Mabadiliko na ushindi wa kweli upo katika kujiunga na ulinganizi wa Khilafah sio makundi ya ‘Hustler na Dynasty

Janga la Covid-19 limeleta machungu na afueni kwa Wakenya. Machungu kutokana na makali yanayotokamana janga hilo kuanzia kuangukwa kwa uchumi ambao umepelekea kuzidi kwa ukosefu wa ajira kutoka asilimia 5.2 hadi 10.4 (The Star, 01/09/2020), majonzi kwa jamii kutokana na jamaa kupoteza wapendwa wao, akiba zikimalizika kwa kutafuta matibabu na sehemu za ibada zikifungwa kabisa. Kwa kuongezea, ratiba ya shule ikifutiliwa mbali na kuwaacha washikadau katika elimu wakijumuisha na sio tu wazazi, wanafunzi na walimu wakiwa katika mkanganyiko mkubwa hususan darasa la 8 na kidato cha 4 kwa kuwa vyeti vya KCPE na KCSE huzingatiwa kuwa ni njia ya kufikia fursa nyingi duniani. Ama kuhusu afueni ni kutokana na kusitishwa kwa kelele za kisiasa zilizokuwa zinapanda kila uchao kwa sababu ya wale wanaojiita wapigiaji debe na wapinzani wa BBI. Kwa mara ya kwanza walala hoi na mabwenyenye waliungana katika hofu ya maisha yao licha ya kwamba hali zao ni tofauti kwa kuwa masikini hawezi kumudu gharama ya matibabu na tajiri anaweza kumudu lakini hakukuwa na tiba!

Ama kwa upande wa serikali ya Kenya Covid-19 ilikuwa baraka kwake kwani iliipatiliza ili kushibisha hamu yake ya ulafi na kuzifuata taasisi za kifedha za kiwango cha kieneo na kimataifa ili kuchukuwa mikopo mikubwa kwa kisingizio kuwa inapambana na janga hilo. Kwa upande mwingine, imeisukuma nchi katika kina cha madeni kinachokaribia trilioni Sh.7 hivi karibuni. Kwa mfano, baina ya Machi na Juni 2020, Kenya ilichukua

jumla ya mkopo wa bilioni Sh.410 takribani bilioni Sh136 kwa mwezi au bilioni Sh.4.5 kwa siku! (Daily Nation, 09/09/2020). Kwa kuwa ule unaoitwa upinzani haupo tena tangu kutokea kwa mkono wa kheri uliofanyika mnamo Ijumaa, 9 Machi 2018. Hivyo basi, serikali ya Kenya inatekeleza sera yoyote inayoitaka pasina wasiwasi kwa kuwa hakuna wakuihesabu.

Njama hadaifu inayoenezwa hivi sasa ni ile ya makundi yanayoitwa hustler, ikiongozwa na William Ruto and dynasty, ikiongozwa na Uhuru Kenyatta, Gideon Moi na Raila Odinga. Raia wanakwenda mbio kujinasibisha na makundi haya. Lakuvunja moyo zaidi ni kwamba makundi haya yanafurahia uungwaji mkono kutoka kwa wale wanaoitwa wanafikra na wasomi! Nukta kiunganishi inayoashiria makundi haya mawili ni kwamba viongozi kutoka kambi zote ni sawa mfano wa mbwa mwitu waliojivika manyoya ya kondoo ili kuweza kuwavizia wengi katika raia ambao hawajazinduka na wanataabika kutokana na maradhi ya UGALI! Maradhi haya ni hatari kwa kuwa yamebuniwa na nidhamu ya elimu ya kisekula ya kirasilimali ambayo msingi wake ni kutotoa fursa kwa watu wenyewe kufikiria kwa kina pasina ushawishi wa kutoka nje kuhusiana na mustakbali wao kwani kimakusudi inawashughulisha kwa kuwa mbioni kutafuta UGALI ili kushibisha njaa yao ya muda mfupi. Hivyo basi, kambi zote mbili sio wageni katika ulingo wa kisiasa bali wamejibadilisha upya ili kuwapatiliza watu kupitia kabila zao. Wao ndio walinzi wa mfumo wa kisekula (wa kutenganisha dini na dola/maisha) wa kirasilimali ambao ndio chanzo cha matatizo mengi yanayoikumba Kenya tangu ‘uhuru bandia wa bendera’ mnamo 1963. Wamejizatiti kutekeleza mfumo wa kisekula wa kirasilimali na nidhamu zake za sumu zinazojumuisha nidhamu ya kiutawala ya kidemokrasia ambayo inawapa wanadamu uhuru usiokuwa na mipaka na ambayo unasababisha majanga kwa wanadamu, nidhamu ya kiuchumi inayotoa nafasi ya kuchukua mikopo ya kuendelea ya riba na utozaji ushuri unaokandamiza, sera ya kigeni iliyochorwa na mabwana wakoloni ili kulinda maslahi yao, nidhamu ya elimu inayojenga vitambulisho vya kisekula ambavyo lengo lake ni kukidhi mahitaji ya kiviungo n.k. Makundi hayo yanadai kuwa yanalingania mabadiliko lakini ndani ya sanduku la kisekula la kirasilimali ambalo ndio chanzo cha matatizo sio tu nchini Kenya bali ulimwenguni!

