Muharram 1441 Hijria Inaingia Lakini Waislamu Bado Hatuna KHILAFAH

Kwa uwezo wake Mwenyezi Mungu Waislamu hivi karibuni wataadhimisha Mwaka Mpya wa Kiislamu wa 1441H. Kwa kila Muislamu anayefuatilia hali ya Ummah wa Kiislamu ndani ya taifa hili na nje atatamaushwa na hali ya vile Uislamu na Waislamu wanavyodhalilishwa kila upande. Mfano hapa nchini Kenya Vita dhidi ya Ugaidi na Misimamo Mikali vimepelekea Waislamu wangapi kuuawa na kupotezwa na Uislamu kudhihakiwa na matukufu yao kuchafuliwa? Nchi jirani za Tanzania na Uganda ni Waislamu wangapi wanaosugua jela kwa tuhuma za Ugaidi? Afrika ya Kati (CAR) ni Maelfu ya Waislamu wangapi waliuawa? Tukija katika ardhi za Mashariki ya Kati namna zinavyoendeshwa na Vibaraka makhaini waliouza roho zao kwa wakoloni wa magharibi dhidi ya ndugu zao Waislamu watukufu; na badala yake kuzifanya Washington na London kama kibla chao. Huku Qibla cha Kwanza cha Waislamu Al Quds kikichafuliwa na umbile la kiyahudi kwa ushirikiano wake na ruwaibidha (Watawala duni) Tukiangalia Asia ya Kati (Tajikistan, Uzbekistan, Kyrgyzstan, Pakistan n.k) tunashuhudia maelfu ya Waislamu wakiozea magerezani kwa tuhuma za kutaka kujifunga na Uislamu Kikamilifu. Hivi sasa ndugu zetu wa Rohingya, Uiyghur, Syria, Crimea, Afghanistan, Libya, Kashmir, n.k wanaishi kwa mashambulizi ya kinyama ambayo nyuma yake yanaendeshwa na maadui wa Ummah huu mtukufu wa Kiislamu.

Masaibu haya yanayokumba Ummah yapaswa yamshughulishe kila Muislamu aliye na yakini na Siku ya Kiyama na kisha ajiulize ni mchango upi anaotoa ili kubadilisha hali hiyo? Na je mchango huo ana uhakika uko katika njia ya sawa kufikia hali ya mabadiliko yatakayopelekea Ummah huu kunusurika na majanga na uadui wa kitaifa na kimataifa?

Matatizo haya kwa hakika ni natija ya kuvunjwa kwa Khilafah (Utawala Wa Kiislamu) ambayo wanavyuoni wameitaja kuwa ndio mama na taji la faradhi zote. Dola ya Khilafah ilivunjwa na Uingereza ikishirikiana na Ufaransa na baadhi ya vibaraka ndani ya Ummah wa Kiislamu mnamo 28 Rajab 1342H sawia na 3 Machi 1924M. Hadi kuvunjwa kwa Khilafah, wamagharibi hao walifanya kazi ya kumezesha Waislamu fikra hatari na sumu kwenye mabongo yao kama vile utaifa, ukabila na uzalendo. Na hii ni baada ya kuiona Khilafah haishindiki kijeshi kwa karne kumi na tatu!   Naam, Waislamu mwanzoni ilikuwa hawashindiki kivita kwa kuwa itikadi yao ilikuwa safi kwenye vifua vyao huku wakipigana Jihadi ili kuhifadhi damu za watu na kuondosha kila kikwazo dhidi ya kueneza uadilifu wa Uislamu. Fikra ya Jihad ilikuwa imekitwa ndani ya mioyo madhubuti kutokana na uchajimungu uliokuwa umeshamiri katika Serikali ya Kiislamu tangu wakati wa Mtume (saw) mpaka Khalifah wa mwisho Abdulmajid wa Pili. Hapo ndipo wakabuni mikakati ya kuivunja Khilafah Uthmani kwa kuanza kuipiga vita kifkra hususan baada ya Khilafah ya mwisho kuanza kudorora katika ufahamu wao uliosababishwa na kurudi nyuma katika uvuaji wa Hukm katika masuala/matukio mapya (ijtihad). Mfano kushindwa kutofautisha baina ya hadhara na madania ipi ya kuchukuliwa na ipi ni ya kuachwa. Ambalo ilipelekea kushindwa na namna ya kulipatiliza suala la Mapinduzi ya Viwanda yaliyoibuka Ulaya na matukio mengine yaliyohusiana na kama hayo na hivyo kupelekea mgawanyiko ndani ya Dola.

Baada ya kuivunja Dola yetu wakatuletea itikadi ya usekula (kutenganisha na dini na maisha) na kutuwekea mfumo wao batil wa urasilimali na nidhamu zake chafu kwa kipimo cha faida/hasara/madhara/maslahi. Na kuigawanya iliyokuwa Dola moja ya Khilafah na kuwa vijidola 54 huku vyengine vikiongozwa na wafalme, wengine maraisi n.k lakini wote wakiwa ni vibaraka watumwa wa wakoloni walioivunja Dola tukufu ya Kiislamu ya Al Khilafah. Tokea wakati huo Ummah huu umezama katika maumivu mazito ya kuvunjiwa Dola yake na kubakishwa yatima bila ngao ya utetezi na ndio maana leo hii tumekuwa duni thamani juu ya mgongo wa ardhi na huku kila mjinga na asiyekuwa na nguvu anatudharau na kutunyanyasa hata kufikia hatua kutuua mamilioni kwa visingizio vya kila aina!

