Jinsi ya Kuifahamu Hadith “Hakuna Kinachoirudisha Qadhaa Isipokuwa Dua”

بسم الله الرحمن الرحيم

 Jibu la Swali

Jinsi ya Kuifahamu Hadith

«لا يَرُدُّ الْقَضَاءَ إِلا الدُّعَاءُ»

“Hakuna Kinachoirudisha Qadhaa Isipokuwa Dua”

(Imetafsiriwa)

Swali:

Katika kitabu At-Tafkeer Al-Islami, ambacho ni mojawapo ya vitabu vilivyo tabanniwa, kinataja kuwa dua hairudishi qadar na haibadilishi qadhaa au elimu ya Mwenyezi Mungu (swt). Lakini kuna nususi kutoka katika Qur’an na Sunnah ambazo nionavyo mimi ni kana kwamba zinagongana na ufahamu huu; imesimuliwa kwamba Mtume (saw) amesema:

«لَا يَرُدُّ الْقَضَاءَ إِلَّا الدُّعَاءُ» “Qadhaa hairudishwi na chochote isipokuwa dua.”

Kuna Hadith nyinginezo nyingi zilizo na maana hii, na zinathibitisha kuwa dua hubadilisha qadar. Sasa vipi tutaoanisha baina ya yale yaliyotajwa katika kitabu hiki na nususi hizi? Mwenyezi Mungu akujazi kheri.

Jibu:

Nadhani unakusudia yale yaliyo elezwa katika kitabu At-Fikr Al-Islami, (Fikra ya Kiislamu) na sio At-Tafkeer Al-Islami ambapo ni kupitikiwa katika swali hili. Pia dosari nyingine katika swali hili kule kusema kuwa (ni mojawapo ya vitabu vilivyo tabanniwa); hakijatabanniwa na imetajwa katika faili la Idara chini ya ibara (vitabu ambavyo havijatabanniwa ambavyo vinachapishwa na Hizb ut Tahrir iwe vinabeba jina la Amiri au jina la mwanachama mwengine vya mitazamo mengine, na havisomeshwi ndani ya halaqa (duara maalumu za masomo) na kisha inataja miongoni mwa vitabu hivi: (Al-Fikr Al-Islami (Fikra ya Kiislamu)). Katika hali yoyote ile kama nilivyo taja mbeleni, inaonekana ulikuwa wakusudia yale tuliyotaja katika kitabu hicho: (Lakini ni lazima iwe wazi kuwa dua haibadilishi yale yaliyomo ndani ya elimu ya Mwenyezi Mungu, haizuii qadhaa, haiondoi qadar, na hakuna litokealo pasi na sababu yake, kwa sababu elimu ya Mwenyezi Mungu haina budi kutimia, na qadhaa ya Mwenyezi Mungu itatendeka pasi na kuepukika. Lau ingezuiwa kwa dua, basi haingekuwa qadhaa ya kiungu, na qadar yatoka kwa Mwenyezi Mungu; hivyo basi, haiondolewi kwa dua). Umesema kuwa hili linagongana na Hadith hii:

«إِنَّ الدُّعَاءَ يَرُدُّ الْقَضَاءَ» “Hakika dua huregesha qadhaa.” Na katika riwaya nyengine:

«لَا يَرُدُّ الْقَدَرَ إِلَّا الدُّعَاءُ» “Qadar hairudishwi na chochote isipokuwa dua.” Swali lako jinsi gani ya kuoanisha baina ya mgongano huu?

Kabla sijakujibu, nitakutajia baadhi ya mambo yanayo husiana kama utangulizi wa swali hili:

1- Hadhi ya dua katika Uislamu na majibu yake, kwa idhini ya Mwenyezi Mungu. Kumekuweko na aya na Hadith juu ya mada hii, ikiwemo:

– Mwenyezi Mungu (swt) asema:

[وَقَالَ رَبُّكُمُ ادْعُونِي أَسْتَجِبْ لَكُمْ إِنَّ الَّذِينَ يَسْتَكْبِرُونَ عَنْ عِبَادَتِي سَيَدْخُلُونَ جَهَنَّمَ دَاخِرِينَ] “Na Mola wenu Mlezi anasema: Niombeni nitakuitikieni. Kwa hakika wale ambao wanajivuna na kuniabudu Mimi wataingia Jahannamu wadhalilike.” [Ghafir: 60]

– Al-Hakim amesimulia katika Mustadrak yake kutoka kwa Abu Huraira (ra) kuwa amesema: Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) amesema:

«لَيْسَ شَيْءٌ أَكْرَمَ عَلَى اللَّهِ مِنْ الدُّعَاءِ» “Hakuna kitu kitukufu zaidi kwa Mwenyezi Mungu kuliko dua.” Ahmad amesimulia katika Musnad yake kutoka kwa Abi Saeed kuwa Mtume (saw) amesema:

«مَا مِنْ مُسْلِمٍ يَدْعُو بِدَعْوَةٍ لَيْسَ فِيهَا إِثْمٌ وَلَا قَطِيعَةُ رَحِمٍ إِلَّا أَعْطَاهُ اللَّهُ بِهَا إِحْدَى ثَلَاثٍ إِمَّا أَنْ تُعَجَّل لَهُ دَعْوَتُهُ وَإِمَّا أَنْ يَدَّخِرَهَا لَهُ فِي الْآخِرَةِ وَإِمَّا أَنْ يَصْرِفَ عَنْهُ مِنْ السُّوءِ مِثْلَهَا قَالُوا إِذاً نُكْثِرُ قَالَ اللَّهُ أَكْثَرُ» “Hakuna Muislamu yeyote anayeomba dua isiyokuwa na uovu wala kukata kizazi ndani yake isipokuwa Mwenyezi Mungu atampa kwa dua hiyo mambo matatu: ima atamjibu dua yake punde tu, au atamuekea Akhera, au atamuondolea kitu kibaya kutokana naye mithili ya kile anachokiomba.” Wakasema, “Basi tuzidishe kuomba.” Akasema, “ Mwenyezi Mungu ni mwingi zaidi wa kulipa.” Pia imesimuliwa na Al-Hakim katika Mustadrak yake kutoka kwa Abi Saeed (ra).

Dalili hizi zaonyesha kuwa Mwenyezi Mungu (swt) anapenda mja wake muumini amuombe na kuongeza kuomba kwake, na kwamba kuna jibu katika dua kwa moja katika hali tatu kama ilivyo katika Musnad ya Ahmad. Na majibu yananakiliwa katika Al-Lawh Al-Mahfudh; kila kitu kinachotokea hunakiliwa milele kama ilivyo onyeshwa katika dalili za qadar hapo chini.

2- Ikiwa kuna dalili ya kukatikiwa juu ya kadhia hii inayo ashiria hukmu maalumu na kuna dalili isiyo ya kukatikiwa iliyo na silsila (isnad) sahih katika kadhia hiyo hiyo inayo ashiria hukmu nyingine ambayo ndani yake kuna shaka (shubha) inayogongana na dalili hiyo ya kukatikiwa, basi katika hali hiyo dalili hizo mbili huunganishwa, kwa sababu kuzitumia dalili hizo mbili ni muhimu zaidi kuliko kuacha moja yao. Ikiwa itakuwa haiwezekani kuziunganisha dalili hizo basi dalili iliyo katikiwa ndio itachukuliwa na maana (diraya) ya dalili isiyo ya kukatikiwa itakataliwa kwa sababu silsila yake (sanad) ni Sahih, lakini ikiwa sanad ni dhaifu, itakataliwa kwa udhaifu wake.

3- Kutokana na dalili za qadar:

– Mwenyezi Mungu (swt) asema:

[وَكَانَ أَمْرُ اللَّهِ قَدَراً مَقْدُوراً] “Na amri ya Mwenyezi Mungu ni kudura iliyo kwisha kadiriwa” [Al-Ahzab: 38]. Maana ya

[قَدَراً] ‘Qadar ‘ hapa ni jambo lolote ambalo limejaaliwa milele, na maana ya

[مَقْدُوراً] Ni kuwa hakuna budi litatokea. Hivyo basi inamaanisha kuwa ni uamuzi uliopitishwa ambao ni lazima utokee.

