Hakika Uislamu si Dini ya kiroho pekee bali ni mfumo kamili wa kimaisha. Hakuna kitu ambacho haukukizungumzia bali uligusa kila kitu. Ni mwongozo kwa wanadamu wote; Waislamu na wasiokuwa Waislamu. Hivyo basi ni wajibu kujifunga nao kikamilifu. Mwenyezi Mungu (swt) asema:
يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا ادْخُلُوا فِي السِّلْمِ كَافَّةً وَلَا تَتَّبِعُوا خُطُوَاتِ الشَّيْطَانِ ۚ إِنَّهُ لَكُمْ عَدُوٌّ مُبِينٌ
“Enyi mulio amini ingieni katika Uislamu kwa ukamilifu, wala musifuate nyayo za shetani; hakika yeye kwenu ni adui aliye wazi” [Al-Baqarah: 208]
Kwa kukosekana mwongozo huu mtukufu kutoka kwa Muumba wa walimwengu na kutawala kwa mfumo batili wa kirasilimali katika dunia imepelekea uchafu na uovu wa kila aina kuzagaa duniani ikiwemo miongoni mwa Waislamu. Leo warasilimali wameamua kutumia njia ya mtandao (internet) ambao uko mikononi mwetu saa 24 kwa siku kupotosha mujtama wetu kwa kueneza uchafu wa zinaa kupitia ‘pornography’.
‘Pornography’ imegawanyika mara mbili; ya kwanza ni zile filamu ambazo wamerikodi, picha za uchi, vipindi vya televisheni nk.
Ya pili ni ile ya usambazaji wa moja kwa moja (live streaming) ima iwe ni maongezi ya simu ya video (video call) au maongezi ya simu ya kawaida ambayo muigizaji anampigia simu na kufanya maigizo ya moja kwa moja kwenye maongezi ya video na kama maongezi ya kawaida unamsikiliza vile anavyotoa sauti ya ashiki.
Pornography ilianzishwa mwaka wa 1969 na Andy Warhol ambapo filamu yake ya kwanza aliyoiita ‘The Blue Movie’ ilipendwa sana huko Amerika. Filamu hii iliwika hadi 1984. Wakati huo walikuwa wakitoa filamu moja moja kwa kuwa waigizaji walikuwa bado wangali na maadili mema na kipimo cha maslahi cha kirasilimali hakikuwa kimekita mizizi sana vile na haya ilikuwa ingalipo nyusoni mwao; hivyo walizishtumu filamu kama hizi. Kwa kuwa urasilimali umeshamiri zaidi leo, sasa wanatoa filamu nyingi mno kwa siku, zinazo waingizia dolari bilioni 97 kila mwaka na hivyo kupelekea ongezeko la makampuni na waigizaji katika sekta hii. Haya, mila na desturi sasa zimewekwa kisogoni na shutma za awali dhidi ya filamu hizi sasa zimetoweka na limekuwa ni jambo la kawaida.
Hali hii imeufanya mujtama wetu kubobea kwenye filamu za ngono kiasi ya kutohisi uovu wala kinyaa. Vijana wetu wa Kiislamu wamekuwa watumwa wa pornography na kama huangalii ama huna kwenye simu unaonekana mshamba.
Mtu huanza kuangalia Pornoghapy kidogo kidogo hatimaye kushindwa kujidhibiti kwa kugeuka kuwa uraibu. Hili limewafanya watoto wetu wamezama kwenye uchafu huu si majumbani, mashuleni, makazini hata kwenye mikusanyiko utaona mtu amezubaa kumbe anaangalia picha za ngono. Wazazi wameona kitu cha kuwapumbaza vijana wao ni kuwanunulia simu na kuwaekea mitandao ya Wi-Fi ili waweze kujipakulia michezo (download games) lakini baada ya hapo hawafuatilii tena kuangalia wanaingia katika tovuti gani bali hata watoto wadogo sana wanaingia kwenye tovuti hizi za ngono na kuangalia uchafu huu. Simu haziangaliliki lau utapewa nafasi uangalie simu za vijana wetu utashindwa kuangalia kwa uchafu ulioko ndani.
