Kwa takriban zaidi ya wiki sasa Wakenya wanafanyiwa sarakasi za malumbano ya tuhuma kati ya Wizara ya Utalii na Wanyamapori na Shirika la Huduma kwa Wanyama wa Pori (KWS) na Muungano wa Madaktari wa Wanyama wa Kenya. Wizara ya Utalii inatuhumiwa kuanzisha zoezi baya la uhamishaji lililolenga kuhamisha Vifaru Weusi 14 kutoka mbuga za wanyama za kitaifa za Nakuru na Nairobi hadi mbuga ya vifaru ya kitaifa ya Tsavo Mashariki; pasi na kuwepo kwa bodi tendakazi ya KWS. Kundi la kwanza la vifaru kumi na moja walio katika hatari ya kuangamia lilihamishwa huko katika jaribio la kukuza idadi mpya ya vifaru. Lakini, kamati ya uchunguzi iliyoundwa mnamo 17 Julai 2018 na Wizara ya Utalii na Wanyama wa Pori iliripoti kuwa maji yaliyo na madini mengi ya chumvi, upotezaji maji mwilini, njaa na shambulizi la bakteria ndio sababu ya vifo vya vifaru weusi 10 kati ya kundi la kwanza lililohamishwa.
Aliyekuwa mwenyekiti wa KWS Richard Leakey na Muungano wa Madaktari wa Wanyama Kenya wote wamemshtumu Waziri wa Utalii na Wanyamapori, Najib Balala na kwamba anatakiwa kubeba lawama. Kinyume chake ni kuwa Balala aliiondolea lawama wizara hiyo, akisema kuwa timu ya kiufundi iliyo na mamlaka kamili ndiyo inayohusika na mpango huo unaofadhiliwa na Hazina ya Kiulimwengu ya Mazingira. Zaidi ya hayo, Waziri huyo aliwatimua maafisa wakuu sita wanaohusika na uhamishaji huo na kumshusha madaraka Mkurugenzi Mkuu wa KWS Julius Kimani mnamo Alhamisi, 26 Julai 2018. Wakenya pamoja na vyombo vikuu vya habari vya humu nchini na vya kimataifa waliendelea kuangazia na kujadili kadhia hii kama kadhia ya kufa na kupona!
Kenya kama dola ya kisekula ya kikoloni ambayo vipaumbele vya sera yake vinaongozwa na mfumo wake batili wa kisekula wa kirasilimali utokao kwa mabwana wakoloni wa kisekula wa kimagharibi, Uingereza. Uingereza huitazama Kenya kama shamba lake la kikoloni na raisi wake kama meneja wa shamba lake la kikoloni. Shamba hili linajumuisha viungo vitatu, meneja, wafanyikazi na ‘wanyama wenye thamani’ wanaomilikiwa na bwana mkoloni. Katika hali hiyo, Kenya huwekeza kwa wingi katika utalii na wanyamapori kwani inataka kuwaridhisha mabwana wake wa kimagharibi na watu wao!
Hiyo ndiyo sababu Utalii nchini Kenya ni chumbuko la pili kubwa la mapato ya ubadilishanaji fedha za kigeni baada ya ukulima na daima imbioni kuunda mikakati; ya jinsi ya kutoa huduma bora zaidi kwa watalii wanaomiliki “utamaduni bora” wa kutembea uchi na unywaji mvinyo miongoni mwa machafu mengine wayafanyayo kila mahali kwa jina la utekelezaji uhuru wa kibinafsi katika shamba lao la kikoloni. Mikakati ya kufufua sekta ya utalii ya Kenya ilizaa matunda baada ya serikali kunakili asilimia 20.3 mnamo 2017 na kupata mapato ya shilingi bilioni 120 licha ya msimu mrefu wa uchaguzi. Haya ni maendeleo kutoka shilingi bilioni 99.69 zilizochumwa mnamo 2016 kwa mujibu wa Waziri wa Utalii, Najib Balala. Takwimu mpya zaidi zilizotolewa na wizara hiyo zaonesha kuwasili kwa wageni wa kimataifa kuliongezeka kwa asilimia 9.8 na kufikia watalii milioni 1.4 kutoka watalii milioni 1.3 mwaka uliopita.
