Je inajuzu kuzuia swala za ijumaa na jamaa misikitini?

Sehemu katika jibu la swali la amiri wa Hizb Ut-Tahrir Ataa bin Khalil Abu rashta: “Athari za Virusi vya Korona”.
بسم الله الرحمن الرحيم
Kusitisha swala za Ijumaa na jamaa kunapotokea kuenea kwa majanga ya maambukizi hakufanywi kwa njia ya kijumla, bali wagonjwa ndio hutengwa na hawaruhusiwi kuingia misikitini kwa swala ya jamaa au Ijumaa, na hatua zote huchukuliwa kuanzia usafi na kuuwa virusi na kuvaa barakoa endapo itahitajika na kadhalika. Kisha watu walio wazima wataendela kuswali Ijumaa na jamaa pasi na kuwazuia, na ikiwa kuna haja ya timu za madaktari misikitini ili kuangalia ni nani anaye shukiwa kuwa mgonjwa miongoni mwa wenye kuabudu, basi hatua hiyo yaweza kuchukuliwa, lakini bila ya kukatiza swala za Ijumaa na jamaa kwa Waislamu walio wazima. Dalili za swala za jamaa na Ijumaa hazijumuishi ukatizaji wa kudumu, bali hazihitaji idadi kubwa  ili kutekelezwa kwake kama tutakavyo eleza, na baadhi ya Waislamu wamepewa udhuru wa kutozihudhuria, kwa sababu zinazo wahusu wao tu, kama ifuatavyo:
1- Ama swala ya jamaa, ni faradhi ya kutoshelezana (kifayah ):
Swala ya jamaa ni faradhi ya kutoshelezana ambayo ni lazima ionyeshwe kwa watu, kwa sababu Abu Dardaa, Mwenyezi Mungu awe radhi naye, amesimulia kwamba Mtume (saw) amesema:
« ﻣَﺎ ﻣِﻦْ ﺛَﻠَﺎﺛَﺔٍ ﻓِﻲ ﻗَﺮْﻳَﺔٍ ﻭَﻟَﺎ ﺑَﺪْﻭٍ ﻟَﺎ ﺗُﻘَﺎﻡُ ﻓِﻴﻬِﻢْ ﺍﻟﺼَّﻠَﺎﺓُ ﺇِﻟَّﺎ ﻗَﺪْ ﺍﺳْﺘَﺤْﻮَﺫَ ﻋَﻠَﻴْﻬِﻢْ ﺍﻟﺸَّﻴْﻄَﺎﻥُ، ﻋَﻠَﻴْﻚَ ﺑِﺎﻟْﺠَﻤَﺎﻋَﺔِ ﻓَﺈِﻧَّﻤَﺎ ﻳَﺄْﺧُﺬُ ﺍﻟﺬِّﺋْﺐُ ﻣِﻦَ ﺍﻟْﻐَﻨَﻢِ ﺍﻟْﻘَﺎﺻِﻴَﺔَ »
“Ikiwa kuna watu watatu katika kijiji au jangwani na wasisimamishe swala (kwa jamaa), shetani amechukua ubwana juu yao; shikamana na jamaa, kwani mbwa mwitu humnyakua kondoo aliye peke yake.”
Imesimuliwa na Abu Dawood kwa Isnad (silsila) iliyo Hasan, na ni kuhusu swala ya jamaa. Ni faradhi ya kutoshelezana; baadhi ya Waislamu walichelewa kuswali jamaa pamoja na Mtume (saw) na Mtume akawaacha baada ya kutishia kuwachoma.
