Njia ya Mtume (saw) Kuleta Mageuzi

بسم الله الرحمن الرحيم

Halaqa 7: Kutengwa na Vikwazo kwa Wabebaji Da’wah na Wafuasi Wao

Katika halaqa hii tutazungumzia mbinu ya tatu ambayo Maqureysh walitumia dhidi ya daa’wah ya Mtume (saw) ambayo ni Kuwatenga na Kuwawekea Vikwazo wabebaji da’wah na wafuasi wao.

Suala la Mkataba (Swahifah)

Maquresh walipoona kuwa Maswahaba wa Mtume (saw) wameshukia  mji wa Habasha na wamepata huko amani na utulivu, na Najashiy amewazuia Maqureysh waliokwenda kwake, na Umar ibnul Khatwab amesilimu! Na akawa yeye na Hamzah ibnu Abdul Mutwalib wako pamoja na Mtume (s.a.w) na Maswahaba zake! Na Uislamu unaenea katika makabila, walikusanyika na wakapanga njama kati yao, waandike mkataba ambao watawafunga Bani Hashim na Bani Abdil Mutwalib, Wasiwaolee; wala wasiwaozeshe, Wasiwauzie wala Wasinunue kwao!

Walipoafiqiana juu ya hilo waliandika mkataba, na kuubandika mkataba ndani ya Kaa’bah, sisitizo kwa nafsi zao. Maquresh wakawafungiza Waislamu na Bani Hashim katika shiibi/ (kichaka) cha Abi Talib, na kKutengwa na Vikwazo kwa Waislamu kuliendelea kwa muda wa miaka mitatu (3) mfululizo. Kutengwa na Vikwazo hivyo vikazidi mpaka wakala majani ya miti kwa njaa!

Kuvunjwa kwa Mkataba:

Miongoni Mwa Maqureysh kulikuwepo na walioridhia na mkataba huo na wengine waliouchukia, wakaenda mbio kuvunja mkataba wale wanaochukia, na ikawa anayesimamia suala hili ni Hisham Ibnu Amru. Na alikuwa akiwasiliana na Bani Hashim katika kichaka akiwapelekea chakula usiku akiwa amejificha, akaenda kwa Zuhayr bin Abi Umayyah akamwambia: “Ewe Zuhayr!Je waridhia unakula chakula na kunywa maji na kuvaa nguo na kuoa wake, na wajomba zako wako katika hali unayoijua? Hawauziwi wala watu hawanunui, hawaoi, wala hawaozeshwi?” Zuhayr akasema “Ole wako mimi peke yangu nitaweza kufanya nini? Lau kungekuwa na mtu mwengine ningesimama kuuvunja mkataba”. Akasema Hisham “Basi umeshapata mtu”. Akasema Zuheyr “Ni nani basi?” Akasema Hisham “Mimi”. Zuheyr akamwambia “Tutafutie mtu wa tatu”. Akaenda Hisham kwa Mut’im Ibnu Adiy na akasema “Je unaridhia vizazi viwili viangamie katika Bani Abdi Manaf, na wewe ni shahidi juu ya hayo na kuwaunga Maqureysh juu ya dhulma hii?” Akasema Mut’im: “Nitafanya nini mimi peke yangu?” Akasema Hisham “Umeshapata wa pili”. Akasema Mut’im “Nani?” Akasema Hisham: “Ni mimi”. Akasema Mut’im: “Tutafutia wa tatu”. Akasema Hisham “Tayari”. Akasema Mut’im “Ni nani?” Akasema Hisham: “Zuhayr bin Abi Umayyah “. Akasema Mut’im: “Tutafutie wa nne”.

Akaenda Hisham bin Amru kwa Bakhtariy Ibn Hisham, akamwambia kama alivyomwambia Mut’im Ibn Adiy Akasema: “Je kuna yeyote atakaye saidia hili? Akasema Hisham: “Ndio”. Akasema Amru: “Ni nani?” Akasema Hisham: “Ni Zuhayr Ibn Umayyah na Mut’im Ibn Adiy na mimi niko pamoja nao”. Akasema Mut’im: “Tutafutie wa tano”.

Akaenda kwa Zam’ah Ibn AL-Aswad akamzungumzisha, akamweleza ukuruba wao na haqi yao, Akasema Zam’ah: “Je hili jambo unalonilingania kuna mtu yeyote?” Akasema Hisham: “Ndio”. Akamwelezea wale jamaa, wakaahidiana usiku kukutana “HUJUN” ni Jabali liko juu katika mji wa Makkah wakakutana huko na wakakubaliana juu ya kuuvunja mkataba, Akasema Zuheyr: “Mimi nitawaanzia na nitakuwa wa kwanza atakaye zungumza”.

Walipopambaukiwa wakaenda katika maskani zao na akaja Zuheyr Ibnu Umayah akiwa amevalia vizuri, akatufu Kaa’bah mara saba, kisha akawaelekea watu. Akasema: “Enyi watu wa Makkah! Je, sisi tunakula chakula, na kuvaa nguo, na Banu Hashim wanaangamia hawauziwi wala watu hawanunui kwao! Wallahi sitokaa mpaka huu mkataba wa dhulma uraruliwe”. Akasema Abu Jahl aliyekuwa katika kipembe cha msikiti: “Umesema uongo Wallahi hauraruliwi!”

Akasema Zam’ah Ibn Al-Aswad: “Wallahi wewe ndiye muongo zaidi hatukuupitia mkataba huu ulipoandikwa!” Akasema Abu Bakhtariy Ibn Adiy “Mumesema kweli nyie wawili na ni muongo atakayesema kinyume na hivyo! Tunajitenga kwa Allah kutokana na mkataba huu na kilicho andikwa ndani yake!”

Akasema Hisham Ibn Amru kama hivyo! Akasema Abu Jahl “Hili jambo limepangwa usiku watu wameshauriana mahala pasipo hapa”. Akasimama Mut’im ili akaurarue mkataba akakuta mchwa wameula isipokua “BISMIKALLAHUMMA” kwa jina lako ewe Mola hapo tu ndio hapakuliwa

Na kwa Njia hii mkataba ukavunjwa, Akatoka katika kichaka Mtume (saw) na aliokuwa pamoja nao. Hakika Maqureysh waliona muujiza mkubwa miongoni mwa miujiza ya Utume wake lakini wao waliipa nyongo na wakazidisha ukafiri juu ya ukafiri wao:

Kama alivyoelezea Allah Ta’ala:

وَإِنْ يَرَوْا آيَةً يُعْرِضُوا وَيَقُولُوا سِحْرٌ مُسْتَمِرٌّ

Na wakiona Ishara hugeuka upande na husema: Huu uchawi tu unazidi kuendelea.

[Al-Qamari: 2]

Itaendelea katika UQAB Toleo 12…In Shaa Allah.