Covid-19 yazidi kuumbua mfumo wa kiuchumi wa Kibepari

 

Ni wazi ndwele ya Covid-19 inaendelea kufichua udhaifu wa chumi za mataifa ya kibepari kote duniani.Tayari wanauchumi wameonya uwezekano mkubwa wa kuanguka kwa uchumi wa dunia. Kuna istilahi mbili zinazotumiwa na wanauchumi kuelezea maana ya msukosuko wa kiuchumi. Wakwanza, ni ule unaojulikana kama ‘Recession’ ambao hufasiriwa kama ile hali ya ukuaji mbaya wa kiuchumi (negative economic growth) inayoshuhudiwa kwa mfululizo wa miezi sita. Wapili; ni Great Depression nao ni hali ya nchi kukumbwa na hali mbaya ya kiuchumi inayoendelea kwa kipindi cha miaka kadhaa.

Janga la virusi vya Corona limelazimu serikali za kibepari kuja na baadhi ya mikakati ya kukabiliana nalo. Nchini Amerika, taifa ambalo kwa sasa ndilo linaloloongoza kwa maambukizi ya Corona, rais Donald Trump alitia saini mpango wa kuimarisha uchumi wa kitita cha $2tn. Hatua kama hii tayari imechukuliwa barani Ulaya ambapo Ujerumani ishapitisha euro 550, Ufaransa  Euro  bilioni 300, na Uhispania euro bilioni 200. Barani Afrika, licha ya kurekodi maambukizi machache lakini janga hili linaendelea kuzua tumbo joto hasa ikizingatiwa serikali nyingi ni zenye mrundiko wa madeni. Kwa mfano, Kenya kwa sasa ina deni la Sh 6.3 tr hali itakayo fanya uchumi wake uendelea kuathirika pakubwa. Benki ya dunia pamoja na shirika la fedha duniani imetowa mwito kwa mataifa makubwa ya kiuchumi kuyapa mataifa masikini kama Kenya muda zaidi wa kulipa madeni yao. Ikumbukwe kuwa serikali ya Kenya imeomba tena mkopo wa kiasi cha bilioni 130 kuweza kukabiliana na janga la Corona.

Kwa kuwa uchumi wa dunia wenyewe umekua ukisuasua tokea kushuhudiwa kwa ule mdororo wa kiuchumi duniani mwaka 2008, ni wazi kwamba hatua zilizochukuliwa na mataifa mengi za kukabaliana na janga la Corona zitapelekea kuudidimiza zaidi bali kupelekea kusambaratika kwa uchumi.Tayari Kenya inaendelea kuhesabu hasara za kiuchumi kutokana na janga la Corona.  Shirika la ndege la Kenya linakadiria hasara ya milioni 800 kwa mwezi. Katika bandari ya Mombasa kumeshuhudiwa harakati chache mno hali inayoonesha kuwa hali sio nzuri. Mapendekezo ya kupunguza ushuru katika mapato na wa viwanda kama jaribio la kuokoa uchumi dhidi ya janga la corona inatajwa kuwa itapelekea Mamlaka ya ukusanyaji ushuru nchini Kenya (KRA) kupata hasa ya Sh 1.3 bilioni kila siku kwa muda wa miezi mitatu. Kulingana na utafiti uliofanywa na muungano wa makampuni katika sekta za kibanafsi (Kepsa), takriban kwenye kampuni kumi, sita kati yake zimerekodi kupata hasara au kiwango kidogo cha faida ya huduma zake. Mbali na hayo, ngazi ya kimataifa bei ya mafuta inaporomoka vibaya sana na chanzo chake ni kusambaratika biashara duniani.

Kwa mara nyengine udhaifu wa  mfumo wa kiuchumi wa kirasilimali umewekwa peupe pepepe!  Ni dhahiri kuwa ni duni kama nyumba ya buibui ambayo kabla ya kutokea majanga tayari yenyewe ni majanga! Majaribio yote yanayofanywa na serikali ati kuokoa uchumi wao na kukabiliana na janga la corona ni kuficha kimakusudi aibu za mfumo wao ambao sasa umekufa bado kutangazwa siku ya mazishi yake! Kuna msemo wa kiingereza ambao ni  maarufu kwa wanauchumi :”God may as well have created the universe but we mortals created paper money and risky banks.” (Mungu aliumba ulimwengu lakini viumbe waovu kwa mikono yao wakajitengezea pesa za makaratasi na mabenki. Msemo huu unaabiri misingi duni iliojengwa juu yake mfumo wa kiuchumi kirasilimali nayo ni pesa za karatasi na riba inayofanya kuporomoka kwake kuwa rahisi mno.

Ama vipi Riba huporomosha uchumi, hii ni rahisi kuelewa kwa kuangalia tu chumi za ulimwengu wa tatu jinsi zinavyojitia kitanzi kwa kusheheni madeni makubwa kiasi cha kutoweza hata kujisimamia miradi yake ya ndani! Na hapa ndio ule msemo usemao creditors have better memories than debtors (wakopeshao ndio walio na kumbukumbu nzuri zaidi kuliko wakopeshwao.) Kwa bahati mbaya msingi huu wa mikopo ya riba ndio uti mgongo wa uchumi na kwa mantiki hii ndio Benki kuu ya Kenya ikapunguza kiwango cha riba kwa dhana kuwa kutachochea watu kuchukua mikopo zaidi kama njia ya kukabiliana na janga hili! Hatua ndio hufilisisha mabenki ya kirasilimali ambayo baadaye hukabiliwa na lile tatizo waliitalo credit crisis.

Ama kuhusu msingi wa pesa za makaratasi, ni kuwa uchapishwaji wa pesa hizi huzidisha tu kuweko kwa mzunguko wa pesa na wala sio kuzidisha bidhaa ambazo ndio huhitajika zaidi pale watu wanapokuwa na pesa. Lakini pesa zinapokuwa nyingi mukabala wa bidhaa kuwa chache inamaana mahitajio huwa mengi na hivyo kusababisha bei kupanda. Fauka ya haya, pesa za makaratasi zenyewe kimaumbile hazina thamani ya bali thamani yake hupangwa na kupanguliwa na mamlaka husika. Kwa maana hii, thamani yake hupimwa na ule uwezo wake wa kubadilisha kitu chengine chenye thamani kwa yule alie na pesa.

Hali inayoendelea kuukumba ulimwengu kwa sasa ni ushuhuda tosha wa haja ya kuletwa kwa mfumo mbadala nao si mwengine ila Uislamu. Huku janga la Covid 19 likiumbua mfumo wa kibepari, ni wakati wa wasomi na mufakirina kuusoma Uislamu na kuufahamu ili waweze kuulingania kwa ajili ya kutekelezwa kivitendo kupitia serikali yake ya Khilafah. Serikali hii ya Khilafah itakaposimama ndio ulimwengu itaweza sio  tu kupambana na majanga kama la Corona bali kung’oa mfumo muovu wa kirasilimali ambao ni hatari zaidi hata kuliko maradhi yoyote yale.

Shabani Mwalimu

Mwakilishi kwa Vyombo Vya Habari

Hizb ut-Tahrir Kenya

10 April 2020.