Al-Bukhari amesimulia kwamba Abu Huraira amesema kwamba Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) amesema,
« ﻭَﺍﻟَّﺬِﻱ ﻧَﻔْﺴِﻲ ﺑِﻴَﺪِﻩِ ﻟَﻘَﺪْ ﻫَﻤَﻤْﺖُ ﺃَﻥْ ﺁﻣُﺮَ ﺑِﺤَﻄَﺐٍ ﻓَﻴُﺤْﻄَﺐَ ﺛُﻢَّ ﺁﻣُﺮَ ﺑِﺎﻟﺼَّﻠَﺎﺓِ ﻓَﻴُﺆَﺫَّﻥَ ﻟَﻬَﺎ ﺛُﻢَّ ﺁﻣُﺮَ ﺭَﺟُﻼً ﻓَﻴَﺆُﻡَّ ﺍﻟﻨَّﺎﺱَ ﺛُﻢَّ ﺃُﺧَﺎﻟِﻒَ ﺇِﻟَﻰ ﺭِﺟَﺎﻝٍ ﻓَﺄُﺣَﺮِّﻕَ ﻋَﻠَﻴْﻬِﻢْ ﺑُﻴُﻮﺗَﻬُﻢْ ﻭَﺍﻟَّﺬِﻱ ﻧَﻔْﺴِﻲ ﺑِﻴَﺪِﻩِ ﻟَﻮْ ﻳَﻌْﻠَﻢُ ﺃَﺣَﺪُﻫُﻢْ ﺃَﻧَّﻪُ ﻳَﺠِﺪُ ﻋَﺮْﻗﺎً ﺳَﻤِﻴﻨﺎً ﺃَﻭْ ﻣِﺮْﻣَﺎﺗَﻴْﻦِ ﺣَﺴَﻨَﺘَﻴْﻦِ ﻟَﺸَﻬِﺪَ ﺍﻟْﻌِﺸَﺎﺀَ »
“Naapa kwa Yule ambaye nafsi yangu imo mikononi mwake, nilikaribia kuamrisha kuni zikusanywe na kisha namrishe mtu aadhini kisha ni mwamrishe mtu aswalishe kisha niende kwa nyuma hadi kwa wale wanaume wasio swali kwa jamaa nizichome moto nyumba zao. Naapa kwa Yule ambaye nafsi yangu imo mikononi mwake, lau mmoja wenu angejua kwamba angepata mfupa uliojaa nyama nzuri au vipande viwili vya nyama katikati ya mbavu mbili, angehudhuria swala ya Ishaa.”
Na ikiwa ni fardh ya lazima (‘Ain) kwa kila Muislamu, hangewaacha waswali yeye aondoke, kwani hii ilikuwa ni swala ya jamaa kupitia kutajwa swala ya Ishaa. Na jamaa kwa uchache inapaswa angaa watu wawili, imam na maamuma (mmoja anaye ongozwa) kutokana na Hadith ya Malik bin Al-Houwarith, aliye sema:
« ﺃَﺗَﻴْﺖُ ﺍﻟﻨَّﺒِﻲَّ ﺻﻠﻰ ﺍﻟﻠﻪ ﻋﻠﻴﻪ ﻭﺳﻠﻢ ﺃَﻧَﺎ ﻭَﺻَﺎﺣِﺐٌ ﻟِﻲ ﻓَﻠَﻤَّﺎ ﺃَﺭَﺩْﻧَﺎ ﺍﻟْﺈِﻗْﻔَﺎﻝَ ﻣِﻦْ ﻋِﻨْﺪِﻩِ ﻗَﺎﻝَ ﻟَﻨَﺎ ﺇِﺫَﺍ ﺣَﻀَﺮَﺕْ ﺍﻟﺼَّﻠَﺎﺓُ ﻓَﺄَﺫِّﻧَﺎ ﺛُﻢَّ ﺃَﻗِﻴﻤَﺎ ﻭَﻟْﻴَﺆُﻣَّﻜُﻤَﺎ ﺃَﻛْﺒَﺮُﻛُﻤَﺎ»
“Nilikuja kwa Mtume (saw) mimi na mwenzangu, na tulipokuwa tunataka kuondoka kutoka kwake, alisema: ‘Pindi wakati wa swala unapo fika, basi adhinini, kisha mkubwa wenu kwa umri awe ndo imamu wenu.’” Imesimuliwa na Muslim.
