CHAGUZI ZA KIDEMOKRASIA NI SARABI, HUDHANIWA NI MAJI KWA MWENYE KIU

Agosti 9 ni siku ya uchaguzi nchini Kenya utakaokuwa wa sita wa vyama vingi tangu kurudishwa tena Demokrasia ya vyama vingi mwaka 1992. Vyama 82 vitashiriki katika uchaguzi huu, kando na wagombea watakao simama bila ya vyama. Walioonesha azma ya kuwania urais ni 47 ila 4 tu ndio walioweza kuidhinishwa na Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC). Kati ya hao ni Raila Odinga wa ODM (Muungano wa Azimio) au William Ruto wa UDA (Muungano wa Kenya Kwanza) ndio walio na tamaa ya kushinda uchaguzi huu. Kama ilivyo ada miungano hii imejipanga kikabila na cheche zake zimedhihirika mapema katika kampeni kiasi ya kutia hofu wadadisi wa kindani na wale wa kimataifa juu ya usalama wa nchi wakati wa uchaguzi na baada yake.

Uchaguzi huu utafanyika wakati wananchi wapo katika hali ya mfadhaiko haswa upande wa kiuchumi na kiusalama ingawa hali hii ngumu imekuwa ikizidi miaka hadi miaka. Hali hizi mbili, zimefikia hali mbaya wala hakuna tamaa ya kutatulika kwa uharaka ila imekuwa ni ajenda iliyodandiwa na wagombea urais kwa malengo ya kuwavutia wapiga kura. Upande wa kiuchumi kila mwaka wa uchaguzi kuna dhihirika mdororo kwa kiasi kikubwa zaidi kuliko miaka mingine isiyokuwa ya uchaguzi. Ukuaji wa uchumi ulishuka katika miaka ya uchaguzi wa mwaka 2002, 2007, 2012, 2017 kwa asilimia 0.2, 0.5, 3.8 na 3.8 mtawalia na yatarajiwa mwaka huu itashuka zaidi. Miongoni mwa mambo yanayochangia kudorora kwa uchumi ni pamoja na:

Kwanza- Mfumuko wa bei ambao umezifanya bidhaa muhimu ikiwemo chakula hususan mahindi kufikia kiwango cha Ksh250 kwa mfuko wa kilo 2.

Pili- Mgogoro wa kivita baina ya Urusi na Ukraine umesababisha upungufu wa ngano na mbolea nchini, kwa kuwa Kenya inaagiza asilimia 90 ya ngano na mbolea kutoka nchi hizo mbili!

Tatu- Makampuni, wafanyibiashara na wawekezaji wa ndani na nje ya nchi wameingiwa na wasiwasi kutokana na hatima ya uchaguzi huu. Huku sababu hizi zikitajwa na wanasiasa kuwa ndio chanzo cha hali ngumu ya maisha hivi sasa, ukweli unabakia kuwa ni mfumo wa kiuchumi wa kibepari ambao asili unajali maslahi ya tabaka la mabwenyenye wanaomiliki uzalishaji na usambazaji wa rasilimali. Kwa uhakika kila mwenye kufikiria kwa kina atafahamu kwamba mfumko wa bei umekuweko hata kabla ya vita huko Ukraine! Hata hivyo, hofu hiyo imekitwa katika msingi wa mvutano wa walionacho ‘dynasties’ na wasiokuwa nacho ‘hustlers’ na imepelekea mzunguko wa pesa kupungua kwa kiasi kikubwa sokoni na hata kupunguza hifadhi ya sarafu za kigeni katika Benki Kuu hususan Dola ya Amerika.

