Msoto wa Kiuchumi: Uislamu Ndio Jibu

Mwenyezi Mungu (swt) asema:

﴿وَٱبۡتَغِ فِيمَآ ءَاتَٮٰكَ ٱللَّهُ ٱلدَّارَ ٱلۡأَخِرَةَ‌ۖ وَلَا تَنسَ نَصِيبَكَ مِنَ ٱلدُّنۡيَا‌ۖ وَأَحۡسِن ڪَمَآ أَحۡسَنَ ٱللَّهُ إِلَيۡكَ‌ۖ وَلَا تَبۡغِ ٱلۡفَسَادَ فِى ٱلۡأَرۡضِ‌ۖ إِنَّ ٱللَّهَ لَا يُحِبُّ ٱلۡمُفۡسِدِينَ﴾

“Na utafute, kwa aliyo kupa Mwenyezi Mungu, makaazi ya Akhera. Wala usisahau fungu lako la dunia. Nawe fanya wema kama Mwenyezi Mungu alivyo kufanyia wema wewe. Wala usitafute kufanya ufisadi katika ardhi. Hakika Mwenyezi Mungu hawapendi mafisadi.” [28. Al-Qasas: 77]

Kwa kuongezea Mtume (saw) alituonya kuhusu namna ya tunavyo chuma mali na kuitumia:

«لاَ تَزُولُ قَدَمَا ابْنِ آدَمَ يَوْمَ الْقِيَامَةِ مِنْ عِنْدِ رَبِّهِ حَتَّى يُسْأَلَ عَنْ خَمْسٍ عَنْ عُمْرِهِ فِيمَا أَفْنَاهُ وَعَنْ شَبَابِهِ فِيمَا أَبْلاَهُ وَمَالِهِ مِنْ أَيْنَ اكْتَسَبَهُ وَفِيمَ أَنْفَقَهُ وَمَاذَا عَمِلَ فِيمَا عَلِمَ»

“Miguu ya wanadamu haitoondoka mbele ya Mola wake Siku ya Kiyama, mpaka atakapoulizwa mambo matano: kuhusu uhai/umri wake na aliufanyia nini, kuhusu ujana wake na aliutumia katika nini, kuhusu mali yake na namna alivyoichuma na kuitumia na alikifanyia nini alichokuwa anakijua.” [Tirmidhi]

Wanadamu wamerithishwa mali za dunia na Mwenyezi Mungu (swt) kwa kuwa Yeye ndiye Muumba wa ulimwengu, mwanadamu na uhai. Hivyo basi, kufaulu katika uchumaji na matumizi ya mali hutakiwa kuwa kwa mujibu wa muongozo wa Muumba. Kinyume chake kutashuhudiwa majanga na ufisadi wa kupindukia kama hali ilivyo sasa duniani kote. Leo ulimwengu unatawaliwa na mfumo wa kisekula wa kirasilimali. Mfumo ambao umechipuza kutoka katika akili za wanadamu. Nidhamu ya kiuchumi ya kirasilimali inatambua tatizo la kiuchumi ni uhaba wa rasilimali. Hivyo basi, nidhamu ya kiuchumi ya kirasilimali humaanisha kutatua tatizo la kukidhi mahitaji ya mwanadamu na njia za kukidhia mahitaji hayo kwa mujibu wa mfumo wa kirasilimali. Kwa maana hiyo msingi wa nidhamu ya kiuchumi ya kirasilimali ipo kwa ajili ya kuweka mipango na kuiboresha ili kutatua tatizo la uhaba wa rasilimali. Huku mahitaji hayo yakizingatia uhuru usiokuwa na mipaka kwa mujibu wa nidhamu huria ya kijamii!

Nidhamu ya kiuchumi ya kirasillimali ipo kwa ajili ya kuwapora watu mali zao kupitia utozaji ushuru uliopewa majina tofauti tofauti. Na kuongezea kupitia mikopo ya riba ambayo huwazidishia watu umasikini na tabu katika maisha. Nchi hususan za ulimwengu wa tatu huchukua mikopo ya riba ambayo huwa na masharti magumu na yenye kuleta madhara makubwa kwa raia wao. Masharti hayo huwa ni kutokana na kushurutishwa na taasisi za kifedha za dunia kama vile Benki ya Dunia (WB) na Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF). Taasisi hizi hushirikiana na benki kuu za nchi husika katika kuwatia vitanzi na kuvikazanisha katika shingo za raia. Hili hupelekea katika kuzidishwa ushuru kwa bidhaa na huduma, na kutozwa ushuru bidhaa na huduma ambazo awali zilikuwa hazitozwi na kufutiliwa mbali ruzuku zote au baadhi, malipo ya riba kuzidi kwa kutegemeza malipo ya mikopo kwa sarafu ya dolari ($) n.k. Hivyo gharama ya maisha hupanda na uwezo wa raia wengi kununua bidhaa na huduma huzidi kuporomoka kwa kasi. Ilhali ukuwaji wa uchumi hupimwa kwa kutegemea faida na hasara ya makampuni na sio uwezo wa raia kukidhi mahitaji yao!

Mfumo wa Uislamu ambao unachipuza kutoka kwa Muumba wa viumbe, Mwenyezi Mungu (swt). Nidhamu yake ya kiuchumi inatambua tatizo la kiuchumi ni usambazaji wa rasilimali. Hivyo basi, nidhamu ya kiuchumi ya Kiislamu humaanisha namna ya kusambaza mali, namna ya kuimiliki na namna ya kuitumia kwa mujibu wa mfumo wa Kiislamu. Kwa maana hiyo msingi wa nidhamu ya kiuchumi ya Kiislamu ni kwenda mbio kuifanyia kazi Shari’ah (Qur’an na Sunnah) ikiwa ni pamoja na kuweka mipango na kuiboresha ili kutatua tatizo la usambazaji wa rasilimali. Kwa kuongezea sera ya kiuchumi ya Kiislamu inadhamini watu binafsi kukidhi mahitaji yao msingi ikiwemo kupata chakula, mavazi na makaazi na pia kukidhi mahitaji ya kimujtama ikiwemo elimu, usalama na matibabu. Kwa kurudisha tena maisha ya Kiislamu kupitia kusimamisha dola ya Kiislamu ya Khilafah kwa njia ya Utume ndio njia pekee ya kuitekeleza nidhamu ya kiuchumi ya Kiislamu. Mapato na matumizi ya Khilafah yamefungwa na Shari’ah na hayajumuishi utozaji raia ushuru wala kuchukuwa mikopo ya riba kwa ajili ya kuwasimamia watu au kuendesha serikali. Utozaji ushuru na mikopo ya riba imeharamishwa katika Uislamu.

Msoto wa kiuchumi unaoshuhudiwa duniani kote hivi sasa suluhisho lake ni watu kusimamisha Khilafah kwa njia ya Utume. Kufanya hivyo kutapatikana mafanikio na maendeleo ya kiuchumi ya kweli.

Ali Nassoro Ali

Mwanachama wa Afisi Kuu ya Habari ya Hizb ut Tahrir