Siku ya Ukoma duniani: Hadaa nyengine ya Kibepari

Tarehe 30 Januari dunia iliadhimisha siku ya maradhi ya Ukoma duniani. Asili siku hii iliteuliwa kama makumbusho ya kifo cha aliekuwa kiongozi wa India Mahatma Gandhi anayedaiwa kuwa ndiye aliyefahamu vyema umuhimu wa kushughulikia maradhi haya. Wamagharibi wanadai kuwa siku hii ilioanzishwa mwaka wa 1954 ni kuwatambulisha wagonjwa hao waweze kufahamika na kujulikana kama binadamu wanaostahili  heshima na kuwapa fursa ya kuchangia jamii kwa vipaji vyao.

Ukoma umeathiri binadamu tangu miaka elfu nyingi zilizopita. Maradhi hayo yamepata jina lake kutoka neno la Kilatini lepra, maana yake ni mwenye gamba kwenye ngozi. Pia hujulikana kwa jina la “maradhi ya Hansen” linalotokana na jina la daktari. Ugonjwa huu husababishwa na bakteria vinavyojulikana kitaalamu kama Mycobacterium leprae na M. lepromatosis.

Baada ya ambukizo kuna kipindi ambapo mgonjwa hana dalili za ukoma. Kipindi hicho bila dalili kinaweza kuendelea hadi miaka 5 au zaidi. Dalili zinazoonekana ni kwa mfano vidonge vya chembe vya neva, vya mfumo wa upumuaji, vya ngozi na vya macho.

Wakati dalili zinapoanza kuonekana mgonjwa hasikii tena baridijoto wala maumivu. Kwa hiyo hatambui kirahisi kama amepata jeraha. Vidonda vinavyotokea haviumi na uchafu pamoja na bakteria hatari zinaingia mwilini. Hivyo vidonda vinaweza kuwa vikubwa zaidi kwa sababu havitibiwi au vinachelewa kutibiwa. Ndiyo sababu pengine wakoma wanapoteza viungo vya mwili kama vidole na hata mguu au mkono kutokana na majeruhi yanayorudiarudia.

Dr Erwin Cooremen mkuu wa jumuia ya Global Leprosy Programme alisema kwenye kongamano la Ukoma lilioandaliwa Uchina mwezi Septemba mwaka jana (2016) “Leprosy is not declining at the pace we would like to see,” ( Ukoma haupungui kwa kasi tunayopenda kuiona) Akaendelea kusema:  “Our new strategy involves leadership and coordination, and focuses not only on medical or public health interventions but also on personal and social aspects – factors that are important for a disease that is still so stigmatized.” (Mkakati wetu unahusisha uongozi na ushirikiano na si tu kuangalia madawa ama kushughulikia afya ya umma bali pia kuangalia hali za kibinafsi na jamii- sababu ambazo ni muhimu kwa ugonjwa huu ambao hadi sasa unafanyiwa unyanyapaa).

Kwa haya inadhihirisha wazi kwamba ubepari kimakusudi haujatabani/kuchukua kidhati suala la maradhi haya. Ndio hadi wa leo maradhi haya yanaendelea kuwa sugu huku India pekee ikiwa na asilimia 60 ya wanaogua maradhi haya kote duniani.

Hadaa za mabepari katika kushughulikia maradhi: Kuwekwa siku kama hizi na mfano wake ni kujaribu tu kuhadaa watu waamini kuwa Urasilimali kweli unajali umma. Warasilimali licha ya kupiga hatua katika utengezaji wa madawa nalo ni jambo zuri linalohimizwa na Uislamu, lakini wao huangalia suala la afya kwa hesabu za manufaa ambayo ndiyo kipimo chao cha kusukuma harakati na mienendo ya wanadamu. Hawaangalii afya kwa msingi kuwa ni hitajio muhimu la kibinadamu bali huliangalia kwa msingi wa tija ya kiuchumi yaani; Je watu ambao afya zao zikiangaliwa zitaleta faida ya kiuchumi. Hivyo watu ambao kwa warasilimali hawajakuwa na umuhimu wa kiuchumi kwao afya zao hudunishwa kwa kunyimwa matibabu na madawa. Ndio maana kauli mbiu ya shirika la Afya duniani imekuwa; ‘Afya na Maendeleo’. Aidha, warasilimali na serikali zao huchukua huduma ya afya kama fadhila kwa raia wake wala sio kama jukumu lao kwa umma.

Ufahamu sahihi kuhusu uzima na maradhi: Katika Uislamu afya huangaliwa kama neema kubwa kwa mwanadamu anayofaa kwayo kumshukuru Allah SWT. Ndio katika mafundisho ya Uislamu tukashajiishwa kutafuta dawa kama ilivyopokelewa kutoka SAAW… akisema:

فعن أسامة بن شريك عن النبي صلى الله عليه وسلم أنه قال (( تداووا يا عباد الله فإن الله لم يضع داء إلا وضع له شفاء إلا داء واحدا الهرم))

“Tafuteni dawa enyi waja wa MwenyeziMungu kwani MwenyeziMungu hakuweka maradhi ila iko dawa yake ispokuwa Uzee hauna dawa.”

