Lipi la kujifunza katika Kisa cha kuzaliwa kwa Masih Isa Bin Maryam (AS)?

Takriban madhehebu mengi ya Ukristo husherehekea Christmas tarehe 25 Disemba ispokuwa dhehebu la Orthodox linalopatikana zaidi huko Ulaya ya kati na mashariki linalosheherekea siku hiyo kila  tarehe 7 Januari. Kimsingi itikadi ya Kinaswara (kikristo) imejengwa juu ya kuamini kuwa Mungu ana utatu utakatifu (Holy Trinity) Mungu Baba, Mungu Mwana na Mungu Roho mtakatifu. Hii ni kumaanisha Christmas inafungamana na sehemu moja muhimu katika itikadi hiyo ya utatu na kwamba wakristo wanapoisherehekea huwa ni kukumbuka kuzaliwa kwa Yesu ‘mwana wa Mungu’. Nadharia hii ni kinyume na itikadi ya Kiislamu inayokanusha kabisa sifa ya kujifanyia MwenyeziMungu mtoto na kuitakidi hivyo ni jambo la hatari kubwa na dhambi zito mno. Asema MwenyeziMungu (Swt):

وَقَالُوا اتَّخَذَ الرَّحْمَٰنُ وَلَدًا  َلقَدْ جِئْتُمْ شَيْئًا إِدّاً  ّتَكَادُ السَّمَاوَاتُ يَتَفَطَّرْنَ مِنْهُ وَتَنشَقُّ الْأَرْضُ وَتَخِرُّ الْجِبَالُ هَدًّا}

أَن دَعَوْا لِلرَّحْمَٰنِ وَلَدًا وَمَا يَنبَغِي لِلرَّحْمَٰنِ أَن يَتَّخِذَ وَلَدًا

Na ( Mayahudi na Manaswara) husema: ‘ MwenyeziMungu mwingi wa Rehema amejifanyia mtoto. Bila shaka mumeleta jambo lichukizalo kabisa. Zinakaribia mbingu kutatuka na ardhi kupasuka na milima kuanguka ikakatika vipandevipande. Kwa kule kudai kuwa MwenyeziMungu mwingi wa rehema ana mtoto.

Waislamu wana kila sababu ya kulinda heshima ya Mitume wa MwenyeziMungu (swt) baada ya kuwaamini. Mmoja katika mitume hiyo ni Isa Bin Maryam (AS) ambaye Allah ametaka uzawa wake uwe ni funzo kubwa kwa walimwengu. Kwa ujumla tufafanue hapa baadhi ya mafunzo yanayopatikana katika mazazi yake.

Kwanza:Uzawa wa Nabii Isa ni moja wapo ya ishara na dalili zinazothibitisha uwepo wa MwenyeziMungu (SWT).

Uislamu ulipokuja kuzungumzia masuala ya kumwamini Mungu ni kwamba kuwepo kwa MwenyeziMungu ni suala la kilazima na wala sio mawazo tu ya kibinadamu. Ama wamagharibi, wao hudai kwamba kuamini Mungu sio jambo la lazima bali ni mawazo mazuri  kwani ati husaidia kuwafanya wanadamu kuwa na tabia njema. Kwa maana hii, utaona hawataki kufanya utafiti wa kina juu ya ishara zinazokinaisha akili na kuondoa shaka juu ya Imani ya kuwepo kwa MwenyeziMungu. Pamoja na hivyo, wamagharibi kwa upande mwengine wakabuni na kumakinisha fikra kwamba wanadamu wasiingize Imani ya Mungu katika kupeleka maisha yao yaani Imani ya Mungu ibakie ni suala la kibinafsi. Fikra hii wakaiita Ilmaaniya (Secularism) kutenganisha dini na maisha hatimaye kuitenga Dini na serikali. Lau madhehebu yanayopinga uwepo wa Mungu (Athiests) yangetumia akili zao juu ya kisa cha mazazi ya Isa (AS) basi wangekomeka na upagani wao huo ambao wenyewe unagongana na akili.Uzawa wake AS) unatupa Imani ya kuwa kuwepo kwa kitu au kitendo kuna msababishaji aliyekisababisha.

Njia pekee ya kuwa na yakini ya kuwepo MwenyeziMungu ni kutafakari mazingira ikiwemo mbingu, ardhi, na kutofautiana usiku na mchana yote hayo ni dalili ya kuwepo kwa MwenyeziMungu. Hivi ndivyo Uislamu ulimvyomtaka mwanadamu kutafakari ishara na alama anazoziona ili athibitishe na kujenga Imani yake kwa MwenyeziMungu. Allah akafafanua kwamba Isa (AS) ni ishara yaani dalili wazi na rahema kutoka kwake ili watu wapate kumwamini yeye MwenyeziMungu.

