Swadaqa ya Mwana Mwema Kumtolea Mzazi Wake Aliyekufa, Thawabu Zitamfikia?

بسم الله الرحمن الرحيم

 Silsila ya Majibu ya Mwanachuoni Mkubwa

Sheikh Ata Bin Khalil Abu Al-Rashtah Amiri wa Hizb ut Tahrir

kwa Maswali Yaliyowasilishwa Katika Ukurasa Wake wa Facebook wa “Kifiqh”

Jibu la Swali

Kwa: Ameer Turman

Swali:

Assalamu Alaikum Wa Rahmatullahi Wa Barakatuh! Maamkuzi kwenu ewe sheikh wetu na amiri wetu, kutoka nyoyoni mwetu.

Amesema Mtume (saw):

 «إذا مات ابن آدم انقطع عمله إلا من ثلاث، صدقة جارية، علم ينتفع به، أو ولد صالح يدعو له»

“Pindi mwanaadamu anapokufa basi (thawabu za) matendo yake hukatika, isipokuwa kutokana na mambo matatu: swadaqa yenye kuendelea, elimu ambayo watu wananufaika nayo, au mtoto mwema anayemuombea dua”.

Je, sadaqa inayoendelea ni sharti iwe ni ile ambayo maiti alikuwa ameitoa kabla ya kufa kwake? Ama hata watoto wake wakiitolea roho yake pia itahisabika?

Mwenyezi Mungu aziweke sawa hatua zenu juu ya haki, na awashike mikono kufikia yenye izza kwa Ummah.

Jibu:

Wa Alaikum Salaam Wa Rahmatullahi Wa Barakaatuh.

Hadith hiyo ni kuhusu matendo ya maiti “matendo yake hukatika, isipokuwa kutokana na mambo matatu” nayo ni: swadaqa inayoendelea, na elimu yenye manufaa, au mwana mwema anayemuombea”

Ama kuhusu matendo ya wengine kumfikia maiti: kuna matendo ambayo wengine wakiyafanya kwa niaba yake thawabu humfikia, na miongoni mwayo ni swadaqa ambayo watoto wake watamtolea, na wakakusudia thawabu zake zimfikie yeye:

1- Amesema Shawkani katika Nail ul-Autwaar:

[Na imepokewa kutoka kwa Abu Huraira kwamba,

«أَنَّ رَجُلاً قَالَ لِلنَّبِيِّ ﷺ: إنَّ أَبِي مَاتَ وَلَمْ يُوصِ، أَفَيَنْفَعُهُ أَنْ أَتَصَدَّقَ عَنْهُ؟ قَالَ: نَعَمْ»

“Mwanaume mmoja alimwambia Mtume (saw) hakika babangu amekufa na hakutoa wasiya, je kutamnufaisha mimi kumtolea swadaqa? Akasema: “ndio” (imepokewa na Ahmad, Muslim, Nasaai, na Ibn Maajah).

Na kutoka kwa Aisha, kwamba

«أَنَّ رَجُلاً قَالَ لِلنَّبِيِّ ﷺ: إنَّ أُمِّي اُفْتُلِتَتْ نَفْسُهَا، وَأُرَاهَا لَوْ تَكَلَّمَتْ تَصَدَّقَتْ، فَهَلْ لَهَا أَجْرٌ إنْ تَصَدَّقْتُ عَنْهَا؟ قَالَ نَعَمْ»

“Mwanaume mmoja alimwambia Mtume (saw) hakika mamangu amekufa ghafla, na nadhani lau angezungumza basi angetoa swadaqah, je atakuwa na malipo ikiwa nitamtolea swadaqah? Akasema: “ndio” (Bukahri na Muslim)

Na kutoka kwa Hasan,

«عَنْ سَعْدِ بْنِ عُبَادَةَ أَنَّ أُمَّهُ مَاتَتْ فَقَالَ: يَا رَسُولَ اللَّهِ، إنَّ أُمِّي مَاتَتْ أَفَأَتَصَدَّقُ عَنْهَا؟ قَالَ: نَعَمْ قُلْتُ: فَأَيُّ الصَّدَقَةِ أَفْضَلُ؟ قَالَ: سَقْيُ الْمَاءِ»

“Kutoka kwa Saad bin Ubaada, kwamba mamake alikufa, akasema (Saad): “Ewe mjumbe wa Mwenyezi Mungu, hakika mamangu amekufa, je, nimtolee swadaqah?” Akasema: “ndio” nikasema: ni ipi swadaqah bora zaidi? Akajibu: “ni kunywesha maji”. Akasema Hasan: huo ndio unyweshaji wa watu wa Saad huko Madina. (imepokewa na Ahmad na Nasaai).

(Mlango wa Thawabu za Jamaa wa Karibu Kuwazawadia Wafu)

Neno lake (hilo litamnufaisha): ndani yake kuna dalili kwamba, mwana anachomfanyia babake Muislamu – kama vile saumu, na swadaqah – thawabu zake humfikia (babake)

… neno lake (ni kunywesha maji): ndani yake kuna dalili ya kwamba, kunywesha maji ndio swadaqah bora zaidi.

