Dhahabu na Fedha ndio Sarafu Mbili Ambazo Dola ya Kiislamu Inapaswa Kuzitabanni
بسم الله الرحمن الرحيم
Jibu la Swali
Kwa: Muhammad Ishak
(Imetafsiriwa)
Swali:
Assalamu alaykum wa rahmatullah wa barakatuhu,
Mwenyezi Mungu (swt) akubariki na akuhifadhi Sheikh wetu…
Swali: Baadhi ya wanafikra katika nchi yetu, Indonesia, wanakataa kuregelea utumiaji wa sarafu za dhahabu na fedha, na kusema kuwa Shari’ah haiagizi kwamba pesa maalum zitumike, wakitumia dalili kwamba Umar ibn al-Khattab alidhamiria kutengeza dirham kutokana na ngozi za ngamia, je rai hii ni sahihi?
Jibu:
Wa Alaikum Assalam wa Rahmatullah wa Barakatuh,
1. Tumeeleza dalili ya Kisheria kwamba dhahabu na fedha ndio sarafu mbili ambazo dola inapaswa kuzitabanni katika Uislamu, na tumetaja maelezo ya hilo katika vitabu, Nidhamu ya Uchumi katika Uislamu na Mali katika Dola ya Khilafah… Pia tumefafanua mada hii katika kitabu, Kielelezo cha Katiba ya Dola ya Khilafah Juzuu ya pili, chini ya Kifungu 167 na ufafanuzi wake… Nitakufikishia yale yaliyotajwa kuhusiana na hili kwa ajili ya uwazi na wepesi wake:
(Kifungu 167: Sarafu ya Dola inapaswa kufungwa kwa dhahabu na fedha, ima iwe imetengezwa kwazo au la. Hakuna aina nyengine ya sarafu ya Dola inayoruhusiwa. Dola inaweza kutoa kitu fulani kama badali ya dhahabu au fedha maadamu Bait ul-Mal itakuwa na kiwango sawia na hicho katika dhahabu na fedha ili kufidia sarafu iliyotolewa. Hivyo, Dola huenda ikatoa sarafu kwa jina lake kutokana na chuma, shaba au noti za karatasi na kadhalika maadamu itakuwa imefinikwa kikamilifu kwa dhahabu na fedha.
Dalili muhimu za hili:
Pindi Uislamu ulipoamua hukmu za uuzaji na uajiri, haukufafanua ni kitu gani ambacho kingebadilishwa kwa bidhaa au huduma na manufaa kiasi ya kuwa kwa msingi huo kitu hicho kingekuwa ni wajib. Bali ulimuachia mwanadamu kufanya ubadilishanaji kwa kutumia kitu chochote kile maadamu kutakuwa na maridhiano ya pande mbili kwa ubadilishanaji huo, na kwa hivyo inaruhusiwa kumuoa mwanamke kwa (mahari) ya kumfunza kushona, na kununua gari kwa badali ya kufanya kazi katika kiwanda kwa mwezi mmoja, na inaruhusiwa kumfanyia mtu kazi kwa kiwango maalum cha sukari. Shariah imeliwacha wazi swala la ubadilishanaji kwa watu ili waweze kulitegemeza juu ya chochote wanachokitaka, ambapo hili linathibitishwa na ujumla wa dalili za biashara na uajiri kama vile:
(وَأَحَلَّ اللّهُ الْبَيْعَ) “Lakini Mwenyezi Mungu ameihalalisha biashara” (TMQ 2:275) – kwa chochote na kupitia chochote, na riwaya:
«أَعْطُوا الأَجِيرَ أَجْرَهُ قَبْلَ أَنْ يَجِفَّ عَرَقُهُ» “Mlipeni mwajiriwa ujira wake kabla jasho lake halijakauka.” (imepokewa na Ibn Majah); kwa maana nyengine, ni kuwa mfanyikazi anapaswa kupokea mshahara wake pindi anapomaliza kazi yake, namna litakavyokuwa umbile la ujira huo.
