Vita dhidi ya Ufisadi kattu havitoshinda chini ya Mfumo fisidifu wa Kirasilimali

Taarifa kwa Vyombo Vya Habari

Muhula wa pili wa rais Uhuru Kenyatta umekumbwa na msururu wa kashfa za ufisadi kwenye idara mbalimbali za Serikali. Kashfa tano tayari zimefichuka ndani ya mashirika makubwa ya umma jambo linaloonesha kuzagaa kwa jinamizi hili la ufisadi. Kashfa ya hivi karibuni ikiwa ni ile inayokumba shirika la usambazaji wa mafuta nchini (KPC) ambapo lita za mafuta milioni 11 zimepotea. Huku kampeni ya Uhuru ya kupambana na ufisadi ikionekana kuteka hisia kubwa za raia, sisi Hizb ut Tahrir /Kenya tungependa kusema yafuatayo:-

Kwanza: Ni udhalimu mkubwa ma-afisa wa ngazi za juu serikalini waliobebeshwa jukumu la kusimamia maslahi ya umma kuwaona wakishindana katika kufuja rasilimali za umma badala ya wao kuboresha maisha ya wananchi wa kawaida.

Pili: Kamatakamata ya wakuu wa mashirika kadhaa inayoshuhudiwa kwa sasa si lolote ila sarakasi ya kisiasa tu inayolenga kuhadaa kina yakhe waamini kuwa vita dhidi ya ufisadi ni vyenye kushinda ndani ya mfumo wa kirasilimali. Na hilo halina ukweli hata chembe kwani washukiwa wengi wa ufisadi walioshtakiwa mahakamani hivi karibuni wamekuwa wakionekana wakiachwa huru kwa madai ya ‘kukosekana ushahidi’. Fauka ya hilo linalopaswa kueleweka ni kuwa Kenya imejifunga na mfumo wa Kibepari uliopandikiza tamaa ya fisi ya kutaka kujilimbikizia mali kwa njia na mbinu zote chafu uhalisia unaofanya kuwa vita dhidi ya ufisadi kamwe havitofua dafu. Mfumo huu muovu umefanya maslahi kuwa ndio kipimo pekee cha kupeleka maisha ya wanadamu jambo linalowafanya watu hasa walioko serikalini kupatiliza fursa ya kung’anga’nia mali kwa mbinu chafu.

Tatu: Ufisadi wa ma-afisa wa kiserikali utawezwa kuondoshwa tu chini ya Uislamu kupitia utawala wake wa Khilafah ambapo kiongozi (Khalifah) hutekeleza sheria za Mwenyezi Mungu (swt). Sheria ambazo huonesha njia ya serikali ya ukusanyaji na matumizi ya rasilimali zake. Isitoshe, Uislamu umewajibisha kuwa afisa yeyote lazima achunguzwe kimakini kabla hajaingia afisini na hata akiondoka. Hili ni kuwa mapato yoyote atakayoyapata mfanyikazi wa serikali kinyume na utaratibu wa kazi yake yatataifishwa na kurudishwa kwa hazina ya serikali (Baitul Mal). Kwa haya tunasema kwamba Khilafah pekee kwa Mfumo wa bwana Mtume (saw) ndio itakomesha tatizo la ufisadi sio tu kwa Kenya bali ulimwengu mzima.

Shabani Mwalimu

Mwakilishi kwa Vyombo Vya Habari Hizb ut Tahrir Kenya

KUMB: 02 / 1440 AH

Jumatatu, 3 Rabi ul Thani 1440 AH /

10/12/2018 CE

Tel.: +254 707458907

Email: mediarep@hizb.or.ke