Ashura ni siku ya kumi ya Muharram(mwezi wa kwanza katika kalenda ya Kiislamu). Hii ni siku maalum kwa umma wa Mtume Muhammad (S.a.w). Inapendekezwa Waislamu kufunga siku ya tisa (Taasua’) na Ashura au kufunga ashura na siku ya baada yake (yaani tarehe 11 ya Muharam). Hii ni njia ya kuwakhalifu Mayahudi na Manaswara ambao pia walikuwa wakiienzi siku hii.Kuna matukio mengi katika historia ya siku hii ambayo kwa bahati mbaya katika zama zetu leo mafunzo ndani yake yamekua yakidharauliwa kila inapoenziwa Ashura.
Katika hadithi alioipokea Imam Bukhari kutoka kwa wa Ibn Abbas asema: Mtume SAW alipoingia Madina aliwapata mayahudi wakiifunga siku ya Ashura wakawa wanasema:“Hii ni siku kubwa kwetu kwani Mwenyezi Mungu alimuokoa Musa(as) na kumgharikisha Firauni. Musa(as) alikuwa akifunga siku hii kama kutoa shukrani kwa Allah(swt).” Mtume Akasema, Mimi niko karibu zaidi na Musa kuliko wao”. Hivyo akafunga siku hiyo na kuamuru Waislamu kuifunga.
Funga hii inapaswa iwe ni kwa ajili ya kutoa shukran kwa Allah pekee kwa kumuokoa Mtume wetu Musa (As) dhidi ya mtawala dhalimu Firaun aliyewatesa waumini na kuwauwa sio kwa sababu yoyote ila kwa kuwa walimuamini Mwenyezi Mungu na wakapania kuvunja utawala wake wa kidhulma na muovu. MwenyeziMungu (Swt) akamuokoa Musa (As) na walioamini pamoja naye na akamgharikisha Firaun na waliokuwa naye kwenye dhulma zake.
Kisa cha Musa As na Firaun kimekaririwa na kutajwa ndani ya Quran ili tuchukue mafunzo makubwa ndani yake. Asema MwenyeziMungu swt:
نَتْلُو عَلَيْكَ مِن نَّبَإِ مُوسَىٰ وَفِرْعَوْنَ بِالْحَقِّ لِقَوْمٍ يُؤْمِنُونَ
Tunakusomea habari za Musa na Firauni kwa haki kwa ajili ya watu wanaomini
[Al-qasas:03]
Usiku mmoja Firaun aliota ndoto kwamba utawala wake ni wenye kuondolewa, hivyo akaamua kutafuta kwa wachawi tafsiri yake. Wachawi wakamueleza kwamba ndoto yake inamaanisha kuwa hivi karibuni kutazaliwa mtoto atakaye ngo’a ufalme wake. Kwa tafsiri hiyo, Firaun kwa kulewa na ufalme akaanzisha kampeni ya kuuwa kila mtoto wa kiume aliezaliwa ama atakaezaliwa miezi michache tu baada. MwenyeziMungu Swt, licha ya kampeni hii akataka kwa uwezo wake Musa alelewe kwa mikono ya huyu mtawala dhalimu. MwenyeziMungu akapenda na kutaka Nana Asiya kumshawishi Firauni kwamba asimuue Musa(as).
MwenyeziMungu SWT akamuamuru Musa AS huku akiwa amempa ishara na miujiza aende kwa Firauni na kupinga upitukaji wake mipaka amlinganie katika kumwabudu MwenyeziMungu. Lakini Firaun akawa na kiburi na jeuri akafikia kusema: Mimi ndie mungu aliejuu. Quran inatueleza mjadala baina ya Firauni na Musa:
قَالَ فِرْعَوْنُ وَمَا رَبُّ الْعَالَمِينَ
(Firaun): “Ni nani huyo Mola wa walimwengu?”
قالَ رَبُّ السَّمَاوَاتِ وَالأَرْضِ وَمَا بَيْنَهُمَا إِن كُنتُم مُّوقِنِينَ
(Musa) akasema: “Muumba wa mbingu na ardhi na vilivyomo ndani yake ikiwa nyinyi ni wenye yakini.”
