Je, Bismillahi ni Sehemu ya Suratul Faatiha?

بسم الله الرحمن الرحيم

 Silsila ya Maswali Yaliyowasilishwa kwa

Amiri wa Hizb ut Tahrir

Sheikh Ata Bin Khalil Abu Al-Rashtah Katika Ukurasa Wake wa Facebook

Jibu La Swali:

Kwa: Bakr Saad

 Swali:

Assalamu Alaikum Wa Rahmatullahi Wa Barakaatuh wa Maghfiratuh…

Namuomba Mwenyezi Mungu awaafikie kwa kila la kheri, kwani hakika yeye ni muweza wa hilo.

Swali langu ni: ikiwa wanazuoni wamekubaliana kwamba, yeyote anayepinga kuwa Bismillahi sio aya katika Al-Faatiha basi hawi kafiri. Kwa sababu (hiyo Bismillahi) imethubutu kwa njia ya Aahaad (kupokewa na watu wachache) na wala sio kwa njia ya Tawaatur (kupokewa na watu wengi sana)… sasa vipi iwe ni nambari katika baadhi ya misahafu mwanzoni mwa Al-Faatiha leo? Na lini iliingia kama aya katika Al-Faatiha? Na je, Al-Faatiha ni aya saba (7) ama sita (6) bila ya Bismillahi? Kwani misahafu imetafautiana katika kuhesabu nambari za Al-Faatiha. Na je, hili linapingana na hifadhi ya Mwenyezi Mungu kwa Qur`an tukufu? Na upi msimamo wa Dola ya Kiislamu ijayo in shaa Allah, juu ya uwepo wa vitu visivyokuwa mutawaatir kwenye msahafu, kama vile Bismillahi na dua iliyo mwishoni mwa msahafu?!

Na Mwenyezi Mungu awabariki.

Jibu:

Wa Alaikum Salaam Wa Rahmatullahi Wa Barakaatuh.

Tumeshatangulia kujibu swali kuhusiana na Bismillahi tarehe 21 Rabiul Akhir 1432 H – sawa na 11/3/2011 M. Na imekuja ndani yake haya yafuatayo:

[Kuhusu Bismillahi: ni aya katika Qur`an tukufu kama ilivyo kipande cha aya katika Surat al-Naml:

إِنَّهُ مِنْ سُلَيْمَانَ وَإِنَّهُ بِسْمِ اللَّهِ الرَّحْمَنِ الرَّحِيمِ﴿

“Imetoka kwa Sulaiman nayo ni: Kwa jina la Mwenyezi Mungu, Mwingi wa rehema, Mwenye kurehemu.” [Al-Naml: 30].

Ama katika mwanzo wa Al-Faatiha, au mwanzoni mwa sura (zengine) hili lina ikhtilaaf kwamba je, ni aya katika sura? Ama ni kipambanuzi tu kati ya sura (na sura nyingine)… na hii ikhtilaafu haidhuru, kwa sababu, pande zote mbili zinakubali kuwa (hiyo Bismillahi) ni katika Qur`an kwenye Surat al-Naml. Na ikhtilaafu ni kuhusu kuiweka mwanzo wa sura isiyokuwa Surat  al-Tawba, je, (hiyo Bismillahi) ni aya pia mwanzoni mwa sura? Ama ni aya mwanzoni mwa Al-Faatiha? Ama sio aya mwanzo wa sura, wala mwanzo wa Al-Faatiha… Maadamu wote wanakubali kuwa (Bismillahi) ni aya katika Surat al-Naml, basi ikhtilaafu kuhusu kuwepo mwanzo wa sura haiathiri isipokuwa kwenye kuisoma katika swala mwanzo wa Al-Faatiha au mwanzoni mwa sura zengine, kusomwa kwa suati au kwa siri au kutoisoma kabisa, kulingana na hukmu za kisheria zilivyovuliwa na wanazuoni wenye kujitahidi] Mwisho wa nukuu.

