UISLAMU NA WAISLAMU WANASHAMBULIWA KWA KISINGIZIO CHA KUPAMBANA NA UGAIDI: IKO WAPI NGAO NA MLINZI WA UISLAMU NA WAISLAMU?

Mnamo Jumapili, 16 Agosti 2020, Waislamu nchini Kenya kwa mara nyingine waliamkia taarifa za kutekwa nyara kwa Sheikh Khalid Swaleh, Ustadh Juma Shamte na Hassan wote kutoka Markaz Noor iliyoko Mtondia, Kaunti ya Kilifi. Watekaji nyara wanadaiwa kuwa ni maafisa kutoka Kitengo cha Kupambana na Ugaidi (ATPU) ambao walivamia majengo hayo mwendo wa saa 7 usiku (Daily Nation, 16/08/2020). Tukio hili linakuja miezi 3 tu baada ya tukio jingine la kinyama ambalo lililotokea mnamo Jumamosi, 30 Mei 2020 eneo la Kibundani, Kaunti ya Kwale ambapo Waislamu waliamkia habari za kuuliwa kwa Muislamu mwanamume, Mohamed Rahma Mapenzi (miaka 41) watoto wake wawili, Swalia Rahma (miaka 6) na Idd Rahma (miaka 3). Kwa kuongezea wanachama wa familia yake iliyobakia walijeruhiwa vibaya mno huku mkewe aliyekuwa na mimba ya miezi minane, Mwanahalima Mwachili alipoteza mimba yake wakati alipopelekwa hospitali ya Msambweni akiwa katika hali mbaya kwa kupigwa risasi tumboni na mguuni (The Standard, 31/05/2020). Ni jukumu letu kushughulishwa na yale ambayo yanawafika kaka na dada zetu Waislamu kwani Mwenyezi Mungu (swt) asema:

إِنَّمَا ٱلۡمُؤۡمِنُونَ إِخۡوَةٌ۬ “Hakika Waumini ni ndugu” (Al-Hujurat: 49: 10)

na Mtume (saw) asema: لا يُؤْمِنُ أَحَدُكُمْ حَتَّى يُحِبَّ لأَخِيهِ مَا يُحِبُّ لِنَفْسِهِ “Hakuna mmoja wenu atakayekuwa na imani mpaka pale atakapomtakia ndugu yake (Muislamu) yale anayojitakia yeye” (Sahih al-Bukhari).

Matukio hayo hapo juu ni sehemu tu ya matukio ya ukandamizaji ambayo Waislamu wanakabiliwa nayo nchini Kenya na duniani kote kwa kisingizio cha kupambana na ugaidi na misimamo mikali. Vitendo hivyo hapo juu vinafichua yafuatayo:

Kwanza, Uislamu na Waislamu ndio kafara katika vita dhidi ya ugaidi na misimamo mikali nchini Kenya na kwingineko. Kwa kuwa asasi za kiusalama zinapotumia ‘kibali’ cha ugaidi basi hatima yako huwa imekwisha na ule unaoitwa msingi wa huna hatia mpaka itakapothibitishwa kuwa una hatia chini ya nidhamu yenye uwezo ya mahakama ambayo haiendeshwi na ushawishi wa serikali na Wamagharibi ni uongo wa wazi!

Pili, Uislamu na Waislamu wanakabiliwa na njama za kudumu kutoka kila kona ya ulimwengu za maadui wa Uislamu na Waislamu ambao wanakwenda mbio kutumia rasilimali zao zote ili kuhakikisha kuwa nuru ya Uislamu haipenyi na kutawala ulimwengu katika nyanja za kisiasa, kiuchumi na kijamii katika ngazi ya kimfumo. Lakini, Mwenyezi Mungu (swt) asema:

وَيَمۡكُرُونَ وَيَمۡكُرُ ٱللَّهُ‌ۖ وَٱللَّهُ خَيۡرُ ٱلۡمَـٰڪِرِينَ

“Wakapanga mipango yao, na Mwenyezi Mungu akapanga yake. Na Mwenyezi Mungu ndiye mbora wa mipango.” (Al-Anfal 8:30).

Tatu, Uislamu na Waislamu wanakabiliwa na mashambulizi ya kijamii kutoka kwa nidhamu ya kihuria inayolazimishwa juu yao na mfumo wa kisekula wa kirasilimali ambao unakwenda mbio kuhakikisha kuwa Waislamu wanabeba ufahamu wa tupo ndani ‘Uislamu Poa’ ambao umejengwa kuhakikisha kuwa Waislamu wanatafuta muongozo kutoka kwa Washington, London na Ufaransa n.k. Hatima yake ni kuishilia kuwa utambulisho wa kisekula lakini wamebakia na majina ya Kiislamu.