وَلِنَجْعَلَهُ آيَةً لِلنَّاسِ وَرَحْمَةً مِنَّا ۚ وَكَانَ أَمْرًا مَقْضِيًّا

Na ili tumfanye kuwa ni Ishara kwa watu, na Rehema itokayo kwetu

Kwa ibara nyengine Uislamu umekataza maigizo na dhana kama njia ya kufikia kwenye Imani thabiti. Allah akashtumu watu wenye kujenga Imani yao juu dhana:

وإن الظن لا يغنى من الحق شيئا

Na dhana haisaidii chochote mbele ya haki

Pili: Uwezo wa MwenyeziMungu. Tukitaamali mazazi ya Isa (AS) tunaweza kuona kwamba lile lisilowezekana kwa wanadamu kwa MwenyeziMungu lawezekana. Msimamo huu ni muhimu sana wanadamu kuwa nao kwani huwafanya siku zote wawe na Imani na yakini juu ya mafanikio licha ya kukabiliwa na changamoto katika maisha yao. Umma wa Kiislamu leo umezongwa na matatizo mengi kiasi ambacho watu huweza kujikatisha tamaa na wengine kufikia hatua ya kujitoa uhai. Waislamu wanatakikana kuchukulia matatizo kama mitihani hivyo aendelee kustahmili kwani hakuna shida za kudumu. Huyu hapa Nana Maryam anashangaa jinsi gani atampata mtoto ilhali hajaingiliwa na mwanaume basi Allah anamjibu kuwa hilo kwake ni jepesi mno.

قَالَتْ أَنَّىٰ يَكُونُ لِي غُلَامٌ وَلَمْ يَمْسَسْنِي بَشَرٌ وَلَمْ أَكُ بَغِيًّا قَالَ كَذَٰلِكِ قَالَ رَبُّكِ هُوَ عَلَيَّ هَيِّنٌ ۖ وَلِنَجْعَلَهُ آيَةً لِلنَّاسِ وَرَحْمَةً مِنَّا ۚ وَكَانَ أَمْرًا مَقْضِيًّا 

(Nitampataje mwana hali mwanaadamu yeyote hajanigusa, wala mimi si kahaba? (Malaika) akasema: Ndio hivyo hivyo! Mola wako Mlezi amesema: Haya ni mepesi kwangu! Na ili tumfanye kuwa ni Ishara kwa watu, na Rehema itokayo kwetu, na hilo ni jambo lilio kwisha hukumiwa.) [TMQ 19:19-20-21]

Hivi hivi nabii Zakaria (AS) akashangaa pale yeye na mkewe ambaye alikuwa miaka yote ni tasa walipofikia uzeeni.Jibril akamjibu jibu hilo hilo alilomjibu Maryam kuwa kwa Mwenyezi Mungu hilo ni jepesi:

قَالَ كَذَٰلِكَ قَالَ رَبُّكَ هُوَ عَلَيَّ هَيِّنٌ وَقَدْ خَلَقْتُكَ مِن قَبْلُ وَلَمْ تَكُ شَيْئًا

Akasema hivyohivyo ndivyo anavyosema Mola wako hilo kwangu ni jepesi (zingatia) kuwa kabla ya kukuumba hukuwa chochote.

Tatu: Kuwajibika kutumia juhudi zetu katika maisha. Uzawa wa Masih Isa Bin Maryam ni kuwa Mwanadamu anatakikana kujipinda katika kutekeleza majukumu yake na kumwachia Mungu matokeo.Bi Maryam alipozidiwa na uchungu wa uzazi aliamua kwenda sehemu ya mbali na kufikia kwenye shina la Mtende. Hali ikawa ngumu kwake na hapo ndipo  amri ya MwenyeziMungu ikamjilia:

(تُسَاقِطْ عَلَيْكِ رُطَبًا جَنِيًّا وَهُزِّي إِلَيْكِ بِجِذْعِ النَّخْلَةِ)

 [Na litikise kwako hilo shina la mtende, utakuangushia tende nzuri zilizo mbivu.) TMQ 19:25).

Tunaona kuwa MwenyeziMungu alimtaka Nana Maryam atikise shina la mtende na wala hii haina maana kuwa MwenyeziMungu alishindwa kumletea tende kutoka mbinguni. Bali ni funzo anatutaka tufanye sehemu yetu katika maisha kisha tumwachie Yeye kutufanikishia mambo yetu. Ufahamu huu ni muhimu sana hasa tukizangatia twaishi kwenye fitina ambapo matatizo yametuzonga kila pembe. Itikadi ya Kisekula imetupelekea wengi kufikiri kuwa kile unachokipata kimetegemea juhudi yako tu. Hivyo juhudi yako na uwezo wako ndio zimekufanya uwe kwenye ufanisi ulionao na kuamua kitu gani waweza kupata au kukosa. Hivyo tunapoangalia matatizo yanayokumba umma leo twafikiri je tutafanikiwa vipi kuyatatua ukiyalinganisha na nguvu zetu dhaifu,elimu yetu ndogo na uhaba wa rasilimali zetu. Muhimu kuelewa kuwa sio nguvu zetu tu zinazotupelekea kupata ufanisi na ushindi bali ni kwa nguvu za Allah SWT.Kwake yeye hakuna kisichowezekana kwani yeye ni mwenye nguvu asoshindwa na yoyote na lolote.

Kwa kisa hiki ndio Waislamu hawatakikani kuangalia nguvu za serikali za Kimagharibi kama kikwazo cha kuregesha tena Uislamu katika ngazi ya utawala kwani wao wanaamini nusra ya MwenyeziMungu iko nao daima maadamu watafanya yale walioamrishwa na Yeye (Swt)

Shabani Mwalimu

Mwakilishi kwa vyombo vya Habari Hizb ut-Tahrir Kenya