 Isitoshe Uislamu ukajaalia kuwa matibabu ni mmoja wapo ya mahitaji msingi ya jamii/umma na ni jukumu la serikali kuhakikishia rai wake haki hii.

Moja katika fahamu za Kiislamu kuhusu matendo ya mwanadamu ni kuwa yapo matendo ambayo hutukia kwa mwanadamu pasina na khiyari yake yaani hutukia pasina matakwa yake haya huitwa Qadhaa yaani MwenyeziMungu pekee ndie aliyeamua kutukia kwake mfano ni Maradhi. Mwislamu hivyo hutakikana kila anapougua maradhi basi atafute dawa lakini wakati huo huo awe na subra kwa kuelewa kua hiyo ni kadhaa ya Allah lau ataisubiria atapata ujira mkubwa.

عَنْ أَبِي سَعِيدٍ الْخُدْرِيِّ وَعَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ (رضي الله عنهما)  عَنْ النَّبِيِّ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ قَالَ:  ((مَا يُصِيبُ الْمُسْلِمَ مِنْ نَصَبٍ وَلاَ وَصَبٍ وَلاَ هَمٍّ وَلاَ حُزْنٍ وَلاَ أَذًى وىَ غَمٍّ حَتَّى الشَّوْكَةِ يُشَاكُهَا إِلاَّ كَفَّرَ اللَّهُ بِهَا مِنْ خَطَايَاهُ))

Kutoka kwa Abu Sa’iyd Al-Khudriyy na Abu Hurayrah (رضي الله عنهما)  kwamba Mtume (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema:

“Muislamu hatopatwa na tabu, wala maradhi, wala hamu wala huzuni wala udhia wala ghamu [sononeko] hata mwiba unaodunga isipokuwa Allaah Humfutia madhambi yake kwa sababu ya hayo” Al-Bukhaariy na Muslim

Muhimu pia kufahamu kuwa kukithiri ufisadi na maasia kwa ujumla hupelekea watu kupata magonjwa. Leo twaishi chini ya mfumo fisidifu wa kirasilimali unaofungua mlango wa kumkufuru na kumuasi MwenyeziMungu tusitarajie kuwa salama. Isitoshe mfumo wa kibepari umezalisha matatizo ya kiuchumi, kisiasa na kijamii kiasi cha jamii kuzongwa na mawazo yanayosababisha maradhi ambayo hayakuweko katika zama za Uislamu ulipokuwa ukiendesha dunia kupita Khilafah yake.  Kwa mfano shirika la Afya duniani limekiri kuwa msongo wa mawazo leo umesababisha maradhi ya vidonda vya tumbo na pressure. Imepokewa kuwa Mtume SAAW amesema

((من كثرَ همُّهُ سقمَ بدنُه))

Mwenye kuwa na shida/hamu? nyingi basi mwili wake huugua”

Maradhi kama mtihani kwetu: Familia nyingi leo hufeli kuelewa kuwa maradhi pia ni sehemu ya Mitihani kwetu kutoka kwa Mola wetu. Imani hii ni muhimu sana kwani ikikosekana watu huingia katika kufuru na ushirikina kwa sababu ya maradhi. Kiislamu tumehimizwa mno kuwa na subra. Hapa ndio huja suala la unyanyapaa yaani kutengwa kwa mwenye maradhi kama vile ukoma, ukimwi na mengineyo. Na hili limekuwa tatizo la wazi katika mfumo wa kibepari kama inavyodhihirika kutengwa kwa wagonjwa katika makambi ya wa ukoma. Katika nchi kama India makambi hayo yapata zaidi ya elfu. Pia China na Afrika makambi haya yanapatikana kwa mia kadha. Katika historia ya Ukoma utakuta kuwa umesababisha wagonjwa wake kubaguliwa kwa miaka mingi. Ubaguzi huo bado ndio huhamasisha wagonjwa kujificha na kukosa matibabu mapema. Na hapa napenda ifahamike kuwa maana ya kumbagua mgonjwa wa ukoma ni kule kutomshughulikia kimatibabu na kumdharau. Ama kutahadhari na wenye ugonjwa huu ili kuepuka maambukizi hili haliingii kwenye unyanyapaa bali ni katika mafunzo ya Uislamu pale SAAW aliposema:

((فر من المجذوم كما تفر من الأسد))

“Kumkimbia mwenye ukoma ni kama kumkimbia samba”

Kwa haya twasema umma utaendelea kupuuzwa kila unapo kumbwa na  maradhi kwa kuhadaiwa na ‘mashirika’ ya kirasilimali ambayo yenyewe hutaka watu waugue bali husaidia kusambaza maradhi kwa watu wa kawaida ili wapate kuuza madawa ambayo kiasili si yenye kutibu kikweli ila kuleta afueni tu ya muda. Kusimamishwa Uislamu kupitia serikali yake halisi ya Khilafah ndio pekee kutashughulikia umma matatizo yake kikweli.

Shabani Mwalimu – Mwakilishi kwa Vyombo vya Habari

Hizb ut-Tahrir Kenya

Kutoka Jarida la UQAB Toleo 1