Nne, Uislamu na Waislamu wanakabiliwa na njama ovu za kiuchumi kiasi kwamba Muislamu yeyote ambaye anajitolea na kujifunga na vitendo vya kutoa msaada anabandikizwa kuwa ni ‘mdhamini wa ugaidi na misimo mikali.’ Hivyo basi anaangamizwa kiuchumi na kuwapelekea Waislamu wengi wakitaabika kimya kimya kutokana na kuwashuhudia kaka na dada zao wakiangamia kwa shida za kiuchumi pasi na msaada wowote kutoka kwa tawala za kisekula za kirasilimali za kilafi.

Tano, wale wanaoitwa walinzi na watetezi wa haki za kibinadamu na utiifu kwa sheria hawaonekani pale Uislamu na Waislamu wanapokabiliwa na mashambulizi. Lakini, pale wanapoamua kujitokeza huja tu kwa ajili ya lengo la kuuza sura na kupatiliza hisia na kuvuna msaada wa kifedha kutoka kwa watu kwa kuwahadaa kuwa wanafanyiakazi ajenda ambayo ina sura mbili iliyosimama kwa msingi kuwa ‘Magaidi na Wenye Misimo Mikali’ hawana haki kwani ni tishio kwa wanadamu.

Sita, wale wanaoitwa watawala na viongozi Waislamu hapa nchini na kimataifa sio chochote bali ni kiunganishi cha asasi za serikali ambao wameuza roho zao kwa shetani na hivyo wanapiga njama dhidi ya Uislamu na Waislamu na kupanga mipango pamoja na maadui. Hivyo basi, wao ndio wanaosimamia mauaji  maovu yanayofanyiwa Waislamu kwa kutunga sheria za kupambana na ugaidi na misimamo mikali.

Orodha ni ndefu kuanzia Pakistan, Somalia, Saudi Arabia, Yemen, Jordan, Misri, Uzbekistan, Tunisia, Urusi, Uchina (Xinjiang), Afghanistan na mataifa mengine.

Saba, Uislamu na Waislamu wamesongeka, hawana nafasi ya kupumua kutokana na uchungu na wako njia panda baada ya kujaribu kila njia za kibinadamu na kufeli. Baadhi yake zikijumuisha kushiriki katika chaguzi za kidemokrasia wakitarajia kuboresha hali zao kwa kuwachagua wasanii wa kisiasa wanaotumia hisia za Kiislamu ili kuingia madarakani lakini hawatimizi kitu. Bali hugeuka na kuwa ndio watekelezaji madhalimu wa ukandamizaji wa Waislamu katika kila nyanja ya maisha kisiasa, kiuchumi na kijamii. Hivyo basi, kila mzunguko mpya wa uchaguzi matumaini yao hupungua! Wanabakia na swali; ni ipi njia ya kujitoa katika mateso haya ya kinidhamu wanayotendewa?

Jibu msingi la swali hilo hapo juu si jingine isipokuwa ni kuitikia ulinganizi wa mabadiliko ya kimfumo kwa msingi wa Shari’ah ya Kiislamu ambayo vyanzo vyake ni: Qur’an, Sunnah, Ijma’ Sahaba na Qiyas. Kwani tupo katika hali hii ya shida kwa sababu ya kwenda kinyume na Shari’ah ya Uislamu kwa kutoitekeleza. Mwenyezi Mungu (swt) asema:                                                                                       وَمَنۡ أَعۡرَضَ عَن ذِڪۡرِى فَإِنَّ لَهُ ۥ مَعِيشَةً۬ ضَنكً۬ا وَنَحۡشُرُهُ ۥ يَوۡمَ ٱلۡقِيَـٰمَةِ أَعۡمَىٰ

“Na atakaye jiepusha na mawaidha yangu, basi kwa yakini atapata maisha yenye dhiki, na Siku ya Kiyama tutamfufua hali ya kuwa kipofu” (TaHa 20: 124).

Badala yake tumekumbatia katiba na sheria zilizotungwa na wanadamu ili kusimamia maisha yetu. Tumemchagua mwanadamu kututungia sheria/kutuhukumu badala ya Mwenyezi Mungu (swt) anayesema:

وَمَنۡ أَحۡسَنُ مِنَ ٱللَّهِ حُكۡمً۬ا

“Na nani aliye mwema zaidi katika kuhukumu kuliko Mwenyezi Mungu”(Al-Ma’idah 5: 50),

إنِ ٱلۡحُكۡمُ إِلَّا لِلَّهِ‌ۖ

“Hapana hukumu ila ya Mwenyezi Mungu” (Al-An’am 6: 57),

إِنِ ٱلۡحُكۡمُ إِلَّا لِلَّهِ‌ۚ

“Hapana hukumu ila ya Mwenyezi Mungu tu” (Yusuf 12: 40).

Ni lazima tufahamu na tuamini yale ambayo Mwenyezi Mungu (swt) anayoyasema:

إِنَّ ٱلدِّينَ عِندَ ٱللَّهِ ٱلۡإِسۡلَـٰمُ‌ۗ

“Bila ya shaka Dini mbele ya Mwenyezi Mungu ni Uislamu” (Aal-Imran: 19).

