Je, Hesabu za Falaki na Kalenda ya Mwezi ni Mbadala wa Kuangalia Mwezi Mwandamo?

 

بسم الله الرحمن الرحيم

 

Maendeleo ya kisayansi na uvumbuzi yamegundua siri kama vile siri za falaki kwa wanaadamu ambazo hazikujulikana kabla. Kutokana na maendeleo hayo, wanaadamu sio tu wameweza kufanya makisio yenye usahihi zaidi kuhusiana na mienendo ya sasa ya mizunguko na vituo vya jua, mwezi na sayari nyengine na nyota, bali pia ya baadaye. Mfano wa karibuni wa haya ni mafanikio ya kutua kwa idadi kadhaa ya roboti zilizopelekwa na shirika la NASA la Amerika kwenye sayari ya Mars. Roboti hizi zilirushwa kutoka ardhini zikikusudiwa eneo maalum la Mars, safari iliohakikishwa ikichukua miezi kadhaa. Hivi leo, kutokana na sayansi ya falaki, mwanaadamu ameweza kuwa na uhakika wa muda na mahala pa kupatwa jua na mwezi kwa siku za usoni, au muda na mahala pa kutokeza mwezi mchanga, na pia uwezekano wa kuonekana kwake.

Ulimwengu wa Kiislamu ukiogopeshwa na maendeleo yaliofikiwa na sayansi, umechochewa na mjadala juu ya kuwa sayansi ina uwezo wa kutambua uzawa wa mwezi mchanga, au uwezekano wa kuonekana kwake, na kwa hivyo, vipimo vya kisayansi (hudaiwa kuwa) vinaweza kutumika kama mbadala wa kuangaliwa mwezi mwandamo. Zaidi ya hivyo, inachukuliwa kuwa Waislamu hawahitajii tena kuangalia mwandamo wa mwezi ili kuanza mwanzo wa mwezi kwa kuwa sayansi ina uwezo wa kutosha wa kutoa taarifa za kuaminika kuhusiana na kuzaliwa mwezi mchanga, hivyo, kuanza kwa mwezi wa Ramadhan na siku ya Iddi zinaweza kujulikana  kupitia msingi huu, na kwa hivyo kuweza kuondosha mzozo. Hoja zifuatazo huwasilishwa kuhusiana na suala hili:

  1. Kwa kuwa sayansi inaweza kuamua uzawa wa mwezi muandamo kwa uhakika wenye kuaminika, ambao mwanzoni ungewezekana tu kwa kuangaliwa, hivyo, hivi leo, vipimo vya kisayansi, ambavyo havina uwezekano wa makosa, vinaweza kutumika badala ya kuangaliwa kwa macho ili kuamua muandamo wa mwezi.
  2. Kwa kuwa inaruhusika katika Uislamu kutumia kalenda ya nyakati za swala kwa ajili ya kutekeleza ibada ya swala, na kwa kuwa kalenda hizi zimeegemea vipimo vinavyohusiana na jua, ina maana kuwa inaruhusiwa kutumia hesabu kuhusiana na nyakati na siku katika mambo ya ibada, na hivyo, kufanya hesabu ya uzawa wa mwezi mwando kwa kuanza kwa miezi ya kalenda ya mwezi, uwezekano wa kuonekana kwake na kuanza kwa mwezi kulingana na makisio haya.

Hebu tuzichunguze hoja hizi kwa uoni wa dalili za kisharia:

Bukhari, Muslim, na Nisai wametaja kuwa Abu Hurayrah (ra) amesimulia kuwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) amesema:

«صُومُوا لِرُؤْيَتِهِ وَأَفْطِرُوا لِرُؤْيَتِهِ، فَإِنْ غُبِّيَ عَلَيْكُمْ فَأَكْمِلُوا عِدَّةَ شَعْبَانَ ثَلَاثِينَ»