Kwa ripoti kama hizo kutoka kwa serikali iliyo katika utumwa na yenye kutegemea mapato ya kigeni kutokana na utalii, kifo cha kifaru mmoja ni janga kubwa kiasi cha kuwa itagharimu hasara nyingi kuanzia kupungua kwa kiwango cha utalii, kupungua kwa idadi ya wageni mahotelini nk. Kwa kuwa manufaa ndiyo kipimo cha vitendo katika serikali hizi za kisekula hakuna kitakachovumiliwa ambacho huenda kikazizuia kutokana na kupata maslahi yao. Kwa mfano onyo la KWS kwa wakaazi kutoua wanyama waliotoroka mbugani wanapoharibu mali zao, au kujaribu kuwadhuru au kuwaua; badala yake wanapaswa kuwaangalia tu wakifanya watakalo na wakaazi wapige ripoti kwa KWS ambayo aghalabu huwa haifanyi chochote au huchukua muda mrefu kutoa fidia licha ya kuwepo kwa kifungu cha sheria cha Hifadhi na Usimamizi wa Wanyamapori cha mwaka 2013. Mwanzoni watu walikuwa wakilipwa fidia ya shilingi 50,000 kwa ajili ya mazao na shilingi 200,000 kwa vifo na leo baada ya kifungu hiki cha sheria kuanza utekelezwaji wake mnamo 2013: sehemu ya 25 ya kifungu hiki cha sheria ya Usimamizi na Hifadhi ya Wanyamapori cha mwaka 2013 kinafafanua kuwa katika hali ya kifo, shilingi milioni 5 zitalipwa kwa waathiriwa. Hali za majeraha zinazosababisha ulemavu wa kudumu zitafidiwa shilingi milioni 3, kwa mujibu wa kifungu hiki. Kulingana na kiwango cha majeraha, majeraha mengine kiwango cha juu cha fidia ni shilingi milioni 2. Uharibifu wa mazao pia hulipwa fidia, kulingana na thamani ya soko ya mazao hayo. Lakini wako watu ambao kesi zao licha ya kuwa za kweli bado wangali wanateseka kwa miaka baada ya kuwasilisha malalamishi ya fidia. Lakushangaza ni mnamo 2017, ambapo ripoti kwa anwani Hali ya Hifadhi ya Wanyamapori Nchini Kenya 2016; aliyekuwa Waziri wa Mazingira Judy Wakhungu alisema malalamishi ya fidia kutokana na matukio ya kuumwa na nyoka yaliongezeka hadi shilingi bilioni 1.5. Baadaye mnamo 2018 serikali inapendekeza marekebisho kwamba vifo na majeraha yanayosababishwa na nyoka wenye sumu, papa, samaki jiwe, nyangumi, taa na nguruwe mwitu zitaondolewa katika orodha ya fidia. Pia inapendekeza kusitisha ulipaji fidia kwa mazao na mali iliyoharibiwa na ndovu, simba, chui, kifaru, fisi, mamba, duma, nyati, pundamilia, paa, nyumbu, nyoka na mbwa mwitu. Lakini, hasara ya mifugo itaendelea kufidiwa!
Katika Khilafa (Dola ya Kiislamu) Bait ul-Maal (Hazina ya Dola) itajumuisha machimbuko ya mapato yafuatayo: ngawira (Fai’ na Ghana’im), kodi ya ardhi (Kharaj), kodi ya raia wasiokuwa Waislamu (Jizya), mapato kutoka katika aina tofauti tofauti za mali ya umma, mapato kutoka katika mali za serikali, kodi kutoka katika ardhi ya ukulima (Ushr), khumusi ya hazina iliyofichwa ardhini (Rikaz), madini, na mali ya Zaka. Zingatia: kodi iliyotajwa hapa (Kodi ya Ardhi na Kodi ya Raia wasiokuwa Waislamu) hazipaswi kuchukuliwa kama zile zinazotozwa kwa sasa na serikali za kisekula kwa watu. Utalii sio wala hautakuwa sehemu ya mapato ya Khilafah kwani utalii kibinafsi ni fikra ya kuendeleza ukoloni au ukoloni mamboleo kwa kisingizio cha kitega uchumi. Hivyo basi, sera ya kigeni ya Khilafah kama inavyoashiriwa na itikadi safi ya Kiislamu kamwe haitaruhusu fikra kama hizo ndani na nje. Khilafah italinda maisha ya watu na yale ya wanyama, kwa sababu wote hawa ni viumbe wa Allah na wanyamapori watatumiwa kwa mujibu wa sera itakayo tabanniwa na Khalifah (mtawala) wakati huo.
Ama kuhusu thamani ya maisha ya wanadamu, Allah (swt) asema:
وَلَقَدْ كَرَّمْنَا بَنِي ءَادَمَ وَحَمَلْنَاهُمْ فِي ٱلْبَرِّ وَٱلْبَحْرِ وَرَزَقْنَاهُمْ مِّنَ ٱلطَّيِّبَاتِ وَفَضَّلْنَاهُمْ عَلَىٰ كَثِيرٍ مِّمَّنْ خَلَقْنَا تَفْضِيلاً
“Na hakika tumewatukuza wanadamu, na tukawabeba nchi kavu na baharini (juu ya vipando vya usafiri), na tumewaruzuku vitu vizuri vizuri, na tumewafadhilisha fadhila kubwa kuliko wengi miongoni mwa tuliowaumba.” [Al-Israa: 70]
Imeandikwa kwa Ajili ya Radio Rahma
Ali Nassoro Ali
Mwanachama wa Afisi ya Habari ya Hizb ut Tahrir Kenya
Makala Na.5 Ijumaa, 21 Dhu al-Qi’dah 1439 | 2018/08/03