Wale Walioondoka Katika Hizb na Kuchelewa kwa Nusra!

بسم الله الرحمن الرحيم

 Jibu la Swali
(Imetafsiriwa)

Swali:

Niwie radhi ikiwa swali hili litakuwa ni lenye kukera, hususan kipande cha pili cha swali hili, lakini limekuweko akilini mwangu kwa muda mrefu… Na kwa vyovyote vile, ikiwa nitapata jibu ni vizuri na ikiwa sitapata jibu basi pia ni vizuri, najua kuwa yule anayeulizwa ana uwezo mzuri zaidi kuliko anayeuliza katika kuamua dhurufu muwafaka za kutoa jibu… swali langu liko katika mafungu mawili:

Sehemu ya kwanza ni: Hizb imekuwa ikifanya kazi kwa muda wa zaidi ya miaka 60 na imekuwa ikifanya kazi ndani ya dhurufu ngumu, ni nadra kwa kundi lolote kuwahi kupitia katika dhurufu kama hizo kama vile Hizb, na sio wanachama wote wanaoweza kubeba amana hii na baadhi yao huondoka (katika Hizb) …Ni kwa nini hali zao hazizingatiwi na hivyo basi kuweza kuwapa nyudhuru badala ya kuwachukulia misimamo ya “kutowanyamazia”?

Sehemu ya pili ya swali: Je, hii miaka mingi pasi na kufikia lengo yamaanisha ukosefu wa ukakamavu katika utafutaji Nusra (usaidizi)?

Narudia yale niliyotangulia kusema mwanzoni kwamba natambua uzito wa swali hili, hususan sehemu yake ya pili… ikiwa kutakuwepo na jibu, basi itakuwa ni vizuri, na vilevile, ikiwa sitapata jibu basi pia itakuwa ni vizuri… nauliza na huku moyo wangu ukiwa umejaa mapenzi kwa Hizb na nauona ukweli wa fikra yake na njia yake. Ninalotafuta katika swali hili ni kheri pekee na wala si uharibifu au uasi… Na Allah ni mjuzi wa yanayohadaa macho na yale yaliyofichika vifuani. Wassalamu Alaikum Wa Rahmatullah Wa Barakatuh.

Jibu

Wa Alaikum Assalam Wa Rahmatullah Wa Barakatuh

Ndio, sehemu ya pili ya swali hili ni nzito; pengine mahali muwafaka pa kutoa jibu sio katika jibu lililochapishwa, lakini katika kikao. Lakini Allah awaangamize madhalimu wanyanyasaji wanaoliandama neno la haki na watu wake popote walipo, na kuwaruhusu watu waovu kufurahia uhuru wa kutembea.

Kwa vyovyote vile, hii ndio Sunnah ya walinganizi wa haki kuanzia Mitume na watu wema kati zama zote ambazo madhalimu, wanyanyasaji na ruwaibidha (wajinga) walitawala, na matokeo bora huwa kwa watu wema.

Siku za nyuma tulikabiliwa na swali kama hili kama mnong’ono au taarifa, kutoka kwa watu wanaouchukia Uislamu na watu ambao hawakuuliza kujua haki bali tu kuongeza uharibifu na kuwatumikia mashetani watu na wafuasi wao kwa ajili ya lengo la kidunia wanalolitafuta. Kamwe hatukutilia maanani kumjibu yeyote katika wao kwa sababu hawaulizi kwa ajili ya kujua haki na kunufaika kwayo, lakini kwa lengo la mjadala na kukanganya katika kauli ili kuzua fitna pasi na kutambua kwamba wao ndio waliotumbikia ndani ya fitna! Kwa hivyo hatukuyatilia maanani maswali yao.

