Ukweli wa Kura ya Maamuzi ya Mradi wa Kujitoa kwa Uingereza (Katika Muungano wa Ulaya)!

بسم الله الرحمن الرحيم

Jibu la Swali
(Imetafsiriwa)

Swali

Bunge la Uingereza mnamo 16/1/2019 liliupigia kura mswada wa kutokuwa na imani na serikali ya May, lakini yeye akashinda: (Waziri Mkuu wa Uingereza Theresa May aliponea kushindwa mnamo Jumatano katika bunge la House of Commons kufuatia mswada wa kutokuwa na imani na serikali yake uliowasilishwa na chama cha upinzani cha Labour. Alishinda imani kwa wingi wa kura 325 dhidi ya 306 … matokea ya kura hizo ya mnamo Jumatano yanaonyesha kuwa takriban wanachama 100 wa Chama cha Conservatives waliopiga kura dhidi ya makubaliano mnamo Jumanne ya kujitoa huko kwa Uingereza, mnamo Jumatano walirudi na kupiga kura dhidi ya kutokuwa na imani na serikali … AFP 16/1/2019) Je, hili tunalifahamu vipi? Takriban wanachama 100 wa Chama cha May walipiga kura dhidi ya mradi wake huo wa kijitoa huku wakiuruhusu upinzani kushinda, ikipelekea kufeli kwa mradi huo wa May kwa kura 432 dhidi ya 202. Kisha Wabunge hao 100 walirudi na kupiga kura dhidi ya wapizani wa May, wakimruhusu May kushinda. Kana kwamba ni ugawanyaji dori! Na ni upi ufafanuzi wa uidhinishaji wa mwanzo wa kujitoa kwa Uingereza mnamo 2016, lakini sasa kabla ya kutabikishwa kwake kwa takriban miezi miwili, unakataliwa?! Allah awajazi kheri.

Jibu

Uingereza ni mahiri katika uovu na ujanja, na katika kupanga na kuakhirisha ili kufikia malengo yake. Ili kupata jibu, tunatathmini mambo yafuatayo:

Kwanza, tutataja baadhi ya yale tuliyoyataja katika makala yetu ya mnamo 5/7/2016 baada ya kura ya maamuzi ya 23/6/2016, yaani, takriban miaka miwili na nusu iliyopita, tulipotarajia yale yaliotokea katika kura ya sasa ya maamuzi ya Uingereza 15/1/2019:

[1- Kura ya maamuzi ilifanywa nchini Uingereza mnamo 23/6/2016 ya kubakia au kuondoka katika Muungano wa Ulaya. Matokeo yalikuwa takriban asilimia 52 kuondoka, ambapo hatimaye Waziri Mkuu Cameron alitangaza kujiuzulu kwake na kwamba serikali hiyo itabakia kwa miezi mitatu. Katika kampeni yake ya uchaguzi, Cameron aliahidi kuwa atafanya kura ya maamuzi kwa mujibu wa suluki ya Uingereza ya kukwepa kura ya maamuzi ili kufikia manufaa maalumu, kupitia kuutishia Muungano wa Ulaya na dola nyenginezo wanachama kwa ghasia za kisiasa na kiuchumi za azimio la kura hiyo ya maamuzi, endapo Uingereza itatoka katika Muungano huo.

2- Sera ya Uingereza ya kutishia kura ya maamuzi ili kupata maslahi kutoka kwa EU si jambo jipya bali imelifanya jambo hili tangu miaka ya mwanzo ya kuingia kwa Uingereza katika muundo wa Ulaya. Uingereza imekuwa mwanachama wa Jumuiya ya Kiuchumi ya Ulaya (EEC) tangu Januari 1973. Inaihifadhi sarafu ya “Pauni ya Sterling” na imesalia nje ya eneo la Schengen linalo wakilisha alama mbili kuu za hali maalumu ambayo Uingereza iliifurahia licha ya uanachama wake kwa EU. Imetumia fikra ya “kura ya maamuzi” kuhusu kubakia katika EU kama njia ya kuzitishia dola za Ulaya ili kupata maslahi zaidi kwa Uingereza ndani ya EU. Mnamo 1975 ilifanya kura ya maamuzi ili kuboresha hali za kubakia kwake ndani ya Muungano huo ambao Waingereza walipiga kura wakipendelea kubakia ndani ya EEC, na hivyo kura za maamuzi za Uingereza ili kupata malengo ya sera hiyo zikafuata kwa hali kama hizo, hata kama ni kwa malengo maovu! Chama cha Tory kilisonga mbele kijanja katika kura ya maamuzi ya mnamo 2016, na wanachama wake wakaendesha kampeni ili kubakia na kutoka wakati huo huo ndani ya Muungano huo!