Ama upande wa kiusalama, tayari raia wameanza kuhisi tishio juu ya maisha yao hususan kutokana na matamshi ya uchochezi kutoka kwa wanasiasa. Miongoni mwa matamshi hayo ni ‘hatutaki madoadoa, kama ni noma iwe noma.’ Matamshi hayo pamoja na kuibuka kwa vikundi na magenge yanayodaiwa kudhaminiwa na kutumiwa na wanasiasa ili kuwahangaisha na kuwashambulia wapinzani wa kisiasa pamoja na wafuasia wao. Kwa kuongezea, Kenya hivi sasa inakodelea janga la kielimu kutokana na kuharakishwa utekelezaji wa mtaala mpya wa elimu maarufu CBC kwa kuwa miundo mbinu na rasilimali msingi hazijawa tayari na hivyo kuhatarisha maisha na mustakbali wa watoto zaidi ya milioni 1.4 wanaotakiwa kujiunga na JSS.

Enyi Waislamu, Wanasiasa pamoja na manifesto zao zote wamefaulu kuhadaa raia kuamini kubwa matatizo yanayowakabili yatatuliwa kupitia uchaguzi. Cha ajabu chaguzi tano zimepita ilhali matatizo huzidi bali ni wazi kuwa manifesto hizi hubakia kwa maandishi tu pasina na kutekelezwa na ushahidi wa haya uko wazi kabisa.

Hakika, chaguzi za kidemokrasia ni sarabi (mazigazi) kwa mwenye kiu hudhaniwa ni maji ilhali sio. Kwa kuwa vyama vyote vya kisiasa na ilani zao zimetenga Uislamu mbali hakuna lolote litakaldhaminia suluhisho la kweli. Chaguzi hizi kiasili hutumika katika kuhalalisha zoezi la upigaji kura na sio kuwa ndio chanzo cha kusuluhisha matatizo kimsingi. Kwa mfano wagombeaji wa urais wanaahidi mengi. Ruto ameahidi kushukisha rasilimali mashinani ili kuwanyanyua walala hoi pamoja na kutenga bilioni Sh200 kwa ajili ya kutoa mikopo ya riba ya chini kwa wafanyibiashara wadogo. Huku Raila akiahidi kutoa Sh6,000 kwa mwezi kwa Wakenya milioni 8 wasiojiweza pamoja na elimu ya bure kutoka msingi hadi chuo kikuu! Hizo ni ahadi hewa hususan tukizingatia kuwa hali ya Kenya kiuchumi haiwezi kuhimili ahadi hizo kutokamana na madeni makubwa yaliyokopwa ndani na nje ya nchi ambayo sasa hivi yamefikia zaidi ya trilioni 8.2!

Hivyo basi, wakati umefika wa watu kufungua macho na kutambua kuwa chaguzi za kidemokrasia ni ndoto za mchana zilizojikita katika mchezo wa patapotea. Kwa kuwa wanasiasa wake hupatiliza dhiki za raia na kuwatumia kama ngazi ili kuingia madarakani. Kisha kuwatupilia mbali na kutowajali hadi msimu ujao baada ya miaka 5. La msingi ni kufanya kazi usiku na mchana ili kurudisha tena maisha ya Kiislamu kwa ushirikiano na harakati ya Kiislamu ya Hizb ut Tahrir. Harakati isiyojali lawama wala ukosoaji kutoka kwa wapenzi wa demokrasia na mfumo wao wa kisekula wa kirasilimali. Ili kujitoa katika vitanzi au minyororo ya kiuchumi, kisiasa, kijamii na kielimu hakuna budi kurudisha tena utawala wa Kiislamu wa serikali ya Khilafah katika nchi iliyotimiza vigezo na masharti yanayo zingatiwa.

 

وَٱلَّذِينَ ڪَفَرُوٓاْ أَعۡمَـٰلُهُمۡ كَسَرَابِۭ بِقِيعَةٍ۬ يَحۡسَبُهُ ٱلظَّمۡـَٔانُ مَآءً حَتَّىٰٓ إِذَا جَآءَهُ ۥ لَمۡ يَجِدۡهُ شَيۡـًٔ۬ا

“Na walio kufuru vitendo vyao ni kama sarabi (mazigazi) uwandani. Mwenye kiu huyadhania ni maji. Hata akiyaendea hapati chochote.” [24. An-Nur: 39]

 

Hizb ut-Tahrir Kenya

29/07/2022 M

30TH Dhul Hijjah 1443 H