Na katika mapokezi ya Abu Dawud:

فَأَيُّ الصَّدَقَةِ أَفْضَلُ؟ قَالَ: الْمَاءُ، فَحَفَرَ بِئْراً وَقَالَ: هَذِهِ لِأُمِّ سَعْدٍ

“Basi ni swadaqah gani bora zaidi?” Akajibu: “Ni maji, basi akachimba kisima, na akasema: hiki kitakuwa (kwa ajili ya mamake Saad”. Na hadith hii imepokewa pia na Daaraqutni kwenye Gharaib ya Malik. Na imepokewa katika Al-Muatwa kwa hadith ya Said bin Saad bin Ubaada kwamba Saad alitoka pamoja na Mtume (saw) kwenye baadhi ya vita vyake, na mamake (Saad) akafikwa na mauti huko Madina, akaambiwa: acha wasiya, akasema: nitatoaje wasiya na mali ni za Saad! Akafa kabla ya Saad kurudi…” Akaitaja hadith (kwa ukamilifu).

Na kumesemwa: yule mwanaume ambaye hakutajwa jina katika hadith ya Bi Aisha na katika hadith ya Ibn Abbas ni Saad bin Ubaada. Na kinachojulisha hilo ni kwamba, Bukhari baada ya hadith ya Aisha ameleta hadith ya Ibn Abbas kwa tamshi: “Hakika Saad bin Ubaada alisema: hakika mamangu amekufa akiwa na nadhiri” na ni kama ameashiria kuwa ambaye hakutajwa jina kwenye ile hadith ya Aisha ni Saad.  Hadithi za mlango huu zajulisha kwamba (thawabu) za swadaqa ya mtoto humfikia wazazi wawili baada ya kufa kwao, hata bila ya wao kuacha wasiya. Hivyo, kwa hadith hizi hufanyiwa takhsisi ujumla wa kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu:

﴾وَأَنْ لَيْسَ لِلإِنْسَانِ إِلا مَا سَعَى﴿

“Na ya kwamba hatapata mtu ila aliyo yafanya mwenyewe?” [An-Najm: 39]. Lakini hakuna katika hadith za mlango huu zaidi ya kwamba swadaqa kutoka kwa mtoto humfikia mzazi, na bila shaka imethubutu kwamba mtoto ni katika matendo yake, kwa hiyo hakuna haja ya kudai takhsisi…].

2- Sherhe ya An-Nawawi juu ya Sahih Muslim:

[…kutoka kwa Aisha,

أَنَّ رَجُلاً أَتَى النَّبِيَّ ﷺ فَقَالَ: يَا رَسُولَ اللَّهِ، إِنَّ أُمِّيَ افْتُلِتَتْ نَفْسَهَا وَلَمْ تُوصِ وَأَظُنُّهَا لَوْ تَكَلَّمَتْ تَصَدَّقَتْ أَفَلَهَا أَجْرٌ إِنْ تَصَدَّقْتُ عَنْهَا؟ قَالَ: نَعَمْ.

“Kwamba mwanaume mmoja alikuja kwa Mtume (saw) akamwambia: “Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu, hakika mamangu amekufa ghafla, na hakuacha wasiya. Na nadhani lau angeongea basi angelitoa swadaqa, hivi je, atakuwa na malipo ikiwa nitamtolea swadaqa? Akajibu: “ndio” …

Na katika hadith hii: swadaqah anayotolewa maiti humnufaisha, na thawabu zake humfikia maiti, na hilo ni kwa makubaliano ya wanazuoni. Na pia wamekubaliana kwamba dua humfikia, na ulipaji deni, kwa mujibu wa nususi zilokuja kuhusiana na hayo yote. Na kumfanyia hajj maiti yasihi ikiwa ni hijjah ya Uislamu (ya faradhi), na hivyo hivyo kama atakuwa ameacha wasiya wa kufanyiwa hijjah ya ziyada (Sunnah) katika kauli sahihi zaidi kwetu (shaafiiyah) na wametafautiana wanazuoni kuhusu la sawa ikiwa mtu atakufa hali anadaiwa saumu, ila kauli yenye nguvu ni kuwa yaruhusiwa kumfungia, kutokana na hadithi nyingi sahihi katika hilo. Na kauli mashuhuri katika madhehebu yetu ni kwamba thawabu za kusoma Qur`an hazimfikii maiti, na kundi katika watu wetu wamesema thawabu zamfikia, na huo ndio msimamo wa Ahmad bin Hanbal. Ama kuhusu swala na ibada zengine: thawabu zake hazimfikii, (huo ndio msimamo) wetu na wa wanazuoni wengi, na Ahmad amesema: thawabu zote zamfikia kama ilivyo (thawabu) za hajj].

Hivyo basi, wewe kumtolea mzazi wako swadaqah na ukamkusudia, thawabu zake zitamfikia Mwenyezi Mungu akipenda.

Na Mwenyezi Mungu ndiye Mjuzi na Mwenye hekima zaidi.

Ndugu Yenu

Ataa Bin Khalil Abu Rashtah

9 Ramadhan 1443 H

10/4/2022 M

 Link ya jibu hili kutoka ukurasa wa Amiri wa Facebook.