Mauwaji ya Waislamu 49 Wakati wa Swala ya Ijumaa

Taarifa kwa Vyombo vya Habari

Masikitiko yetu ya dhati yaenda kwa waathiriwa na familia zao waliolengwa katika shambulizi baya zaidi la kigaidi wakati wa swala ya Ijumaa mnamo 16 Machi eneo la Christchurch, New Zealand, ambapo watu 49 walichinjwa na mwanamgambo aliyepeperusha moja kwa moja mauwaji yake kwa silaha za kiotamatiki katika mitandao ya kijamii. Hili sio tukio la kipekee, kama ambavyo baadhi, kama vile Raisi wa Amerika Trump, anavyojifanya. Hii ni miongoni mwa kampeni ya kiulimwengu ya mrengo wa kulia ambayo haiwezi kukomeshwa kwa urahisi.

Wanasiasa wakuu na vyombo vikuu vya habari vya kimagharibi vimekuwa vikisambaza mafuta na hewa ya oxygen vinavyohitajika kuchochea moto wa chuki dhidi ya wahamiaji na Waislamu. Udhihirishaji wa hofu hadharani umekithiri juu ya dhana potofu ya mzungu kuwa raia wa tabaka la pili katika nchi yake yeye mwenyewe kwa sababu ya wahamiaji, hususan wale wanaotoka katika biladi za Waislamu.

  • Wahamiaji wamekuwa ndio walengwa wa hofu na chuki kwa pande zote za Atlantiki tangu kampeni za 2016 za Uraisi wa Amerika na kujiondoa kwa Uingereza kutoka katika Muungano wa Ulaya. Zote zikiwa zinaangazia dhana ya kuwepo kwa mvutano wa kitambulisho pamoja na fikra jumla ya thaqafa ya Anglo-Saxo chini ya tishio kutoka nje. Walengwa wakiwa ni Waislamu, Wamexico, Wapole na wengineo. Wote wanadaiwa kuwatishia Waingereza ‘weupe’ masikini au mfanyikazi wa Kiamerika aliyepoteza ajira na kuangamia kwa thaqafa na lugha yake.
  • Laura Ingraham wa shirika la habari la Fox News amesema kuwa “Amerika tuijuayo na kuipenda haiko tena” kwa sababu “Mabadiliko makubwa ya watu yamelazimishwa juu ya watu wa Amerika na ni mabadiliko ambayo hakuna yeyote kati yetu kamwe aliyeyapigia kura na wengi wetu hatuyapendi.”
  • Mjumbe wa Bunge la Congress Steve King alionya kuwa “Hatuwezi kuregesha hadhara yetu kwa watoto wa wengine.”
  • Trump alipatiliza hofu hii barabara, na mwanamgambo huyo akaacha nyuma manifesto ya kurasa 74 iliyomsifu Trump “kama nembo mpya ya kutathmini utambulisho wa watu weupe na lengo la pamoja.”

* Fikra hii ni maarufu na Anders Breivik wa Norway pia alituma manifesto kabla ya kuwauwa watu 77 mnamo 2011. Hakuwa akiwalenga moja kwa moja wahamiaji wala Waislamu bali alikuwa akitaka kuwaadhibu Wazungu wanaoegemea upande wa kushoto kwa kuidhinisha tamaduni nyingi, ambazo aliziona kupelekea “utekaji nyara fulani wa Uislamu wa Ulaya ili kuupiku Ukristo wa Ulaya ndani ya miaka mia ijayo”.

* Mashambulizi mengi ya vyombo vya habari vya upande wa kulia dhidi ya wahamiaji yamelenga juu ya Waislamu. Trump alitoa wito wa “kuzuiwa kikamilifu kwa Waislamu” akiwa kama mgombezi na kutoa agizo la raisi kupiga marufuku Waislamu kusafiri kwenda Amerika. Pia, huku wanasiasa wengi wa Ulaya wakiwa na ujuzi wa kutosha katika matamshi ya chuki dhidi ya Waislamu, Trump aliwaonya kuwa uhamiaji “umebadilisha sura ya Ulaya – na musipo chukua hatua ya haraka sana, kamwe (Ulaya) haiwezi tena kuwa kama ilivyokuwa.”