Lakini katika swali lako nimeona ndani yake ikhlasi na njia nzuri ya uulizaji na kauli njema, kutokana na hili nitalijibu swali lako Allah akipenda, kwa yale yanayotosheleza ili kukupa ufahamu, hususan kwa sehemu ya pili ya swali hili pasi na kutoa ufafanuzi usio muhimu. Nasema kwa usaidizi wa Allah:

1- Jibu la sehemu ya kwanza ya swali:

Neno “kutowanyamazia” kama lilivyotumika katika swali, haliko wazi, na pengine limekusudiwa liwe katika hali maalumu za baadhi ya wale walioondoka, na sisi hatuwaonei huruma, na wala hatuwatilii maanani kutokana na kukosea kwao. Ikiwa hivi ninavyofahamu ni sahihi, kadhia ni kama ifuatavyo:

Tunaelewa kuwa mwanachama hawezi kuchukua mzigo wa kubeba ulinganizi kwa dhurufu fulani anazopitia, hususan katika zama hizi ambapo ulinganizi huu umezungukwa na msongamamo wa matatizo yaliyo jaa juu ya mengine, kwa hivyo mzigo wa ulinganizi huu huenda ukawa mzito na, hivyo basi, baadhi ya wanachama kuacha kubeba ulinganizi na kudhoofika mbele ya matatizo haya, na kughilibiwa na mapenzi ya dunia na starehe zake kuliko radhi za Allah na mapenzi ya Akhera. Ikiwa utamuuliza kwa nini umeondoka (katika Hizb), atasema kuwa dhurufu fulani hazikumwezesha kubeba ulinganizi na kwamba atajaribu kuzishinda ili arudi tena, Allah akipenda. Tunaelewa uhakika wa wanachama hawa, na kudumisha mahusiano mazuri nao na kuwaombea kwamba Allah awaongoze katika njia sahihi, na warudi kuubeba ulinganizi huu, na kufidia madhambi yao kwa kupuuza ulinganizi huu kwa matendo mema, kwani matendo mema hufuta matendo maovu kwa idhini ya Allah.

Ama kwa wale ambao sisi “hatuwaonei huruma na hatuwatilii maanani kutokana na makosa yao” na ndio ambayo unaiita katika swali lako kuwa ni misimamo ya “kutowanyamazia”, ni wale ambao walipotoka kutoka katika njia na kuondoka, na badala ya kumuomba Allah (swt) msamaha na kutubia na kubadilisha madhambi yao na kupotoka kwao kwa maneno na matendo mema; badala ya hilo walijengea hoja misimamo yao na kupotoka kwao kwa tuhuma nyingi za kirongo dhidi ya chama hiki, uongozi wake na wasimamizi (Mas’oul). Na wakaona ni rahisi kudanganya ilhali ni dhambi kubwa sana mbele ya Sharia ya Allah. Muslim amesimulia katika Sahih yake, akisema: Al-A’mash alitwambia, kutoka kwa Shaqiq kutoka kwa Abdullah, amesema: Mtume wa Allah (saw) amesema:

«…وَإِيَّاكُمْ وَالْكَذِبَ فَإِنَّ الْكَذِبَ يَهْدِي إِلَى الْفُجُورِ وَإِنَّ الْفُجُورَ يَهْدِي إِلَى النَّارِ وَمَا يَزَالُ الرَّجُلُ يَكْذِبُ وَيَتَحَرَّى الْكَذِبَ حَتَّى يُكْتَبَ عِنْدَ اللَّهِ كَذَّابًا»

“Ole wenu na urongo! Haki ya urongo hupelekea katika uovu na hakika ya uovu hupelekea katika Moto wa Jahannam. Na mtu hatawacha kusema urongo na kudumu na kusema urongo mpaka ataandikwa mbele ya Allah kuwa mrongo.”

Lakini, walizua na kudanganya! Hawaishi wala hawaruhusu kuishi, kama isemwavyo, lakini wanaanza kuchapisha kurasa nyeusi za urongo wa wazi wazi. Hawa ndio wale ambao “hatuwaonei huruma na hatuwatilii maanani kutokana na makosa yao”. Ama kwa wale walio wakweli, lakini huacha mzigo huu mzito kutokana na dhurufu zao, tunaelewa hali yao na kuzungumza nao vizuri na kuwasaidia tuwezavyo kuzishinda dhurufu hizo.