Katika Uislamu, Muhammad ibn Abdullah (saw) alituonya: لاَ يُلْدَغُ الْمُؤْمِنُ مِنْ جُحْرٍ وَاحِدٍ مَرَّتَيْن “Muumini haumwi mara mbili (na kitu) kutoka katika shimo hilo hilo.” (Sahih al-Bukhari 6133). Kama Waislamu tumeshiriki katika “shimo la kidemokrasia” la kubahatisha tangu mnamo 1963 tukitarajia kwamba hali zetu zitabadilika lakini mambo yanazidi kuwa magumu kila kukicha kama vile ukandamizaji na mauaji kwa kisingizio cha kupambana na ugaidi na misimamo mikali n.k. Mtume (saw) alisema,

الْحَلاَلُ بَيِّنٌ وَالْحَرَامُ بَيِّنٌ وَبَيْنَ ذَلِكَ أُمُورٌ مُشْتَبِهَاتٌ لاَ يَدْرِي كَثِيرٌ مِنَ النَّاسِ أَمِنَ الْحَلاَلِ هِيَ أَمْ مِنَ الْحَرَامِ فَمَنْ تَرَكَهَا اسْتِبْرَاءً لِدِينِهِ وَعِرْضِهِ فَقَدْ سَلِمَ وَمَنْ وَاقَعَ شَيْئًا مِنْهَا يُوشِكُ أَنْ يُوَاقِعَ الْحَرَامَ كَمَا أَنَّهُ مَنْ يَرْعَى حَوْلَ الْحِمَى يُوشِكُ أَنْ يُوَاقِعَهُ أَلاَ وَإِنَّ لِكُلِّ مَلِكٍ حِمًى أَلاَ وَإِنَّ حِمَى اللَّهِ مَحَارِمُهُ

“Halali iko wazi na haramu iko wazi, na baina ya hayo yapo mambo yaliyo na shaka (ambayo hayako wazi); wengi katika watu hawajui kama ni halali au haramu. Kwa hiyo yeyote anayewachana nayo ili kulinda dini na heshima yake, basi atakuwa salama na yeyote ambaye atakayeingia katika kitu kutoka kwayo, kisha hivi karibuni atakuwa ameingia katika haramu. Kama vile mtu anavyolisha (wanyama wake) karibu na hifadhi (mpaka), muda si mrefu ataingia ndani yake. Hakika, kwa kila mfalme anahifadhi yake (mpaka), na hakika hifadhi ya Mwenyezi Mungu ni yale Aliyo yaharamisha.” (Jami` at-Tirmidhi 1205)

na Mwenyezi Mungu (swt) asema:

إِنَّ ٱلدِّينَ عِندَ ٱللَّهِ ٱلۡإِسۡلَـٰمُ‌ۗ  
Hakika, dini (mfumo) mbele ya Mwenyezi Mungu ni Uislamu” (Aal-Imran 3: 19).

Kwa kuongezea, Yeye (swt) asema:

وَمَن لَّمۡ يَحۡكُم بِمَآ أَنزَلَ ٱللَّهُ فَأُوْلَـٰٓٮِٕكَ هُمُ ٱلۡكَـٰفِرُونَ

“Na wasio hukumu kwa aliyo teremsha Mwenyezi Mungu, basi hao ndio makafiri.” (Al-Ma’idah 5: 44).