Zaidi ya hayo, vitu hivi vinavyotumiwa kwa ubadilishanaji sio vitendo kiasi ya kuwa asili yake iwe imefungwa (kwa dalili) na hivyo ruhusa yake itahitaji dalili, bali ni vitu. Asili ya vitu ni kuwa vinaruhusiwa (mubah) maadamu hakuna dalili ya kuviharamisha, na hakuna dalili iliyoripotiwa inayoharamisha matumizi ya chochote katika ubadilishanaji, na hivyo basi inaruhusiwa kutekeleza miamala ya Shariah kwavyo ima katika uuzaji na ununuzi, utoaji zawadi au ubadilishanaji isipokuwa kwa kitu ambacho kuna andiko (nasw) kuharamisha ubadilishanaji wake. Kutokana na hili, ubadilishanaji wa bidhaa kwa pesa, na pesa kwa bidhaa unaruhusiwa bila ya pingamizi zozote, isipokuwa kwa ubadilishanaji wa pesa kwa pesa kwa sababu una dalili maalum na hivyo umefungwa kwa dalili hizo. Kwa namna iyo hiyo, ubadilishanaji wa juhudi kwa pesa, na pesa kwa juhudi, unaruhusiwa bila ya pingamizi yoyote isipokuwa bidhaa au huduma ziwe zimetajwa ndani ya andiko kuwa ni haramu. Kutokana na haya, ubadilishanaji wa bidhaa kwa umbo fulani la pesa, na kwa namna iyo hiyo ubadilishanaji wa huduma au juhudi kwa kiwango fulani cha pesa, pia inaruhusiwa bila ya pingamizi yoyote, namna kitakavyokuwa kiwango cha pesa hizo. Hivyo bila ya kujali kwamba kiwango hicho hakitegemezwi na chochote, kama vile sarafu ya kikanuni, au ikiwa imeegemezwa kwa kiwango maalum cha dhahabu, kama vile sarafu ya karatasi iliyohifadhiwa, au ikiwa kiwango kimeegemezwa kwa dhahabu na fedha katika thamani yake kama vile sarafu wakilishi ya karatasi, zote hizi zinakadiriwa kuruhusiwa kufanya biashara kwazo.
Hivyo basi, ni sahihi kubadilisha bidhaa au huduma kwa kiwango chochote cha pesa na inaruhusiwa kwa Muislamu kuuza kwa sarafu ya aina yoyote na kununua kwa sarafu ya aina yoyote na kuajiri kwa sarafu ya aina yoyote na kuajiriwa kwa sarafu ya aina yoyote.
Lakini, ikiwa Dola itataka ardhi ambazo inazitawala zitabanni aina maalum ya pesa, kiasi ya kuwa itatabikisha hukmu za Shariah kuhusiana na pesa katika upande wa utajiri kama Zaka, ubadilishanaji, riba na chochote chengine, na hukmu zinazohusiana na mtu binafsi anayemiliki utajiri kama vile pesa za fidia ya umwagaji damu (diya), kiwango cha chini cha mali inayoibiwa ambacho kitakadiriwa kuwa ni wizi, na kadhalika, basi haihitaji kuacha wazi matumizi ya kiwango chochote maalum cha pesa, bali inafungwa kutumia aina maalum ya pesa pekee na sio nyenginezo. Shariah imefafanua aina ya pesa, kutoka katika umbile maalum ambalo andiko imelitaja, na hili ni dhahabu na fedha. Hivyo ikiwa Dola itataka kutoa sarafu, inafungwa pesa zake ziwe dhahabu na fedha na sio chengine chochote. Shariah haikuiwacha Dola itoe pesa inazoziridhia, kwa aina yoyote inayoitaka, bali imefafanua aina ya pesa ambazo Dola yaweza kuzifanya kuwa sarafu yake endapo itataka kutoa sarafu kwa viwango maalum vya pesa; ambayo ni dhahabu na fedha pekee. Dalili ya hili ni kuwa Uislamu uliunganisha dhahabu na fedha kwa hukmu maalum, na bila ya mabadiliko yoyote.
Hivyo pindi pesa za fidia ya umwagaji damu zilizofafanuliwa, zilifafanuliwa kwa kiwango maalum cha dhahabu, na pindi ukataji mwizi mkono ulipofaradhishwa, kiwango cha chini ambacho adhabu hiyo ingetekelezwa kilifafanuliwa kwa dhahabu; Mtume (saw) alisema katika ujumbe wake kwa watu wa Yemen:
«وَأَنَّ فِي النَّفْسِ المُؤْمِنَةِ مِاْئَةٍ مِنَ الإِبِلِ، وَعَلَى أَهْلِ الْوَرَقِ أَلْفُ دِينَارٍ»
“Na kwa nafsi ya muumini (inapouliwa) ni ngamia elfu moja, na kwa watu wa fedha ni Dinar elfu moja” (imetajwa na Ibn Qudamah katika Al-Mughni kutoka kwa yale yaliyopokewa kutoka kwa ‘Amru b. Hazim kutoka kwa barua ya Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) kwa watu wa Yemen “na kwa watu wa dhahabu ni Dinar elfu moja” mahali pa: “watu wa fedha”. Na yeye (saw) amesema: «لا تُقْطَعُ يَدُ السَّارِقِ إِلاَّ فِي رُبْعِ دِينَارٍ فَصَاعِدًا» “Mkono wa mwizi haukatwi isipokuwa kwa robo Dinar na zaidi” (imepokewa na Muslim kutoka kwa Aisha (ra)).