Ikimaanisha “Fungeni kwa kuonekana kwake mwezi mwandamo (wa Ramadhan), na fungueni kwa kuonekana mwezi mwandamo (wa Shawwal), na kama mawingu yataziba (msiweze kuuona), basi kamilisheni idadi ya siku thalathini za Shaaban.” Bukhari na Muslim wamesimulia zaidi kuwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) amesema:

«إِذَا رَأَيْتُمُوهُ فَصُومُوا، وَإِذَا رَأَيْتُمُوهُ فَأَفْطِرُوا، فَإِنْ غُمَّ عَلَيْكُمْ فَاقْدُرُوا لَهُ»

“Pindi mtakapouona mwezi mwandamo (wa Ramadhan), anzeni kufunga, na pindi mtakapouona mwezi mwandamo (wa Shawwal) basi fungueni, na kama mawingu yataziba (na msiweze kuuona) basi kadirieni siku za Ramadhan kuwa 30” Ni wazi kutokana na Hadithi hizi kuwa amri ya صُومُوا (fungeni nyote) inafungamana na sharti la رَأَيْتُمُوهُ (mtakapouona) yaani hukmu (amri) ya kuanza/kumalizika kwa mwezi wa Ramadhan itatumika wakati wa muonekano wa mwezi. Hukumu (amri) ya kuanza/kumalizika kwa mwezi wa Ramadhan haitotumika katika jambo jengine mbali ya kuonekana, isipokuwa kama kungepatikana dalili ya kisharia inayoonyesha hili, yaani dalili inayoruhusu utumiaji wa hukumu kwa kuanza/kumalizika kwa mwezi wa Ramadhan katika jambo jengine mbali ya kuonekana mwezi. Imam Malik, Bukhari, Muslim na Nisai wametaja kuwa Abdullah ibn Umar (ra) amesimulia kuwa Mtume (saw) ameitaja Ramadhan na akasema:

«لَا تَصُومُوا حَتَّى تَرَوْا الْهِلَالَ وَلَا تُفْطِرُوا حَتَّى تَرَوْهُ، فَإِنْ غُمَّ عَلَيْكُمْ فَاقْدُرُوا لَه»

“Msifunge hadi muuone mwezi mwandamo (wa Ramadhan), na wala msifungue hadi muuone mwezi mwandamo (wa Shawwal), kama mawingu yametanda basi kadirieni (yaani hisabuni Shaaban kuwa siku 30).” Hadithi hii ya Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) inakataza waziwazi utumiaji wa hukmu ya kuanza/kumalizika kwa Ramadhan isipokuwa kwa kuonekana mwezi mwandamo. Dalili hizi zinaonyesha wazi kuwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) amefanya kuonekana kwa mwezi muandamo, baada ya siku ya 29, kuwa ni sharti kwa kuanza/kumalizika kwa mwezi wa Ramadhan, na kukosekana kuonekana kwake kunatulazimu kukamilisha siku 30 kabla ya kuanza kwa mwezi unaofuata. Zaidi ya hayo katika Hadithi hizi, Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) amekataza waziwazi kutumika kwa tendo jengine katika kutambua kuanza kwa miezi ya muandamo.

Kwa haya, ni muhimu kufahamu kuwa Sharia imeweka sababu (sabab) ya kutekelezeka kila hukmu ya kisharia ili sababu inapopatikana hukmu ya Kisharia hutekelezwa. Hii ina maana kuwa sababu ni sifa iliyojengwa juu ya dalili ya Kisharia, na kuwepo kwake kunalazimisha kutekelezwa kwa hukmu za Kisharia, kwa mfano, katika kutambua kuingia kwa swala ya Magharibi, sababu yake ni kuzama kwa jua, na kutambua kuingia kwa swala ya Adhuhuri sababu yake ni kupinda kwa jua (kuelekea upande wa magharibi). Bayhaqi amepokea kutoka kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw):  «إِذَا زَالَتِ الشَّمْسُ فَصَلُّوا» “Jua litakapopembeuka basi swalini”. Katika suala la Dola ya Khilafah kutekeleza Jihad ya mashambulizi (ya kukomboa maeneo), uwepo wa dola za Kikafiri na mifumo yao ni sababu ya kupatikana Jihad ya mashambulizi. Vivyo hivyo, kutokana na maneno ya Hadith «صوموأ لرؤيته»  “fungeni kwa kuonekana kwake” ni wazi kuwa sababu inayotambuliwa na Sharia ya kuanza/kumalizika kwa miezi yote muandamo, ikiwemo Ramadhan ni kuonekana kwa muandamo wa mwezi (yaani kuonekana kwa macho pekee).