[ومَا يَعْزُبُ عَنْ رَبِّكَ مِنْ مِثْقَالِ ذَرَّةٍ فِي الْأَرْضِ وَلا فِي السَّمَاءِ وَلا أَصْغَرَ مِنْ ذَلِكَ وَلا أَكْبَرَ إِلا فِي كِتَابٍ مُبِينٍ] “Na hakifichikani kwa Mola wako Mlezi chenye uzito hata wa chembe katika ardhi na katika mbingu, wala kidogo kuliko hicho wala kikubwa ila kimo katika Kitabu kilicho wazi” [Yunus: 61]

[عَالِمِ الْغَيْبِ لا يَعْزُبُ عَنْهُ مِثْقَالُ ذَرَّةٍ فِي السَّمَاوَاتِ وَلا فِي الأَرْضِ وَلا أَصْغَرُ مِنْ ذَلِكَ وَلا أَكْبَرُ إِلا فِي كِتَابٍ مُبِين] “… Mwenye kujua ya ghaibu! Hapana kinacho fichika kwake hata chenye uzito wa chembe tu, si katika mbingu wala katika ardhi, wala kilicho kidogo kuliko hivyo, wala kikubwa zaidi; ila vyote hivyo vimo katika Kitabu chake chenye kubainisha” [Saba: 3]

[مَا أَصَابَ مِنْ مُصِيبَةٍ فِي الأَرْضِ وَلا فِي أَنْفُسِكُمْ إِلا فِي كِتَابٍ مِنْ قَبْلِ أَنْ نَبْرَأَهَا إِنَّ ذَلِكَ عَلَى اللَّهِ يَسِيرٌ]… “Hautokei msiba katika ardhi wala katika nafsi zenu ila umekwisha andikwa katika Kitabu kabla hatujauumba. Hakika hayo kwa Mwenyezi Mungu ni mepesi” [Al-Hadid: 22]

– Pia kuna Hadith juu ya mada ya qadar au kuandikwa katika Al-Lawh Al-Mahfudh, ikiwemo:

Kutoka kwa Abu Huraira, asema, Mtume (saw) amesema:

«جَفَّ الْقَلَمُ بِمَا أَنْتَ لاَقٍ» “Kalamu imekauka baada ya kuandika yale utakayo kumbana nayo” [Bukhari]; yaani, yote utakayo yakabili ambayo kwayo milele yameandikwa.

Hadith ya Umar kutoka kwa Mtume (saw) kuhusu kuwasili kwa Jibril aliye uliza kuhusu Uislamu na Iman; Hadith hiyo inasema: “Nipe habari kuhusu Iman.” Yeye (Mtume) akajibu,

«أَنْ تُؤْمِنَ بِاللَّهِ وَمَلائِكَتِهِ وَكُتُبِهِ وَرُسُلِهِ وَالْيَوْمِ الآخِرِ وَتُؤْمِنَ بِالْقَدَرِ خَيْرِهِ وَشَرِّهِ» “Ni kumuamini Mwenyezi Mungu na malaika Wake na Vitabu Vyake na Mitume Yake na Siku ya Mwisho, na kuamini qadar kheri yake na shari yake.” [Muslim] yaani, kuamini kuwa Mwenyezi Mungu amekidhia kheri na shari kabla ya kuumba viumbe.

Kutoka kwa Jabir, amesema; Mtume (saw) amesema:

«لاَ يُؤْمِنُ عَبْدٌ حَتَّى يُؤْمِنَ بِالْقَدَرِ خَيْرِهِ وَشَرِّهِ حَتَّى يَعْلَمَ أَنَّ مَا أَصَابَهُ لَمْ يَكُنْ لِيُخْطِئَهُ وَأَنَّ مَا أَخْطَأَهُ لَمْ يَكُنْ لِيُصِيبَهُ» “Hatoamini mja (wa Mwenyezi Mungu) mpaka aamini qadar, kheri yake na shari yake, hadi atambue kuwa lile lilomsibu halikuwa ni lenye kumkosa, na kwamba lile lililomkosa halikuwa ni lenye kumsibu.” [Tirmithi]

Kutoka kwa Abi Abbas Abdullah ibn Abbas (ra) kuwa amesema: Siku moja, nilikuwa nimepanda farasi nyuma ya Mtume (ﷺ) pindi aliposema:

«يا غُلاَمُ، إِنِّي أُعَلِّمُكَ كَلِمَاتٍ، احْفَظْ اللَّهَ يَحْفَظْكَ، احْفَظْ اللَّهَ تَجِدْهُ تُجَاهَكَ، إِذَا سَأَلْتَ فَاسْأَلِ اللَّهَ، وَإِذَا اسْتَعَنْتَ فَاسْتَعِنْ بِاللَّهِ، وَاعْلَمْ أَنَّ الأُمَّةَ لَوْ اجْتَمَعَتْ عَلَى أَنْ يَنْفَعُوكَ بِشَيْءٍ لَمْ يَنْفَعُوكَ إِلاَّ بِشَيْءٍ قَدْ كَتَبَهُ اللَّهُ لَكَ، وَلَوْ اجْتَمَعُوا عَلَى أَنْ يَضُرُّوكَ بِشَيْءٍ لَمْ يَضُرُّوكَ إِلاَّ بِشَيْءٍ قَدْ كَتَبَهُ اللَّهُ عَلَيْكَ، رُفِعَتْ الأَقْلامُ وَجَفَّتْ الصُّحُفُ» “Ewe kijana! Hakika mimi nitakufundisha maneno, muhifadhi Mwenyezi Mungu Naye atakuhifadhi, muhifadhi Mwenyezi Mungu nawe utampata yuko mbele yako, unapo omba muombe Mwenyezi Mungu pekee; na unapo taka msaada taka msaada kwa Mwenyezi Mungu pekee; na ujue lau watu wote watakusanyika ili kutaka kukunufaisha kwa jambo kamwe hawawezi kukunufaisha isipokuwa kwa lile alilokuandika Mwenyezi Mungu; na lau wote watakusanyika kutaka kukudhuru wewe kwa jambo hawawezi kukudhuru isipokuwa kwa lile alilokuandikia Mwenyezi Mungu juu yako. Kalamu zishanyanyuliwa na kurasa zishakauka.”

4- Sasa tutazijadili Hadith hizi mbili; kuwa Dua hurudisha qadhaa na katika riwaya nyingine, hurudisha qadar:

Al- Hakim amesimulia katika Al-Mustadrak kutoka kwa Ibn Abbas, kutoka kwa Thawban, kuwa Mtume (saw) amesema:

«إِنَّ الدُّعَاءَ يَرُدُّ الْقَضَاءَ» “Hakika dua hurudisha qadhaa” Katika riwaya nyingine ya Al-Hakim kutoka kwa Abdullah Ibn Abi Al-Ja’d, kutoka kwa Thawban (ra), amesema; Mtume (saw) amesema:

«لَا يَرُدُّ الْقَدَرَ إِلَّا الدُّعَاءُ» “Qadar hairudishwi na chochote isipokuwa dua.” Al-Hakim amesema: (Hadith hii ina Sahih Sanad, lakini hawakuisimulia)

5- Kupitia kusoma kwa makini yale yaliyo tajwa juu ya qadar, hususan aya zilizo katikiwa katika maana, inafahamika kutokana na dalili hii kuwa hakuna chochote duniani au mbinguni isipokuwa Mwenyezi Mungu amekikidhia na kukinakili. Hakuna kinacho tokea isipokuwa tayari kimepasishwa na Mwenyezi Mungu na kimo ndani ya nakili yake. Kilicho kidhiwa hapana budi ni lazima kitokee, yaani, hakuna cha kusitisha na kuzuia qadar.

Inafahamika kutokana na Hadith hizo mbili zilizo tangulia kutajwa kuwa dua huzuia qadar, au qadhaa. Maana yake hapa ni sawa, hivyo hakuna tashwishi (shubha) inayogongana na dalili ya kukatikiwa juu ya qadar, na kama ilivyo tajwa juu, kwanza ni kuziunganisha Hadith hizo mbili zilizo na dalili za kukatikiwa, endapo itawezekana; isipo wezekana, basi maana (diraya) ya Hadith itakataliwa.

6- Hivyo basi, baada ya kulisoma jambo hili kwa makini, mimi nasema kwa tawfiq ya Mwenyezi Mungu:

A- Hadith:

«لَا يَرُدُّ الْقَدَرَ إِلَّا الدُّعَاءُ» “Qadar hairudishwi na chochote isipokuwa dua,” katika maana yake halisi ya neno (kurudishwa qadar) yaani kuiondoa kutoka katika Al-Lawh Al-Mahfudh, Hadith hii katika maana (diraya) hii inakataliwa, kwa sababu jambo lililo kidhiwa au kupasishwa limenakiliwa katika Al-Lawh Al-Mahfudh, na hapana budi ni lazima litokee na hakuna cha kulizuia lisitokee, yaani, haiwezekani kufutwa katika Al-Lawh Al-Mahfudh; hivyo basi, Hadith hii inakataliwa katika upande wa maana yake endapo haitawezekana kuunganishwa (pamoja na ile Hadith nyingine), na hapo dalili zilizo katikiwa juu ya qadar zitachukuliwa yaani, qadar ni lazima itokee na haiwezi kuzuiwa. Lakini kabla ya kuikataa maana (diraya) hii, juhudi ni lazima zifanywe ili kuziunganisha pamoja dalili zote za kukatikiwa na zisizo za kukatikiwa, kwa sababu kuzitumia dalili zote ndio kipaumbele zaidi kuliko kuiacha mojawapo.

