Miaka 57 ya kujitawala: Bado tupo kwenye uwanja wa matatizo.

بسم الله الرحمن الرحيم

Habari na Maoni

Habari:Kila tarehe Mosi Juni, Kenya husherehekea siku kuu ya Madaraka, siku inayosheheni mbwembwe za kila aina pamoja na Makala mbalimbali yanayoangazia  tamaduni za Kenya na hatua za kimaendeleo ilizozipata  tokea kupata kwake  mamlaka ya kujitawala kutoka kwa wakoloni wa kiingereza.Tofauti na miaka mengine,sherehe za mwaka huu zimefanywa ikulu jijini Nairobi ili kujifunga na sharti la kukaa mbali kama hatua za kujikinga na maambukizi ya janga  la Corona.

Maoni:

Madaraka neno la Kiswahili linalomaanisha mamlaka, hivyo Juni Mosi husherehekewa kitaifa katika kukumbuka siku ambayo Kenya ilipata “mamlaka” ya kujitawala kutoka kwa wakoloni waingereza. Tarehe 27 May, mwaka 1963, mwanzilishi wa taifa la Kenya Jomo Kenyatta alisema:

“Tutajenga nchi ambayo kila raia atakua na mazingira ya kuendeleza vipawa vyake kikamilifu vyenye kulenga lengo kubwa ya kuunda jamii yenye usawa kwa wote. Hakutokuwa na hulka ya kuwapendelea wachache. Sote kwa pamoja tutahakikisha kila jamii fulani itakayofanyiwa ubaguzi au kupitia unyanyasaji kutoka jamii za walio wengi’’

Siku za kwanza tu za utawala wa Jomo Kenyatta, ahadi hii iligeuka kuwa vumbi hewani ambapo nchi ilipoanza kuonekanwa ikitumbukia kwenye mauaji ya kisiasa, khiyana za kisiasa na ufisadi wa kiwango cha juu miongoni mwa matatizo mengi. Mwito wa kutaka mabadiliko ukasikika tena mara hii ikiwa ni kutaka kubadilishwa kwa katiba! Hii ikizingatiwa kuwa katiba ya Kenya ya mwaka wa Kenya kupata uhuru ilikuwa imetungwa na wakoloni wenyewe ‘ katiba ya Lancaster House’ ambayo wakoloni wa Kiingereza ndio waliokuwa wakiitumia katika kutawala koloni za barani Afrika hivyo ikabadilishwa mwaka wa 1969. Na mwaka 2010, katiba ikabadilishwa upya kwenye mchakato ulioshuhudia ufujwaji wa pesa za umma na kusifiwa kwa mbwembwe kwamba ni mabadiliko makubwa, hata hivyo nchi ikawa bado inaendelea kushuhudia umasikini wa hali ya juu, elimu duni, hali mbaya ya huduma za afya na mapigano ya kikabila. Na kwa sasa hali bado ni yenye kutamausha huku nchi ikisherehekea miaka 57 ya kujitawala bado mfumu wake wa afya upo kwenye hali mbaya wakati kunakoshuhudiwa janga la Covid-19.

Huku raia wengi wasojua mambo wakiamini kwamba kupata uhuru ili ni jambo na fikra nzuri kwani Wakoloni ndio vyanzo vya matatizo ya Kenya, walichokosa kufahamu kihakika ni kwa hata suala lenyewe la ‘uhuru’ pia ni suala la kikoloni. Kuwa na uhuru au kujitawala hakukumaanisha Kenya ilijikomboa kwenye makucha ya ukoloni ambao kiuhalisia ulibadilisha tu rangi kutoka ule ukoloni mweupe kwenda kwa ukoloni mweusi. Kwa maneno mengine, wakoloni wa Kiingereza walidanya kuwa wanatoka mlangoni kisha wakarudi na dirishani kupitia mawakala wao comprador Bourgeoise( watawala weusi)! Yule aliekuwa ndiye kiini cha matatizo ya Kenya akajifanya ati ndiye mtoaji wa suluhisho. Kimaumbile hali hii ikawa matatizo yakawa ni yenye kutarajiwa kuendelea hata baada ya Kenya uhuru.

Jamii ya Kenya inahitaji Mfumo utakao badilisha maisha yao kimsingi. Kinachofanya Kenya kushindwa kutatua matatizo msingi ya umma ni kuegemea kwake mfumo wa kikoloni wa Kirasilimali uliojengwa juu ya akili ya mwanadamu na wala sio kwa wahyi kutoka MwenyeziMungu swt. Kwa hakika kwa serikali inayotekeleza mfumo bora wa Kiislamu, miaka 57 ni kipindi cha kutosha kufikia kwenye mafanikio makubwa. Ndani ya kipindi kifupi mno chini serikali ya kikweli iliokua huru, maendeleo makubwa yaliwezwa kuafikia na watawala halisi wa Kiislamu walioutabikisha Uislamu. Serikali iliokuwa na uwezo wa kufanya maamuzi yake pasina muingiliano wowete wa taifa jengine tofauti na hali ya ‘serikali zinazoendelea’ leo ambao hadi sasa bado zinachukuliwa kama mateka na mabwana zao wa kikoloni. Huyu hapa Umar Bin Khattab Khalifa wa pili, ambaye kwa miaka tu kumi na mbili na nusu ya utawala wake akapata ufanisi wa hali ya juu katika kila sekta ikiwemo ya kiuchumi ambapo aliweza kuwalipa mishahara raia wote wasojiweza ili wasiwe ombaomba.Kwa hakika utawala wake ulitegemea Uislamu uliomwezesha kufikia ufanisi huu wa hali ya juu. Kwa hivyo, suluhisho la kipekee litapatikana kwa serikali inayotekeleza Uislamu ambao ni mfumo ulio na utatuzi kutoka Mwenyezi Mungu ajuaye vyema maisha ya wanadamu kuliko yoyote yule.Mwenyezi Mungu anasema:

أَلَا يَعْلَمُ مَنْ خَلَقَ وَهُوَ اللَّطِيفُ الْخَبِيرُ

Oh Asijue Aliyeumba! Naye ndiye avijuaye visivyojulikana na vinavyojulikana

[Almulk: 14]

 

Imeandikiwa Ofisi Kuu ya Habari ya Hizb ut-Tahrir na Shabani Mwalimu

Mwakilishi kwa Vyombo Vya Habari Hizb ut-Tahrir Kenya

Juni Mosi, 2020.