Hali Ngumu ya Kiuchumi: Matunda ya Mti mouvu wa Mfumo wa Kiuchumi wa Kibepari uliong’olewa ardhini.

Hali Ngumu ya Kiuchumi: Matunda ya Mti mouvu wa Mfumo wa Kiuchumi wa Kibepari uliong’olewa ardhini.

Mwaka mmoja baada ya serikali ya Kenya Kwanza kuchukua hatamu za uongozi, hali ya kiuchumi na maisha ya raia wa kawaida imezidi kua mbaya. Ni dhahiri shahiri kwamba matarajio makubwa ya wananchi kurahisishiwa gharama za maisha na utawala ulioko mamlakani sambamba na kuondokewa na malimbikizi ya deni la taifa, yamegeuka kuwa mangati/mazigazi.

Nasi twawajibika kueleza yafuatayo:-

Hali hii ya taifa inayoshuhudiwa ni dhihirisho la kufilisika kwa mfumo wa kiuchumi wa kirasilimali (ubepari) na siasa yake ya Kidemokrasia. Ni bayana kuwa wanasiasa wa Kidemokrasia hujulikana kwa sifa yao ya siasa za debe tupu,na hata yale maneno wasemayo kwenye kampeni za uchaguzi huwa si lolote ila kuupa uhai mfumo kandamizi wa kiuchumi wa kirasilimali uliokwisha feli zamani. Kimaumbile, ubepari huzalisha wanasiasa wenye hulka ya siasa za undumakuwili haijalishi wawe kwenye mrengo na muungano wowote ule wa kisiasa. Kwa sababu hii imekuwa ni ada na dasturi ndani ya Demokrasia kwa wanasiasa wake kuwa warongo huku wakitupiana lawama ilhali tatizo hasa si lolote ila ni Mfumo wenye wa kiuchumi.

Kwa kuchukua sera za kimakosa kama vile utozaji mkubwa wa ushuru, viwango vya juu vya riba, kukopa na mikakati mengine ya kukata matumizi, mfumo huu kattu hauthamini utu wa mwanadamu. Hii ikimaanisha kwamba gharama kubwa za maisha, kiwango cha juu cha ukosefu wa ajira, maovu ya kijamii na ongezeko la visa vya utovu wa usalama yote haya kwa wanauchumi wa kirasilimali hayatiliwi umuhimu wowote. Zaidi ya haya, kosa kubwa la Urasilimali ni kuangalia uchumi kwa msingi wa kutegemea data na tarakimu na kwa kuzifanya kama ndio kipimo kikubwa cha ustawi wa kiuchumi pasina na kuangalia ule uhalisia wa maisha ya mwanadamu.

Uislamu ndio chaguo pekee la kumkomboa mwanadamu kutokana na majanga haya ya kiuchumi ya mara kwa mara na mfumo wa kiuchumi wa kibepari ulishindwa kutatua matatizo. Hii ni kwa kuwa Uislamu hudhamini mali yote ya umma sio kwa lengo jengine ila kwa maslahi ya umma. Udhamini huu kimsingi huondosha suala la utozaji wa ushuru kwa sura ya kibepari ambao umelifanya kuwa ndio chanzo muhimu cha mapato yake hivyo Uislamu huacha matumizi ya bidhaa na vyanzo vya mapato kupelekwa na nguvu ya soko yaani kuegemea mahitaji na usambazaji). Kihistoria Uislamu unabeba ushahidi wa kuthibitisha jinsi gani wanadamu waliweza kukombolewa dhidi ya utumwa wa zigo la ushuru, riba na ubarakala wa kisiasa. Tunaamini kwamba maisha ya watu yatakua sahali mno pale ambapo mfumo wa uchumi wa Kiislamu utatekelezwa chini ya dola ya Khilafah itakayosimamishwa hivi karibuni katika moja wa nchi za Kiislamu.

﴿ أَلَمْ تَرَ كَيْفَ ضَرَبَ اللَّهُ مَثَلًا كَلِمَةً طَيِّبَةً كَشَجَرَةٍ طَيِّبَةٍ أَصْلُهَا ثَابِتٌ وَفَرْعُهَا فِي السَّمَاءِ )تُؤْتِي أُكُلَهَا كُلَّ حِينٍ بِإِذْنِ رَبِّهَا وَيَضْرِبُ اللَّهُ الْأَمْثَالَ لِلنَّاسِ لَعَلَّهُمْ يَتَذَكَّرُونَ (

Je hukuona jinsi MwenyeziMungu alivyopiga mfano wa neno zuri? Ni kama mti mzuri mizizi yake ni imara na matawi yake yamenyoka juu. Hutoa Matunda yake kila kwa idhini ya Mola wake Na MwenyeziMung huwapigia watu mfano ili wapate kukumbuka. [Ibrahim: 24-25]

Shabani Mwalimu

Mwakilishi kwa Vyombo Vya Habari

Hizb ut Tahrir Kenya