KUH: OMBI LA KUTAKA KUFUNGULIWA MISIKITI

بسم الله الرحمن الرحيم

Kwa: Waziri wa Usalama wa Ndani na Ushirikiano wa Serikali ya Kitaifa

Kwa: Waziri wa Afya

Kwa: Maimamu wote, Wadau wote Wakiislamu na Jamii ya Kiislamu

 

Huku janga la virusi vya Corona likiendelea kutikisa nchi na ulimwengu kwa ujumla, serikali ilitoa amri ya kuifunga misikiti yote humu nchini, hatua iliopelekea kusitishwa ndani yake kwa swala za Jamaa na ile ya Ijumaa  kwa kipindi cha takriban miezi miwili sasa. Marufuku hii iliyotolewa mwezi March,2020, ambapo kisa cha kwanza cha Covid-19 kiliripotiwa nchini hadi sasa inaendelea kutekelezwa sawia ni ile ilani ya  kutotoka nje kuanzia saa moja jioni hadi saa kumi na moja alfajiri iliongezwa muda wake hadi tarehe 6 Juni,2020.

Tunapokiri vyema  athari ya gonjwa la  Covid-19  humu nchini na ulimwengu kwa ujumla, tunakariri kwamba ipo haja kubwa ya kuzingatia na kujifunga na hatua za kuzuia msambao wa maambukizi ya maradhi haya hatari hasa ikizingatiwa kufanya hivyo ni miongoni mwa mafunzo ya Uislamu aliyokuja nayo Mtume wetu (s.a.w) kwa zaidi ya karne 14 zilizopita.

Sisi tunafahamu vyema kwamba ndwele hii inaendelea kuwa changamoto kubwa bali ni  mtihani utokao kwa Muumba katika kuwatahini  waja wake, hivyo  tunapaswa  kurudi Kwake kwa kutubia na kutwii amri Zake. Kwa muktadha huu, kufungwa misikiti ni jambo linalochukiwa sana katika Dini ya Mwenyezi Mungu na waja wake ambao bila shaka nyoyo zao ni zenye kuungulika kwa maumivu yaliyokuwa makubwa zaidi ndani ya Mwezi mtukufu wa Ramadhani. Kwa masikitiko makubwa, hata kabla ya hatua ya serikali baadhi ya viongozi wa Kiislamu waliamua kuifunga misikiti badali ya kuchukua hatua za tahadhari za kuwafanya wawe salama huku wakiendelea kuswali swala ya jamaa! Cha kuumiza wakenda mbali zaidi katika kupindisha dalili za Kiislamu zioane na hatua yao hii ya kihatari!

Tungependa kupaza sauti yetu kuhusu kufungwa kwa Misikiti kwa kusema yafuatayo:

Kwanza: Usitishwaji wa swala za Ijumaa pamoja na zile za Jamaa ni hatua inayogongana moja kwa moja na mafundisho matukufu ya Dini yetu. Katika kipindi cha mkurupuko wa maradhi, kinachotakikana na sheria ya Kiislamu sio kuzuia Waislamu wote kijumla kuswali za jamaa bali kinachotakikana ni kuwatenga na kuwazuia wale wagonjwa kuingia misikitini.Hatua za kuzuia maambukizi ya maradhi kama vile udumishwaji wa usafi, kuvaa vitamvua (vibarakoa) upimaji wa watu wengi na kuosha mikono lazima zichukuliwe. Dalili ya haya ni hadithi iliopo katika Mustadarak ya Al-haakim kutoka kwa Twariq bin Shihab aliepokea kwa Abi Musa kutoka Kwa Mtume SAAW kwamba alisema:

((الْجُمُعَةُ حَقٌّ وَاجِبٌ عَلَى كُلِّ مُسْلِمٍ فِي جَمَاعَةٍ إِلَّا أَرْبَعَةٌ: عَبْدٌ مَمْلُوكٌ، أَوِ امْرَأَةٌ، أَوْ صَبِيٌّ، أَوْ مَرِيضٌ ))

((Swala ya Ijumaa ni haki ya uwajibu kwa kila Muislamu katika jamaa ispokuwa kwa watu wanne: Mja anaemilikiwa, Mwanamke, mtoto na mgonjwa.))