Hili ni tukio ambalo mimi nililishuhudia:

Nilipokuwa msimamizi (Mas’oul) katika baadhi ya nchi, nilipokea kutoka kwa Sheikh wetu wa pili, Allah awe radhi naye, ombi la kukutana na mmoja wa wale walioondoka na kujadili kurudi kwake, kwa kuwa siku za nyuma alikuwa miongoni mwa watu wazuri mno katika utambuzi na ufahamu, kama tunavyofahamu sisi. Kwa hivyo nikamwendea:

Nikasema mbona usirudi katika Hizb? Akasema, Ewe Abu Yasin: “Mimi sina nguvu ya kubeba mzigo huu mzito. Nilikamatwa na sikuweza kuvumilia siku chache, kwa hivyo nikakisaliti chama na kuondoka, kwa sababu nilitambua kwamba uwezo wangu ulikuwa dhaifu kushinda mzino huu mzito.” Ingawa sikufaulu kumshawishi kurudi tena, lakini alibakia kuwa mfuasi na wala hakukipinga chama hiki. Hivyo basi mtu mithili ya huyu ni mkweli, tunamuheshimu na kumtakia kila la kheri.

Ama kwa yule anayejengea hoja udhaifu wake kupitia kuwatuhumu wengine na kusema kuwa ameondoka kwa sababu ya Mas’oul fulani na fulani na kumtuhumu kimakosa, hata kumzulia urongo, na kudhani kuwa anafanya wema, badala ya kumuomba Allah amsamehe na kutubia kwa Allah, utamuona anaondoka katika Hizb akiwa amejaa chuki dhidi ya uongozi na kuuzulia urongo pasi na kumcha Allah, Al-Muntaqim Al Jabar. Watu kama hao walioondoka hawahitaji kupewa nyudhuru, lakini ndio, hatuwaonei huruma na wala hatuwatilii maanani kwa makosa yao.

2- Ama kwa sehemu ya pili swali hili:

Kabla nikujibu, nataka kutoa utangulizi kuhusu ombi la Mtume (saw) la Nusra (usaidizi):

Baada ya kifo cha Mama wa waumini, Khadija Allah awe radhi naye, ambaye alikuwa mfuasi bora wa Mtume (saw), Abu Talib alikufa, ammi yake Mtume (saw), aliyekuwa akimuhifadhi (saw) kutokana na madhara ya Maquraysh, na hiyo ilikuwa katika mwaka wa kumi wa Utume; mwaka huo uliitwa Mwaka wa Huzuni.

Kisha Allah akamkirimu Mtume wake (saw) kwa mambo mawili makuu: Isra’ na Mi’raj, na idhini ya kutafuta Nusra (usaidizi). Mtume wa Allah (saw) aliomba Nusra mara chungu nzima kutoka kwa Bani Thaqeef, Bani A’mir, Bani Shaiban, na Bani Hanifa… nk. lakini hawakumkubalia. Baadhi yao walimpa Mtume (saw) majibu mabaya na kumjeruhi, ikipelekea kumwaga damu yake.

Kisha baadaye yeye (saw) alimtuma Mus’ab Madina, ambaye Allah alimpa mafanikio na baadhi ya watu wenye nguvu miongoni mwa Maanswari walimuitikia na kuja Makkah katika msimu (wa hajj) na kutoa ahadi ya utiifu kwa Nusra, bay’ah ya pili ya Aqaba, na kisha Mtume wa Allah (saw) akaguria Madina na dola ikasimamishwa.

Swali ni: Je, Mtume wa Allah (saw) hakuwa mzuri/shupavu katika kuomba Nusra, ndio maana hakukubaliwa? Au Mus’ab alikuwa bora kumshinda Mtume wa Allah (saw) katika uombaji wa Nusra? Jibu bila shaka ni hapana kwani kila jambo lina wakati wake.

