Nyuma ya Shambulizi la Bomu la Nuklia Jijini Nagasaki Magharibi ni Adui wa Waislamu na Wanadamu

 Taarifa kwa Vyombo vya Habari

(Imetafsiriwa)

Mnamo 9/8/2018, Japan iliadhimisha miaka 73 ya waathiriwa wa bomu la atomiki lililoangushwa na Amerika juu ya Nagasaki wakati wa siku za mwishoni mwa Vita vya Pili vya Dunia. Takriban watu 74,000 walifariki kutokana na athari ya bomu hilo, huku bomu lililolipiga jiji la Hiroshima mnamo 6/8/1945 likisababisha vifo vya watu 140,000 ambao walikadiriwa na Kanali wa Amerika Cunningham kuwa shabaha halali. Na hata kuwakadiria wakaazi wote wa Japan kama shabaha halali. Shambulizi hili la kinuklia ni kumbukumbu dhahiri ya kukosekana thamani ya kiakhlaqi, utu au ya kiroho katika sera za nchi za kikafiri za kikoloni. Itahitaji rekodi ndefu ndipo tuweze kuhesabu uhalifu uliojaa aibu uliotekelezwa na nchi za kimagharibi katika kampeni zao katili za kuukoloni ulimwengu katika karne zote zilizopita, pasi na kusaza sehemu yoyote ulimwenguni kutokana na uhalifu huu; tutataja baadhi ya uhalifu mkuu: vita vya kuangamiza wahindi wenyeji wa Amerika katika ulimwengu mpya (Kaskazini, Katikati na Amerika Kusini), au vita vya kufuja utajiri wa Afrika na kuwafanya watumwa watu wake, au vita maarufu vya opium ambavyo Uingereza (maarufu kwa msemo: “mzigo wa mzungu”) ilitaka kutajirisha hazina yake kwa gharama ya Wachina, moja kwa moja mpaka mabomu ya kinuklia ya Amerika yalioangushwa jijini Hiroshima na Nagasaki pasi na uhalali wa mkakati wowote wa kijeshi. Hii ni kupitia ushuhuda wa makamanda wakuu wa kijeshi nchini Amerika, akiwemo Jenerali Eisenhower kamanda wa majeshi ya Amerika barani Ulaya, na admirali William Halsey, waliosema, “bomu la kwanza la atomiki lilikuwa ni jaribio lisilokuwa na umuhimu… lilikuwa ni kosa… [wanasayansi] walikuwa na umbile hili na walitaka kulijaribu, kwa hivyo wakaliangusha!”     

Bila shaka, rekodi ya uhalifu wa Wamagharibi haukukomea hapa; historia ya Vietnam, vijiji na viungani inatoa ushuhuda wa kiwango hiki cha uovu wa Amerika ambao licha ya kusimamisha ile inayodaiwa kuwa sanamu ya uhuru katika kisiwa cha Ellis jiijini New York, viongozi wake wa kisiasa na kijeshi hawakupumzika wakifurahia vinyago vyao, ikiwemo silaha zilizopigwa marufuku kimataifa, kuanzia napalm hadi vita vya kemikali vya Agent Orange, ambazo zimepigwa marufuku karatasini pekee. Kinyume na hayo vita vya kisasa (kuanzia Vita vya Kwanza hadi Vita vya Pili vya Dunia) vimeona yale ambayo kalamu haiwezi kuyasifia katika maangamivu, yakiwemo mauwaji ya wafungwa waliojeruhiwa mahospitalini. Zaidi ya hayo kuanzisha vita kamili visivyo tofautisha kati ya mtoto au mwanamke, mzee au mwanamke, maisha ya mwanadamu hayana thamani mbele ya mashetani watu hawa, uhalifu wote huu unatekelezwa chini ya jina gani? Ili kupata maslahi ya kikoloni kwa warasilimali wachache wanaodhibiti nchi hii na watu wake!!    

Hivyo basi, ni ajabu unaposikia au kusoma taarifa ya mmoja au mwengine katika watoto wa Waislamu akitoa mwito kwa “jamii ya kimataifa” kutekeleza uamuzi fulani kupitia Baraza la Usalama au Umoja wa Mataifa, ambazo huungana tu kwa ajili ya uovu na uhalifu. Ya hivi karibuni ni matakwa ya wanaoitwa “wawakilishi” wa upinzani wa Syria kutoka katika taasisi za kimataifa, na Baraza la Usalama kutia “shinikizo” kwa muuwaji wa serikali ya Damascus kuwaachilia huru wafungwa! Je, ni wajinga juu ya ukweli kuwa “jamii ya kimataifa” ndio ya kwanza kujua ukweli wa uhalifu wa Bashar na kabla yake babake Hafez aliyefariki, pamoja na uhalifu wa Sisi, na mithili yao ya watawala wa Waislamu wahalifu wasioheshimu mkataba wowote au mafungamano na waumini? Ikiwa hawajui hilo ni janga, na ikiwa wanajua, hilo ni janga kubwa zaidi.  

Wakati umewadia kwa Ummah kutambua uhalisia wa mzozo uliomo ndani yake, ambao unaulazimisha kumtambua rafiki kutoka kwa adui: wakoloni Wamagharibi, pamoja na washirika wa Kirusi, ndio adui, na zana za kutekeleza sera za kimagharibi kutoka kwa taasisi za kimataifa na ile inayoitwa “jamii ya kimataifa” na “mamlaka ya kimataifa” zote ni zana hatari ambazo hazina budi kupingwa. Ni lazima tufanye kazi kuregesha uamuzi wa Ummah mikononi mwake. Haipaswi kuziruhusu dola za kiimla kuchukua udhibiti wa kadhia zetu au kupigia debe masuluhisho yake yenye sumu. Hili ni kwa kadhia zetu zote kuanzia Palestina hadi Syria, Sudan, Kashmir na nyenginezo. 

Dkt. Osman Bakhach
Mkurugenzi wa Afisi Kuu ya Habari ya Hizb ut Tahrir

H.  2 Dhu al-Hijjah 1439 Na: 1439 AH / 031
M.  Jumatatu, 13 Agosti 2018