Hivyo basi ni jukumu la kila Muislamu popote alipo kuchangamka na kuhakisha kuwa Waislamu wanarudi tena katika hali yao ya Kuishi kwa mujibu wa Uislamu. Nayo ni kupitia kufanyakazi usiku na mchana na kusimamisha tena Serikali ya Kiislamu ya Khilafah kwa njia ya Utume. Hakika kurudi kwa Khilafah ni ahadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu (swt):

وَعَدَ اللَّهُ الَّذِينَ آمَنُوا مِنْكُمْ وَعَمِلُوا الصَّالِحَاتِ لَيَسْتَخْلِفَنَّهُمْ فِي الْأَرْضِ كَمَا اسْتَخْلَفَ الَّذِينَ مِنْ قَبْلِهِمْوَلَيُمَكِّنَنَّ لَهُمْ دِينَهُمُ الَّذِي ارْتَضَىٰ لَهُمْ وَلَيُبَدِّلَنَّهُمْ مِنْ بَعْدِ خَوْفِهِمْ أَمْنًا ۚ يَعْبُدُونَنِي لَا يُشْرِكُونَ بِي شَيْئًا ۚ وَمَنْ كَفَرَ بَعْدَ ذَٰلِكَ فَأُولَٰئِكَ هُمُ الْفَاسِقُونَ 

“Mwenyezi Mungu amewaahidi wale walio amini miongoni mwenu na wakatenda mema, ya kwamba atawafanya makhalifa katika ardhi kama alivyo wafanya wa kabla yao, na kwa yakini atawasimamishia Dini yao aliyo wapendelea, na atawabadilishia Amani baada ya khofu yao. [An-Noor: 55]

Na ni bishara kutoka kwa Mtume (saw):

 ثم تكون ملكاً جبريا، فتكون ما شاء الله أن تكون، ثم يرفعها إذا شاء أن يرفعها، ثم تكون خلافة على منهاج النبوة، ثم سكت

 “…Kisha kutakuwepo na utawala wa utenzaji nguv, utakuwepo kwa muda ambao Allah atataka uwepo kisha Allah atauondoa wakati anapotaka kuuondoa, kisha itakuwepo Khilafah katika njia ya Utume,” Kisha akanyamaza. [Ahmad]

Ndugu zenu Hizb ut Tahrir wanawaita mujiunge nao katika kulibeba jukumu hili zito ambalo limewapelekea baadhi na wengi kati yao kuozea katika magereza ya viongozi hawa ruwaibidha na wakoloni. Kwa kufahamu kuwa ni ahadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu na bishara kutoka kwa Mtume (saw) matukio hayo ya kuogofya hayajapelekea wabebaji da’wah kurudi nyuma au kukata tamaa mbele ya hawa vikaragosi ambao Allah (swt) anawapa muhula kisha atawapa adhabu ambayo haina mfano wake. Kuuliwa, Kudhuriwa, Kufungwa gerezani au Kufutwa kazi n.k yote hayo ni Sunnah katika da’wah na ni mipango ya Allah (swt) ikiwa amekupangia ikufike:

قُلْ لَنْ يُصِيبَنَا إِلَّا مَا كَتَبَ اللَّهُ لَنَا هُوَ مَوْلَانَا ۚ وَعَلَى اللَّهِ فَلْيَتَوَكَّلِ الْمُؤْمِنُونَ 

“Sema: Halitusibu ila alilo tuandikia Mwenyezi Mungu. Yeye ndiye Mola wetu Mlinzi. Na Waumini wamtegemee Mwenyezi Mungu.” [At-Tawba: 51]

Kwa hiyo tuchangamkeni ndugu zangu wakati ni huu:

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا اسْتَجِيبُوا لِلَّهِ وَلِلرَّسُولِ إِذَا دَعَاكُمْ لِمَا يُحْيِيكُمْ وَاعْلَمُوا أَنَّ اللَّهَ يَحُولُ بَيْنَ الْمَرْءِ وَقَلْبِهِ وَأَنَّهُ إِلَيْهِ تُحْشَرُونَ

“Enyi mlio amini, muitikieni Mwenyezi Mungu na Mtume wake anapo kuiteni jambo la kukupeni uzima wa milele.       Na jueni kuwa Mwenyezi Mungu huingia kati ya mtu na moyo wake, na kwamba hakika kwake Yeye tu mtakusanywa” [Al-Anfaal: 24]

Ali Nassoro Ali

Mwanachama wa Afisi ya Habari ya Hizb ut Tahrir Kenya

Makala Na.60: Ijumaa, 29 Dhul-Hijja 1440 | 2019/08/30