Na swala ya jamaa haiondolewi isipokuwa kwa udhuru wa kisheria, ambao kwao kuna andiko kama baridi au usiku wenye mvua, kwani Hadith ya Bukhari ambayo Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) amesema:
« ﻛَﺎﻥَ ﻳَﺄْﻣُﺮُ ﻣُﺆَﺫِّﻧﺎً ﻳُﺆَﺫِّﻥُ ﺛُﻢَّ ﻳَﻘُﻮﻝُ ﻋَﻠَﻰ ﺇِﺛْﺮِﻩِ ﺃَﻟَﺎ ﺻَﻠُّﻮﺍ ﻓِﻲ ﺍﻟﺮِّﺣَﺎﻝِ ﻓِﻲ ﺍﻟﻠَّﻴْﻠَﺔِ ﺍﻟْﺒَﺎﺭِﺩَﺓِ ﺃَﻭْ ﺍﻟْﻤَﻄِﻴﺮَﺓِ ﻓِﻲ ﺍﻟﺴَّﻔَﺮِ »
“Alikuwa akimwamuru muadhini aadhini kisha aseme mwisho wake, “Swalini majumbani katika usiku wenye baridi au mvua au katika safari.”
2- Ama swala ya Ijumaa, ni swala ya faradhi ya lazima (Fardh Ain) , na hairuhusiwi kuondolewa isipokuwa kwa udhuru, na dalili ya hilo ziko nyingi, ikiwemo:
Maneno ya Mwenyezi Mungu (swt)
[ ﺇِﺫَﺍ ﻧُﻮﺩِﻱ ﻟِﻠﺼَّﻼَﺓِ ﻣِﻦْ ﻳَﻮْﻡِ ﺍﻟْﺠُﻤُﻌَﺔِ ﻓَﺎﺳْﻌَﻮْﺍ ﺇِﻟَﻰ ﺫِﻛْﺮِ ﺍﻟﻠَّﻪِ ﻭَﺫَﺭُﻭﺍ ﺍﻟْﺒَﻴْﻊَ ]
“Enyi mlio amini! Ikiadhiniwa Sala siku ya Ijumaa, nendeni upesi kwenye dhikri ya Mwenyezi Mungu, na wacheni biashara.” [Al-Jumu’a: 9]
Ombi lililo katika ayah hii ni la wajib kutokana na dalili ya Qareenah (kiashiria) cha katazo la kufanya lililo mubah, ishara ya ombi la kukatikiwa (jazim). Na Al-Hakim amesimulia katika Al-Mustadrak juu ya Al-Sahihain kutoka kwa Tariq bin Shihab, kutoka kwa Abu Musa, kutoka kwa Mtume (saw) kwamba yeye amesema:
« ﺍﻟْﺠُﻤُﻌَﺔُ ﺣَﻖٌّ ﻭَﺍﺟِﺐٌ ﻋَﻠَﻰ ﻛُﻞِّ ﻣُﺴْﻠِﻢٍ ﻓِﻲ ﺟَﻤَﺎﻋَﺔٍ ﺇِﻟَّﺎ ﺃَﺭْﺑَﻌَﺔٌ : ﻋَﺒْﺪٌ ﻣَﻤْﻠُﻮﻙٌ، ﺃَﻭِ ﺍﻣْﺮَﺃَﺓٌ، ﺃَﻭْ ﺻَﺒِﻲٌّ، ﺃَﻭْ ﻣَﺮِﻳﺾٌ »
“Swala ya Ijumaa kwa jamaa ni wajib kwa kila Muislamu, isipokuwa watu wanne: mtumwa anaye milikiwa, au mwanamke, au mtoto, au mgonjwa.” Al-Hakim amesema: “Ni Hadith Sahih kwa masharti ya masheikh wawili.” Na sio wajib kwa yule aliye hofu, kutokana na yale yaliyo simuliwa na Ibn Abbas, Mwenyezi Mungu awe radhi naye, kwamba Mtume (saw) amesea:
« ﻣَﻦْ ﺳَﻤِﻊَ ﺍﻟﻨِّﺪَﺍﺀَ ﻓَﻠَﻢْ ﻳُﺠِﺒْﻪُ ﻓَﻠَﺎ ﺻَﻠَﺎﺓَ ﻟَﻪُ ﺇﻟَّﺎ ﻣِﻦْ ﻋُﺬْﺭٍ، ﻗَﺎﻟُﻮﺍ : ﻳَﺎ ﺭَﺳُﻮﻝَ ﺍﻟﻠﻪِ ﻭَﻣَﺎ ﺍﻟْﻌُﺬْﺭُ؟ ﻗَﺎﻝَ : ﺧَﻮْﻑٌ ﺃَﻭْ ﻣَﺮَﺽٌ »
“Yeyote anaye sikia adhana basi na aitikiye kwani hakuna swala isipokuwa kwa mwenye udhuru. Wakasema: Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu na ni upi udhuru? Akasema: hofu na maradhi.” Imepokewa na Al-Bayhaqi katika Al-Sunan Al-Kubra. 