3- Kwa kuichunguza sera hiyo ya chama tawala cha conservative ambacho Cameron anakiongoza kuhusiana na kadhia kura ya maamuzi iliotajwa, basi inaashiria kwamba Cameron alitarajia matokeo yake kutokuwa ya mwisho, kama vile kutoka sare, ili iwe ni jambo la kukubali au kukataa ili kuweko na mwanya wa marudio au kuyachukua matokeo hayo yasio ya mwisho kama nafasi kwa majadiliano mapya pamoja na EU. Ni kwa sababu hii ndio chama cha conservative chenyewe kilikuwa kikisimamia kampeni ili kubakia ndani ya Muungano pamoja na kampeni ya kujitoa kutokana nao. Kati ya kampeni zote hizi hakuna iliyokuwa makini kuhusu kubakia au kuondoka, mbali na kuwa zote mbili zilikuwa na umakinifu kuhusu kura hiyo ya maamuzi inayo wakilisha njia ya kufikia maslahi ya ziada kutoka EU. Kwa sababu hiyo, inatarajiwa kuwa Uingereza itasitisha kuondoka kwa muda mfupi na kwa hakika huenda kukarefushwa hadi miaka kadhaa. Hiyo ni ikiwa itaondoka huku ikiwa mahiri katika matumizi ya mbinu chafu na uhadaifu. Na kuhusiana na kile kilicho wazi na dhahiri kutokana na maoni, na yale ambayo vyombo vya habari vimetangaza kwa njia ya taarifa; yote hayo yanafanya kusita kwa mujibu wa utabikishaji wa kura hiyo ya maamuzi kutarajiwa zaidi, bali hata zaidi ya hayo kama kupindua na kugeuza hatua kuhusiana na kura ya maamuzi yenyewe (30 Ramadhan 1437 H – 05/07/2016 M)] Mwisho wa nukuu.

Pili: Yanayojiri sasa yanazungumza karibia yote tuliyo kwisha yasema kuhusiana na “mchezo wa kura ya maamuzi” na kucheleweshwa na kuzungushwa ili kufikia maslahi ya Uingereza, hata kama ni maovu. Haya yanathibitishwa kupitia kuyafahamu yafuatayo:

1- May amepokea kushindwa kukubwa katika bunge la House of Commons baada ya “makubaliano ya kujitoa Muungano wa Ulaya yaliyofikiwa kwa idadi kubwa kukataliwa, katika kushindwa kukubwa kabisa kwa serikali bungeni katika historia ya nchi hiyo … Mnamo Jumatano Wabunge 432 walipiga kura kukataa makubaliano hayo,” (Chanzo shirika la habari la BBC, 16/1/2019). Hii inamaanisha kuwa makubaliano hayo, ambayo yalitiwa saini ili kuitoa Uingereza nje ya Muungano wa Ulaya mnamo 29 Machi, hayatatabikishwa. Mazungumzo ya kujitoa hayakufuata miondoko ya desturi ya chama tawala cha Conservative badala yake wanachama 118 wa Chama cha Conservative walipiga kura bungeni dhidi ya makubaliano ya waziri mkuu, na kujiunga na vyama vya upinzani. (Huku ni kushindwa kukubwa kabisa katika Bunge la Uingereza tangu 1924 … matokeo yake ni kushindwa kubaya sana na bunge kwa serikali ya Uingereza katika enzi hizi za sasa … (Chanzo: CNN Arabic 15/1/2019)”.