Na ili kuzidi kuweka wazi zaidi na kujibu mambo mengine katika swali lako, nitataja mambo yafuatayo:

1- Imekuja kwenye kitabu cha “Shakhsiya” – Juzuu ya Kwanza – ukurasa wa 159 hadi 160 [Hakika Jibril alikuwa akisoma yote yaliyoteremshwa kwa Mtume (saw) katika Qur`an mara moja kila mwaka. Na katika ule mwaka ambao Mtume (saw) alikufa, Jibril alimsomea Mtume Qur`an yote mara mbili. Imepokewa kutoka kwa Aisha (ra) kutoka kwa Fatima (as) “Mtume (saw) alinieleza kwa siri kwamba Jibril alikuwa akinisomea Qur`an yote kila mwaka mara moja, na hakika yeye amenisomea mwaka huu mara mbili, na sioni ila ni kwamba wakati wangu (wa kufa) umefika” (imepokewa na Bukhari). Na imepokewa kutoka kwa Abu Huraira akisema: “Alikuwa (Jibril) akimsomea Mtume (saw) Qur`an nzima kila mwaka mara moja, na akamsomea mara mbili kwenye mwaka ambao alikufa ndani yake” (imepokewa na Bukhari).

Jibril kumsomea Mtume (saw) Qur`an kila mwaka mara moja, maana yake ni kumsomea kwa mpangilio wa aya zake kulingana na baadhi yake, na kwa mpangilio wa aya zake kwenye sura zake. Kwa sababu, kuaridhi kitabu maana yake ni kusoma ibara, matamshi, na mpangilio wake. Na Mtume kusomewa mara mbili katika ule mwaka aliokufa ndani yake, maana yake hivyo hivyo ni kusomewa kwa mpangilio wa aya zake kulingana na baadhi yake, na kupangilia aya zake ndani ya sura zake. Na pia yaweza kufahamika hivyo hivyo kutokana na hiyo hadithi kusoma kwa mpangilio wa sura zake kulingana na baadhi yake. Isipokuwa tu zimekuja hadithi zengine sahihi zikiwa wazi katika kupangilia aya, kwani zinaeleza wazi kupangilia aya kulingana na baadhi yake na kupangilia aya kwenye sura zake: «ضَعُوا هَذِهِ الآيَاتِ فِي سُورَةِ كَذَا بَعْدَ آيَةِ كَذَا» “(Mtume akiwaambia) ziwekeni aya hizi kwenye sura kadhaa baada ya aya kadhaa” «ضَعُوا هَؤُلَاءِ الْآيَاتِ فِي السُّورَةِ الَّتِي يُذْكَرُ فِيهَا كَذَا وَكَذَا» “Ziwekeni aya hizi kwenye sura ambayo ndani yake kunatajwa kadhaa na kadhaa”. Na ilikuwa sura hukamilika na kuanza nyengine kwa maelekezo kutoka kwa Mwenyezi Mungu kupitia kwa njia ya Jibril. Imepokewa kutoka kwa Ibn Abbas akisema: “Mtume (saw) alikuwa hajui kumalizika kwa sura hadi inapoteremka Bismillahi ar-Rahmaani Ar-Rahiim” na katika mapokezi mengine: “Pindi inapoteremka Bismillahi ar-Rahmaani arRahiim ndipo wao hujua kuwa sura imemalizika” (Sunan al-Baihaqi na Abu Dawud). Yote hayo yanajulisha kwa kukatikiwa kwamba, mpangilio wa aya katika sura zake, na muundo wa sura kwa idadi ya aya zake na maweko yake, yote hayo yalikuwa kwa maelekezo yatokayo kwa Mwenyezi Mungu Mtukufu. Na hivyo ndivyo Umma ulivyopokea kutoka kwa Mtume wao (saw), na hayo yakathubutu kwa njia ya Tawaatur (mapokezi ya watu wengi kutoka kwa wengi …]

