Ramadhan ya 1442 Hijria inatukaribia na ilhali bado Waislamu na wanadamu jumla wamebakia mayatima. Wamezungukwa na majanga ya kila aina yakijumuisha ya kisiasa, kiuchumi, kijamii, kielimu n.k. Watawala wajinga (ruwaybidha) wanaendelea kutawala kwa kutumia ufisadi kwa ushirikiano na wakoloni Wamagharibi. Ufisadi – kujisalimisha kwa itikadi ya kisekula (ilmaniya). Hivyo basi, kusimamia mambo ya watu kwa mujibu wa mfumo wa kirasilimali na nidhamu zake ovu hususan demokrasia.
Nidhamu ya kidemokrasia ndio nguzo muhimu baada ya ile ya kiuchumi katika mfumo wa kirasilimali. Ndio inayowapa wanadamu nguvu za kujitwika jukumu la Mwenyezi Mungu (swt). Jukumu ambalo ni haki ya Muumba wa viumbe (ulimwengu, mwanadamu na uhai), nalo ni utungaji sheria. Badala yake leo wanadamu wanajitungia sheria kwa mujibu wa akili zao zenye kikomo na zisizodiriki dhati ya Mwenyezi Mungu (swt). Wanahalalisha na kuharamisha kwa kutegemea mapenzi ya nafsi zao!
Kupitia utekelezwaji wa mfumo wa kisekula wa kirasilimali na nidhamu zake, tunaendelea kushuhudia kwa kasi mporomoko na majanga makubwa. Hakuna nyanja hata moja katika maisha imesalimika na jinamizi hilo. Waislamu na wasiokuwa Waislamu wamo katika wasiwasi wa kudumu. Kwa kuongezea kila mmoja anatapatapa kujinasua kwa njia awezayo. Wote wakijifunga na kufirikia ambako kunalirudia sanduku hatari la mfumo wa kisekula wa kirasilimali na nidhamu zake.
La msingi ni kujua kwamba chanzo cha tabu zote tunazozipata wanadamu hivi leo ni kwa sababu ya kutoizingatia kauli ya Mwenyezi Mungu (swt): ﴿وَمَنۡ أَعۡرَضَ عَن ذِڪۡرِى فَإِنَّ لَهُ ۥ مَعِيشَةً۬ ضَنكً۬ا وَنَحۡشُرُهُ ۥ يَوۡمَ ٱلۡقِيَـٰمَةِ أَعۡمَىٰ﴾ “Na atakaye jiepusha na mawaidha yangu, basi kwa yakini atapata maisha yenye dhiki, na Siku ya Kiyama tutamfufua hali ya kuwa kipofu.” [Ta Ha 20: 124]. Baada ya kufahamu hilo tunatakiwa kurudi nyuma na kutathmini tulipokosea na kurekebisha kwa haraka na dharura.
La kusikitisha licha ya kujua mzizi wa matatizo bado wanadamu wamo katika kujipa matumaini feki kwa kutafuta suluhisho ndani ya takataka zilezile ambazo ndio tatizo haswa! Kwani wameweka juhudi katika kupitisha, kubadilisha na kurekebisha katiba na kanuni walizozitunga! Wengine wakiweka juhudi katika kuwaweka au kuwatoa mamlakani viongozi! Lakini hatua zote hizo hazija punguza kasi ya mporomoko na majanga bali kila kukicha ndio kunazidi ukosefu wa usalama, utulivu na ustawi.
Bila shaka kila mwenye akili tambuzi anafahamu kwamba mti wenye sumu utaendelea kuzaa matunda ya sumu. Na hata ukatumia juhudi na nguvu kiasi gani katika kuudhibiti mti huo ikiwemo mfano kukata tagaa au kuyaondosha majani. Kattu mti utaendelea kuzaa matunda ya sumu kwa kuwa mizizi yake ipo! Hatua pekee ni kuung’oa mti huo pamoja na mizizi yake na mahali pake kupandwa mti wenye kuzaa matunda yasiokuwa na sumu. Kupitia mti huo mpya wanadamu watanufaika na kusalimika.
Ramadhan hii itakuwa ni ya 100 pasina kuweko Dola ya Kiislamu, Khilafah ikiongozwa na mtawala, Khalifah. Mtawala anayetumia Qur’an na Sunnah katika kuwasimamia watu mambo yao. Mtawala atakaye kuwa mlinzi, ngao na mtetezi wa Ummah pasina kuzingatia dini, kabila wala rangi za anao watawala. «إِنَّمَا الإِمَامُ جُنَّةٌ يُقَاتَلُ مِنْ وَرَائِهِ وَيُتَّقَى بِهِ» “Imamu (Khalifah) ni ngao kwao. Wanapigana nyuma yake na kujilinda kwake.” [Muslim].
Ni fursa adhimu katika mwezi wenye baraka ambao nafsi za Waislamu zimejaa hamu na shauku ya kupata msamaha kwa madhambi yao kutoka kwa Mwenyezi Mungu (swt). Ni mwezi ambao wanaume na wanawake hushindana katika kutafuta kheri za Mwenyezi Mungu (swt). Nafsi huzidi kulainika na kuwa haraka katika kumuitikia Mwenyezi Mungu (swt) Anapowaita waumini. Huu ndio msimu wa kuwavuna wapenda kheri wenye kuipenda Dini yao ya Uislamu hususan katika zama hizi ngumu.
Ulinganizi wa kurudisha maisha ya Kiislamu kwa kusimamisha Khilafah kwa njia ya Utume ni mchakato adhimu. Hakika unawahitaji wapenda kheri walio tayari kujitoa muhanga kumnusuru Mwenyezi Mungu (swt) na Mtume (saw). Ili kujiunga na kufanyakazi pamoja ili kuwakomboa wanadamu jumla kutoka katika makucha ya mfumo wa kisekula wa kirasilimali na nidhamu zake chafu. Tuzidisheni juhudi katika ulinganizi wa kurudisha Khilafah kwani ndio mama wa faradhi zote.
Khilafah pekee ndiyo itakayotuunganisha kuwa Ummah mmoja, Dola moja chini ya Mtawala mmoja. Kuwepo kwake ndipo heshima, hadhi, damu na mali za watu zitahifadhiwa kiukweli. Hatimaye tutapata utulivu, ustawi na maendeleo kutokana na kutekelezwa kwa Qur’an na Sunnah katika nyanja za maisha.
Ali Nassoro Ali
Mwanachama wa Afisi Kuu ya Habari ya Hizb ut Tahrir