AU Kuidhinisha Kenya Kujiunga na UNSC: Ni Fursa ya Kuwahudumikia Wakoloni!

Mnamo Jumatano, 21 Agosti 2019, Muungano wa Afrika (AU) uliidhinisha Kenya kupata kiti ili kuwakilisha Afrika Mashariki katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa (UNSC) lililo na wanachama 15; baada ya kuishinda Djibout kwa kura 37 dhidi ya kura 13 katika mchuano wa pili wa uchaguzi uliofanywa na Kamati ya Wanachama wa Kudumu wa Muungano wa Afrika (AUPRC) mjini Addis Ababa, Ethiopia. Hili linatokea baada ya Kenya kuchaguliwa tena katika Baraza la Amani na Usalama la Muungano wa Afrika (AUPSC)  lililo na wanachama 15 kuhudumu kwa miaka mitatu mnamo Ijumaa, 8 Februari 2019 kwa kupata kura 37 dhidi ya Ethiopia na Sudan. Kikwazo kilichobakia ili Kenya kuwa rasmi mwanachama wa muda katika UNSC ni lazima kupiga debe ili dola wanachama wa UN kuipigia kura Kenya kwa takribani thuluthi mbili za kura za dola wanachama wa UN wakati wa uchaguzi huo utakaofanyika huko New York mnamo Juni, 2020.

Umoja wa Mataifa ni chombo cha kisiasa kinachomilikiwa na nchi koloni za Kimagharibi hususan Amerika baada ya kuibuka kuwa dola kuu duniani katika Vita vya Pili vya Dunia. Hivyo basi, Amerika na washirika wake imeutia minyororo ulimwengu kupitia sera zake ovu zinazopitia UN. Ama kuhusu UNSC ni moja katika nguzo msingi sita za UN zinazodhibitiwa na wanachama watano wa kudumu (Amerika, Uingereza, Ufaransa, Uchina na Urusi) walio na kura ya turufu na wanaodai kuwa ni wadhamini wa usalama na amani duniani! Wanachama kumi waliobakia ni wa muda wanaojiunga ili kuleta uso wa pamoja! Maamuzi ya UN yanapitishwa, kupigiwa kura ya turufu au kupuuzwa na wanachama watano wa kudumu kwa kutegemea maslahi na manufaa yao! Kinaya ni wanachama watano wa kudumu wa UNSC wanahusika katika uhalifu, uvamizi, vita na uporaji wa rasilimali za mataifa mengine. Ifuatayo ni baadhi ya mifano ya moja kwa moja au yasiyokuwa moja kwa moja ya ukandamizaji unaofanywa na wanachama wa watano wa kudumu wa UNSC:

  1. Uvamizi wa Ufaransa wa kijeshi ndani ya Mali mnamo Ijumaa, 11 Januari 2013 kwa kisingizio cha kuzuia kusimama kwa dola ya kigaidi baada ya mapinduzi ya kijeshi katika mji mkuu wa Bamako uliopelekea kukosekana uongozi nchini kote! Pia mnamo Disemba 2013 kwa kisingizio cha kutuliza na kumakinisha nchi ya Jamhuri ya Afrika ya Kati (CAR) baada ya mzozo wa kinyama baina ya Waislamu na Wakristo! Kwa muda wote huo nia yao ikiwa ni kupora rasilimali nyingi zinazopatikana Mali na CAR!
  2. Uvamizi wa Urusi na kuiteka Crimea mnamo 2014. Muendelezo wa mashambulizi dhidi ya Uislamu kwa kisingizio cha kupigana na ugaidi na misimamo mikali; kwa hiyo ikiwafunga kwa muda mrefu Waislamu wengi hususan wale wanaotoka katika chama cha kimfumo na kisichotumia vurugu cha Hizb ut Tahrir!
  3. Marekani kwa ushirikiano na umbile la Israel limo katika uvamizi wa Jerusalem (Al-Quds) kwa kuitambua kuwa ni mji mkuu wa Israel mnamo Jumatano, 6 Disemba 2017 na kuhamisha ubalozi wake kutoka Tel Aviv mnamo Jumatatu, 14 Mei 2018! Urusi na Marekani walikutana mnamo Jumanne, 29 Septemba 2015 katika UN na siku ifuatayo mnamo Jumatano, 30 Septemba 2015 Urusi ilivamia Syria kijeshi na inaendelea mpaka sasa!
  4. Uingereza hivi sasa imo katika vita na Marekani ili kudhibiti Mashariki ya Kati na rasilimali zake nyingi; kwa hivyo Uingereza na Marekani zinawatumia watawala vibaraka katika mataifa watumwa wao ili kuweza kuingia uongozini na katika mchakato huo wakimwaga damu isiyokuwa na hatia ya Waislamu watoto, wanawake na watu wazima na kuharibu miundo mbinu iliyojengwa kwa makarne!
  5. Uchina hivi sasa inaendeleza ukandamizaji dhidi ya Wauyghur Waislamu wanaoishi ndani ya Turkistan Mashariki. Uhalifu ndani ya Turkistan Mashariki hauelezeki. Waislamu huko wanafungwa na kunyongwa katika vigogo vya miti, simiti na zege zinamwaga midomoni mwao kuwaziba pumzi, wanawake wanazuiwa kushika mimba na kuzaa, wanaume wanahasiwa. Serikali ya kikafiri ya China inaweka Mchina kafiri katika kila nyumba ya Muislamu ili kuwachunguza chini ya kisingizio cha kuwaelimisha utamaduni wa Kichina, wakipuuzilia mbali faragha yao na matukufu yao. Waislamu wanazuiwa kufunga mwezi Mtukufu wa Ramadhan. Zaidi ya hayo ni kuwa Uchina iko katika, “kampeni kubwa ya kujenga shule za mabweni kwa kasi mno” ili kuwatia kizuizini kwa nguvu watoto wa Uyghur Waislamu kutoka Turkestan Mashariki ambao wako uhamishoni au wanashikiliwa ndani ya ‘kambi za kuwapa elimu upya’ ambamo hivi sasa ndani yake Waislamu milioni 1 wamefungwa! Wasimamizi wa idara za Uchina wanadai kuwa wanatumia nguvu ili kupambana na ugaidi, misimamo mikali na kujitenga!

Hakika, maangamivu hayo yanatekelezwa na wanachama wa UNSC walio na nguvu za turufu, inathibitisha kwamba ni kikundi tu cha watu mataifa machache; ambao mikono yao imejaa damu na wanaendelea kumwaga zaidi damu isiyokuwa na hatia. Zaidi ya hayo, wanasababisha majanga duniani kote chini ya njama yao ya kirongo ya kueneza amani na usalama; ilhali ukweli ni kwamba wanapigia debe mfumo batili wa kisekula wa kirasilimali na nidhamu zake zinazonuka kwa kupitia ukoloni! Kufeli kwa mfumo wa kisekula wa kirasilimali na nidhamu zake katika kuwasimamia watu mambo yao kumefichuka kwa kila mtu isipokuwa wale ambao ni vipofu wa kifikra na hivyo kila mmoja anatafuta mbadala ili kuubadilisha! Hivyo basi UNSC ipo kubakisha hali halisi na kuzuia uongozi mbadala wa kidunia.

Inasikitisha kwa taifa kama Kenya kutumia rasilimali zake na muda wake adhimu kufanya kampeni kupata kiti kinacholenga kuendeleza mateso kwa raia wake na wa nchi jirani kwa madai ya kupigana na ugaidi na misimamo mikali/siasa kali! Hakika, uovu unakumbatia uovu kwani Kenya ilituma mwakilishi wake katika ufunguzi rasmi wa ubalozi wa Amerika ndani ya Jerusalem mnamo Jumatatu, 14 Mei 2018. Kenya ili thibitisha kwamba hakika ni rafiki wa Amerika na umbile la Israel ambao wote ni wavamizi wa Ardhi Tukufu ya Palestina na maadui wa Uislamu na Waislamu ndani ya Al-Quds na duniani kote.