2- Kiongozi wa Chama cha upinzani cha Uingereza cha Labour, Corbyn, alitangaza baada ya bunge kukataa kujitoa kwa ufalme huo kutoka katika Muungano wa Ulaya kwamba amewasilisha mswada wa kutokuwa na imani na serikali ya Theresa May ili ujadiliwe. Alisema: “Serikali hii imepoteza imani ya Baraza hili … Nataka kukujulisha, Bwana Spika, kwamba nimewasilisha mswada wa kura ya kutokuwa na imani kwa ajili ya majadiliano … Ninafuraha kuwa mapendekezo haya yatajadiliwa kesho” (Chanzo: RT Arabic, 15/1/2019), lakini matokeo ya kura hiyo yalimpendelea May kwa sababu wanachama 118 wa Chama cha Conservative walirudi kukipigia kura dhidi ya upinzani, na wakazuia kura ya kutokuwa na imani juu ya May, na hivyo “Waziri Mkuu wa Uingereza Theresa May mnamo Jumatano, 16/1/2019 akaponea kushindwa katika Bunge la House of Commons kufuatia kufeli kwa mswada huo wa kutokuwa na imani juu ya serikali yake uliosalimishwa na Chama cha Upinzani cha Labour, baada ya kushindwa kwake juu ya makubaliano ya kujitoa kwa Uingereza (Brexit). Lakini serikali yake ilishinda imani kwa kura 325 dhidi ya 306, ambapo ilisitisha kufanyika kwa uchaguzi mkuu mpya. Hii ndio mara ya kwanza kuwepo na kura ya imani juu ya serikali katika Bunge la House of Commons kwa miaka 26. Mara moja viongozi wa upinzani waliitisha mkutano naye kwa ajili ya mazungumzo juu ya kujitoa kwa Uingereza (Brexit) na kuanzia mnamo Jumatano.

Matokeo ya kura ya Jumatano yalionyesha kuwa karibu Wabunge 100 wa Chama cha Conservative waliopiga kura Jumanne dhidi ya makubaliano ya kujiondoa kwa Uingereza (Brexit) walirudi mnamo Jumatano na kupiga kura dhidi ya mswada wa kutokuwa na imani dhidi ya serikali.” (Chanzo: Agence France-Presse, mnamo 16/1/2019). Hivyo basi kuwa na fursa hadi Jumatatu, 21/1/2019) ili kuwasilisha “mpango mbadala”, na yeye ana machaguo kadhaa, kama vile ahadi ya kurudi katika majadiliano jijini Brussels, au kuomba kuakhirisha kwa tarehe ya kujitoa kwa Uingereza (Brexit), iliyopangwa kuwa 29 Machi 2019, au kujitoa pasi na makubaliano! Raisi wa Tume ya Ulaya alisema: “Natoa wito kwa Uingereza kufafanua nia zake haraka iwezekanavyo. Hakuna muda zaidi” (Chanzo: News site on 17/1/2019)

3- Hivyo basi, mchezo wa waamuzi wa Kiingereza uko wazi; badala ya kura ya kutokuwa na imani na May mnamo 16/1/2019, kwa sababu ya kufeli kwa mradi wake wa Brexit katika kura ya maamuzi ya mnamo 15/1/2019, May alishinda kura ya kuwa na imani ingawa kuanguka kwa mradi wake na kujishindia kwake imani ni kadhia mbili zanazo kinzana! Lakini endapo unajua ni kwa nini, inaongezea kizungumkuti zaidi!! Wabunge 118 wa Chama cha May walipiga kura dhidi ya mradi wa May, hivyo kuongeza sauti kwa upinzani uliopelekea kufeli kwa mradi wa May!  Lakini wanachama hao 118 wa chama cha May walirudi na kupiga kura dhidi ya upinzani, yaani dhidi ya kura ya kutokuwa na imani na May, na hivyo May akashinda kura ya kuwa na imani na hakuanguka kwa kuanguka mradi wake!