Hivyo, swala ya Ijumaa ni wajib kwa kila Muislamu, isipokuwa kwa wale ambao kuna andiko (nasi) la kisheria linalo watoa, huku wengine wasiokuwa wao ambao hawana andiko la kuwatoa, Jum’a ni faradhi ya lazima (Fardh Ain) juu yao. Hizi ndizo nyudhuru za kisheria na qiyas haipimwi juu yake. Udhuru wa Kisheria ni ule ulio tajwa katika andiko la kisheria na haujumuishi vitendo vyovyote vya ibada, kwa sababu hazina ‘illa (sababu ya kisheria) hivyo qiyas haiwezi kuvuliwa kutokamana nazo. Na inahitajika kwa swala ya Ijumaa kuwa na idadi ya Waislamu, na Maswahaba walikubaliana kuwa ni lazima kuwe na idadi fulani ya kutekeleza swala ya Ijumaa, kwa hivyo ndani yake ni lazima kuwe na idadi fulani (ya watu). Haihitajiki idadi maalumu, kwa hiyo idadi yoyote huitwa jamaa na hukadiriwa kuwa idadi na itaifanya swala ya Ijumaa kuwa halali maadamu idadi hiyo inakadiriwa kuwa ni jamaa, kwa sababu jamaa katika swala ya Ijumaa imefungwa kupitia hadith ya Tariq:
« ﺍﻟْﺠُﻤُﻌَﺔُ ﺣَﻖٌّ ﻭَﺍﺟِﺐٌ ﻋَﻠَﻰ ﻛُﻞِّ ﻣُﺴْﻠِﻢٍ ﻓِﻲ ﺟَﻤَﺎﻋَﺔٍ »
“Swala ya Ijumaa kwa jamaa ni wajib kwa kila Muislamu.”
Na kwa sababu idadi yake imefungwa kwa ijmaa ya Maswahaba, na hakuna hadith katika hadhi ya kukadiria inayo ashiria idadi maalumu ya kusimamisha swala ya Ijumaa. Lakini, kwa sababu kufikia jamaa na idadi ni muhimu, na hili laweza kupatikana pekee kupitia watu watatu au zaidi, kwani wawili hawakadiriwi kuwa ni jamaa. Kutokana na haya, watu watatu wale wanao pelekea kusimama kwa swala ya Ijumaa wanahitajika ili swala ya Ijumaa iwe sahihi. Ikiwa watakuwa wachache kuliko hao, itakuwa sio sahihi na haitaitwa swala ya Ijumaa kwa sababu idadi haijafika, na ijmaa ilikuwa ni kwamba ni lazima kuwepo na idadi (watu) kwa swala ya Ijumaa.