Hivyo basi, kujiunga na makundi haya au mengine yaliyobuniwa kwa msingi wa mfumo wa kisekula wa kirasilimali kwa maana vyama vya kiasia ya kidemokrasia imekatazwa kwa mujibu wa Shari’ah ya Kiislamu (Qur’an, Sunnah, Ijma’ Sahaba na Qiyas). Kwa kuwa makundi haya yanalingania kumpa mwanadamu nguvu za kupangilia/kutunga sheria ili kusimamia maisha ima kwa kubakisha Katiba ya 2010 iliyoko au kuibadilisha kwa kutumia BBI au njia yoyote ile iliyopo. Hivyo basi, imewafanya watu kuwa ndio mabwana kwa kuwa itikadi yao ni usekula.

Hakuna shaka kuwa kila mwanaharakati mkweli wa kisiasa anatambua kuwa makundi haya yanapiga njama kwa ajili ya maslahi yao binafsi na yale ya mabwana zao Wamagharibi. Kwa hiyo wanaharakati hao watakuwa wanatafuta mabadiliko ya kweli mbadala ambayo yataweza kuwapa watu ushindi nchini Kenya na duniani kote. Fursa pekee iliyopo ni kujiunga na Hizb ut Tahrir, chama cha Kiislamu cha kisiasa ambacho mfumo wake ni Uislamu. Ni chama cha Kiislamu kilichobuniwa mnamo 1953 na msomi, Sheikh Taqiuddin an-Nabahani (rahimahu Allah) ndani ya Ardhi Tukufu ya Palestina (kuliko na Qiblah cha kwanza cha Waislamu -Msikiti al-Aqsa). Msingi wake ni kuitikia mwito wa Mwenyezi Mungu (swt):

َلۡتَكُن مِّنكُمۡ أُمَّةٌ۬ يَد بِٱلۡمَعۡرُوفِ وَيَنۡهَوۡنَ عَنِ  ٱلۡمُنكَر ۡعُونَ إِلَى ٱلۡخَيۡرِ وَيَأۡمُرُونَ ‌ۚ

“Na kiwepo miongoni mwenu umma (chama) kinacholingania kwa kheri (Uislamu) na kuamrisha mema na kukataza maovu” (Aal-Imran 3: 104).

Hizb ut Tahrir ina lengo moja pekee nalo ni kurudisha tena maisha ya Kiislamu kwa kusimamisha Dola ya Kiislamu ya Khilafah ndani ya taifa ambalo limetimiza vigezo muhimu vinavyojumuisha: kwanza-usalama uwe katika mikono ya Waislamu na pili-Shari’ah ya Kiislamu iwe ndio Bwana (inayotumika katika kuwahukumu na kupangilia mambo ya watu). Hizb ut Tahrir haitumii fujo au nguvu kufikia lengo lake.

Mabadiliko na ushindi wa kweli ni kutawaliwa na sheria kutoka kwa Muumba na Mpangiliaji wa ulimwengu, mwanadamu na uhai. Hilo haliwezekani katika hali iliyoko sasa ndani ya dola za kisekula duniani kote. Ni kwa kukumbatia ulinganizi wa kusimamisha Khilafah ndipo wanadamu watakombolewa kutoka katika majanga ya kila siku yanayotekelezwa na makucha ya mfumo wa kisekula wa kirasilimali na nidhamu zake mbaya zikisimamiwa na wakoloni Wamagharibi wakiongozwa na Amerika, Uingereza, Ufaransa na washirika wao. Khilafah itawaweka wamwagaji damu wote pale wanapostahili katika debe la taka za historia kwa kuwalipizia kisasi yale waliyowafanyia Waislamu na Uislamu. Wakati ni sasa wa kujiunga na juhudi ambazo zinadhamini amani na utulivu. Kuishi kwetu ni kwa ajili ya kuhakikisha kuwa jina la Mwenyezi Mungu (swt) liko juu ya kila kitu lakini hivi sasa hali iko kinyume na hivyo ambapo Ukafiri na Makafiri wako juu ya Uislamu na Waislamu. Ilhali Mwenyezi Mungu (swt):

وَلَن يَجۡعَلَ ٱللَّهُ لِلۡكَـٰفِرِينَ عَلَى ٱلۡمُؤۡمِنِينَ سَبِيلاً

“wala Mwenyezi Mungu hatawapa makafiri njia ya kuwashinda Waumini” (An-Nisa’ 4: 141). Usichelewe, wakati wa kubahatisha umekwisha na sasa ni fursa ya kubadilisha mabaya kwa mazuri kwa kushiriki katika yale ambayo yanayopeana uhai kwa kuitikia anayotuitia Mwenyezi Mungu (swt):