4- Kwa kuelewa hilo la juu, ni wazi kuwa kura ya maamuzi ya 2016 ilidhamiria kuihalalishia Uingereza kuboresha masharti ya uhusiano mpya pamoja na Muungano wa Ulaya. Hii ndio sababu May aliwaruhusu wanachama 118 wa chama chake kupiga kura dhidi yake pamoja na upinzani ili kuupotosha upinzani na kuupa nguvu ili mradi wake wa Brexit ufeli! Lau angetaka kura ya maamuzi ya 2016 kubakia imara, hangeruhusu idadi hii ya chama chake kupiga kura dhidi yake, lakini pindi kura ya kutokuwa na imani ilipofanywa, idadi hiyo ilifanywa kupiga kura dhidi ya upinzani ili May aokoke! Hii ni ili May aendelee kuutishia Muungano wa Ulaya ili kupata manufaa na maslahi na kuweka masharti kwa ajili ya uhusiano mpya pamoja na Ulaya. Uingereza haiwezi kuondoka kwa hatima kutoka Ulaya kama ambavyo haiwezi kubakia pamoja na sheria za Muungano zilizopo kwa sasa. Kujitoa kwa hatima kuna athari kubwa katika mshikamano wa Waingereza wenyewe, hususan Scotland na vile vile Ireland Kaskazini, na hivyo basi inataka kubakia lakini kwa masharti yake, au ikiwa hakuna hiari isipokuwa kuondoka, basi iwe na uwezo wa kupata maslahi kwa gharama ya Muungano huo!

5- Kwa upande wake, EU inaisihi UK “kufafanua nia zake” juu ya kujiondoa kwa Uingereza kutoka katika EU “haraka iwezekanavyo…” Alionya hatari ya kujiondoa kwa ghasia kwa kura hii.” (Chanzo: CNN Arabic 15/1/2019) Mwisho. Tayari tumeshataja katika makala yetu baada ya kura ya maamuzi ya 2016.

“Inaoneka Ulaya imeshatambua na kugundua michezo ya Uingereza na hivyo inataka kufanya mkataba usio rasmi ili kulinda maslahi yake juu ya msingi wa muundo wa Norway na Sweden kabla ya kuamua kufanya kazi pamoja na Kifungu cha 50 cha Mkataba wa Lisbon ili kuanza michakato ya kujitenga. Lakini, tofauti na Norway na Sweden, Uingereza inataka kuingia soko la Ulaya lakini iko dhidi ya matembezi huru ya watu, ambayo iliwakilisha kadhia kuu kwa wapiga kura wa Kiigereza. Merkel aliuondoa kwa nguvu uwezekano huo kwani matembezi huru ya watu ni mojawapo ya uhuru ambao EU inautukuza pamoja na uhuru wa ubadilishanaji bidhaa, huduma na rasilimali.

EU inauhisi ujanja wa Uingereza. Kwa hiyo, Raisi wa Tume ya Ulaya, Jean Claude Juncker, alisema: “Wacha niwe wazi kabisa, hatuwezi kuwa na majaribio ya kisiri ya kuiweka pembeni serikali ya Uingereza, ili yawe majadiliano ya siri, yasio rasmi” na akasema: “Nimetoa amri wazi kabisa kwa makamishna na wafanyikazi wote wa Tume; ni marufuku kuwepo majadiliano ya siri, hakuna majadiliano ya siri” (Chanzo: Evening Standard, 28/06/2016).

Merkel, Chansela wa Ujerumani, alielekeza ujumbe mkali jijini London alipo sema: “Yeyote anayetaka kuondoka katika familia hii asitarajie kubwaga majukumu yake yote na kisha kudumisha maslahi yake” (Chanzo: (DPA 28/06/2016)] Mwisho wa nukuu.

