MWEZI WA RAJABU

Imeandama Rajabu, nduzangu nawaarifu,

‘Meutea wahabu, akaupa  usharafu,

Huwa mine kwa hisabu, mieziye mitukufu,

Ilianguka Khilafah, kwenye mwezi wa Rajabu,

Ukumbusho nakhutubu, tuweni wahadharifu,

Na mawi tujitanibu, tusiyafanye machafu,

Tuche ya Mola adhabu, kali isiyokhafifu,

Ilianguka khilafah, kwenye mwezi wa Rajabu,

Kwa mjuzi wa ghaibu, tuweni ni watwiifu,

Ya wajibu ni wujubu, kutenda kikamilifu,

Na yalo mustahabu, kwetu zaida faafu,

Ilianguka khilafa, kwenye mwezi wa Rajabu,

Tulizotenda dhunubu, yuwazijuwa Raufu,

Kwake yeye na tutubu, toba iliyonyoofu,

Maana ndiye Tawwabu, mpa toba watubifu,

Ilianguka khilafah, kwenye mwezi wa Rajabu,

Pepo wataisuhubu, watu waliyonadhifu,

Walofuata kitabu, na sunna zilo ng’arifu,

Kwa ndia ya mujtabu, tena kwa ubainifu,

Ilianguka khilafah, kwenye mwezi wa Rajabu,

Namba Enyi mahabubu, isilamu masharifu,

Kusimamisha wajibu, khilafah yetu kingifu,

Alishasema habibu, tumwa wetu ashirafu,

Ilianguka khilafah, kwenye mwezi wa Rajabu,

Rajabuni ilisibu, umma wetu muongofu,

Pigo kubwa la ajabu, myaka mia ishakifu,

Ilivundwa sikadhibu, khilafah na wavundifu,

Ilianguka khilafah, kwenye mwezi wa Rajabu,

Zimeondoshwa za Rabbu, sharia za uongofu,

Watu walizoratibu, zikapawa utiifu,

Kila pembe na janibu, u wazi ufisidifu,

Ilianguka khilafah, kwenye mwezi wa Rajabu,

Zinavuliwa hijabu, wahalalishwa uchafu,

Zaandamwa taratibu, za kitwaghuti potofu,

Demokrasia harabu, inapigiwa dufufu,

Ilianguka khilafah, kwenye mwezi wa Rajabu,

Tughati wanamsubbu, mtumi wetu hanifu,

Kiwa kweli twamhubbu, tulinde yake sharafu,

Twasaliaje mabubu, ama nasi tunakhofu?,

Ilianguka khilafah, kwenye mwezi wa Rajabu,

Mayahudi ni madubu, waovu tena khawafu,

Waikalia kwa gubu, AL-QUDSI  tukufu,

Wafanyayo ya aibu, kila leo twayashufu,

Ilianguka khilafah, kwenye mwezi wa Rajabu,

Umma una maswaibu, na madhila maradufu,

Makafiri ahzabu, dini yetu hukashifu,

Hutupiga kwa sababu, tushakuwa madhaifu,

Ilianguka khilafah, kwenye mwezi wa Rajabu,

Dola yetu munaswabu, ni khilafah adilifu,

Ni suluhisho na jibu, kwa kila tatizo tafu,

Wakatiwe u karibu, bishara zi dhahirifu,

Ilianguka khilafah, kwenye mwezi wa Rajabu,

Iishile wino nibu, hapano natawakafu,

Yote naloyakutubu, pimani ni yakinifu,

Fedha pamwe na dhahabu, ndo ya khilafah sarafu,

Ilianguka khilafah, kwenye mwezi wa Rajabu,

MTUNZI – MOHAMMED BAKARI

ALMUFTI

MOMBASA – KISAUNI