بسم الله الرحمن الرحيم
Kwa: Tarek Ifaoui
(Imetafsiriwa)
Swali:
Assalamu Alaikum wa Rahmatullahi wa Barakatuh,
Ni ipi hukmu ya kuswali na nguo zilizoyunyiziwa marashi yenye pombe? Mwenyezi Mungu akulipe kheri.
Jibu:
Wa Alaikum Assalam wa Rahmatullahi wa Barakatuh,
Kwanza: Marashi yaliyochanganywa na pombe ya ethyl huhesabiwa kuwa ni Khamr (pombe), na huamiliwa kwa mujibu wa Shariah kama Khamr na hivyo ni najisi. Tumeelezea haya yote katika majibu mengi, likiwemo Jibu la Swali mnamo 23 Jumada I 1435 H sawia na 24/03/2014 M, ambapo yafuatayo yamekuja ndani yake:
(Kama nilivyojifunza kutoka kwa wataalamu wa sayansi ya pombe kuwa kuna aina mbili: Pombe ya Ethyl na Pombe ya Methyl. Kwa hivyo ikiwa jina, lililomo ndani ya swali, “Ethanol” ni pombe ya Ethyl basi jibu ni hili:
- Pombe ina tabaka linaloitwa pombe ya methyl, na niliambiwa kwamba sio kilevi lakini ni sumu hatari. Mafuta ya Spirit yanatoka katika tabaka hili, na huchukuliwa kutoka kwa taka za mbao na kwengineko. Kuinywa husababisha upofu na inaweza kusababisha kifo ndani ya siku kadhaa. Kwa hivyo, methyl sio Khamr, na haichukui Hukm ya Khamr kwa upande wa najisi na uharamu (Tahreem), isipokuwa upande wa matumizi ya methyl kama sumu kwa msingi wa kanuni ya kusababisha uharibifu, , kwani Ibn Majah ameripoti kutoka Ubadah Bin As-Samit:
»أَنَّ رَسُولَ اللَّهِ صلى الله عليه وسلم ، قَضَى أَنْ لَا ضَرَرَ وَلَا ضِرَارَ«
“kwamba hakuna Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) amepitisha kwamba hakuna kudhuriwa wala kudhuru”.
- Tabaka jengine la pombe linaitwa pombe ya ethyl, ambayo hutumiwa katika vinywaji vilioumka au vileo vilivyochujwa, na spirit ya matibabu ni ya aina hii. Pombe ya Ethyl pia hutumiwa katika tasnia kama kihifadhi cha baadhi ya nyenzo, kama kikali (kukausha maji mwilini), kama vimumunyisho kwa alkali na mafuta (vilainishi), kama dawa ya kuzuia kuganda, kama kuyeyushi cha baadhi ya dawa, kama kiyeyushi cha kutengenezea vitu vyenye kunukia kama marahi na manukato, na inahusika katika utengenezaji wa vifaa vya useremala. Matumizi haya ni ya aina tatu:
- Katika aina moja, pombe hutumiwa kama kiyeyushi pekee, au kama nyongeza ya baadhi ya nyenzo. Katika matumizi kama hayo, pombe haipotezi kiini chake au sifa zake za kemikali; badala yake, inabaki haibadilika katika muundo wa kemikali na athari yake ya kulewesha. Kwa hivyo, matumizi ya pombe katika aina hii ni haramu kabisa, kama mfano wa marashi. Kwa hivyo, matumizi ya cologne (marashi) hayaruhusiwi na inabaki kuwa ni najisi, kwa sababu ina najisi (Najasa) ambayo imechanganywa nayo, na pombe inabaki kuwa haikubadilika. Kwa hivyo inajumuisha nyenzo ambazo zimechanganywa na Khamr, na Khamr ni najisi. Dalili ya hili ni Hadith ya Al-Khushani: Ad-Daraqtani ameripotia kutoka kwa Al-Khushani ambaye alisema:
قال: قلت: يا رسول الله إنا نخالط المشركين وليس لنا قدور ولا آنية غير آنيتهم، قال: فقال: «استغنوا عنها ما استطعتم فإن لم تجدوا فارحضوها بالماء فإن الماء طهورها ثم اطبخوا فيها«
“Mimi alisema: Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu, sisi tunaingiliana na washirikina na ilhali hatuna sufuria wala vyombo zaidi ya vyombo vyao “. Asema: “Kisha yeye (saw) akasema: “Jiepusheni nao kadri ya uwezo wenu, lakini ikiwa hamtapata vyombo vyengine, basi visuzeni kwa maji, hakika maji ndio tohara yake, kisha pikeni ndani yake.”