B- Katika Usul al-Fiqh pindi inapokuwa haiwezekani kupata ukweli kutokana na kiashiria (qareena), kuzibika kwa maana halisi, ambayo hapa ni dalili za kukatikiwa juu ya qadar iliyo tajwa juu, hivyo basi ufahamu wa kimajazi wa Hadith ndio huchukuliwa endapo inawezekana kwa mujibu wa lugha. Hili hapa linawezekana; neno qadar au qadhaa katika Hadith hii liko katika maana yake ya kimajazi na linafahamika kwa matokeo yake yaani, athari yake; kwa maana nyingine ni kuwa, kinacho sababishwa nalo kutokana na fungamano lake. Hivyo, inataja sababu lakini maana ndiyo inayo kusudiwa, kama vile unapo sema: (ardhi ilikuza mvua) ukataja sababu (mvua) na kumaanisha natija ya mvua (mmea) na hapa qadar pia imetajwa lakini kinacho kusudiwa ni maana ya kimajazi, yaani, athari yake au ile natija yake, na hivyo basi kizuizi sio kwa qadhaa au qadar, bali kwa athari zake, kwa mfano, ikiwa qadhaa au qadar itamuangukia Muislamu, kama ugonjwa au kupoteza mtoto, au kupoteza pesa, na kupoteza biashara nk, hapo basi dua huzuia athari yake, kama ilivyo katika Hadith ya Al-Hassan Bin Ali (ra) aliposema: kuwa Mtume (saw) alinifunza kusema maneno katika Qunut ya Al-Witr:

«اللَّهُمَّ اهْدِنِي فِيمَنْ هَدَيْتَ… وَقِنِي شَرَّ مَا قَضَيْتَ…» “Ewe Bwana mwenye kuabudiwa kwa haki, niongoze mimi miongoni mwa uliowaongoza … na uniokoe mimi na shari za uliyo yakidhia.” Muumini, anapo muomba Mwenyezi Mungu katika dua na kuongeza dua ili amlinde kutokana na uovu wa qadhaa, basi Mwenyezi Mungu atamsahilishia athari yake na kumsaidia kuvumilia na kusubiri juu yake. Kisha Mwenyezi Mungu atampa utulivu katika maisha yake hata baada ya qadhaa hiyo kumuangukia juu yake. Yaani, Mwenyezi Mungu atamsahilishia qadhaa hiyo juu yake na kufanya wepesi athari yake. Ni kana kwamba dua yake imezuia qadhaa hiyo kimajazi. Yaani, Mwenyezi Mungu amemsaidia kuvumilia qadhaa hiyo na kumpa subira. Ni wanaume wangapi wanachomwa na miba, na kudhoofika na kutingishika? Na ni wanaume wangapi wanapitia majanga na ilhali ndimi zao zimelowa kwa Dhikr ya Mwenyezi Mungu; mtu humuomba Mwenyezi Mungu amlinde kutokana na uovu wa janga na athari yake, na huruzukiwa subira na mambo yake kunyooshwa kana kwamba kimajazi dua yake imezuia janga hilo.

Hivyo basi, inafahamika kuwa qadar haina budi na ni lazima itokee, lakini dua ya muumini yenye ikhlasi na imani itazuia athari yake juu yake, yaani, athari yake itasahilishwa na atasaidiwa kuivumilia na kuwa na subira kukabiliana nayo na kuufanya wepesi mzigo wa janga juu yake, na kisha kufurahia maisha kana kwamba janga hilo halikutokea. Yote haya yamenakiliwa katika Al-Lawh Al-Mahfudh; Mwenyezi Mungu ameyakidhia na kuyajua tangu jadi. Yaani, imenakiliwa katika Al-Lawh Al-Mahfudh, kwamba imepitishwa kuwa janga litamwangukia mja wake huyu na litatokea, na mja huyu atamuomba Mwenyezi Mungu dua ili amlinde kutokana na uovu wake. Mwenyezi Mungu (swt) atamjibu na kumsaidia kulivumilia na kuwa na subira kukabiliana nalo kana kwamba kimajazi halikumwangukia juu yake.