Kwa kuwa kufunga ni kitendo cha ibada ni lazima kitekelezwe kwa mujibu wa njia iliyowekwa na Sharia ambayo Mwenyezi Mungu (swt) ameiteremsha kwetu. Ama kwa upande wa nyakati za swala, ambazo zinahusishwa na kuonekana kwa mwezi muandamo, Mwenyezi Mungu (swt) ameweka sababu kwa utekelezaji wa swala kuwa ni misimamo ya jua, kama ambavyo Yeye (swt) alivyoweka sababu kwa matendo mengine ya kiibada. Hivyo basi, tofauti baina ya sababu iliyowekwa na shariah  kwa utekelezwaji wa swala na utekelezwaji wa Ramadhan iko wazi, yaani kwa utekelezwaji wa swala sababu ni misimamo ya Jua, na kwa kuanza na kumalizika miezi miandamo sababu ni kuonekana kwa mwezi.

Tofauti nyengine ambayo lazima izingatiwe hapa ni kwamba katika kuiweka sababu ya swala, Sharia haikuweka mipaka ya mbinu ambazo kwazo utambuzi wa misimamo ya jua huthibitishwa. Kwa hivyo, kuthibitisha misimamo ya jua, kivuli kinachotolewa na jua kinaweza kuangaliwa, saa zinaweza kutumika, jua linaweza kuangaliwa moja kwa moja, au njia nyengine kutumika kwa sababu mipaka iliyowekwa inahusiana na uwepo wa msimamo maalum wa jua (sababu ya kisharia), na sio kuhusiana na mbinu ambayo kwayo utambuzi wa uwepo wa sababu (sababu ya swala) unapatikana.

Kinyume chake, kwa upande wa kuanza kwa mwezi mwandamo, sababu ni kuuona mwezi kwa kutumia macho, hivyo kuonekana kwa mwezi moja kwa moja kwa macho ni sababu pekee ambayo imetambuliwa na Sharia kwa kuanza kwa miezi ya mwandamo. Hivyo, katika kuangaliwa kwa mwezi mwandamo inaruhusika kuangaliwa ukiwa ardhini, au kwa kupanda juu ya mlima, au kutokea juu ya paa la nyumba ilio ndefu, au kuangaliwa na mtu mmoja mmoja, au kwa kundi la watu. Hata hivyo, ikiwa tendo jengine lisilokuwa kuuangalia mwezi linafanyika, kama kwa kutumia elimu ya falaki kufanya hesabu zenye kuthibitisha uwepo wa mwezi mwandamo, basi kitendo hicho sio kuuangalia mwezi katika uhalisia wake, wala neno ‘kuuona’ (ru’yah) halitekelezeki kwake. Kwa kuwa inawezekana hapa kutumia maana ya asili ya neno ‘kuuona’ (ru’yah), sio sahihi basi kutumia maana zozote za sitiari. Kwa kuwa tofauti iko wazi katika amri hizi mbili za kisharia (sababu ya swala na sababu ya miezi miandamo), hivyo, sio sahihi kufanya kiasi ya hesabu zinazohusiana na uzawa wa mwandamo wa mwezi juu ya hesabu zinazohusiana na misimamo ya jua. Sababu ya Kisharia ya kuanza kwa miezi ya miandamo ni kuona muandamo kwa kutumia jicho, na sio elimu ya uzawa/uchomozaji au uwepo wake.