6- Lakini, Uingereza haijagundua utambuzi wa Muungano wa Ulaya wa nia za Uingereza kwa umakinifu bali inaendelea na mchezo wa kura ya maamuzi iliyopita ya mnamo 15-16/1/2019 unaofutilia mbali kura ya maamuzi juu ya mradi wa Brexit. Hauondoi imani juu ya May, mhandisi wa mradi huo, bali unafufua imani kwake ili kuanza mradi mpya na mpango mbadala! Hususan ili kutatua kadhia ya Ireland, katika hali ya kubakia au kuondoka kwake, na hivyo ndivyo ilivyo kuwa, vyombo vya habari viliripotia mipango ya May juu ya hili:

a- Waziri Mkuu wa Uingereza, Theresa May, aliliambia bunge mnamo Jumatatu, 21/1/2019, (mpango wake “badali”, baada ya Wabunge kukataa makubaliano yake pamoja na Muungano wa Ulaya, juu ya “Brexit”. Uingereza itaondoka katika Muungano wa Ulaya mnamo 29 Machi, bila ya makubaliano, endapo Wabunge hawatawezi kuakhirisha tarehe ya kujiondoa, au kufikia mpango mbadala unaoridhisha Tume ya Ulaya vile vile … Baada ya mipango ya May kukamilika juu ya jinsi ya kusonga mbele, Wabunge wataanzisha msururu wa marekebisho, yatakayo pigiwa kura, mnamo 29/1/2019. Mojawapo ya vipengee vyenye utata mkubwa katika makubaliano hayo kilicho kataliwa na bunge ni kifungu cha “kusimama nyuma”, dhamana ya usalama wa matembezi huru katika mipaka ya Ireland. Endapo Uingereza haitakubaliana na Muungano wa Ulaya juu ya mkataba wa muda mrefu wa biashara huru, gazeti la Sunday Times liliripoti kuwa May huenda akapendekeza mipangilio ya kujitenga pamoja na Dublin. Chanzo: AFP mnamo 21/1/2019) mwisho

b- Gazeti la The Telegraph lilinukuu duru za EU ambazo hakutajwa majina zikisema kuwa (matakwa ya May yanaendelea kupanuka kutoka kuunda mpaka wa muda wa kisheria hadi mpaka wa Ireland, ikiipatia Uingereza haki ya kujiondoa kipeke yake au kujifunga na mkataba wa biashara kabla ya 2021, ambayo inazuia utabikishwaji wa mipangilio maalumu kwa kadhia ya mipaka ya Ireland … Chanzo: … News of Libya on 21/1/2019)

c- (May alitangaza mnamo 21/1/2019 kuwa ananuia kurudi Brussels ili kujadili marekebisho ya makubaliano yake na viongozi wa Ulaya mwezi uliopita juu ya kadhia ya “kusimama nyuma”, ambayo yanapasa kuzuia kurudi katika kuasisiwa mipaka imara kati ya Ireland mbili hizo baada ya Brexit. May alisema: “Nitaendelea kukutana na wenzangu wiki hii – ikiwemo maafisa wa chama cha Democratic Unionist Party cha Ireland Kaskazini – ili kuona namna tutakavyojifunga na majukumu yetu,” ikiwemo kuzuia kurudi kwa mipaka, “katika njia ambayo italeta usaidizi mpana iwezekanavyo” katika Bunge la House of Commons. Aliendelea: Nitaonyesha tamati ya mazungumzo haya kwa Muungano wa Ulaya.” Nchi nyenginezo 27 za Muungano wa Ulaya zinafuatilia kwa karibu hatua inayofuata itakayochukuliwa na May … (Chanzo: France 24 / AFP mnamo 21/1/2019) Mwisho

d- May alifichua baadhi ya mabadiliko katika msimamo wake juu ya Brexit. Waziri mkuu huyo aliahidi “kuonyesha mnyumbuko zaidi” katika mazungumzo pamoja na bunge hilo na kufikia matakwa ya chama cha upinzani cha Labour ya kuhakikisha haki za wafanyikazi wa Uingereza na kuondoa hofu yote kuhusu kurudi kwa mipangilio mikali ya ushuru wa forodha baina ya Ireland Kaskazini na Jamhuri ya Ireland. Imepangwa kuwa Theresa May alilikabidhi Bunge la Uingereza mpango mpya juu ya masharti ya kujiondoa kwa UK kutoka Muungano wa Ulaya, baada ya Bunge mnamo 15/1/2019 kukataa mpango wa kwanza ulioafikiwa kati ya serikali ya May na Brussels. Bunge la Uingereza litapiga kura juu ya mpango mpya mnamo 29/1/2019. (Chanzo: RT Arabic 21/1/2019).

