TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Harakati ya Kiislamu ya Hizb ut-Tahrir Kenya inasikitishwa mno na mamilioni ya raia wanaokumbwa na baa la njaa. Inahuzunisha kuona picha za wazee madhaifu wanaoshindwa kusimama huku watoto wakililia mama zao kwa sababu ya njaa! Kwa masikitiko makubwa huku hali hii ya kutamausha ikionekana, wanasiasa wa pande zote (serikalini na upinzani) wanazunguka huku na kule wakitoa maneno matupu na kuwinda kura za uchaguzi wa Agosti mwaka huu!
Tunaeleza bayana kuwa njaa hii haijasababishwa tu na ukame kama inavyodaiwa na wadau wa serikali bali hasa ni utepetevu wa kiserikali na kutelekeza/kudharau jukumu la kusimamia raia wake. Dalili ya haya ni kuwa watabiri wa hali ya hewa walitoa onyo mapema juu ya hali hii lakini serikali ikajitia hamnazo.
Kenya ina rasimali za kutosha ikiwemo madini, mito na ardhi kubwa yenye rutuba lakini kwa sababu ya sera mbovu za mfumo wa kiuchumi wa kibepari, utajiri huu wote humilikiwa na mabwenyenye wachache wanaojinufaisha huku raia wa kawaida wakiambulia patupu! Kihakika serikali inayowajibika kikweli na kuwa na nia ya kuondosha njaa kikweli hutakikana kuekeza zaidi katika sekta ya kilimo na wala sio kutegemea uagizaji wa vyakula kutoka mataifa ya nje ama kutegemea misaada ya kigeni. Serikali ya kikweli iliyo na nia kweli ya kuondosha umasikini ungeikuta ikiimarisha kilimo kwa kuja na mikakati kama kuwanunulia wakulima mbolea na kuwapa pesa za kutayarisha mashamba yao, kuweka miradi ya unyunyizaji wa mashamba. Mikakati hii ndio hudhaminia raia usalama wa chakula. Kwa bahati mbaya, haya hayafanyiki kwenye tawala zinazojifunga na mfumo wa kirasilimali ambapo wanasiasa wake hupuuza kusudi mikakati hiyo badali yake hunufaika kila kunapotokea baa la njaa kwa kudhibiti biashara za uagizaji wa mahindi na bei ya unga wa mahindi hupanda zaidi.
Tunatamatisha kwa kuwaomba matajiri wote wa Kiislamu na wasokuwa wa Kiislamu kufanya juhudi maradufu kusaidia waathiriwa wa baa la njaa. Twapenda wakati huo huo kuikumbusha jamii ya Kenya kusimama wazi kufichua maovu ya urasilimali na wanasiasa wake wanaong’ang’ania tu uongozi wapate kushibisha matumbo yao.Sisi tunaamini kuwa mfumo wa Uislamu ukitabikishwa/ukitekelezwa chini ya utawala wa Khilafah utamwezesha kiongozi kugawanya na kuzipeleka rasilimali hadi katika maeneo kame. Hivi ndivyo hali ilivyokuwa katika utawala wa Umar bin Khattab (ra) ambaye chini ya utawala wake aliwajibika kama kiongozi na kukabiliana ukame. Umar (ra), aliandikia barua magavana wake wa maeneo ya Misri, Sham, Palestina na Iraq akiwataka kuleta msaada wa chakula nao wakafanya hivyo pasina kusita hadi mamia ya raia wakaokolewa kutokana na baa la njaa.
Shabani Mwalimu
Mwakilishi kwa Vyombo vya Habari
Hizb ut-Tahrir Kenya
Kutoka Jarida la UQAB Toleo 1