Imam Bukhari amejumuisha mlango «لاَ نَكْتُبُ وَلاَ نَحْسُبُ»  “Hatuandiki wala hatufanyi hesabu” katika Kitabu cha Swaum, na imepokewa kutoka kwa Abdullah ibn Umar (ra) kuwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) amesema:

«إِنَّا أُمَّةٌ أُمِّيَّةٌ، لَا نَكْتُبُ وَلَا نَحْسُبُ الشَّهْرُ هَكَذَا، وَهَكَذَا يَعْنِي مَرَّةً تِسْعَةً وَعِشْرِينَ، وَمَرَّةً ثَلَاثِينَ»

“Sisi ni watu tusiojuwa kusoma, hatuandiki wala hatuhesabu. Mwezi mara huwa hivi na mara huwa vile – yaani baadhi huwa ishirini na tisa na mara nyengine huwa thalathini.” Katika Hadithi hii, neno ‘tusiojua kusoma na kuandika’ (ummiyah) haina maana kuwa Waislamu wawe wajinga, yaani wasiwe na elimu ya kuhesabu, kwa sababu Waislamu wametakiwa kufuata hukmu kama Zakat, Ushr na ugawanyaji wa mirathi, ambazo hazitoweza kutekelezwa bila elimu ya hesabu.

Bali lengo la kuambiwa Ummah haujui kusoma wala kuandika ni kuweka wazi kuwa pindi mwezi unapokuwa haukuonekana siku ya 29, mwezi hutakiwa kukamilishwa baada ya siku thelathini, badala ya kuingiza mchakato huu kwenye ugumu wa hesabu na kujaribu kutambua ima mwezi mwandamo utaojitokeza ama la. Hivyo maneno haya ya Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw)  «إِنَّا أُمَّةٌ أُمِّيَّةٌ، لاَ نَكْتُبُ وَلاَ نَحْسُبُ» ni katika muundo wa ufasaha (balagha) kutilia mkazo kuwa hesabu zisitumike katika kutambua kuanza kwa miezi ya mwandamo. Hivyo, jambo ambalo hesabu hazitakiwa kutumika ni suala maalum la kuangalia mwezi mwandamo. Hivyo, kwa upande mmoja amri ya wazi imetolewa ya kutumia muangalio mwandamo kuamua kuanza kwa miezi miandamo, na kwa upande mwengine pia imekatazwa kutumia hesabu katika jambo hili.

Kwa kinaganaga, dalili za Kisharia zinaeleza waziwazi kuwa sababu za Kisharia kwa kuanza mwezi wa Ramadhan ni kuonekana kwa mwandamo wa mwezi kwa kutumia macho, na sio elimu ya uzawa au umri (kuchomoza au muda) wake. Suala hili liko tofauti kabisa na sababu ya Kisharia ya swala, ambapo sababu ni msimamo au hali maalum ya jua, na sio uonekanaji wa jua au kivuli chake kwa kutumia macho. Kwa hivyo, japokuwa ukuaji wa elimu ya falaki umewawezesha wanaadamu kufahamu siri nyingi zilizojificha za ulimwengu, lakini haiwezi kwa namna yoyote ile kupelekea kubadilisha hukmu za Sharia. Funga ni kitendo cha ibada, maelezo yake, ikiwemo muda wa kuanza na kumalizika kwake, yametufikia sisi kupitia Wahyi kutoka kwa Mwenyezi Mungu (swt), na matendo ya kuabudu yanayokubaliwa na Mwenyezi Mungu (swt) ni yale yanayofanywa pekee kulingana na maamrisho na makatazo ya Mwenyezi Mungu (swt). Tunamuomba Mwenyezi Mungu (swt) Atuwezeshe kutekeleza matendo yetu yote ya ibada kulingana na maamrisho Yake na Atupatie ufahamu wa Dini yetu ulioepukana na ushawishi wote na imani zisizokuwa za Kiislamu. Amiin

Imeandikwa kwa Ajili ya Afisi Kuu ya Habari ya Hizb ut Tahrir na

Mun’im Ahmed – Wilayah Pakistan