2- Na wakati maswahaba (ra) walipotegemea msahafu wa Uthmaan walithibitisha ndani yake Bismillahi mwanzoni mwa Al-Faatiha na mwanzoni mwa sura zengine isipokuwa Surah al-Baraa`ah (Tawba) lakini haikuwa wazi ikiwa hilo lamaanisha kwamba Bismillahi ni aya katika kila sura ambazo wamethibitisha Bismillahi mwanzoni mwake, yaani Al-Faatiha na sura zilobakia isipokuwa Baraa`ah, au kwamba hiyo (Bismillahi) ni ya kupambanua baina ya sura na sura nyengine. Hivyo basi kukapatikana ikhtilaafu kati ya wanazuoni kuhusu kuwa Bismillahi ni aya katika Al-Faatiha, na kuwa ni aya katika sura zengine… lakini pamoja na hii ikhtilaaf wote wanakubali kwamba, Bismillahi imethibitishwa kimaandishi kwenye msahafu ambao maswahaba watukufu walikubaliana juu yake mwanzo wa Al-Faatiha na katika mwanzo wa sura zengine isipokuwa mwanzo wa Surah al-Baraa`ah, na hayo ni kwa makubaliano ya maswahaba radhi za Mwenyezi Mungu ziwe juu yao wote.

3- Imekuja katika kitabu cha As-Suyutwi (Al-Itqaan Fii Ulum al-Qur`an 1/234)

[Al-Faatiha: msimamo wa wengi ni aya saba, watu wa Kuffah na Makka wakahesabu Bismillahi bila ya kuhesabu ﴿أَنْعَمْتَ عَلَيْهِمْ﴾  “…ulio waneemesha” [Al-Faatiha: 7] kuwa ni aya, na waliobaki ni kinyume. Na amesema Al-Hasan: ni aya nane, akazihesabu zote mbili kuwa aya. Na baadhi yao wamesema ina aya sita, hivyo hawakuzihesabu. na wengine wakasema ina aya tisa, wakazihesabu hizo pamoja na ﴿إِيَّاكَ نَعْبُدُ﴾. “Wewe tu tunakuabudu” [Al-Faatiha: 5] (kuwa ni aya kivyake). Na inayotilia nguvu kauli ya kwanza ni hadith iliyopokewa na Ahmad, Abu Dawud, At-Tirmidhi, Ibn Khuzaima, Al-Hakim, Daaraqutniy na wengineo, kutoka kwa Ummu Salama kwamba Mtume (saw) alikuwa akisoma hivi:

(بِسْمِ اللَّهِ الرَّحْمَنِ الرَّحِيمِ * الْحَمْدُ لِلَّهِ رَبِّ الْعَالَمِينَ * الرَّحْمَنِ الرَّحِيمِ * مَالِكِ يَوْمِ الدِّينِ * إِيَّاكَ نَعْبُدُ وَإِيَّاكَ نَسْتَعِينُ * اهْدِنَا الصِّرَاطَ الْمُسْتَقِيمَ * صِرَاطَ الَّذِينَ أَنْعَمْتَ عَلَيْهِمْ غَيْرِ الْمَغْضُوبِ عَلَيْهِمْ وَلا الضَّالِّينَ)