Hili linafafanua hukmu maalum kwa Dinar na Dirham, na uzani wa Dinar hupimwa kwa dhahabu, na Dirham hupimwa kwa fedha, ambapo kupitia qiyas imezifanya kuwa pesa kwa thamani ya vitu au juhudi. Pesa hizi ndio sarafu na msingi wake. Kule kuwa Shariah kimaandiko imeziunganisha dhahabu na fedha kwa hukmu za kisheria pindi hukmu hizi ziliponasibishwa kwa sarafu ni dalili kuwa sarafu haiwezi kuwa ila kutokana na dhahabu na fedha pekee.
Zaidi ya hayo, pindi Mwenyezi Mungu (swt) alipofaradhisha Zaka, Yeye (swt) aliifaradhisha juu ya dhahabu na fedha pekee, na kufafanua Nisab kutokana na dhahabu na fedha, na hivyo kukadiria kwamba Zaka ya pesa ni kwa dhahabu na fedha ni ufafanuzi kuwa sarafu ni dhahabu na fedha, na endapo kungekuwa na sarafu nyengine kando na hizi basi Zaka ya pesa ingekuwa ni faradhi juu yake. Kwa sababu hakuna andiko la Zaka juu ya pesa isipokuwa juu ya dhahabu na fedha, hii yaashiria kuwa hakuna ukadiriaji wowote kwa aina nyengine ya pesa. Pia, hukmu za ubadilishanaji wa sarafu ambazo ziliteremshwa kuhusiana na miamala ya kipesa zimezungumzia dhahabu na fedha pekee na miamala yote ya mali iliyotajwa katika Uislamu huamiliwa katika dhahabu na fedha. Na ubadilishanaji wa sarafu ni uuzaji wa pesa kwa pesa, ima kuuza aina moja ya pesa yenyewe kwa yenyewe, au kuiuza kwa aina nyengine ya pesa, na kwa maana nyengine ubadilishanaji wa sarafu ni kuuza sarafu kwa sarafu. Shariah imefafanua ubadilishanaji wa sarafu – ambapo ni muamala kamili wa kipesa – kwa dhahabu na fedha pekee, ambapo ni dalili wazi kuwa sarafu ni lazima iwe kutokana na dhahabu na fedha na sio chengine chochote. Yeye (saw) amesema:
«وَبِيعُوا الذَّهَبَ بِالْفِضَّةِ وَالْفِضَّةَ بِالذَّهَبِ كَيْفَ شِئْتُمْ»
“Na uzeni dhahabu kwa fedha na fedha kwa dhahabu mpendavyo” (imepokewa na Al-Bukhari kutoka kwa Abu Bakra). Na Muslim amepokea mithili ya hii kupitia Ubada Bin Al-Samit. Mtume (saw) pia amesema:
«الذَّهَبُ بِالْوَرِقِ رِباً إِلاَّ هَاءَ وَهَاءَ»
“Dhahabu kwa fedha ni riba isipokuwa ikibadilishwa mkono kwa mkono” (imepokewa kwa itifaki kutoka kwa Umar).
Juu ya hilo, Mtume (saw) alifafanua dhahabu na fedha kama pesa, na kuzifanya pekee kuwa ndio vipimo vya thamani ya pesa ambayo thamani ya bidhaa na juhudi hupimwa dhidi yake, na kwa msingi wake miamala hutekelezwa. Vipimo vya sarafu hii vilikuwa ni Awqiya, Dirham, Daniq, Qirat, Mithqal, na Dinar. Hizi zilijulikana vyema na zilikuwa maarufu katika zama za Mtume (saw), na watu wangefanya miamala kwazo. Na imethibitishwa kuwa yeye (saw) aliziidhinisha. Biashara na ndoa zote zilifanyika kwa dhahabu na fedha, kama ilivyo thibitishwa na riwaya nyingi sahih, na hivyo kule kwamba Mtume (saw) alizifanya dhahabu na fedha kuwa sarafu, na kule kwamba Shariah ilifungamanisha baadhi ya hukmu za Shariah kwazo pekee, na kwamba Zaka ya pesa imefungwa kwazo, na ubadilishanaji wa sarafu na miamala ya mali ilifungwa kwazo, zote hizi ni dalili wazi kuwa pesa katika Uislamu ni dhahabu na fedha pekee na si chengine chochote.) Nukuu kutoka kitabu, Kielelezo cha Katiba, imemalizika.