يَـٰٓأَيُّہَا ٱلَّذِينَ ءَامَنُواْ ٱسۡتَجِيبُواْ لِلَّهِ وَلِلرَّسُولِ إِذَا دَعَاكُمۡ لِمَا يُحۡيِيڪُمۡ‌ۖ وَٱعۡلَمُوٓاْ أَنَّ ٱللَّهَ يَحُولُ بَيۡنَ ٱلۡمَرۡءِ وَقَلۡبِهِۦ وَأَنَّهُ ۥۤ إِلَيۡهِ تُحۡشَرُونَ

“Enyi mlio amini! Muitikieni Mwenyezi Mungu na Mtume anapo kuitieni jambo la kukupeni uzima wa milele. Na jueni kuwa Mwenyezi Mungu huingia kati ya mtu na moyo wake, na kwamba hakika kwake Yeye tu mtakusanywa.” (Al-Anfal 8: 24).

Mfumo wa kisekula na kirasilimali na nidhamu zake zimefeli kupindukia kutokana na ufisadi wake kwa viumbe hai kuliko shamiri ardhini na baharini.

Hii ni fursa ya watu kushindana sio kwa ukusanyaji wa dunia kama tulivyo tahadharishwa na Mwenyezi Mungu (swt): حَتَّىٰ زُرۡتُمُ ٱلۡمَقَابِرَ* أَلۡهَٮٰكُمُ ٱلتَّكَاثُرُ

“Kumekushughulisheni kutafuta wingi (dunia), mpaka mje (mkishtuka mnapelekwa) makaburini.” (At-Takathur 102: 1 – 2). Badala yake tushindane kwa ajili ya kutenda kila kheri hususan kufanya kazi ya kusimamisha Khilafah kwa kuwa ndio mama wa faradhi zote kwa kumuitikia Mwenyezi Mungu (swt):

فَٱسۡتَبِقُواْ ٱلۡخَيۡرَٲتِۚ

“Basi shindaneni kwa mambo ya kheri.” (Al-Mai’dah 5: 48).

Huu sio mchakato wa kubahatisha bali ni zoezi adhimu lenye malipo makubwa kwani ni ahadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu (swt):

وَعَدَ ٱللَّهُ ٱلَّذِينَ ءَامَنُواْ مِنكُمۡ وَعَمِلُواْ ٱلصَّـٰلِحَـٰتِ لَيَسۡتَخۡلِفَنَّهُمۡ فِى ٱلۡأَرۡضِ ڪَمَا ٱسۡتَخۡلَفَ ٱلَّذِينَ مِن قَبۡلِهِمۡ  

“Mwenyezi Mungu amewaahidi wale walio amini miongoni mwenu na wakatenda mema, ya kwamba atawafanya makhalifa katika ardhi kama alivyowafanya wa kabla yao” (An-Nur 24: 55). Kwa kuongezea Mtume (saw) amebashiri kuhusu kurudi kwa Khilafah pale aliposema (saw):

 ثم تكون ملكاً جبريا، فتكون ما شاء الله أن تكون، ثم يرفعها إذا شاء أن يرفعها، ثم تكون خلافة على منهاج النبوة، ثم سكت

“Kisha kutakuwepo na utawala wa utenzaji nguvu, utakuwepo kwa muda ambao Mwenyezi Mungu atataka uwepo kisha Mwenyezi Mungu atauondoa wakati anapotaka kuuondoa, kisha itakuwepo Khilafah kwa njia ya Utume,” Kisha akanyamaza. [Ahmad]

Kwa kutamatisha, yale yanayojiita makundi ya ‘hustler na dynasty’ au mfano wake yanalenga kumkasirisha Mwenyezi Mungu (swt) kwa kudumisha hali iliyoko ambayo inampa mwanadamu nguvu za utungaji sheria kwa kutumia akili yake iliyo na kikomo. Badala yake lazima tufanye kazi turudishe Khilafah ili iwatawale wanadamu kwa msingi wa Shari’ah ya Kiislamu inayotoka kwa Muumba na Mpangiliaji wa ulimwengu, mwanadamu na uhai.

Ali Nassoro Ali
Mwanachama wa Afisi Kuu ya
Habari ya Hizb ut Tahrir