Hotuba ya Tillerson Juu ya Sera ya Amerika Nchini Syria Kidhahiri Inavutia Lakini ni Hadaifu Mithili ya Ujanja wa Mbweha

Taarifa kwa Vyombo vya Habari
(Imetafsiriwa)

Waziri wa Kigeni wa Amerika Rex Tillerson alitoa hotuba katika Chuo Kikuu cha Stanford, jimbo la California mnamo 17/1/2018 na kuonyesha raghba ya kufafanua sera ya Amerika nchini Syria. Suala la Syria halikuja tu kama kadhia, bali ndilo lililokuwa kadhia pekee katika hotuba ya Tillerson. Baada ya kutathmini matukio nchini Syria, ambapo alipasua mbarika kwa kuchanganya ukweli na urongo ili kuikomboa Amerika kutokana na dhima ya damu ya watu wa Syria na kujidhihirisha kwao kama rafiki anaye wajali, Tillerson akatamatisha na kujumlisha malengo ya sera ya Amerika nchini Syria kuwa: 1. Kumpiga vita adui mkuu wa Amerika, ISIS, pamoja na al-Qaeda na kuyazuia makundi haya kutokana na kuwa hatari kwa Amerika na washirika wake. 2. Amerika itaangazia juu ya “kudhaifisha” athari ya Iran nchini Syria na kutoiwezesha kuasisi ukanda unaoanzia kutoka Iran mpaka kufikia bahari ya Mediterranean. 3. Kwa sababu hizi, majeshi ya Amerika hayatajiondoa kutoka eneo la Kaskazini Mashariki mwa Syria, lakini litaimarisha uwepo wake wa kijeshi na wa kidiplomasia maeneo ya Kikurdi kuhakikisha kuwepo kwa hali tulivu mpaka wakati suluhu ya kisiasa itakapo tekelezwa kuambatana na azimio la 2254. 4. Amerika haitaruhusu usaidizi wa kimataifa wa kujengwa upya kwa eneo lolote lililo chini ya udhibiti wa serikali ya Assad. 5. Kufanya uchaguzi huru na wazi chini ya ufadhili wa Umoja wa Mataifa, ikiwemo kushiriki kwa wakimbizi wa kiusalama wa Syria na wote waliolazimika kukimbia mzozo, hatimaye kupelekea kung’atuka kwa Assad na familia yake kutoka uongozini.

Ni wazi kuwa uamuzi wa Amerika wa kuimarisha uwepo wake wa kijeshi na wa kidiplomasia unalenga kulazimisha uhalisia mpya utakao iwezesha Amerika kudhibiti kwa kina matukio nchini Syria, ima kijeshi, au kupeleka vita dhidi ya ugaidi kama kisingizio nchini Syria. Tillerson, mrongo aso na haya, amedai kuwa Amerika haitarudia tena kosa lake la Iraq nchini Syria ilipoondoa majeshi yake nchini humo mnamo 2011; kuondoa majeshi huku kulitoa mwanya wa kuzuka kwa kundi la ISIS ambalo hatimaye lilisababisha kuzuka kwa maafa (kama alivyodai). Bila shaka, hakuona haja ya kueleza ni vipi na kwa nini uongozi wa jeshi la Iraq ulivyo lisalimisha eneo la Kaskazini mwa Iraq pamoja na uwezo wake wote wa kijeshi na wa kifedha kwa kundi la ISIS wakati wa kiangazi cha 2014.

Taarifa yake, pamoja na uamuzi wa kuunda kikosi cha wanajeshi 30,000 wa mpakani, yadhihirisha kuwa Amerika ina malengo maovu na nia ya kuchochea migogoro ya kufuatana ili ivumbue njia ya kufikia maslahi na malengo yake katika eneo hili. Kuendelea kuwepo kwa majeshi ya Amerika nchini Afghanistan, iliyo ikalia katika uvamizi wake mnamo 2001, ni ushahidi tosha kwa haya tuyasemayo. Kisingizio cha vita dhidi ya ugaidi dhidi ya al-Qaeda (jana) na ISIS (leo) ni urongo na uzushi ili kufinika uhalisia wa nia za Amerika. Katika hotuba yake alisema: “Amerika itadumisha uwepo wake wa kijeshi nchini Syria utakao jitolea kuhakikisha kuwa ISIS haitanuki tena.” Aliongeza: “Operesheni yetu ya kijeshi nchini Syria itabakia kwa msingi wa masharti.” Akimaanisha kuwa majeshi haya hayana tarehe maalum ya kuondoka kwao au viwango fulani vya kupima kufaulu kwa operesheni hiyo. Pindi Seneta Tom Udall alipo muuliza afisa wa Wizara ya Kigeni David Satterfield, “Iweje vita hivi vigeuke na kutokuwa na mwisho wake?” Jibu la Satterfield lilikuwa ni mnong’ono wa kuhadaa kwa maneno yasiyo eleweka.

Bila shaka, mbweha Tillerson hakuwa na budi kuficha sumu ndani ya asali, alijaribu kuipamba hotuba yake na kumwaga machozi ya mamba alipodai kuwa Amerika inajali raia. Yaani waathiriwa wa kibaraka wa Amerika, katili wa Damascus. Tillerson ameapa kuwa Amerika kamwe haitaruhusu matumizi ya silaha za kemikali nchini Syria na kwamba Amerika itawahisabu wale watakaohusika… huku akikosa kuzungumzia kuhusu waathiriwa wa mabomu na mvua ya makombora yaliyo haribu mahospitali, misikiti na majumba juu ya vichwa vya raia, katika kamusi ya Tillerson inaonekana kama ambaye hii ni aina ya mauaji ya “huruma”, na hivyo basi kuyafungia macho.

Tunatamatisha kwa kusema kuwa baada ya kufichua ukweli wa uhalifu wa Amerika na kuonyesha kuwa ukatili wa Damascus ni sehemu tu ya uhalifu mwingi wa mhalifu halisi, Amerika. Ni aibu kwa baadhi ya viongozi wa upinzani (mapinduzi) wa lile linaloitwa Jeshi Huru kufukuzia mangati ya ahadi ya Trump ya pepo. Ingawa Trump alikataa kukutana nao jijini Washington, na kuwaruhusu tu kufanya baadhi ya mikutano jijini Washington, wakati huo huo ujumbe wa kundi la majadiliano unakimbia kutoka jiji moja kuu hadi jengine kujaribu kushawishi nchi husika kuwa majeshi ya mapinduzi yako makini kudhamini maslahi ya nchi hizo zaidi kuliko Bashar mtumizi wa kemikali. Haya yanajiri huku makundi mengine yakipigana kufikia malengo ya Erdogan katika eneo la Afrin badala ya kuelekeza juhudi zao dhidi ya katili huyu wa Damascus.

Kila mmoja ni sharti atambue kuwa njia fupi zaidi ya kumng’oa Bashar na ukatili wa genge lake ni kwa kupitia kuunganisha juhudi zote kuzalisha pigo kuu litakalo angamiza serikali hii ya Damascus na wala si vyenginevyo. Hii yahitaji uongozi mmoja unaotafuta radhi za Allah na kupinga usaidizi wa makhaini wanaopanga njama dhidi ya mapinduzi ya Ash-Sham. Kinyume chake watu wetu wa Ash-Sham wataendelea kuteseka kwa muda mrefu zaidi.

Dkt. Osman Bakhach
Mkurugenzi wa Afisi Kuu ya Habari ya Hizb ut Tahrir

H.  9 Jumada I 1439 Na: 1439 H / 008
M.  Ijumaa, 26 Januari 2018