IMEANDAMA

Leo swaumu ni mosi, ramadhani ‘meandama,

Vije tusitaanasi, na nyoyoni kuterema,

Ndio mwezi makhususi, unaofungwa mzima,

Kuifunga Ramadhani, ni faradhi yake Mola,

 

Majaliwa ya Qudusi, kwetu mwezi kutuama,

Ni faradhi kwetu sisi, tulio waisilama,

Kufunga pasi kuasi, hadi ufike khatima,

Akanae uwajibu, wa kufunga ni kafiri,

 

Malipo yaso kiasi, ‘meitunuku Karima,

Swaumu tufungaosi, na kila lililo jema,

Natuongezeni kasi, ya kutenda yalo mema,

Swaumu ni ya Mwenyezi,  na jazaye iko kwake,

 

Kwa uzito na wepesi, yatubidi kujituma,

Kutenda yalo asasi, ya sunna na ya lazima,

Qur’ani tudarasi, tujipinde kuisoma,

Qur’ani ni kitabu, cha kuwaongoa watu,

 

Kufuturisha unasi, hunu ni mkubwa wema,

Japo tende na nanasi, na viazi vya kuchoma,

Na bajia hata bisi, au pilau ya nyama,

Na dua tuzimimine, wakati wa kufungua,

 

Tuwaauni baisi, wajane na mayatima,

Nawapatiwe fulusi, za zaka waweze kwima,

Ambao ni mufilisi, waso pato lakut’uma,

Usimamizi wa zaka, unahitaji khilafah,

 

Kuwata yote maasi, ndio funga ilo njema,

Zitapofunga hawasi, zote za mwanaadama,

Ndiyo saumu khususi, ilo na tele ghanima,

Tut’ungeni funga yetu, ili iwe na daraja,

 

Tufunge kwa ikhilasi, na thawabu kuzichuma,

La uchaM’ngu libasi, jama ni hini swauma,

Ni yenye kutukingasi, na moto wa jahanama,

Mbele yake Maulana, funga itatuombea,

 

Wangapi hawajikisi, pindi juwa likizama,

Hufanya yalo najisi, wala si wenye kukoma,

Si njema zao nafusi, zikali na tele homa,

Ramadhani ni mtana, pamwe na usiku wake,

 

Hapano kunena basi, itamatile nudhuma,

Kufunga sio rakhisi, kwataka Imani jama,

Pokeya Ya Rabba nasi, tuifungayo swiyama,

Kwa huku kufunga kwetu, tupe pepo ya Rayyani,

 

MTUNZI – MOHAMMED BAKARI

 

              ALMUFTI

 

MOMBASA – KISAUNI