Kukatikiwa kwetu lazima tuitikie mwito wa Mwenyezi Mungu (swt)

: يَـٰٓأَيُّهَا ٱلَّذِينَ ءَامَنُواْ ٱدۡخُلُواْ فِى ٱلسِّلۡمِ ڪَآفَّةً۬ وَلَا تَتَّبِعُواْ خُطُوَٲتِ ٱلشَّيۡطَـٰنِ‌ۚ إِنَّهُ ۥ لَڪُمۡ عَدُوٌّ۬ مُّبِينٌ۬

“Enyi mlio amini! Ingieni katika Uislamu kwa ukamilifu, wala msifuate nyayo za Shetani; hakika yeye kwenu ni adui aliye wazi” (Al Baqarah 2: 208).

Njia pekee ya kutoka katika maangamivu ipo katika kujiunga na juhudi za Hizb ut Tahrir na kufanya kazi pamoja kwa ajili ya kusimamisha Dola ya Kiislamu ya Khilafah kwa njia ya Utume. Khilafah chini ya kiongozi mukhlis, Khalifah, itakuwa ndio ngao na mlinzi madhubuti wa Uislamu, Waislamu na raia wasiokuwa Waislamu popote walipo pasi na kuzingatia rangi, cheo au kabila. Imesimuliwa kutoka kwa Abu Huraira kwamba Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) alisema:

إِنَّمَا الإِمَامُ جُنَّةٌ يُقَاتَلُ مِنْ وَرَائِهِ وَيُتَّقَى بِهِ

“Imam (Khalifah) ni ngao kwao (Waislamu). Nyuma yake wanapigana na wanajilinda (kutokana na madhalimu na wakandamizaji)” (Muslim).

Pia ni dhambi kubwa kutofanyakazi ya kusimamisha Khilafah kwani Mtume (saw) asema:

Yeyote anayeondosha mkono wake kutoka katika utiifu (wa Khalifah) atakutana na Mwenyezi Mungu ilhali hana ushahidi juu yake, na yeyote anayekufa pasi na ahadi ya utiifu (kwa Khalifah) juu ya shingo yake anakufa kifo cha kijahiliyya” (Muslim).

Ni mfumo wa Kiislamu chini ya Khilafah iliyosimama kwa njia ya Utume ndio pekee inayodhamini utulivu, hadhi na heshima sio tu kwa Waislamu bali kwa wanadamu wote duniani ambao wanataabika kutokana na majanga ya kila siku yanayoendelezwa na wakoloni Wamagharibi wakiongozwa na Amerika na washirika wake. Hakuna mbadala isipokuwa #TurudisheKhilafah ambayo ndio hitajio la wakati huu na matumaini pekee kwa Uislamu, Waislamu na wanadamu wote baada ya kumaliza njia zote ambazo haziingii akilini kuanzia mashariki na magharibi na kaskazini hadi kusini.

Wakati ni sasa kuwekeza juhudi pale palipo na malipo ya hapa duniani kwa muda mfupi na akhera ya milele. Hakuna kupoteza nguvu katika yale ambayo yanamkasirisha Mwenyezi Mungu (swt) kama vile kujiunga na vyama vya vya kisiasa vya kisekula vya kirasilimali ambavyo vinalingania suluhisho za kidemokrasia ambao wanaopigia debe na washindi ni vibaraka wa mabwana wakoloni. Bali, jiunge na uwe sehemu ya chama cha Kiislamu cha Hizb ut Tahrir kilichobuniwa kwa msingi wa mfumo wa Kiislamu ambacho macho yake yako makini kuleta mabadiliko ya kimfumo duniani kwa njia ya Uislamu kwa kurudisha maisha ya Kiislamu kwa kusimamisha Khilafah ambayo ni ngao, mlinzi na mama wa faradhi zote za Kiislamu. Mwenyezi Mungu (swt) asema:

بِنَصۡرِ ٱللَّهِ‌ۚ يَنصُرُ مَن يَشَآءُ‌ۖ وَهُوَ ٱلۡعَزِيزُ ٱلرَّحِيمُ*وَعۡدَ ٱللَّهِ‌ۖ لَا يُخۡلِفُ ٱللَّهُ وَعۡدَهُ ۥ وَلَـٰكِنَّ أَڪۡثَرَ ٱلنَّاسِ لَا يَعۡلَمُونَ

“Kwa nusura ya Mwenyezi Mungu humnusuru amtakaye. Na ndiye Mwenye nguvu Mwenye kurehemu. Ni ahadi ya Mwenyezi Mungu. Mwenyezi Mungu havunji ahadi yake. Lakini watu wengi hawajui” (Ar-Rum 30: 5 – 6).

Ali Nassoro Ali

Mwanachama wa Afisi Kuu ya Habari ya Hizb ut Tahrir