Pornography ni haramu (hairuhusiwi) kuangalia. Hatuna budi kulipatiliza hili jinamizi ili kuwanusuru vijana na jamaa zetu kwa ujumla.
Mwenyezi Mungu (swt) asema:
قُلْ لِلْمُؤْمِنِينَ يَغُضُّوا مِنْ أَبْصَارِهِمْ وَيَحْفَظُوا فُرُوجَهُمْ ۚ ذَٰلِكَ أَزْكَىٰ لَهُمْ ۗ إِنَّ اللَّهَ خَبِيرٌ بِمَا يَصْنَعُونَ
“Waambie waumini wanaume wainamishe macho yao, wazilinde tupu zao. Hilo ni takaso bora kwao. Hakika Mwenyezi Mungu anazo habari za wanayo yafanya” [An-Nur: 30]
وَقُل لِّلۡمُؤۡمِنَـٰتِ یَغۡضُضۡنَ مِنۡ أَبۡصَـٰرِهِنَّ وَیَحۡفَظۡنَ فُرُوجَهُنَّ وَلَا یُبۡدِینَ زِینَتَهُنَّ إِلَّا مَا ظَهَرَ مِنۡهَاۖ
“Na waambie waumini wanawake wainamishe macho yao, na wazilinde tupu zao, wala wasionyeshe uzuri wao isipokuwa unao dhihirika.” [An-Nur: 31]
Na katika Hadith Abdulrahman, mtoto wa Abu Said al-Khudri, amepokea kutoka kwa babake kuwa Mtume (saw) amesema; “Mwanamume asiangalie uchi wa mwanamume mwenzake na mwanamke asione uchi wa mwanamke mwenzake na pia mwanamume asilale na mwanamume mwenzake kwa kujifunika shuka moja na mwanamke pia asilale na mwanamke mwenzake na kujifunika shuka moja”. (Sahih Muslim).
Kwa dalili hizi zaonyesha wazi kuwa ni haramu kuangalia pornography bila ya shaka yoyote. Ni jambo baya na hatuna budi kujiepusha nalo.
Ni tabia mbovu na utovu wa adabu. Mojawapo ya sifa za Muislamu ni lazima ajihifadhi na ajilinde kutokana na tabia mbovu kama hizi ili kujiepusha na Moto mkali wa Jahannam lakini kuwa mfumo wa kisekula wa kirasilimali umetufanya sisi kuona haramu ni halali na halali kuiona ni haramu. Kwa kuangalia sana uchafu huu unamfanya mtu afanye mambo mabaya; zaidi inachangia pakubwa mtu kufanya zinaa na hata kuwa na tabia za ubakaji na uhanithi. Kama alivyo sema Mwenyezi Mungu (swt):
وَلَا تَقۡرَبُوا۟ ٱلزِّنَىٰۤۖ إِنَّهُۥ كَانَ فَـٰحِشَةࣰ وَسَاۤءَ سَبِیلࣰا
“Wala msiikaribie zinaa, hakika huo ni uchafu na njia mbaya”. [Al-Isra’: 32]
Ndoa nyingi zimevunjika na upendo wa dhati kati ya wanandoa umetoweka kwa kupunguza hisia ya jimai baina ya mume au mke wa halali, pia kwa kutaka kuiga yaliyomo ndani ya filamu hizi kinyume na maadili ya Kiislamu. Uchunguzi uliofanywa na shirika la Wasserman mnamo 2004 umeonyesha kuwa waasi na wenye kwenda kinyume na ndoa zao huwa kumesababishwa na kukithiri kuangalia filamu za ngono. Utafiti huu ni uzindushi muhimu sana kwa wanandoa miongoni mwa Ummah walionaswa na mtego huu wajinasue na kuachana na munkar huu na warudi kwenye njia ya sawa na kushikamana na Uislamu ili waweze kuhifadhi ndoa zao. Mfano nchini Amerika pekee kila baada ya dakika tatu watoto kumi wanabakwa licha ya kuweko sheria kali ya kifungo cha maisha gerezani. Mwenyezi Mungu (swt) asema:
وَلَقَدۡ ذَرَأۡنَا لِجَهَنَّمَ كَثِیرࣰا مِّنَ ٱلۡجِنِّ وَٱلۡإِنسِۖ لَهُمۡ قُلُوبࣱ لَّا یَفۡقَهُونَ بِهَا وَلَهُمۡ أَعۡیُنࣱ لَّا یُبۡصِرُونَ بِهَا وَلَهُمۡ ءَاذَانࣱ لَّا یَسۡمَعُونَ بِهَاۤۚ أُو۟لَـٰۤىِٕكَ كَٱلۡأَنۡعَـٰمِ بَلۡ هُمۡ أَضَلُّۚ أُو۟لَـٰۤىِٕكَ هُمُ ٱلۡغَـٰفِلُونَ
“Na hakika tumeiumbia Jahannam majini wengi na watu. Wana nyoyo, lakini hawafahamu kwazo. Na wana macho, lakini hawaoni kwayo. Na wana masikio, lakini hawasikii kwayo. Hao ni kama wanyama howa, bali wao ni wapotofu zaidi. Hao ndio walio ghafilika”
[Al-A’raf:179]
Na mwenye kuzama kufanya munkar basi yeye huwa ni kama mnyama bali huwa zaidi ya mnyama. Anapokuwa faragha huhisi hamu ya kuangalia pia anapokuwa na mtu faragha huwa anafikiria kumbaka bila kujali umri wala jinsia; bali hata wanyama wamekuwa hatarini kubakwa!
Pornography zimetumalizia vijana na jamaa zetu kwa kukataa kuasi ukapera na kuamua kushibisha ghariza zao kuangalia picha za ngono na hatimaye kujipiga punyeto. Mojawapo ya mashirika ya kirasilimali ya kusimamia vijana limezungumza upuzi na upotofu kusema kuwa kuna haja kubwa ya watoto kuanzia miaka minane walio katika shule za msingi waweze kufundishwa kuweza kujipiga punyeto ili washibishe ghariza zao kwa kuwa mara nyingi watoto hawa huangalia pornography na wakimaliza kuangalia huwa ashiki zao ziko juu; na kwa kukosa mtu kumshibisha ashiki zake mtoto kama huyu huathirika kwa msongo wa mawazo na ukosefu wa furaha. Hivyo basi shirika hili linaonelea kuwa watoto wote wakiume na wakike wafundishwe namna ya kutumia mikono yao wenyewe kujistarehesha kiasi cha kusema kuwa kwa sasa ni dharura kwa watoto wa shule kuwekewa somo kama hili yaani kwa maana nyingine ni kuwa hili ni miongoni mwa haki za watoto!!!
Zaidi ya hayo, kama mwendelezo wa vita dhidi ya Uislamu, maadui wa Uislamu sasa wamepania kuwatumia wasichana wetu kuchafua sura ya Uislamu na vazi la mwanamke wa Kiislamu. Mia Khalifa msichana wa Kiislamu kutoka Beirut nchini Lebanon aligonga vichwa vya habari kwa kujiunga na uigizaji filamu hizi huku akiwapa motisha wasichana wa Kiislamu wajiunge na kuwa watapewa chumo kubwa na hifadhi kama alivyopewa yeye baada ya kupata vitisho vingi vya kuuwawa kutoka kwa familia yake endapo watampata kwa kuvunja heshima yao, lakini hakujali lolote pale Wamagharibi walipomhakikishia kuwa watampatia hifadhi. Huku akipewa lakabu ya ‘Hijab Pornstar’ yaani mwigizaji filamu za ngono aliyevalia hijab kwa kuwa alikuwa akirekodi filamu hizi huku amevalia vazi la hijab ambalo ni vazi la Kiislamu!! Leo hii umekuwa sasa ndio mtindo kwa wasichana wetu kusajiliwa na makampuni haya kuigiza katika filamu hizi huku wengi wao wakiwa kutoka Indonesia na India.