* Wanawake wamekuwa walengwa haswa katika vitisho. Agosti mwaka jana, Boris Johnson wa Uingereza aliwamithilisha wanawake wanaovaa hijab kama “masanduku ya barua” na “wezi wa benki” na aliyekuwa Waziri Mkuu, David Cameron, alilalamikia kuhusu “utiifu wa kimila” wa wanawake wa Kiislamu. Kwa sasa, kwa kushindwa ‘Daesh’ kikaragosi cha Uislamu, vyombo vya habari vimejaa maoni kuhusu wale wanaoitwa “mabiharusi wa ISIS’. Mwanamke wa Kiislamu, hususan katika kushikamana kwake na maadili ya Kiislamu ya kujisitiri kimavazi, amelengwa sana katika kudunishwa, na miongoni mwa mandhari mbaya zaidi ambazo mshambulizi wa eneo la Christchurch alizipeperusha moja kwa moja ni ile ya kuuwawa kwa kupigwa risasi mwanamke wa Kiislamu katika masafa ya mbali na muuwaji huyu na kisha kumpiga risasi tena kwa masafa ya karibu huku akiwa amelala kifudifudi katika barabara nje ya msikiti akiitisha usaidizi. Muuwaji huyo hakumsaidia, bali hata wale wanasiasa waovu wanaojiita wakombozi pia hawakumsaidia, huku bado wakiendelea kumtisha na kumtusi kinyama mwanamke wa Kiislamu.

* Itakuwa ni makosa kuuona uenezaji huu wa chuki kama natija ya uovu wa wanasiasa wa upande wa kulia pekee. Kuna tatizo baya sana la ubaguzi wa rangi na utaifa, kwa sababu ufahamu mpya wa Kimagharibi wa uraia umezunguka juu ya ubaguzi wa rangi. Ubwana wa kitaifa humaanisha hivyo haswa, na kwa zaidi ya karne mbili zilizopita dola za Ulaya zimejijenga juu ya misingi ya utaifa na zimevumbua upya historia zake pambizoni mwa mashujaa na malenga wa tamaduni zao na lugha zao wenyewe. Hii ni fahamu mpya ya kisiasa barani Ulaya, na kuibuka kwa Nazi ya Ujerumani sio janga la kipekee ambalo nguvu ya utambuzi wa ‘utaifa’ imeunda usoni mwa mporomoko wa kiuchumi na kijamii. Kuunganishwa kwa utaifa katikati ya kitovu cha fahamu ya Kimagharibi ya uraia yamaanisha kuwa wanasiasa wa Kimagharibi hawawezi kuiondoa chuki au kuchora mstari safi mchangani kati ya misemo ‘halali’ ya utambulisho wa kitaifa na uchochezi unaopelekea chuki kwa ‘wengine’.

Ni nidhamu ya Khilafah Rashida pekee ambayo yaweza kuleta utulivu baina ya rangi tofauti. Ulimwengu kwa sasa unakosa muundo makhsusi wa namna watu wa jinsi tofauti tofauti na hata tamaduni zote zaweza kuishi pamoja bila ya hisia yenye nguvu kutishiwa na dhaifu wakati wa ugumu. Nidhamu ya utawala ya Kiislamu iliasisiwa na Mtume Muhammad (saw) miaka 1400 iliyopita, iliyo hudumu kama mwenge wa nuru katika zama za giza za Ulaya, na kukosekana kwake tangu mwanzoni mwa karne iliyopita kumekuwa ni janga, sio tu kwa Waislamu pekee, bali kwa wanadamu wote. Kwa kukosekana kwake, vita viso idadi vya kirangi na mauwaji vimethibitisha hilo. Waislamu wanaijua historia yao, lakini sio hivyo kwa wengine ulimwenguni, na ni wajib katika zama zetu kwa Waislamu kubeba mzigo huu wa kuwabadilisha viongozi wafisadi wa biladi zao mabegani mwao wanaochafua sura ya Waislamu kupitia dhuluma zao na tabia ya umwagaji damu. Wakati ambapo damu za Waislamu zinaonekana kuwa rahisi nchini Yemen, Iraq, Misri na Syria na kwengineko, hata ndani ya balozi zao wenyewe, inapaswa kukumbukwa kuwa wengine wanatazama na kuhukumu, na katika ujinga wao wanasoma mafunzo ya kimakosa kuhusu sisi. Khilafah Rashida itatia shinikizo la maana juu ya wale wanaotaka kuutusi Uislamu na Waislamu, na itafungua mikono kwa wahamiaji pasi na hofu kama iliyopenya Ulaya.

Afisi Kuu ya Habari ya Hizb ut Tahrir

H.  12  Rajab 1440 Na: 1440 H / 025
M.  Jumanne, 19 Machi 2019