Kanuni Msingi: La Hafifu katika Maovu Mwili au La Hafifu katika Madhara Mawili

بسم الله الرحمن الرحيم

Jibu la Swali:

Kwa: Walid Elmi‎

(Imetafsiriwa)

Swali:

Assalamu Alaikum, Sheikh wetu. Nina swali linalohusiana na kanuni msingi hizi mbili: “La Hafifu katika Maovu Mwili au La Hafifu katika Madhara Mawili”, zinazonukuliwa na wabebaji ulinganizi wengi na harakati nyingi za Kiislamu ili kushiriki katika uchaguzi wa ubunge na urais. Je! Hizi zote ni kanuni za Shariah? Je! Baadhi ya wanachuoni wa fiqh wamezitabanni? Je! Dalili zake ni zipi na majibu kwake ni yapi? Barak Allah Fiik

Jibu:

Wa Alaikum Assalam Wa Rahmatullah Wa Barakatuh

Ama kuhusu kanuni hii, tumeijibu mnmo 29/8/2010, na nitakunukulia jibu hili:

[Kanuni: “La Hafifu katika Maovu Mawili au La Hafifu katika Madhara Mawili”

Hii ni kanuni ya Shariah iliyotabanniwa na wanachuoni wengi wa fiqh. Na kwa mujibu wa wasomi wanaoitabanni, ina maana moja ambayo ni ruhusa ya kutekeleza moja ya vitendo viwili vilivyokatazwa, ambacho ni cha hafifu katika vitendo viwili vilivyokatazwa ikiwa mtu aliyekalifishwa (Al-Mukalaf) na Mwenyezi Mungu hana hiari ila kutekeleza moja ya vitendo hivyo viwili vilivyokatazwa na hawezi kujiepusha na vyote hivyo viwili, kwa sababu iko nje ya uwezo wake kwa kila njia.

Mwenyezi Mungu (swt) asema: [لَا يُكَلِّفُ اللَّهُ نَفْساً إِلَّا وُسْعَهَا] “Mwenyezi Mungu haikalifishi nafsi yoyote ila kwa kadiri ya iwezavyo” [Al-Baqara: 286]. Mwenyezi Mungu (swt) asema: [فَاتَّقُوا اللَّهَ مَا اسْتَطَعْتُمْ] “Basi mcheni Mwenyezi Mungu kama mwezavyo” [At-Taghabun: 16].

Yaani kanuni hii kulingana na wale wanaoitabanni inatumika tu ikiwa hakuna njia ya kuepuka kutekeleza moja ya marufuku mbili, ikiwa huwezi kukwepa vitendo vyote vilivyokatazwa isipokuwa kwa kufanya tendo kubwa zaidi ya yaliyokatazwa, basi la hafifu katika maovu mawili linachukuliwa. Wasomi hawa pia hawafasili la hafifu katika maovu mawili kulingana na matamanio, lakini badala yake kulingana na hukmu za Shariah. Kwa mfano, ulinzi wa roho mbili huchukua nafasi ya kwanza kuliko kuhifadhi nafsi moja, na kuhifadhi nafsi tatu ni bora, na kadhalika. Kuhifadhi roho huja kabla ya kuhifadhi utajiri. Kuhifadhi Dar ul Islam kunakuja chini ya kuhifadhi Dini ambayo ni muhimu zaidi kuliko kuhifadhi roho na utajiri. Vivyo hivyo, Jihad na Imamah (uongozi) mkubwa, yako chini ya kuhifadhi Dini ambayo ni ya juu na muhimu zaidi ya mahitaji. Msomi Ash-Shatibi amesema katika Al-Muwafaqat: “Nafsi zinaheshimiwa na kuhifadhiwa na lazima ziokolewe, ikiwa uchaguzi utakuja kati ya kuruhusu roho kuishi au kupoteza utajiri juu yake, au kuua roho na kutunza utajiri, basi kuweka roho hai ni jambo linalotangulia kwanza.”

