JE UKO TAYARI KUFA KESHO?

Wakaazi wa Kaunti ya Kwale siku ya Jumapili tarehe 29/12/2019 walishtushwa na habari za kifo cha ghafla cha naibu mwenyekiti wa tume ya kitaifa ya uwiano na utengamano Bi Fatuma Tabwara (Mola amsamehe madhambi yake amrehemu na amweke mahala pema peponi).Kikawaida kifo huleta huzuni ambayo huwa kubwa zaidi ikiwa kimetokea ghafla.Miongoni mwa mafunzo makubwa ya Kiislamu ni kuamini kuwa MwenyeziMungu pekee ndio hufisha waja wake na kwamba sababu ya Kifo ni moja tu nayo ni kumalizika umri wa mwanadamu.

Bi Tabwara kama mwanadamu yoyote yule bila shaka alikuwa amepanga mipango yake ya siku, wiki, mwezi na mwaka ujao,lakini hakujua kwamba asubuhi ya Jumapili hiyo ndio mwisho wa pumzi zake! Baada ya matamshi yake kwa muda mchache tu akakumbwa na mauti. Kwa hakika mwanadamu hata awe mjuzi kiasi gani katu hajui siku,wakati na eneo la kukumbana na kifo chake.

Miongoni mwa hekima za MwenyeziMungu kuwafichia wanadamu wakati wake wa umauti  ni kuwataka wawe na shauku ya hali ya juu katika kutumia kila sekunde, dakika, saa na siku katika kufuata maamrisho ya MwenyeziMungu na kukatazika na makatazo Yake. Aidha, ni kuwajenga ufahamu kwamba kuishi ndio bahati na kifo ni lazima hivyo ukipaumbaukiwa basi usitumaini utaishi hadi jioni, ukiingiliwa na usiku basi usiwe na yakini ya kuona asubuhi! Hekima hii kwa bahati mbaya  leo ni wachache mno wanaoidiriki kwani wengi wamekuwa wakilevywa na dunia wakajiona kama kwamba wataishi milele huku wakijichukulia kuwa huru wa kufanya chochote bila kujali sheria za MwenyeziMungu.Swahaba muongofu Ali Bin Abi Taalib,(Radhi za MwenyeziMungu ziwe juu yake)  alisema kauli maarufu inayotoa muelekeo mzuri wa jinsi kuishi na kuyakabili mauti akasema:

اعمل لدنياك كأنك تعيش أبدا واعمل للآخرة كأنك تموت غدا”

Shughulikia mambo ya dunia yako kama kwamba utaishi milele na ishughulikie akhera yako kama kwamba utakufa kesho.” Maana ya usemi huu ni kutaka mwanadamu aweze kujenga mizani baina  ya uhai wake duniani na umauti. Kimaumbile mwanadamu yoyote ana ghariza (hisia) ya kupenda uhai wa kidunia. Hisia hii huweza kumpelekea kuhadaika na dunia ikawa hutoa juhudi zake nyingi katika kufikia mafanikio ya kimadda (kidunia). Hapa Ali (RA) akumbusha kwamba mwanadamu lazima ajitahidi kufanya kazi ili kuweza kukimu mahitaji yake msingi kula, kuvaa na makaazi, wakati uo huo ajipinde maradufu kila wakati kufanya mema na kuachana na mabaya huku akisawarisha  kwamba fursa yake ni ule wakati alio nao wala sio wakati ujao. Ufahamu huu ndio utamfanya Muislamu daima asiwe na muda wa kupoteza kiholelaholela kwani anatambua wakati wowote huenda akafariki dunia.

Mara nyingi kwa watu walioathirika na mawazo duni ya kiliberali yasemayo kuwa lengo kuu la maisha ni  kufikia kwenye starehe za upeo wa juu. Wao hudai  kwamba muhimu ni kupatiliza uhai wa kidunia katika kuponda mali kwani kifo kinakuja! Kwa mtazamo huu ndio utawaona wakiepuka mazungumzo kuhusu kifo.Na hata wanapokizungumzia hukitaja pasina kufikiria kwa kina kwa nini watu wanaishi kisha wanakufa? Na Je kifo kina maana gani? Kuna wengine nao huwa wana hofu kubwa ya mauti kwa msingi wa je; mtu akifa huona nini na kitu gani kinachojiri akiwa yeye ni maiti?  