Hivyo basi Mtume (saw) asema: «فَإِنَّ الْمَاءَ طَهُورُهَا»“hakika maji ndio tohara yake (Tahara)”.
Inamaanisha kuwa vyombo hivi vilikuwa ni Najisi, kwani vilikuwa vimejazwa Khamr (pombe), na vilitakaswa baada ya kusafishwa. Hii inathibitisha kuwa Khamr ni Najisi na swali lilihusu vyombo ambavyo vilijazwa Khamr, kama ilivyoelezwa katika riwaya ya Al-Khushani, iliyoripotiwa na Abu Dawood kutoka kwa Abi Tha’laba Al-Khushani, kwamba alimuuliza Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) akasema:
عن أبي ثعلبة الخشني، أنه سأل رسول الله ﷺ قال: إنا نجاور أهل الكتاب وهم يطبخون في قدورهم الخنزير ويشربون في آنيتهم الخمر، فقال رسول الله ﷺ: «إن وجدتم غيرها فكلوا فيها واشربوا، وإن لم تجدوا غيرها فارحضوها بالماء وكلوا واشربوا«
“Sisi ni majirani na watu wa kitabu na wao hupika nyama ya nguruwe kwenye sufuria zao na kunywa pombe katika vyombo vyao.” Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) akasema: “Ikiwa mtapata vyengine visivyokuwa hivyo basi kuleni na munywe ndani yake. Ikiwa hamtapata vyengine, basi visuzeni kwa maji na mule na munywe”.
Nyama ya nguruwe na Pombe zote ni Najisi. Kwa hivyo vyombo ambavyo vimewekwa ndani yake vinakuwa Najisi. Lazima vioshwe ili kuregesha usafi wake (Tahara) kabla ya matumizi yake.
- Katika aina nyingine, dhati ya pombe hubadilika na hupoteza sifa yake ya ulevi. Inabadilishwa, pamoja na vitu vingine, kuwa dutu mpya iliyo na sifa tofauti na ile ya pombe. Dutu hii mpya haina sumu; kwa hivyo, haichukui Hukm ya Khamr na ni safi (Tahir) kama kitu kingine chochote kinachoanguka chini ya kanuni ya Sharia “asili ya vitu ni vyenye kuruhusiwa isipokuwa ikiwa kuna dalili ya kuharamisha”.
- Katika aina nyingine, pombe hubadilishwa katika dhati yake na hupoteza sifa yake ya ulevi. Inaunda, pamoja na vitu vingine, dutu mpya yenye sifa ya kemikali tofauti na ile ya pombe, lakini dutu hii mpya ni sumu, kwa hivyo iko chini ya Hukm ya sumu: Ni tohara, lakini matumizi yake kwa kunywa au kusababisha madhara kwazo kwako mwenyewe au kwa wengine ni Haram.
- Kwa hivyo, ikiwa pombe ya ethyl imechanganywa na vitu vingine basi Hukm kuhusu hiyo inategemea kujua ikiwa mchanganyiko wa ethyl hupoteza sifa yake ya ulevi au la, na ikiwa mchanganyiko huo ni sumu au la. Hii inahitaji kuchunguza uhalisia uliopo kupitia wajuzi na wataalamu. Ikiwa itathibitishwa kisayansi au itaonyeshwa kuwa mchanganyiko huu ni ulevi basi itachukua Hukm ya Khamr, ikionyesha kwamba ethyl kwenye mchanganyiko haijapoteza sifa yake ya kulewesha na dhati yake katika mchanganyiko huu. Walakini, ikiwa itathibitishwa kisayansi au kivitendo kwamba mchanganyiko huu sio ulevi tena wala kwamba una sumu, basi haichukui Hukm ya Khamr au Hukm ya sumu. Walakini, ikiwa itathibitishwa kisayansi au kivitendo kwamba mchanganyiko huo hauna ulevi tena lakini unabaki na sumu, basi haichukui Hukm ya pombe, lakini iko chini ya Hukm ya sumu.
Kutokana na haya, ikiwa mchanganyiko utakaopatikana una ulevi kama marashi basi utachukua Hukm ya Khamr, kwa Hadith ya Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) kama ilivyosimuliwa na Al-Bukhari na Muslim kutoka kwa Aisha, Mama wa waumini (ra), kwamba alisema:
»كُلُّ شَرَابٍ أَسْكَرَ فَهُوَ حَرَامٌ«
“Kila kinywaji chenye kulewesha ni Haramu”.