7- Tamati ni kuwa Uingereza haina sifa ya kujitolea katika makubaliano yoyote, lakini mabadiliko na mabadiliko kupitia mchezo wa kura ya maamuzi, na ni mahiri, mwerevu na mjanja katika jambo hili ili kufikia maslahi yake maovu. Jana, kura ya maamuzi ya Uingereza iliidhinisha mradi wa Brexit na leo kura ya maamuzi ya Uingereza imeidhinisha kutupilia mbali mradi wa Brexit! Hii ni ili kuutishia Muungano wa Ulaya kuleta marekebisho kwa mradi huo kwa gharama ya Muungano huo. Ingawa warasilimali Wamagharibi hawana vima vya kudumu, lakini Uingereza kupitia historia yake ya ukoloni imepata ujanja na uovu zaidi kushinda wengine. Uingereza haitaki kujiondoa kwa hatima kutoka katika Muungano huo lakini inataka mpangilio mwengine sio wa kujiondoa wala wa kubakia! Yaani kuondoka katika Muungano huo na wakati huo huo kubakia ndani yake! Kwa hivyo iendelee kunufaika kutokana na mahusiano ya kifederali bila ya kutii sheria za Muungano huo, lakini isipokuwa lile tu lenye maslahi kwake. Na kama ilivyotajwa, Chansela wa Ujerumani Angela Merkel, baada ya kura ya kwanza ya maamuzi na kuzuka kwa uakhirishaji wa Uingereza, alituma ujumbe wazi jijini London: “Yeyote anayetaka kuondoka katika familia asitarajie kubwaga majukumu yake yote na kisha kudumisha maslahi yake” (Chanzo: DPA 28/06/2016). Muungano wa Ulaya waweza kuifanya Uingereza kuteseka kutokana na matokeo endapo itasisitiza juu ya mradi wa Kwanza wa Brexit pasi na kurekebisha vifungu vyake vyovyote. Ni ima vikubaliwe na kutabikishwa na Uingereza Uingereza au Uingereza ijiondoe kutoka kwa Muungano huo. Endapo EU itafanya hivi, Uingereza itakuwa imeanguka ndani ya uovu wa kazi yake; endapo itakubali masharti ya Uingereza hapo Uingereza itaipa maamrisho hadi iimalize pasi na yenyewe kujua!

Hii ndio hali ya mataifa yanayo tabanni usekula kwa dola na mfumo wa kirasilimali. Yanachimbiana mashimo marefu ambapo kundi miongoni mwao au wote hutumbukia ndani yake. Hawana vima vinavyo wazuia au maadili yanayo wakataza, bali vita miongoni mwao ni vikali kama yalivyo mataifa mengine yasiyojifunga na hukmu ya Allah.

 (بَأْسُهُمْ بَيْنَهُمْ شَدِيدٌ تَحْسَبُهُمْ جَمِيعاً وَقُلُوبُهُمْ شَتَّى ذَلِكَ بِأَنَّهُمْ قَوْمٌ لَا يَعْقِلُونَ)

“Vita vyao baina yao ni vikali. Utawadhania kuwa wako pamoja, kumbe nyoyo zao ziko mbali mbali. Hayo ni kwa kuwa wao ni watu wasio na akili.” [Al-Hashr: 14].

Ulimwengu huu hautakuwa mahali pazuri na mateso yanayouzunguka hayataondoka isipokuwa sheria ya Allah isimamishwe katika utawala kupitia kusimamishwa Khilafah Rashida. Haitaeneza tu uadilifu na kheri katika miji yake, bali itasambaza uadilifu na kheri hii ulimwengu mzima biidhnillah.

 (وَلَتَعْلَمُنَّ نَبَأَهُ بَعْدَ حِينٍ)

“Na bila ya shaka mutajua habari zake baada ya muda.” [Sad: 88]

19 Jumada Al-Awwal 1440 H
25/1/2019 M