Mifano iliyotajwa na wasomi hawa katika matumizi ya kanuni hii inajumuisha:

1- Ikiwa mwanamke anakabiliwa na hatari wakati wa kuzaa na inakuwa vigumu kumwokoa mama pamoja na mtoto na uamuzi wa haraka unahitajika: ama kumwokoa mama ambapo itapelekea kifo cha mtoto, au kumwokoa mtoto ambapo inamaanisha kifo cha mama, na ikiwa hali hii itaachwa na mmoja kati ya hao wawili kutolewa kafara ili kumwokoa mwingine au mmoja kuokolewa kwa kifo cha mwingine, hii inaweza kusababisha kifo cha wote wawili. Katika hali hii tunaweza kutumia “la hafifu katika maovu mawili, au haramu mbili, au madhara mawili”, ambayo ni kutekeleza hatua ya kumwokoa yule anayehitajika katika hali hii, ambaye ni mama, hata kama hatua hiyo hiyo itamuua wa pili.

2- Kwamba mtu anazama majini au kuuawa na mtu mwingine, au kuumizwa vibaya mwili wake na viungo vyake, au mwanamke aliyevamiwa kwa zinaa, mbele ya mtu aliyekalifishwa na Mwenyezi Mungu (Mukalaf) ambaye anaweza kuzuia maovu haya na ana swala ya lazima ambayo huenda akaikosa wakati wake, ima azuie kitendo hicho cha haramu na akose utekelezaji wa wajibu, Au ikiwa atatekeleza jukumu hilo kwa wakati, basi kitendo hicho haramu kitatukia, na wakati hautoshi kufanya yote mawili kwa pamoja. Hapa utumikaji wa kanuni hii ya sheria, na mizani pia unaamuliwa na Shariah, ambayo imefanya uondoaji marufuku hizo zilizotajwa hapo awali kutangulia kuliko ya kutekeleza jukumu lililotajwa hapo awali, lakini ikiwa inawezekana kutekeleza majukumu yote kwa pamoja, basi hiyo inakuwa ni wajib.

3- Hii ni mifano mingine iliyotajwa na Imam al-Ghazali na Izz al-Din ibn Abd al-Salam, Mwenyezi Mungu awarehemu, ambayo inaonyesha matumizi ya kanuni ya “la hafifu katika maovu mawili”, kulingana na wao, na pia inaonyesha kusawazisha kati ya hukmu. Al-Ezz amesema katika kitabu chake “Qawa’id Al-Ahkam Fi Masalih Al-Anam”: “Ikiwa uovu mkubwa umeunganishwa, ikiwa inawezekana kuuzuia, tutauzuia. Ikiwa ni vigumu kuzuia maovu yote tunazuia lililo na madhara zaidi ikifuatiwa na mabaya zaidi, ”kwamba mtu analazimishwa kumuua Muislamu, na ikiwa atakataa inamaanisha kuwa atauawa, kwa hivyo, yeye lazima aepuke madhara ya kumuua (Muislamu) kwa kuwa na uvumilivu wa kuuawa, kwa sababu uvumilivu wake wa kuuawa hauna madhara zaidi kuliko kutekeleza mauaji (ya Muislamu) …” Huu ni mfano dhahiri kwamba ni chaguo la hafifu katika madhara mawili au makatazo mawili, kwa sababu hawawezi kuyaacha yote mawili, na ikiwa anaweza kuzuia madhara hayo mawili, lazima afanye hivyo.

Na amesema katika mfano mwingine: “Vivyo hivyo, ikiwa analazimishwa kumuua mtu kwa kutoa ushahidi wa uongo au hukmu ya uongo (dhidi ya Muislamu), au atauawa. Ikiwa yule anayelazimishwa kutoa ushahidi au kutoa hukmu ambayo inapelekea kuuawa kwa mtu fulani, au kumtenganisha, au kufanya zinaa basi ushuhuda au hukmu hiyo hairuhusiwi, kwa sababu kujisalimisha ili kuuawa kunachukua nafasi ya kwanza kuliko kusababisha mauaji ya Muislamu bila dhambi lolote alilofanya, au kumtenganisha bila ya uhalifu, au kufanya Zinaa … “, yaani, ikiwa ima auwe au kutoa ushahidi wa uongo dhidi ya mwingine ambayo yatapelekea kumuua au kumtenganisha, au kushambulia heshima yake, basi hairuhusiwi kwake kutoa ushahidi lakini badala yake anapaswa kuwa mvumilivu kwa kuuawa, kwa sababu kujisalimisha kuuwawa kunachukua nafasi ya kwanza kuliko kumuua Mwislamu mwingine …