KWA JINA LA MWENYEEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU. Sifa njema zote ni za Mwenyeezi Mungu, Mola Mlezi wa viumbe vyote; Mwingi wa Rehema Mwenye Kurehemu; Mwenye kumiliki siku ya malipo. Wewe tu tunakuabudu, na wewe tu tunakuomba msaada. Tuongoe njia iliyonyooka. Njia ya ulio waneemesha, siyo ya walio kasirikiwa, wala walio potea. [Al-Faatiha: 1-7] akazikata aya baada ya aya, na kuzihisabu kama wanavyohisabu mabedui. na akahisabu:( بِسْمِ اللَّهِ الرَّحْمَنِ الرَّحِيمِKwa Jina la Mwenyeezi Mungu Mwingi wa Rehema Mwenye Kurehemu” kama aya, na hakuhisabu ﴿عَلَيْهِمْ﴾. “juu yao” kuwa ni aya. Na amepokea Daaraqutniy kwa Sanad sahihi kutoka kwa Abd Khair akisema kwamba Ali aliulizwa kuhusu “Sab’ ul Mathaani” akajibu: ni ﴿الْحَمْدُ لِلَّهِ رَبِّ الْعَالَمِينَ﴾ “Sifa njema zote ni za Mwenyeezi Mungu, Mola Mlezi wa viumbe vyote” akaambiwa: lakini hiyo ina aya sita! akasema: (بِسْمِ اللَّهِ الرَّحْمَنِ الرَّحِيمِKwa Jina la Mwenyeezi Mungu Mwingi wa Rehema Mwenye Kurehemu” ni aya] Mwisho wa Nukuu.

Na hii ina maana kwamba ikhtilaafu kuhusu maudhui ya Bismillahi kuwa aya…. n.k haya yanaingia katika mlango wa ijtihaad kwa dalili sahihi kwa wenye kujitahidi, na kuwafuata wanazuoni wenye kujitahidi na wanaozingatiwa, hilo ni jambo limo ndani ya sheria…

4- Na hakika yaliyooingizwa kwenye msahafu kama vile vitone, irabu, na kuwekwa alama za vikomo, na alama za hukmu za kusoma… n.k au yaliyowekwa mwishoni mwa baadhi ya misahafu kama dua, au yaliyoko pambizoni kama vile tafsiri na ufafanuzi… yote hayo hayaathiri katika Qur`an kuchanganyika na vitu vyengine. Kwani Waislamu wameihudumia Qur`an huduma kubwa, na mamilioni miongoni mwao wameihifadhi, na maandishi yake yamekuwa kwa mapokezi ya wengi kutoka kwa wengi, hivyo ikawa haitarajiwi kuwa itachanganyika na vitu vyengine na kuwatatiza watu. Kwa hiyo, ndio maana Waislamu tangu mamia ya miaka wameingiza kwenye misahafu baadhi ya mambo yanayosaidia kuisoma Qur`an kama vile vitone na irabu na vitu vyengine, na wala hayo hayakuathiri maandishi ya Qur`an tukufu… kwa hiyo basi, Dola ya Khilafah haitozuia uwepo wa hizi irabu na alama za vikomo… ndani ya misahafu.

Ufupisho ni kwamba, kutokea kwa ikhtilaafu katika ijtihaadi kuhusiana na Bismillahi kwamba ni aya katika Al-Faatiha au sio aya, au kwamba Al-Faatiha aya zake ni 6 au 7… au kwamba yasomwa kwa siri au kwa sauti… yote hayo hayaathiri katika hifadhi wa Mwenyezi Mungu kwa Qur`an tukufu, kwani, Bismillahi ni aya katika Surat al-Namli. Na Qur`an imekusanywa kwenye msahafu mmoja tangu zama za Makhalifa waongofu Mwenyezi Mungu awaridhie, kama ilivyoandikwa mbele ya Mtume (saw), na kama walivyoisoma kutoka kwa Mtume wa mwenyezi Mungu. Na amesema kweli Mwenyezi Mungu Mtukufu kwa neno lake:

(إِنَّا نَحْنُ نَزَّلْنَا الذِّكْرَ وَإِنَّا لَهُ لَحَافِظُونَ)  “Hakika Sisi ndio tulio teremsha Ukumbusho huu, na hakika Sisi ndio tutao ulinda.” [Al-Hijr: 9]

Natumai hayo yanatosheleza na Mwenyezi Mungu ndiye Mjuzi na Mwenye hekima zaidi.

Ndugu Yenu,

Ataa Bin Khalil Abu Rashtah

 26 Dhul Qa’adah 1443 H

25/6/2022 M

Link ya jibu hili kutoka ukurasa wa Amiri wa Facebook.