Pensheni kwa Wabunge wa Zamani: Mpango wa Kuwakandamiza Wanyonge

بسم الله الرحمن الرحيم

Mnamo Alhamisi, 6 Agosti 2020, Bunge la Kitaifa la Kenya lilipitisha Mswada wa 2019 wa Mabadiliko ya Pensheni ya Bunge, ambao kwamba lau Rais ataweka saini utakuwa sheria na kuifanya serikali kuwalipa wabunge wa zamani kitita cha takribani bilioni Sh1.15 kama pensheni ya ziada (Daily Nation, Alhamisi, 06/08/2020).

Maamuzi hayo yanalenga kumakinisha hali iliyoko na kuipa kipaombele badala ya masuala muhimu yanayowakabili Wakenya ambao wanataabika katika maisha yao kutokana na sababu zifuatazo:

Kwanza, janga la Covid-19 limevunjilia mbali uti wao wa kijamii na kiuchumi kiasi kwamba biashara nyingi zinafungwa na ilhali nyingine ziko katika mchakato wa kuwaachisha kazi baadhi ya wafanyakazi wao ili kukabiliana na athari za janga hilo la kiulimwengu. Kwa kuongezea, serikali inapatiliza janga hilo ili kuvuna manufaa ya kifedha kutoka kwa taasisi za kifedha na wale wanaoitwa washirika wa kimaendeleo kwa kuchukua mikopo mipya na kutafuta misaada ya kifedha kwa kisingizio cha kupambana na maradhi.

Pili, kuzidi kwa deni la umma ambalo limekuwa kutoka trilioni Sh5.7 mnamo 2019 hadi trilioni Sh6.65 kufikia Mei 2020! Imeifanya hali ya deni ya Kenya kuwa suala la kutia wasiwasi na kulazimisha mashirika ya kimataifa kutathmini upya hali ya kutamausha ya deni la Kenya na kuitoa katika kiwango cha chini hadi juu na mustakbali unaendelea kuwa mbaya (The Star, Jumatatu, 20/07/2020). Madeni yanaongezeka kutokana na hamu ya serikali kubuni miradi ghushi mikubwa ili kuwahadaa raia kuwa kukamilika kwake itabadilisha hali zao za maisha; lakini badala yake sio chochote bali ni njia za kufuja fedha na kuendeleza ufisadi! Mambo yatazidi kuwa mabaya kwani Baraza liliidhinisha mnamo Machi 2020, Sera ya Deni la Ummah na Kukopa ya 2020 ili kuziwezesha serikali za kaunti kukopa (The Star, Jumatatu, 27/07/2020).

Tatu, sekta ya elimu imekwama huku wazazi hawajui mustakbali wa watoto wao kwani kalenda ya masomo ya 2020 imefutiliwa mbali kwa ukamilifu. Uwekezaji wa kifedha na kiakili wote umepotea. Yote haya ikiwa ni natija ya kukosekana fedha za kutosha kuweza kukidhi gharama za ujenzi wa miundo mbinu inayotimiza masharti ya usalama kwa mujibu wa Covid-19.

Nne, kuzidi kwa mikakati ya ushuru inayowapatliza watu ambayo inatozwa na serikali ambayo ina hakikisha kuwa inakazanisha kitanzi cha kiuchumi katika shingo za raia kwa kuwatoza asilimia 3 za ushuru wa uzalendo kwa wafanyi biashara wadogo na asilimia 15 za ushuru wa makadirio. Na kuyapelekea maisha kuwa magumu zaidi kwa raia wengi ambao wanaishi kwa njia ya mkono kuelekea kinywani maishani mwao!

Sababu hizo hapo juu ni sehemu tu ya sababu nyingi ambazo zinafichua kwamba tawala za kisekula za kirasilimali hazisimami juu ya msingi wa kulinda na kusimamia mambo ya watu katika hali ya ubinadamu. Badala yake zipo kuwahudumikia wachache waliojibandika kuwa ndio viongozi na ambao wanafanya bidii kudumisha hali iliyoko kwa kujizawadi na kujilinda kutokamana na moto wa kiuchumi kwa kutumia migongo dhaifu ya mashini za kupiga kura “raia”! Kwani tawala hizi zipo kuhakikisha tu zinafikia maslahi na manufaa yao ya kilafi.

Kinyume chake ni kuwa ndani ya nidhamu ya uongozi ya Khilafah inayoongozwa na kiongozi mchamungu, Khalifah ni msimamizi wa raia wote Waislamu na wasiokuwa Waislamu katika hali ambayo anafahamu jukumu alilopewa na Mwenyezi Mungu (swt) na haki walizopewa raia na Mwenyezi Mungu (swt). Khalifah ni mchungaji wa raia na atahesabiwa Siku ya Kiyama kuhusu hilo.

عَنْ عَبْدِ اللَّهِ بْنِ عُمَرَ رَضِيَ اللَّهُ عَنْهُمَا أَنَّ رَسُولَ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ قَالَ أَلَا كُلُّكُمْ رَاعٍ وَكُلُّكُمْ مَسْئُولٌ عَنْ رَعِيَّتِهِ فَالْإِمَامُ الَّذِي عَلَى النَّاسِ رَاعٍ وَهُوَ مَسْئُولٌ عَنْ رَعِيَّتِهِ…

Abdullah ibn Umar ameripoti: Nabii wa Mwenyezi Mungu rehema na amani ziwe juu yake, alisema, “Kila mmoja wenu ni mchungaji na atahesabiwa kwa uchunga wake. Kiongozi (Khalifah) wa watu ni mlinzi na atahesabiwa kwa anaowatawala…” Uislamu unadhamini mtu binafsi katika raia wa Khilah mahitaji yake msingi; chakula, mavazi na makaazi; na Khilafah itafanya bidi kuhakikisha inatoa mahitaji ya jamii; afya na elimu miongoni mwa mengine na wakati huo huo kutoa nafasi ili kukidhi mahitaji ya ziada.

Katika nidhamu ya Khilafah hakuna aliye juu y sheria na kila mmoja anatakiwa kutendewa kwa mujibu wa maelekezo ya Shari’ah ya Kiislamu pasina kuzingatia ima yuko uongozini au la, rangi, kabila au cheo. Hivyo basi, upendeleo na unyanyapaa wa aina yoyote hautoruhusiwa kattu! Hivyo basi tufanyeni kazi usiku na mchana kwa ushirikiano kuondosha hali iliyoko duniani na kuleta hali mpya chini ya uongozi wa uadilifu, Khilafah.

Ali Nassoro Ali

Mwanachama wa Afisi Kuu ya Habari ya Hizb ut Tahrir