho na makatazo ya Mwenyezi Mungu, na kipimo chake kibakie daima ni halali na haramu. Uislamu ndiyo mfumo pekee ulioridhiwa na Mwenyezi Mungu:

إِنَّ الدِّيْنَ عِنْدَ اللهِ الإِسْلاَمُ

Bila ya shaka Dini (mfumo) mbele ya Mwenyezi Mungu ni Uislamu.

[Aali-Imran: 19]

Na Uislamu ndio mfumo aliokuja nao Muhammad (saw) mtume wa mwisho na kila mwanadamu anatakiwa kujisalimisha kwake:

وَماَ أَرْسَلْنَاكَ إِلاَّ رَحْمَةً لِّلعَالَمِيْنَ

Nasi hatukukutuma (Muhammad) ila uwe ni Rehema kwa walimwengu wote.

[Al-Anbiyaa: 107]

Uislamu unatakiwa kutawala maisha ya watu kikamilifu na hilo kattu haliwezekani mpaka kupatikane Serikali ya Kiislamu ya Khilafah. Khilafah iliyosimamishwa kwa njia ya Utume pekee ndiyo itakayoweza kuwakomboa wanadamu kwa kuing’oa na kisha kuichoma mizizi ya ufisadi wa mfumo wa urasilimali na itikadi yake ya usekula. Na sehemu yake kuweka mfumo wa Uislamu na itikadi yake safi na inayotoka kwa Muumba wa mwanadamu, uhai na ulimwengu. Utampangilia mwanadamu kwa ukamilifu kupitia nidhamu zake safi za Kiislamu ikiwemo ya Nidhamu ya Kiuchumi, Kijamii, Kisiasa, Elimu n.k. Zote zikitekelezwa kikamilifu kwa sura ya uchajimungu unaopatikana baada ya kupata Utambulisho wa Kiislamu (Shaksiyatul Islam) utakaodhaminiwa kupitia Khilafah. Huku mwanadamu akijengwa kumnyenyekea na kumugopa Mwenyezi Mungu na kumuheshimu binadamu mwenzie kinyume na hali ilivyo sasa ambapo binadamu anamuogopa binadamu mwenzie. Hivyo basi lengo la maisha chini ya Uislamu ni kutafuta radhi za Mwenyezi Mungu na mbio zote (vitendo vyote) maishani zimekitwa katika lengo hilo pekee. Hatima yake ni kuwa maisha ya dunia yana mwisho nako ni Kufariki na kisha kufufuliwa ambako kutapelekea kuhesabiwa vitendo vya kila mmja na baada yake ni kutolewa hukumu ya kuingia maisha ya kudumu peponi au motoni milele.

Kwa kumalizia isifahamike kuwa lau kutawekwa muongozo wa kusoma Qur’an kinyume na Biblia labda ndiko kutatatua ufisadi nchini Kenya kwa kuwa Uislamu ni mfumo. La! Qur’an inatakiwa kutekelezwa kwa ukamilifu wake chini ya Serikali ya Kiislamu ya Khilafah na wala sio serikali hizi za kisekula za kirasilimali zinazodhibitiwa na wakoloni wamagharibi na vibaraka wao walioko mamlakni. Hivyo basi inatakiwa wanadamu wote hususan Waislam wafanye bidi katika kulingania kurudi (kusimamisha) tena serikali hii ya Kiislamu ambayo haipo duniani kwa sasa tangu kuangushwa kwake mnamo 3 Machi 1924.

Ali Nassoro Ali

Mwanachama wa Afisi ya Habari ya Hizb ut Tahrir Kenya

Makala Na.14: Ijumaa, 25 Muharram 1440 | 2018/10/05