Tunatarajia lau Kenya itajiunga na UNSC baada ya kura za UN mnamo Juni 2020, uadui wake dhidi ya Uislamu na Waislamu kwa kisingizio cha kupambana na misimamo mikali na ugaidi utazidi kwa kiwango kikubwa tukizingatia kutiwa saini mswada wa kanuni ya Sheria zilizofanyiwa marekebisho jumla ya mwaka 2019 ikiwemo ile kanuni ya kuzuia ugaidi (The Statute Law (Miscellaneous Amendment) Act 2019 – No. 21 of 2019)). Kutia saini huko kunamaanisha kujumuishwa kwa Huduma ya Kitaifa ya Polisi, Wizara ya Masuala ya Kigeni, Afisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma, Huduma ya Wanyama Pori, Huduma za Magereza na Mamlaka ya Usafiri wa Angani zimejumuishwa na kuwa wanachama wa Kituo cha Kupambana na Ugaidi. Fauka ya hayo, njama ya kuwasilisha Mswada wa 2018 wa Kuzuia Ugaidi ambao unalenga kuwasajili wasimamizi wa idara za elimu kushiriki katika kupambana na siasa kali!

Hakika, lau Kenya ina azma ya kushiriki na kufurahia amani na usalama wa kweli basi ni lazima ikate mahusiano yake kwa mabwana zake wakoloni ambao ndio chanzo cha majanga ambayo yanashuhudiwa ndani ya Kenya na duniani kote na ambayo yamesababisha Kenya na Afrika kuganda kiuchumi, kisiasa, kijamii na kielimu. Majanga yanajumuisha kuvunjika kwa familia na mujtama kutokana na utekelezwaji wa nidhamu ya kijamii ya huria, uchumi unaotegemea riba unaopigia debe umasikini na kuzidisha pengo kati ya matajiri na masikini, uongozi duni uliosimama juu ya nidhamu ya kidemokrasia, sera ya kigeni iliyokitwa katika ukoloni miongoni mwa maovu mengine! Baada ya kukata mahusiano ya kikoloni, ni lazima wakumbatie mwito wa kurudisha tena maisha ya Kiislamu kupitia kusimamisha Khilafah kwa njia ya Utume. Mtume (saw) alisema kwamba utawala wa kidhalimu na taasisi zake kama UNSC zitaondoshwa:

«…ثُمَّ تَكُونُ مُلْكاً جَبْرِيَّةً فَتَكُونُ مَا شَاءَ اللهُ أَنْ تَكُونَ ثُمَّ يَرْفَعُهَا إِذَا شَاءَ أَنْ يَرْفَعَهَا ثُمَّ تَكُونُ خِلَافَةٌ عَلَى مِنْهَاجِ النُّبُوَّةِ ثُمَّ سَكَتَ»

“…kisha kutakuweko na utawala wa kidhalimu, kwa muda autako Mwenyezi Mungu, kisha Mwenyezi Mungu atauondosha lau Atataka, kisha kutakuweko na Khilafah kwa Njia ya Utume, na kisha yeye (saw) akanyamaza.”

Ni Khilafah pekee itakayo dhamini utulivu, amani na usalama wa kweli kwa damu, mali na heshima za watu pasina kuzingatia rangi au dini zao. Kwa kukosekana Khilafah, uovu umeshamiri katika nyanja zote za maisha! Upande wetu, lazima tuendelee kufanya kazi ya ulinganizi wa Khilafah tukiwa na msimamo huku tukiweka juhudi zetu na matumaini yetu kwa Mwenyezi Mungu (swt) pekee: (وَمَا النَّصْرُ إِلاَّ مِنْ عِنْدِ اللَّهِ إِنَّ اللَّهَ عَزِيزٌ حَكِيمٌ)”Na haupatikani ushindi ila kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye nguvu na Mwenye hikima.” [An-Anfal: 10]

Ali Nassoro Ali

Mwanachama wa Afisi ya Habari ya Hizb ut Tahrir Kenya

Makala Na.59: Ijumaa, 22 Dhul-Hijja 1440 | 2019/08/23