Kwa maana nyengine, hali ambapo mtu anaamua kutumia kanuni ya la hafifu katika makatazo mawili au madhara mawili, ni wakati mtu ameshindwa kuepuka au kuyazuia mambo yote mawili yaliyokatazwa.

Hii ni mifano ya matumizi ya kanuni ya “la hafifu katika maovu mawili”, kulingana na kile wasomi hao wanaoitabanni. Walakini, Kile wanachopigia debe wasomi wa serikali au wale wanaotaka Waislamu wakengeuke kutoka kwa hukmu za Shariah kwa kupotosha na uongo si katika mifano ya kanuni hii.

Wale ambao hutumia kanuni hii ili kufanya kitendo hiki kilichokatazwa badala ya kitendo hicho kilichokatazwa, wakihalalisha matendo yao kwa kuogopa kufungwa jela au kufutwa kazi, huu sio mfano wa kanuni hii.

Vivyo hivyo, wale wanaosema tunashiriki katika utawala wa kikafiri ingawa imeharamishwa, ili tusiachie nafasi zote za utawala kwa waovu, kwa sababu kuwaachia wao ni haramu zaidi … hii sio moja ya matumizi ya kanuni hii, badala yake ni kama mtu anayesema tunafungua baa (ya pombe) na kupata pesa kutoka kwake badala ya kumwachia kafiri afungue na kupata yeye pesa …

Sio kati matumizi ya kanuni kwa mtu kuwasilishwa na mambo mawili yaliyokatazwa na kuchagua la hafifu wakati ana uwezo wa kuacha yote mawili, kama vile kusema wale wanaosema mchagueni fulani na fulani, hata kama yeye ni kafiri msekula au muovu, au kumuunga mkono fulani na fulani na kutomuunga mkono mwingine, kwa sababu wa kwanza hutusaidia na wa pili hautusaidii, au chochote chengine mfano wa hicho, lakini kile kinachosemwa hapa ni: Maswala haya mawili yaliyowasilishwa mbele yetu yameharamishwa, kwa hivyo hairuhusiwi kumchagua mtu msekula na hairuhusiwi kumpa uwakilishi wa Waislamu katika maoni, kwa sababu hashikamani na Uislamu, na kwa sababu hufanya vitendo vilivyokatazwa ambavyo haviruhusiwi kwa mjumbe kutekeleza kama utunzi wa sheria na kuidhinisha miradi iliyoharamishwa, na kutoa wito wa vitu vilivyokatazwa, kuvikubali na kuvifuata, yaani anakataza mema na kuamrisha maovu. Kwa hivyo, hakuna hata mmoja wao anayepaswa kuchaguliwa; kwa sababu kumchagua yeyote kati yao ni haramu. Na kujiepusha na uchaguzi wa yeyote kati yao iko ndani ya uwezo wa mtu.

Si katika mojawapo ya matumizi ya “la hafifu katika maovu maovu mawili” kwamba Muislamu akabiliwe na vitendo viwili vilivyokatazwa, na ana uwezo wa kujiepusha na yote mawili, lakini anachagua la rahisi zaidi kulingana na matamanio yake, na analifanya akidai kwamba ni vigumu kukomesha haramu zote mbili…! Badala yake ni lazima ajiepushe na haramu zote maadamu hiyo inawezekana kwake kwa mujibu wa hukmu za Shariah.

Hii ndio taswira fupi ya “la hafifu katika maovu mawili” au “la hafifu katika madhara mawili”] Mwisho.

Ndugu yenu,

Ata Bin Khalil Abu Al-Rashtah

10 Rabii’ Al Awwal 1442 H

27/10/2020 M

Link ya jibu hili kutoka kwa Ukurasa wa Amiri wa Facebook.