Habari Na Maoni
Habari:
Kuanzia tarehe 18 Aprili 2024, mafuriko yalikumba Kenya, na kuathiri watu katika magatuzi 21 kati ya 47. Mji mkuu wa Nairobi na maeneo jirani yaliathirika vibaya. Mto Nairobi na ule wa Athi yote ilipasua kingo zake na kuwafanya watu 40,000 kuyahama makazi yao. Zaidi ya 130,000 wametoroka nyumba zao, 91 hawajulikani walipo, 29 wamejeruhiwa, na 169 wameripotiwa kufariki dunia. Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kuratibu Misaada ya Kibinadamu pia iliripoti mifugo isiyopungua 960 na ekari elfu 24 za mashamba zilikumbwa na mafuriko. Mafuriko yalizidi katika sehemu kutokana na El Niño. Asubuhi ya Jumatatu, 29 Aprili 2024, bwawa lilipasuka na Mai Mahiu, na kuua watu wengine 42.
Maoni
Kwa mara nyengine tena ni jambo la kuhuzunisha kuona maisha ya watu na mali ya thamani ya mabilioni ya pesa yamepotezwa kwa sababu ya kutojali aibu ya uzembe! Ukweli wa mambo ni kwamba, mafuriko ya maeneo ya mijini siku zote yamekuwa zigo kwa masikini hususan wanaoishi kwenye mitaa ya mabanda.
Lile ambalo nchi inapitia kwa sasa ni kule kufeli kwa uongozi katika kupangalia mambo. Maafa haya ya mafuriko yanayoendelea yanaonesha bayana utepetevu sio tu kwa uongozi bali mfumo wote wa kisiasa wa Kidemokrasia uliovunja rekodi ya kuwa na uzembe wa kiuhalifu. Ni uzembe mkubwa Serikali kusubiri majanga yatokee ndipo kwenye kilele cha maafa kuonekana kuhesabu hasara!
Ukiangalia uharibifu unaotokea nchi nzima tatizo ni ukosefu mkubwa wa miundombinu sahihi. Kwa kukithiri kwa rushwa, viraka vya barabarani ambavyo havizuii chochote hufanyika kila siku ambapo yakitokea manyunyu, barabara hizo hugeuka mito isiyopitika! Kwa sifa ya uroho wa kibepari viongozi wa serikali ya kitaifa na kaunti wamekuwa wakitoa vibali vya ujenzi wa nyumba na majengo katika maeneo ya mito.
Mafuriko na majanga mengine ya kimaumbile yanaendelea kufichua mzunguko wa kudumu wa utawala wa kibepari wa usimamizi mbovu na kutojali kabisa kwa raia wao wenyewe. Hali hii ya kutamausha isingeweza kufikia kiwango hiki iwapo serikali ingewajibika kwani ingechukua hatua za mapema.
Kama mfumo kamili na utaratibu kamili wa Maisha, Uislamu umeeleza kwamba jukumu haswa la usimamizi wa mambo ya umma kimsingi ni juu ya serikali. Mtume Rehma na Amani Za MwenyeziMungu zimshukie alisema:
«الإِمَامُ رَاعٍ وَهُوَ مَسْئُولٌ عَنْ رَعِيَّتِهِ»
Imam/Kiongozi ni mchungaji naye ni mwenye kuulizwa juu ya uchungaji wake
Kenya na ulimwengu kwa ujumla inahitaji mfumo ulio bora nao ni Uislamu unaozalisha na kuwalea viongozi wanaomcha Allah SWT na kuhisi hisia ya kuwajibika kwani daima wanajua kwamba watawajibishwa Siku ya Kiyama. Omar bin Khattab, Khalifa wa pili wa Mtume Muhammad (SAW), alieongoza serikali ya Kiislamu aliwahi kusema siku moja hadharani: “Ikiwa mbuzi atajikwaa njiani, ninaogopa kwamba kwa hakika Mwenyezi Mungu atanihesabu kwa kushindwa kutengeneza barabara!” Kama Umar chini ya uongozi wake aliogopa kumdhuru mnyama, basi hebu fikiria jinsi angekua na woga zaidi kuona watu wakipigwa na baridi kali baada ya nyumba zao kusombwa na mafuriko.
Shabani Mwalimu
Mwakilishi kwa Vyombo Vya Habari Hizb ut Tahrir Kenya.
01/05/2024