Suluhisho
Hatuna budi kufichua muozo wa maadili ya mfumo huu wa kirasilimali kama kichocheo cha uovu huu. Na kusimama kidete kuung’oa mizizi yake na kurudisha mfumo badali ulio na maadili mema ya kijamii unaokwenda sambamba na maumbile ya mwanadamu kwa kutambua kuwa ameumbwa na ghariza ya kijinsia inayohitaji kushibishwa. Na ili kushibishwa kwa njia inayoleta utulivu yahitaji kuwekewa muongozo na sio kuachwa huru na vile vile kuambatanishwa na majukumu yake nayo ni kuendeleza kizazi na kuwajibika juu yake kwa kupitia ndoa. Mfumo huo badali ni Uislamu chini ya Dola yake Khilafah kwa njia ya Utume.
Kwa kuwa mfumo wa Kiislamu umejengwa kwa msingi wa uchamungu, mujtama hujifunga mambo yake yote kwa kipimo cha halali na haramu na lengo kuu kwake huwa ni kupata radhi za Mwenyezi Mungu (swt). Vijana wetu watahimizwa kuoa huku kivitendo dola ya Khilafah ikiwafanyia usahali katika ibada hii ya ndoa ikiwemo kuwalipia mahari na masrufu ya familia kwa wasio na uwezo, na ndoa zitakuwa zimejaa furaha na baraka nyingi.
Ama kwa hivi sasa ambapo Dola haijasimama, zifuatazo ni njia ambazo zaweza kumsaidia mwathirika kuachana na uraibu huu muovu: –
- Istighfari na Kujiepusha Kuangalia
Kumuogopa Mwenyezi Mungu na kuamua kuacha tabia hii kwa kutambua kuwa Mwenyezi Mungu ameharamisha hili na endapo ataliwacha na kutubia kikweli, Mwenyezi Mungu atamsamehe na kuyageuza maovu yake kuwa mema. Vile vile ajikurubishe kwa Mwenyezi Mungu kupitia ibada za faradhi na za Sunnah na kukithirisha Dhikr.
- Faragha
Kujiepushe kukaa pekee yako kwani hakika faragha ni miongoni mwa mbinu za shetani za kumshawishi mtu katika maasi ikiwemo yale aliyo athirika nayo ya filamu za ngono. Hivyo basi, jipe shughuli.
- Chaneli au Tovuti za Ngono
Kama wazazi ni lazima tuwe waangalifu kwa vijana wetu tusiwaache tu ovyo bali tuwe nao karibu na kuwafuatilia kila wanacho kifanya. Tuwalee kwa malezi ya Kiislamu kwa kuifanya Aqeedah ya Kiislamu ndio maregeleo ya matendo yao yote na kuwafahamisha kila lililo jema na ovu na kuyafungamanisha na kuhesabiwa mbele ya Mwenyezi Mungu. Endapo tumewanunulia simu kwa ajili ya mawasiliano tuchukue tahadhari ya ziada kwa kuzibana chaneli za filamu au vipindi vichafu vya ngono mitandaoni ili kuwaokoa kutokana na ushawishi wake. Haya pia yawe kwa wazazi lau wao wenyewe watakuwa ni waathirika.
- Usuhuba Mbaya.
Tujiepushe sisi pamoja na watoto wetu kutokana na marafiki wabaya ambao wanatuathiri katika maovu yao ikiwemo kuangalia filamu hizi kwa sababu kama Mtume (saw) alivyo sema katika mafhumu ya Hadith “Ukisuhubiana na mtengeza manukato utafaidika ima kwa kukugawia au nguo zako kunukia vizuri na endapo utasuhubiana na mhunzi utaathirika ima kwa kunuka moshi au nguo zake kutoboka kwa cheche za moto”.
Mohammad Abdurahman Bates
Mwanachama wa Hizb ut Tahrir Kenya