Na Muslim amesimulia kutoka kwa Ibn Umar, aliyesema: Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) amesema:
«كُلُّ مُسْكِرٍ خَمْرٌ، وَكُلُّ مُسْكِرٍ حَرَامٌ…»
“Kila chenye kulewesha ni Khamr, na kila chenye kulewesha ni Haramu”.
Na katika riwaya nyengine ya Ibn Umar:
«كُلُّ مُسْكِرٍ خَمْرٌ، وَكُلُّ خَمْرٍ حَرَامٌ»
“Kila chenye kulewesha ni Khamr, na kila Khamr ni Haramu”.
Zaidi ya hayo, Khamr imeharamishwa katika dhurufu kumi sio inaponywewa pekee. At-Tirmidhi ameripotia kutoka kwa Anas Ibn Malik aliyesema:
«لَعَنَ رَسُولُ اللَّهِ ﷺ فِي الخَمْرِ عَشَرَةً: عَاصِرَهَا، وَمُعْتَصِرَهَا، وَشَارِبَهَا، وَحَامِلَهَا، وَالمَحْمُولَةُ إِلَيْهِ، وَسَاقِيَهَا، وَبَائِعَهَا، وَآكِلَ ثَمَنِهَا، وَالمُشْتَرِي لَهَا، وَالمُشْتَرَاةُ لَهُ»
“Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) amelaani katika pombe watu kumi: mgemaji wake, mwenye kugemewa, mnywaji wake, mbebaji wake, mwenye kubebewa, msafirishaji wake, muuzaji wake, mwenye kula thamani yake, mnunuzi wake, na mwenye kununuliwa.”
Yoyote katika dori hizi kumi ni Haramu). Mwisho.
Pili: Manukato yaliyo na pombe kama marashi ya cologne, kwa mfano, ni najisi, na mojawapo ya masharti ya kuswihi swala ni tohara ya nguo na mwili, kama ilivyoelezwa katika dalili ifuatayo:
1. Kuhusiana na sharti la tohara ya mwili kwa ajili ya swala: Kilicho simuliwa na Ibn Abbas, kwamba Mtume (saw) amesema:
«تَنَزَّهُوا مِنَ الْبَوْلِ فَإِنَّ عَامَّةَ عَذَابِ الْقَبْرِ مِنْهُ»
“Jilindeni na mikojo kwani hakika adhabu jumla ya kaburi inatokana nayo”, imepokewa na Ibn Hamid. Na daaraqutni amesimulia kutoka kwa Abu Huraira aliyesema: Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) amesema:
«أَكْثَرُ عَذَابِ الْقَبْرِ في الْبَوْلِ»
“Adhabu nyingi ya kaburi ni kutokana na mikojo”.
2. Kuhusiana na sharti la tohara ya nguo kwa ajili ya swala, Mwenyezi Mungu (swt) asema:
﴿وَثِيَابَكَ فَطَهِّرْ﴾
“Na nguo zako, zisafishe.” [Al-Muddathir: 4], na yale ambayo Al-Bukhari amesimulia katika Swahih yake kutoka Asmaa binti Abi Bakr: Mwanamke mmoja alimuuliza Mtume wa Mwenyezi Mungu, “Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu! Tunapaswa kufanya nini, ikiwa damu zetu za hedhi zitaanguka kwenye nguo zetu?”, Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) akamjibu:
«إِذَا أَصَابَ ثَوْبَ إِحْدَاكُنَّ الدَّمُ مِنْ الْحَيْضَةِ فَلْتَقْرُصْهُ ثُمَّ لِتَنْضَحْهُ بِمَاءٍ ثُمَّ لِتُصَلِّي فِيهِ»“
“Ikiwa damu ya hedhi itaanguka juu ya nguo ya yeyote kati yenu, na aishike kisha alisuze kwa maji, kisha aswali na nguo hiyo …”
3. Hivyo basi, kuswali na nguo au mwili ulio na manukato yaliyo na pombe ndani yake ni swala batili.
Hii ndio rai yangu katika suala hili na Mwenyezi Mungu ni Mjuzi Zaidi na ni Mwingi wa Hekima.
Ndugu yenu,
Ata Bin Khalil Abu Al-Rashtah
19th Rabii’ Al-Awwal 1442 H
05/11/2020 M
Link ya jibu hili kutoka kwa ukurasa wa Amiri wa Facebook:
https://www.facebook.com/HT.AtaabuAlrashtah/posts/2790278647884808