 (إِنَّ اللَّهَ بَالِغُ أَمْرِهِ قَدْ جَعَلَ اللَّهُ لِكُلِّ شَيْءٍ قَدْرًا)

“Hakika Allah anatimiza amri yake. Allah amejaalia kila kitu na kipimo chake” [at-Talaq: 3].

Na sisi, ndugu yangu, tunamfuata Mtume wa Allah (saw); tunafanya bidii na kujitolea kuomba Nusra, na tunaendelea na kutafuta Nusra kwa kheri na ubora ambao umo ndani ya uwezo wetu, tukimtegemea Allah (swt) katika mambo yote, kwa uchunguzi na kuthibitisha kadhia ili kuhakikisha utekelezaji wa amri za Allah kama inavyohitajika kwa idhini ya Allah.

Huku tunapoendelea katika njia hii, nyoyoni na akilini mwetu muna mambo mawili:

La kwanza ni kuwa licha ya kheri katika kazi hii ya kusimamisha Khilafah, ni Allah, Al-Qawi Al-Aziz ndiye anayeamua ni lini na wapi itasimamishwa.

La pili ni kuwa Sunnah ya Allah yahitaji kwamba Khilafah isisimamishwe kwa mikono ya wavivu, wala kwamba malaika wateremke kutoka mbinguni na kufanya kazi ya kusimamisha Khilafah kwa niaba yetu. Bali, itasimamishwa kwa mikono ya waumini wenye ikhlasi na wanaofanya kazi kwa bidii na kwa umakinifu; wale ambao pindi Allah akiwapa Nusra ya mapema watakuwa miongoni mwa wale wenye kushukuru, na ikiwa Nusra itacheleweshwa, watakuwa miongoni mwa wenye kusubiri na kutokata tamaa na rehma ya Allah, na hawatapuuza kazi ya kusimamisha hukmu ya Allah mpaka amri ya Allah ipatikane na hali wao wako katika hali hiyo.

Kwa kutamatisha:

1- Haimaanishi kuwa kuchelewa kwa Nusra katika kusimamisha Khilafah ni kwa sababu uombaji Nusra haufanywi vyema. Mtume (saw) aliomba Nusra mara kadhaa na hakuna aliyemuitikia, na yeye (saw) ni mzuri kwa amali zote, na Mus’ab, Allah awe radhi naye, alikubaliwa, ingawa amali yake si bora kumshinda Mtume (saw); hakika, kwa kila jambo lina wakati wake.

2- Na sisi, Allah akipenda, twatambua vitu kama vilivyo, na kuvifuata kwa njia bora zaidi. Na sisi twafanya kazi na nyoyo zetu zikiwa na imani kuwa Al-Aziz Al-Hakeem ataturuzuku lile ambalo Yeye (swt) aliwaruzuku ndugu zetu katika imani kabla yetu.

 (وَاذْكُرُوا إِذْ أَنْتُمْ قَلِيلٌ مُسْتَضْعَفُونَ فِي الْأَرْضِ تَخَافُونَ أَنْ يَتَخَطَّفَكُمُ النَّاسُ فَآوَاكُمْ وَأَيَّدَكُمْ بِنَصْرِهِ وَرَزَقَكُمْ مِنَ الطَّيِّبَاتِ لَعَلَّكُمْ تَشْكُرُونَ)

“Na kumbukeni mlipokuwa wachache, mkionekana wanyonge katika ardhi, mnaogopa watu wasikunyakueni, naye akakupeni pahala pazuri pa kukaa, na akakutieni nguvu kwa nusra yake, na akakupeni riziki nzuri ili mupate kushukuru” [Al-Anfal: 26].

Sio tu Yeye (swt) ataturuzuku makao lakini pia atatunusuru kwa ushindi, pamoja na kutubariki na mambo mazuri, na sifa njema zote ni za Mola wa walimwengu.
Kwa kumalizia, natuma salamu zangu kwa muulizaji swali, na kumuomba Allah amruzuku kheri.

Jumapili 10 Shawwal 1439 H
24/6/2018 M