Hivyo, katika dola ya Khilafah, swala ya Ijumaa au jamaa haisitishwi. Bali, yule ambaye ana udhuru wa kisheria yeye ndio hatahudhuria na walio bakia watahudhuria. Ama kusema kuwa kuna uwezekano kwa uchache wa shaka kuwa kila mmoja yuko hatarini kuambukizwa na hawezi kuepushwa licha ya hatua au tahadhari zitakazo chukuliwa, ni uwezekano dhaifu, hususan kwa kuwa idadi ya chini ya swala ya jamaa ni watu wawili na swala ya Ijumaa ni watu watu, na hili kupatikana kwake lawezekana kabisa. Endapo tutadhania kuwa uwezekano upo, itashughulikiwa katika eneo lake ipasavyo, hivyo basi, jambo hilo ni lazima lidhibitiwe barabara na kwa ikhlasi. Ikiwa idadi itapatikana kwa uchache wa shaka, basi swala ya Ijumaa na jamaa hazitasitishwa, bali hatua na tahadhari zote zitachukuliwa. Kuchukua tahadhari hakumaanishi kuacha faradhi, bali ni hutekelezwa pamoja na kuchukua tahadhari na hatua ili kuzuia maambukizi.
Hii ndio hukmu iliyo na nguvu zaidi katika jambo hili. Endapo dola itafunga misikiti pasi na kufanya kila juhudi kuthibitisha uchache wa shaka (ghalabat adh-Dhan ) kama tulivyo onyesha juu, kisha ikawazuia watu kutokana na kuhudhuria misikitini kwa swala za Ijumaa na jamaa, hapo itakuwa imefanya dhambi kubwa la kukatiza swala za Ijumaa na jamaa.
Kwa kutamatisha, hakika ni uchungu kwamba watawala katika biladi za Waislamu wanafuata hatua za wakoloni makafiri, shubiri kwa shubiri na dhiraa kwa dhiraa, na ikiwa nchi hizo zinatatizika kutafuta tiba ya maradhi fulani, wao huziiga, na endapo watapendekeza suluhisho, hata kama halifai, watawala hawa katika biladi za Waislamu huwashangilia, na hulikadiria hilo kuwa afya na tiba! Ni uchungu kwamba janga hili (virusi vya Korona) vimesababisha nchi na watu wake kusimama na kukwama, hata maisha ya umma ya kila siku yamekaribia kusimama. Hii ndio hali licha ya biladi za Waislamu kuwahi kupitia hali sawa na hii: zilikumbwa na tauni huku zikiwa vitani na Waruni katika Ash-Sham mwaka wa kumi na nane Hijria, na Umma kupata mtihani katikati mwa karne ya sita Hijria kwa janga la “Al-Shaqfa” na sasa inaitwa majipu, ambayo yalienea kuanzia Ash-Sham mpaka Morocco, ambayo yanakadiriwa kuwa ni vidonda vinavyo tokana na ngozi kuathiriwa na staphylococcus bakteria (aina ya bakteria). Waislamu pia walipata mtihani katikati mwa karne ya nane Hijria (749 H) kwa ile inayoitwa Tauni Kubwa jijini Damascus, na katika kesi zote hizi misikiti kamwe haikufungwa wala swala za Ijumaa na jamaa hazikusitishwa. Na watu hawakufungiwa majumbani mwao, bali wagonjwa ndio walio tengwa, na wazima waliendelea na shughuli zao, za jihad na kuimarisha ardhi. Walikwenda misikitini kuswali na kumuomba Mwenyezi Mungu dua ili awalinde kutokana na shari ya maradhi haya, hii ni pamoja na kufuata tiba ya kiafya kwa wagonjwa. Huu ndio ukweli
[ ﻓَﻤَﺎﺫَﺍ ﺑَﻌْﺪَ ﺍﻟْﺤَﻖِّ ﺇِﻟَّﺎ ﺍﻟﻀَّﻠَﺎﻝُ ]
“Na kipo kitu gani baada ya haki, isipokuwa upotovu tu?” [Yunus: 32].
02 Sha’ban 1441 H
26/3/2020 M
#Covid19 #Korona ﻛﻮﺭﻭﻧﺎ#