Kulingana na Uislamu, uhai na umauti ni mtihani kwa wanadamu je miongoni mwao ni nani atapeleka maisha yake kwa njia alioitaka Muumba wake?  Mtu anapokufa huingia hatua inayoitwa ‘barazakh’ ambayo hudumu hadi siku ya kufufuliwa. Katika kituo hiki cha kwanza cha barazakh (maisha ya kaburini) kuna imma neema na adhabu. Kwa maana hii jinsi alivyoishi mwanadamu duniani huona natija yake baada tu ya kufa. Waliomuamini MwenyeziMungu na kupeleka maisha yao kulingana na Imani hiyo basi Kifo kwao huwa ni hatua ya kwanza kuingia katika neema Akhera na kinyume waliokufuru na kuhadaika na dunia yanayokuja baada ya umauti wake ni mazito zaidi kushinda hata yale aliyokumbana nayo duniani.

الَّذِي خَلَقَ الْمَوْتَ وَالْحَيَاةَ لِيَبْلُوَكُمْ أَيُّكُمْ أَحْسَنُ عَمَلًا وَهُوَ الْعَزِيزُ الْغَفُورُ
Ambaye ameumba umauti na uhai ili kukujaribuni(kukufanyieni mtihani) ni nani miongoni mwenu

Mwenye vitendo vizuri zaidi.Naye ni Mwenye nguvu na Mwenye msamaha.

[TMQ 77:2]

Umauti ni miongoni mwa matukio yanayomtukia mwanadamu yake pasina mapenzi yake ishara wazi kuwa uhai wa wanadamu una kikomo (Limit). Ukomo huu wa kiumri kuwa ni dalili yeye ni kiumbe aliyeumbwa ambaye si mwengine ispokuwa ni Mwenyezi Mungu.Yeye MwenyeziMungu ndiye pekee aliyetuleta duniani kwa mapenzi yake wala sio kwa mapenzi yetu hivyo tutaondoka duniani sio kwa mapenzi yetu bali kwa mapenzi yake. MwenyeziMungu pekee ndiye mmiliki wa uhai wetu basi matendo yetu hapa duniani lazima yaambatane na utaratibu aliouweka MwenyeziMungu.

Uislamu umehimiza sana kukithirisha kukumbuka mauti jambo linalosaidia sana katika kulainisha nyoyo na kujipinda katika kumtii MwenyeziMungu. Aidha, katika kuyakumbuka mauti hufanya mtu kuidharau dunia kwa kutoghurika na yote aliyoyachuma ya kidunia bali siku zote utamuona akikimbilia kufanya haraka katika kuomba toba kwa mola wake kwa madhambi anayoyafanya. Mtume Rehma na Amani za MwenyeziMungu zimshukie alitaja mtu mwerevu kuwa ni yule anayekumbuka mauti na akajitayarisha nayo kwa kufanya yatakayomfaa baada yake.

الكَيِّس مَنْ دَانَ نَفْسَهُ، وَعَمِلَ لِما بَعْدَ الْموْتِ، وَالْعَاجِزُ مَنْ أَتْبَعَ نَفْسَه هَواهَا، وتمَنَّى عَلَى اللَّهِ

Mwenye akili  ni yule atakayewajibisha nafsi yake (kuipindisha iweze kufuata twaa ya MwenyeziMungu) na akafanya yale yatakayomfaa baada ya mauti na mjinga ni yule atakayefuata matamanio ya nafsi yake na akatarajia kwa MwenyeziMungu kuwa atampatia malipo mazuri)

Twamoumba MwenyeziMungu swt atupe mwisho mwema aturuzuku toba kabla ya mauti yetu kwetu, atupe shahada wakati wa mauti yetu na msamaha baada ya kufa kwetu.

Shabani Mwalimu

Mwakilishi kwa Vyombo vya Habari wa Hizb ut Tahrir Kenya