2. Hivyo, tunapata kuwa dalili za Shariah zilizothibitisha katika kuonyesha kuwa sarafu zinazotabanniwa na dola katika Uislamu ni dhahabu na fedha, na kwamba haitabanni sarafu ya aina nyengine yoyote, na ingawa uidhinishaji wa Mtume (saw) wa sarafu hizi mbili unatosheleza pekee kuthibitisha hukmu ya kisheria juu ya mada ya sarafu katika Uislamu, Shariah haikukomea kwa uidhinishaji wa Mtume (saw) wa sarafu hizo mbili, bali ilikwenda mbele zaidi ya hilo kuweka dalili juu ya mada ya riba, mada ya Zaka, mada ya pesa za fidia ya umwagaji damu… nk.
3. Imesimuliwa kutoka kwa Umar, Mwenyezi Mungu awe radhi naye, kuwa alidhamiria kutengeza dirham kutokana na ngozi ya ngamia, na kwa mujibu wa yale tuliyoyafanyia utafiti, hii iliripotiwa katika silsila ya riwaya mbili:
– Al-Baladhari amesimulia katika kitabu chake, Futuh Al-Buldan (3/578): Amr al-Naqed alisema: Watu, ambao walikuwa ni makafiri, walijua hadhi ya dirham hii machoni mwa watu, hivyo waliipamba na kuilinda, lakini ilipokuja kwenu, mulidanganya na kuiharibu. Na Umar ibn Al-Khattab alisema:
Nimefikiria kutengeza dirham kutokana na ngozi za ngamia. Aliambiwa kwamba katika hali hiyo hakutakuwepo na ndama wa ngamia, akaachana na wazo hilo.
– Abdul-Razzaq Al-San’aii (aliyekufa mnamo 211 H) amesimulia katika kitabu chake “Tafsir ya Abdul-Razzaq”: Mu’ammar na Yahya wamesema: Ayoub amesmea: Ibn Sirin amesema: kwamba Umar ibn Al-Khattab alitaka kutengeza dirham kutokana na ngozi ya ngamia, hivyo wakamwambia: “wao (ngamia) wataadimika, hivyo akaachana na wazo hilo.”
Baadhi walijaribu kumaanisha kupitia hili kuruhusiwa kwa dola katika Uislamu kutotengeza sarafu yake kwa dhahabu na fedha na kutengeza pesa kutoka na sarafu yoyote inayojulikana kama ngozi na mfano wake… Kama ulivyotaja katika swali lako, baadhi ya watu wa zama hizi wanakataa kurudi katika kiwango cha dhahabu na fedha na kuidhinisha noti za benki, wakijengea madai yao juu ya msingi wa maneno haya yaliyosimuliwa kutoka kwa Umar, Mwenyezi Mungu awe radhi naye… na katika kujibu jambo hili, kuna pande tofauti tofauti kama ilivyo fafanuliwa chini:
A- Kama tulivyotaja na kufafanua juu, dalili ya kisheria imethibitisha katika kuonyesha kuwa sarafu katika Uislamu ni dhahabu na fedha, kutokana na uidhinishaji wa Mtume (saw) na kutokana na hukmu nyingi za Shariah zilizofungamanishwa na dhahabu na fedha ikizikadiria kama sarafu… hivyo vipi dalili hizi zote zitaachwa na kuwekwa pembeni, na kugeukia riwaya moja tu kuhusu Umar, Mwenyezi Mungu awe radhi naye, kuthibitisha taarifa inayogongana na dalili wazi na madhubuti? Je, hili si jambo la kushangaza, lililo mbali na maana sahihi ya dalili ya Kisheria?!
