Kuhifadhi Utumwa wa Kikoloni ili Kupata Malipo Duni

Habari:

Base Titanium, kampuni ya kuchimba madini katika Kaunti ya Kwale, iliilipa kampuni iliyo na mahusiano nayo ya Base Resources kitita cha bilioni Sh6.5 katika mwaka ulioisha Juni, ikiashiria faida kubwa katika biashara yake ya uchimbaji madini. Malipo hayo yaliiweka kampuni hiyo kuwa nambari mbili katika orodha ya kampunii ya kigeni ambayo migao yao imewekwa wazi. South Africa Vodacom Group ndio ya kwanza yenye kupata mgao mkubwa kutoka soko la nchi, ikipokea pato la bilioni Sh19.2 kutoka kwa Safaricom kwa mwaka ulioisha Machi. (Business Daily, Alhamisi 09/09/2021).

Maoni:

Kenya kama shamba la kikoloni la Uingereza, sera zake zimetiwa minyororo zikizingatia maslahi ya bwana. Maslahi ambayo msingi wake ni nidhamu ya kiuchumi ya kirasilimali ya kisekula. Hivyo basi natija yenye hatari lazima ienee kote katika shamba la kikoloni! Maslahi ya bwana yanaweka kipaumbele yafuatayo:

Kwanza, kuwaweka watawala vibaraka watiifu wasiona mbali, wenye kupiga hesabu za muda mfupi na kumakinisha kipote kichache wa wanasiasa watiifu.

Pili, kuwadhoofisha raia wenyeji kupitia mipango ya kuwatoza ushuru wenye kuwakandamiza amali zao za kiuchumi ili kuhakikisha kuwa hawawi tishio kwa kipote kilichomakinika.

Tatu, kuulinda uwekezaji wa kampunii ya kigeni kwa kutumia kila mbinu hata ikibidi kuvunja sheria na kanuni zozote kwa kisingizio cha kinga kwa miradi ya uwekezaji wa kigeni wa moja kwa moja.

Nne, kuripoti kwa uchache rasilimali zilizopo na utoaji wa mikataba ukiwa umezingirwa na usiri huku kukikosekana uwajibikaji.

Tano, kuendelea kuisifu sura ya bwana nchini na kimataifa ili kuhakikisha ukiritimba wake unakita shambani! Kupitia kutekeleza mfumo wake wa kirasilimali wa kisekula na nidhamu zake zilizo na sumu kama vile nidhamu ya elimu ya kisekula, nidhamu ya kiuchumi ya kirasilimali, nidhamu ya kijamii huria na nidhamu ya utawala ya kidemokrasia n.k.

Hayo hapo juu ni baadhi ya misingi ambayo inachora njia zenye kufuatwa na tawala sio tu nchini Kenya bali duniani kote ambako Uingereza na washirika wake wana ushawishi. Hivyo basi, sio jambo la kushangaza kushuhudia ripoti za kutamausha za malipo makubwa kwa kampunii ya kigeni ambayo yanapora rasilimali za nchi kwa uchu na kiu chao kisichoisha! Kwa kuongezea, serikali zimeridhika na vijiada vinavyolipwa na kampunii hayo.

Kwa hakika, hiyo ndio bei ambayo mataifa hulipa kwa ajili ya kuhifadhi utumwa wao wa kikoloni kwa mabwana zao Wamagharibi. Pasina kuzingatia madhara yasiyohesabika yanayopatikana kupitia mahusiano hayo.

Kinyume chake ni nidhamu ya utawala ya Kiislamu, Khilafah iliyosimamishwa tena kwa njia ya Utume, inaelekeza kwamba Khilafah ni mlinzi na ngao kwa raia wake. Ipo kwa ajili ya kusitisha ufujaji wa rasilimali za umma na dola kupitia kampuni za kigeni au watu binafsi huku raia wakihangaika! Badala yake Khilafah itajizatiti kutumia rasilimali kwa manufaa ya raia kama ilivyopangiliwa katika nidhamu ya kiuchumi ya Kiislamu iliyotolewa kutoka vyanzo vya Kiislamu vya Shari’ah (Qur’an, Sunnah, Ijm’a Sahaba na Qiyas).

Kwa kuongezea, Khilafah sio zana ya kikoloni inayotegemea michoro ya kikoloni. Kwa sababu hiyo itafanya hima kubakia huru kutokamana na wakoloni Wamagharibi kwa kufichua mfumo wao wa kirasilimali wa kisekula na nidhamu zake ovu ambazo ndio chanzo cha majanga yanayoikumba dunia leo. Kwa hivyo, Khilafah itakwenda mbio kutatua tatizo la kweli la kiuchumi ambalo ni usambazaji wa rasilimali kwa raia ili waweze kukidhi mahitaji yao msingi: chakula, mavazi na makazi. Pia mahitaji ya kijamii: elimu, usalama na huduma ya afya; na mahitaji ya ziada. Ikilinganishwa na nidhamu ya kiuchumi ya kirasilimali ni kinyume. Kwani inadai kuwa tatizo la kiuchumi ni uhaba wa rasilimali. Kwa hiyo ipo kuzidhibiti rasilimali ziwafae wachache wenye ushawishi kwa gharama ya maskini!

Imeandikwa kwa ajili ya Afisi Kuu ya Habari ya Hizb ut Tahrir na

Ali Nassoro Ali

                        Mwanachama wa Afisi Kuu ya Habari ya Hizb ut Tahrir