Ama kuhusiana na swala za jamaa, Sheria imeeleza bayana kwamba swala hiyo ni faradhi ya kutoshelezeana (Fardhul kifaya).AbuDarda radhi za Mwenyezi Mungu zimshukie amepokea kutoka kwa Mtume SAAW kwama alisema:

((مَا مِنْ ثَلَاثَةٍ فِي قَرْيَةٍ وَلَا بَدْوٍ لَا تُقَامُ فِيهِمْ الصَّلَاةُ إِلَّا قَدْ اسْتَحْوَذَ عَلَيْهِمْ الشَّيْطَانُ، عَلَيْكَ بِالْجَمَاعَةِ فَإِنَّمَا يَأْخُذُ الذِّئْبُ مِنَ الْغَنَمِ الْقَاصِيَةَ))

((Hawawi watu watatu katika mji wala mashamba ndani yao ikawa haisimamishwi ndani yao Swala ispokuwa Sheitani huwa amewatawalia, jilazimishe na swala za jamaa kwani mbwa mwitu hula mbuzi aliekuwa peke yake)). [Abu Daud]

Kwa msimamo huu, tunakariri kwamba amri ya kufungwa Misikiti haikuwa hatua mwafaka kwani imepekelea jamii ya Kiislamu katika dhambi kubwa kwani wameacha kuswali swala za jamaa na zile za kila wiki za Ijumaa. Kwa hivyo, tunaitaka serikali ifungue misikiti haraka iwezekanavyo. Kwa hakika ni jambo lenye kuwabughudhi Waislamu wanapoiona  serikali hivi karibuni ikiruhusu mikahawa kuwa wazi kwa hoja ya kutaka kunasua hali ya kiuchumi huku wakati huohuo inaendelea kufunga nyumba za Ibada ambazo ndani yake hutukuzwa Jina la Mwenyezi Mungu (Swt).

Pili: Serikali lazima iwajibike katika kuweka hatua kama vile kuhakikisha kwamba kuna udumishwaji wa usafi, kuvaa vitamvua na upimaji wa watu wengi na kuosha mikono ili kuzuia msambao wa maradhi kwa Waumini. Na endapo yoyote miongoni mwa waumini atagundulika kuwa na ishara za Covid-19, basi azuiliwe kuingia msikitini huku wale ambao ni wazima waweze kuruhusiwa kuendelea na ibada. Ni jukumu la kimsingi kwa serikali kuwapa raia wake vifaa na huduma za afya hasa ikizingatiwa kwamba ni jambo linalojuliakana kwa wote kwamba kuna ufadhili mkubwa wa kifedha  iliopokea kwa wahisani wa humu nchini kadhalika na mikopo ya mataifa ya nje. Hata ingawa tuna imani kwa kuna waumini wa kweli wangelipenda kusaidia utoaji wa vifaa husika vya kuzuia maambukizi misikitini ikiwa ni yenye kufunguliwa.

Tatu: Huku mwezi mtukufu wa Ramadhani ukikurubia kukamilika itakuwa kosa kubwa vilevile kwa Waislamu ikiwa hawatoweza kuswali swala yoyote ya jamaa ndani ya mwezi huu  mzima ikiwemo suna iliosisitizwa ya Swala ya Idul Fitr inayoswalia siku ya kwanza baada ya kumalizika mwezi huo mtukufu. Kwa hivyo, tunaomba kuwa suala hili lichukuliwe kwa unyeti na udhati. Kwa hakika Waislamu wamekuwa na subra ya hali ya juu na sasa ni wakati wa kurudi kwao Misikitini huku wakiwa ni wenye kuchukua tahadhari.

Nne: Tunawakumbusha Maimamu, Viongozi wa Kiislamu na Waislamu wote kwa ujumla kwamba ni katika jukumu lao kutia shindikizo la kufunguliwa Misikiti. Tungependa kuwanasihi kuwa kunyamazia hali hii inayoumiza na chukivu kwa Dini na watu wake bali kosa kubwa ambalo siku ya Qiyama watakuwa ni wenye kuulizwa.  Basi, simameni na mzungumze ukweli ili  hadhi yenu kwa Mwenyezi Mungu ipate kunyanyuka kwani Yeye Allah(S.W.T) amawaamurini kusema ukweli pasina hofu wala upendeleo muweze kufikia daraja za maswahaba watukufu,(Radhi za Mwenyezi Mungu ziwe juu yao) waliosimama kuzungumza haki katika hali ngumu na hapo ndipo wakaweza kunali daraja kubwa baada ya zile za Manabii na Mitume (Rehema na Amani ziwashukie wote) waliotumilizwa kwa wanadamu.

 

Ewe Allah shuhudia kwamba tumefikisha ujumbe Wako!

 

Hizb ut-Tahrir Kenya.

26th Ramadhan, 1441 Hijri/

Jumanne, May 17, 2020