قَالَ إِنَّ رَسُولَكُمُ الَّذِي أُرْسِلَ إِلَيْكُمْ لَمَجْنُون
(Firauni) akasema: “ Bila shaka Mtume wenu aliyetumwa kwenu ni mwendawazimu.”
Katika ubatili wake alifilisika fikra zake zote hivyo ikawa silaha pekee anayoweza kuitumia dhidi ya Musa na waumini ni ukatili na mateso. Akajawa na ghadhabu hivyo akakusanya jeshi lake katika oparesheni ya kuwawinda Waumini. Musa na wafuasi wake ikawa wanakimbia ili kuhifadhi maisha yao.
MwenyeziMungu anasema:
فَلَمَّا تَرَاءى الْجَمْعَانِ قَالَ أَصْحَابُ مُوسَى إِنَّا لَمُدْرَكُونَ قَالَ كَلَّا إِنَّ مَعِيَ رَبِّي سَيَهْدِينِ
Na yalipoonana majeshi mawili haya (watu wa nabii Musa na jeshi la Firauni) watu wa Musa walisema hakika sisi tutakamatwa. Musa akasema laa! niko pamoja na Mola wangu ataniongoza
Musa akaonesha msimamo wake na yakini yake juu ya MwenyeziMungu swt aliemuamrisha apige bahari kwa fimbo yake, bahari ikapasuka na kutoa njia kumi na mbili za kila kabila la Bani Israel ambao hatimaye walivuka upande wa pili. Kwa udhalimu na uadui wake Firauni na watu wake wakaingia baharini na kuangamizwa, na firaun alipoona anagharikishwa akasema: ‘ sasa nimeamini kuwa hakuna mola mwengine apaswae kuaminiwa ila yule Mungu anayeaminiwa na Bani Israel na mimi ni miongoni mwa waislamu”. Hii ndio ilikua hatima ya Firauni, ambapo MwenyeziMungu anasema:
اليوم ننجيك ببدنك لتكون لمن خلفك أية وإن كثيرا من الناس عن اياتنا لغافلون
Basi leo tutakuokoa kwa kuuweka mwili wako ili uwe dalili kwa ajili ya wa nyuma yako wajue kuwa wewe hukuwa Mungu na watu wengi wameghafilika za ishara zetu.
Twapasa kujifunza yafuatayo kwenye kisa hiki:
Kwanza:Hakuna utawala wowote ule uwezao kuzuia maamuzi na matakwa ya MwenyeziMungu. Na hii ni kwa kuwa licha ya kampeni yake firauni ya kuuwa watoto lakini kwa mikono yake akamlea Musa ambaye baadaye ndiye aliempinga na dhulma zake.Katika tawala kuu duniani leo, licha ya kudhihirisha uadui wao dhidi ya Uislamu na Waislamu twasikia sauti za raia wao waloshikimana na Uislamu zikipinga dhulma na maonevu yao.
Pili: Njia ya batili ni fupi na wenye kuifuata hawawezi kufaulu asilani. Watu wema daima dawamu ndio wenye kufaulu kwani wapo katika haki ambayo ililetwa duniani ili kutokomeza batili. Licha ya kujipigia debe mfumo wa kibepari na siasa yake chafu ya Kidemokrasia lakini fedheha zake ni zenye kudhihirika kila uchao dalilili ya kuwa utaangamia hivi karibuni.
Tatu:Mapambano na mvutano baina ya haki na batili, baina ya watawala dhalimu na raia wanaodhulumiwa, wanyanyasaji na wanaonyanyaswa ni yenye kuendelea hadi siku ya Qiyama. Musa As aliingia kwenye mvutano wa kifikra na mapambano ya kisiasa kwa lengo la kufanya jina la MwenyeziMungu liweze kutawala juu ya mfumo dhalimu wa Firauni ambapo hatimaye Musa as aliibuka mshindi. Hivyo leo Waislamu lazima waamke kifikra na kufichua dhulma za watawala kwa lengo la kuusimamisha Uislamu uchukue hatamu za uongozi.
Nne:Lazima tuwe na matumaini makubwa kwamba MwenyeziMungu Swt huwanusuru waumini na kuwaondosha kwenye watawala waovu ambao ni vizazi vya Firauni.
Wasumilie visa ili wapate kutafakari.
Shabani Mwalimu
Mwakilishi kwa vyombo vya Habari
Hizb ut-Tahrir Kenya