Kulipa Deni kwa Njia Nzuri

Ufupisho wa Suali na Jawabu – 4

Kwa mujibu wa Hadith ya Mtume (saw) kuhusu kulipa deni kwa njia nzuri, hakumaanishi kuzidisha idadi, uzani au kipimo. Bali ilimaanisha kulipa idadi ileile, uzani uleule au kipimo kilekile, lakini inaruhusiwa kulipa bidhaa uliyokopesha kwa iliyo na ubora zaidi. Mfano mtu amemkopesha mtu mwengine ngano iliyo na uzani wa kilo 10, anaweza kulipa kwa ngano bora zaidi lakini kwa uzani ule ule wa kilo 10. Lau angelikopa kilo 10 za mchele wa Local kwa mfano anaruhusiwa kulipa kwa mchele wa Pishori lakini kwa uzani ule ule wa kilo 10. Lau angelikuwa amekopa kondoo ndama anaruhusiwa kulipa kondoo mkubwa ambaye si ndama lakini awe kondoo mmoja. Hiyo ndiyo maana ya kulipa deni kwa njia nzuri, na wala sio kwa kuzidisha uzani, kipimo au idadi. Kwa ushahidi kutoka kwa Abu Rafi alisema:

“Mtume (saw) alikopesha ngamia mdogo, na kisha akapokea Sadaka ya ngamia na akaniamrisha kuwa mimi nimlipe yule mtu ngamia wake mdogo kutokana na ngamia aliopokea. Nikamwambia kuwa sioni isipokuwa ngamia mzuri wa miaka minne, kwa hiyo Mtume (saw) akaniambia ‘Mpe, hakika katika watu wazuri ni wale wanaolipa vizuri’” (Imesimuliwa na Abu Dawood na wengine)

Kwa kumalizia, kulipa deni kwa njia nzuri sio kuzidisha uzani, idadi au kipimo bali ni kwa kulipa kwa uzani uleule, idadi ileile na kipimo kilekile, lakini inaruhusiwa kuwa cha ubora zaidi ikiwa mkopaji anataka kulipa kwa ubora zaidi bila kushurutishwa na mkopeshaji kwa sababu Mtume (saw) alilipa na kilichokuwa bora zaidi pasi na kushurutishwa na mkopeshaji.

Napia haisemwi kuwa kulipa kwa ubora zaidi ni faida kwa mkopeshaji na hivyo imekuwa riba kama ilivyosimuliwa na al-Harith bin Abi Usamah kutoka kwa Hadith ya Ali (ra) alisema:

Mtume (saw) ameharamisha kila mkopo ulio na faida” na katika riwaya nyingine “Kila mkopo uliyo na faida ni riba”

Si sawa kusema hivyo kwa sababu Mtume (saw) aliliruhusu hilo na kuliona kuwa ni kulipa deni kwa njia nzuri.

Mwenyezi Mungu ni Mjuzi, Mwenye Hekima.

Link ya Kiengereza: http://hizb-ut-tahrir.info/en/index.php/qestions/jurisprudence-questions/15278.html

Chanzo: Hizb ut Tahrir Kenya

18 Shaaban 1439 Hijria

04 Mei 2018 Miladi