Hivi ndivyo namna Hadith inavyo fahamika. Hii ndiyo rai ninayoiona kuwa yenye nguvu Mwenyezi Mungu ndiye Mjuzi zaidi na Mwenye hekima zaidi.

7- Kwa maelezo zaidi, nitataja yafuatayo:

A- Katika kitabu changu (At-Tayseer Fi Usul At-Tafseer) kinaeleza:

[Kujibiwa kwa dua hakumaanishi kubadilika kwa qadhaa au yale yaliyo andikwa katika Al-Lawh Al-Mahfudh au katika elimu ya Mwenyezi Mungu, yaani, muitiko wa Mwenyezi Mungu haumaanishi kuwa Yeye (swt) hakujua kuhusu dua hiyo ya mja wake na kwamba Mwenyezi Mungu ataijibu, na hivyo basi haikunakiliwa katika Al-Lawh Al-Mahfudh, bali Mwenyezi Mungu anaijua na imenakiliwa tangu jadi. Qadar ni elimu ya Mwenyezi Mungu, yaani, kile kilicho andikwa katika Al-Lawh Al-Mahfudh na kila kitu ambacho kitatokea kimeandikwa ndani yake tangu jadi. Mwenyezi Mungu (swt) anajua kuwa mtu atamuomba dua. Ikiwa Mwenyezi Mungu amekidhia kujibu, imeandikwa kuwa mtu ataomba dua jambo kadha na kadha na kwamba hilo litakuwa kadha na kadha. Dua sio insha mpya isiyo kuwemo ndani ya elimu ya Mwenyezi Mungu au isiyo andikwa ndani ya Al-Lawh Al-Mahfudh, vilevile jibu. Bali yote ambayo yatatendeka yamenakiliwa ndani ya Al-Lawh Al-Mahfudh; Mwenyezi Mungu anajua yasiyo onekana na anajua ayafanyayo mja kwa kauli au kitendo, na kila kitu tayari kilikwisha andikwa tangu jadi. Dua inayo ombwa na mja inajulikana na Mwenyezi Mungu na imenakiliwa kama ilivyo. Vilevile jibu la Mwenyezi Mungu (swt) kama alitakavyo Mwenyezi Mungu (swt) limenakiliwa tangu jadi. Dua na jibu hilo haviko juu ya elimu ya Mwenyezi Mungu, bali vimenakiliwa katika Al-Lawh Al-Mahfudh kama vilivyo na namna vitakavyo tokea. Mwenyezi Mungu ni mjuzi wa yasiyo onekana na yanayo onekana

[لَا يَعْزُبُ عَنْهُ مِثْقَالُ ذَرَّةٍ فِي السَّمَاوَاتِ وَلَا فِي الْأَرْضِ] “… Mwenye kujua ya ghaibu! Hapana kinacho fichika kwake hata chenye uzito wa chembe tu, si katika mbingu wala katika ardhi…” [Saba: 3]

B- Imeelezwa katika Sharh As-Sunnah na Abu Muhammad Al-Hussein Al-Baghawi Ash-Shafi’I (aliye kufa 516 H): [(Abdul Wahid ibn Ahmad Al-Malihi alitwambia … kutoka kwa Abdullah Ibn Abi Al-Ja’d kutoka kwa Thawban, aliye sema: Mtume (saw) amesema:

«لا يَرُدُّ الْقَدَرَ إِلا الدُّعَاءُ» “Qadar hairudishwi na chochote isipokuwa dua” … Nikasema: Abu Hatim Al-Sajistani amesema (kuwa mtu anayedumu kuomba dua atakubali kuipokea qadhaa, kana kwamba imezuiwa)].

C- Imeelezwa katika “Murqat Al-Mafateeh Sharh Mishkat Al-Masabih” na Abu Al-Hassan Nur ud-Din Al-Mullah Al-Harawi Al-Qari (aliye kufa: 1014 H):

[Maneno Yake:

«لا يَرُدُّ الْقَضَاءَ إِلا الدُّعَاءُ» “Qadhaa hairudishwi na chochote isipokuwa dua” Qadaa’ ni jambo lililo kidhiwa … au alimaanisha kwa neno “kuzuiwa” kwa qadhaa ikiwa alimaanisha kuisahilisha na kulifanya jambo hilo kuwa jepesi, kana kwamba halijatumwa …]

Nataraji kuwa hii inatosheleza, na Alhamdulillah, Mola wa Walimwengu.

 

16 Rabii’ Al-Awwal 1441 H

Jumatano, 13/11/2019 M