B- Kuna tatizo katika riwaya hii pamoja na silsila zake mbili za upokezi, kwani silsila zote mbili za riwaya zimekatika kwa sababu msimulizi wa kwanza kutoka kwa Umar ibn al-Khattab ni al-Hasan al-Basri, ambaye hakukutana na Umar, Mwenyezi Mungu awe radhi naye, na hakuchukua (elimu) kutoka kwake kwa sababu alizaliwa mwishoni mwa Khilafah ya Umar, muda mfupi kabla ya kifo chake. Na msimulizi katika riwaya ya pili ni Ibn Sirin, naye pia hakukutana na Umar ibn al-Khattab, na hakusimulia kutoka kwake, na inasemekana kuwa alizaliwa mwishoni mwa Khilafah ya Umar, na inasemekana wakati wa Khilafah ya Uthman…sasa vipi itakuwa sahihi kuchukua riwaya hizi ambazo zimekatika katika silsila ya upokezi kinyume na hadith sahih za Mtume?!
C- Riwaya ya Al-Hasan Al-Basri ambayo Umar bin Al-Khattab, Mwenyezi Mungu awe radhi naye, alisema: “Nafikiria kutengeza dirham kutokana na ngozi ya ngamia”, yamaanisha kuwa jambo hilo halikwenda zaidi ya kuwa tu “fikra” ya Umar katika kufanya kitendo, na hakuitekeleza fikra hiyo… hivyo vipi tutaitumia kama dalili ya kuruhusu utumiaji wa nyengine isiyokuwa dhahabu na fedha kama sarafu? Kwa maana nyengine, vipi tutategemea “fikra” pekee kutoka kwa Umar ambayo haikutimizwa kwa badali ya dalili kutoka kwa Qur’an Tukufu na dalili madhubuti kutoka kwa Mtume wa Mwenyezi (saw) ambazo ziko wazi katika kuifunga sarafu katika Uislamu? Je, hili si jambo la kushangaza?!
D- Jambo lisilo badilika ni kuwa Makhalifa Waongofu walitumia, mithili ya Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw), dhahabu na fedha kama sarafu, ikimaanisha kuwa sarafu iliyotumika katika zama za khilafah ya Umar, Mwenyezi Mungu awe radhi naye, ilikuwa ni dinar ya dhahabu na dirham ya fedha… hivyo vipi tutaliacha jambo hili la daima na thabiti katika zama za Mtume (saw) na makhalifa waongofu, akiwemo Umar, na kuchukua riwaya inayosema kwamba Umar, Mwenyezi Mungu awe radhi naye, alifikiria kutengeza dirham kutokana na ngozi za ngamia?! Yaani, vipi tutachukua riwaya kuhusu “fikra” yake na kuacha lile lilothibitishwa na kitendo chake cha kutumia dhahabu na fedha kama sarafu katika zama za Khilafah yake, Mwenyezi Mungu awe ardhi na maswahaba wote?
Hivyo ni wazi kuwa kinachomaanishwa na maneno yaliyosimuliwa kutoka kwa Umar, Mwenyezi Mungu awe radhi naye, ni maana isiyo sahihi na hivyo haisimami kama dalili ya taarifa kuwa Uislamu haukufafanua sarafu ya dola, na pia haifai kutumiwa kupinga dalili yenye nguvu zaidi na iliyothubutu…
4. Kuongezea zaidi yaliyotajwa juu, kuacha hukmu ya dhahabu na fedha ulimwenguni na kutabanni noti za benki imepelekea maafa mengi na makubwa kama kuyumba kwa viwango vya ubadilishanaji, udhibiti wa dolari ya Amerika wa masoko, maafa ya sarafu za nchi dhaifu na kupungua nguvu yao ya ununuzi kwa viwango vikubwa sana, pamoja na majanga mengine yanayojulikana na kila mtu anayefuatilia upande wa kipesa, mali na kiuchumi…
Maafa haya hayatamalizwa kutokana na udhibiti wa nchi kuu za kirasilimali, hususan Amerika isipokuwa kupitia kurudishwa kwa kiwango cha dhahabu na fedha na kuzitabanni kama sarafu ili kuondoa maafa hayo yanayotokana na utawala wa pesa za karatasi za nchi za kikoloni za kikafiri na udhibiti wa uchumi wa dunia, hususan kutoka Amerika… na dola ya Khilafah ndio nchi iliyofuzu kufanya hivyo, kwa idhini ya Mwenyezi Mungu…
Yote hayo ya juu yanaonyesha dhahiri umuhimu wa dhahabu na fedha kuwa ndio sarafu pekee halali ya dola ya Khilafah… Na Mwenyezi Mungu ni Mjuzi Zaidi Mwingi wa Hekima.
Ndugu yenu,
Ata Bin Khalil Abu Al-Rashtah
24 Muharram 1442 H
12/09/2020 M