Mwaka wa 2017, ni mwaka wa uchaguzi mkuu nchini Kenya ambapo viongozi wa kisiasa wanashughulika na kuwashughulisha wananchi vikali na matayarisho ya uchaguzi kama huu.Sekta zote za maisha zimechovywa siasa ndani yake.Wananchi na viongozi wote wanaimba wimbo mmoja; ‘Siasa’ ilimradi kila mtu ameshughulishwa kwa njia moja au nyengine na joto la uchaguzi mkuu. Siasa zimepamba moto kila mahali; ni siasa…siasa… kila mmoja apenda kuizungumzia kama isemwavyo na wenyewe ‘asie na mwana aeleke jiwe’.
Viongozi wa vyama tofauti tofauti na wapambe wao wanashughulika sana katika kuzitafuta kura za uchaguzi huu mkuu.Wanafanya kila juhudi ili mambo yawanyookee.Kila watakaloona bora kufanya na la kuendeleza mbele kampeni basi wanaropokwa na kufanya lolote bila kujali chochote. Wamebadilisha sherehe na hafla mbalimbali kama vile matanga, harusi na mazishi kuwa majukwaa ya kisiasa. Wao na wapambe wao wakijaribu kuuza sera zao potofu za kidemokrasia katika majukwaa haya.
Raia na viongozi watarajiwa hawakubakisha lolote ila wamehakikisha kufanya lolote lile ili kufanikisha malengo yao.Wanawake nao pia wametumiwa katika ufanikishaji huo wa malengo yao. Wameingizwa katika ulingo wa siasa na kutumiwa bila wao kujua kama wanatumiwa.Maskini! wanaona ni raha kwani hupewa vijipesa ndani yake, basi hawafikirii athari ya yale wanayoyafanya kwa jina la kupigia debe viongozi wao.
Mabanati wamebandikwa majina “Warembo na Uhuru” na “Warembo na Joho” wakijinasibisha na viongozi wanaowapigia debe. ‘Warembo’ hawa kama walivyoitwa hujirembesha na kuzunguka barabarani wakiimba na kucheza ngoma wakiwa nusu uchi hadharani waonekane na kusikika wakiwafanyia kampeni viongozi waliowachagua. Mama zetu na dada zetu wanajidhalilisha barabarani. Wakaivua stara ya Allah (swt) kwa ajili ya kampeni za siasa potofu ya Kidemokrasia.
Demokrasia pamoja na njia zake za kufikia kwenye uongozi ni upotofu mtupu. Imemdunisha mwanamke thamani yake na inazidi kumfedhehesha na tawala za kidemokrasia za kitwaghut. Heshima aliyoekewa mwanamke na Uislamu leo haipo tena, imewavuka wanawake kama nguo inavyovuliwa mwilini. Wanawake wamefanywa leo kama chombo cha sanaa na biashara kuendeleza uchumi wa taifa. Picha za wanawake wakiwa uchi zimesheheni leo kwenye mabango ya biashara. Na sasa wameingizwa uwanjani bila ya mazoezi, wacheze watakavyocheza, iwe ni rafu au vipi bora wafunge mabao. Hivyo basi mwanamke amejisahau, baada ya kujitosa uwanjani, amesahau kama kuna sheria za uchezaji na anacheza atakavyo.
Hilo la kuzungushwa na ngoma na nyimbo haitoshi, wanawake wameshauriwa kuwanyima waume zao haki zao za ndoa mpaka wawaonyeshe kadi zao za kura. Hii harakati ya kutafuta kura imewatia watu wazimu haswa viongozi wanaotaka kuchaguliwa, wanaamua na kufanya chochote kinachowajia akilini bila kujua athari yake ni nini katika jamii. Wanawake nao wamekuwa kama bendera ambayo hufuata upepo.
Haya ni yakutarajiwa kutokamana na nidhamu hii ya Kidemokrasia ambayo imemgeuza mwanamke kama chombo cha matangazo ya biashara. Matangazo yakiwa na wanawake nusu uchi yametapakaa kila mahali. Kweli kabisa mfumo fisadi wa kirasilimali umemdunisha mwanamke. Kila kitu lazima kiwe na ufisadi. Ni wakati sasa sisi Waislamu tusitishe kuunga mkono upuzi huu na kujikita katika majukumu yetu kama Waislamu; maanake tuna mengi ya kujibu kuhusu yanayotokea kwa familia zetu, mama zetu na dada zetu. Ama tumejitia upofu au uziwi kuhusu mambo haya? Je hatuwaoni kina mama zetu na dada zetu wakijidhilalisha mabarabarani? Tutaulizwa kuhusu haya; tujiandae kutuoa majibu sahihi kwa Allah (swt))
Ni Khilafah kwa Njia ya Utume pekee inayoweza kuwapa hadhi na heshima wanawake wa Ummah huu bora uliotiwa korokoroni na mfumo batili wa Urasilimali ambao umewatoa wanawake katika jukumu lao msingi la kuwa mama na mke; na kuwafanya kuwa vyombo vya kampeni na kutafuta usemi wa kisiasa.
Mgeni J Salim
Kutoka Jarida la UQAB Toleo 1