Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Kwa uchache watu wapatao 100 wameuwawa na robo milioni yao wakiachwa bila makao katika visa vya mafuriko tangu kuanza kwa msururu wa mafuriko makubwa nchini Kenya. Maeneo yaliyo athirika pakubwa ni Tana Delta, Tana River, Garissa, Isiolo na Kisumu. Uharibifu mkubwa wa mimea na barabara umetokea, pamoja na usafi wa maji na miundo mbinu.
Hizb ut Tahrir / Kenya imesikitishwa na kupotea kwa maisha na mali na ingependa kutoa wito kwa jamii yote, hususan jamii ya Kiislamu, kuchangia misaada mbali mbali kwa waathiriwa kwani hilo ndilo linalo himizwa na Uislamu. Inavunja moyo kuona kwamba maelfu ya watu wanapigwa na baridi kali baada ya nyumba zao kuharibiwa na mafuriko. Mtume (saw) amesema: «مَنْ فَرَّجَ عَنْ مُسْلِمٍ كُرْبَةً، فَرَّجَ اللَّهُ عَنْهُ كُرْبَةً مِنْ كُرُبَاتِ يَوْمِ القِيَامَةِ» “Mwenye kumfariji Muislamu kutokana na tatizo moja, Allah (swt) atamfariji kutokana na tatizo miongoni mwa matatizo ya Siku ya Kiyama”.
Mafuriko haya yanaonesha wazi kufeli kwa miundo mbinu nchini. Hata kama ni kweli kuwa mafuriko yaweza kuharibu barabara, lakini ni kweli pia kuwa barabara nyingi nchini hazikujengwa kwa madhubuti. Kwa kuenea ufisadi, viraka barabarani visivyo weza kuzuia chochote huwekwa kila siku ambapo pindi kunyeshapo, barabara hizo hugeuka kuwa mito isiyo pitika! Baya zaidi, baadhi ya maeneo hayana hata mfumo wa barabara ilhali serikali hutoza ushuru mkubwa unaotosheleza kuzijenga na kuziboresha!
Aghalabu majanga kama haya yakitokea, hufichua umbile halisi la mfumo tata wa kirasilimali na nidhamu zake za utawala la kutoyapa kipaumbele maslahi ya umma. Katika mashindano ya uongozi, wanasiasa wa kirasilimali hutembea kote nchini kwa ndege za helikopta wakitafuta kura lakini wakati wa mafuriko hutazama tu kupitia katika runinga huku watu wakizama! Huu ndio uhadaifu halisi wa urasilimali na viongozi wake wa kuthamini maisha yao na kutojali maisha ya mafukara.
Tunaamini kuwa hali hii isingefikia kiwango hiki lau serikali ingewajibika kwa kuchukua hatua za mapema. Hata kama tunafahamu kikamilifu kuwa kimaumbile mwanadamu hawezi kuyazuia majanga kama haya, lakini pia tunatambua kuwa Allah (swt) amemuamrisha mwanadamu huyu huyu kuchukua hatua za tahadhari kwa kuweka mipangilio maalumu kama njia ya kutatua majanga kama haya yanapotokea.
Uislamu kama mfumo kamili wa maisha unafafanua jukumu la kuchunga mambo ya Ummah kimsingi kuwa juu ya serikali na sio la watu binafsi au mashirika ya kibinafsi. Mtume (saw) asema: «الإِمَامُ رَاعٍ وَهُوَ مَسْئُولٌ عَنْ رَعِيَّتِهِ»“Kiongozi (Imam) ni mchungaji na yeye ataulizwa kuhusu raia wake.”
Hivyo basi, dola ya Kiislamu, al-Khilafah, imewajibishwa kujenga barabara na kurahisisha uchukuzi. Ama kuhusu maafa kama mafuriko na mitetemeko ya ardhi, dola ya Kiislamu hutumia mali kutoka kwa hazina ya Bait ul-Maal kuhudumia waathiriwa na hili ni jukumu lake kwa Ummah na wala sio fadhila. Ikitokea hakuna mali ya kutosha katika hazina ya dola, hapo Khalifah (kiongozi wa Kiislamu) atalazimika kuwatoza kodi matajiri kwa kiwango maalumu ili kufidia hali hiyo. Hivi ndivyo namna Khilafah inavyo tarajiwa kuchunga maslahi ya raia wake bi idhnillah Ta’ala.
Shabani Mwalimu
Mwakilishi kwa Vyombo vya Habari wa Hizb ut Tahrir Kenya
KUMB: 09 / 1439 H
Ijumaa, 18 Shaaban 1439 H/
04/05/2018 M
Simu: +254 707458907
Pepe: mediarep@hizb.or.ke