بسم الله الرحمن الرحيم
Halaqa 1: Kuanza kwa Da’wah ya Mtume Muhammad (saw)
Baada ya wahyi kumshukia Mtume (s.a.w) na kukalifishwa kubeba Risala na kuamrishwa kuifikisha kwa kauli zake Taa’la:
ياأيها المدثر قم فأنذر
“Ewe uliejifunika funika simama uonye”
[Al-Muddaththir: 1 – 2]
وأنذر عشيرتك الأقربين, واخفض جناحك لمن اتبعك من المؤمنين, فإن عصوك فقل إني بريئ مما تعملون
“Na uwaonye Jamaa zako wa karibu, Na uinamishe bawa la unyonge kwa watakaokufuata miongoni mwa waumini, Wakikuasi basi sema Hakika yangu mimi niko mbali na mnayoyatenda”
[Ash-Shuaraa: 214 – 216]
يا أيها الرسول بلغ ما أنزل إليك من ربك وإن لم تفعل فما بلغت رسالته والله يعصمك من الناس إن الله لا يهدي القوم الكافرين
“Ewe Mtume!Fikisha uliyo teremshiwa kutoka kwa Mola wako Mlezi. Na usipofanya hivyo (ukafupisha katika ufikishaji na ukaficha kitu) Basi utakua hujafikisha Ujumbe wake (utakua umefanya dhambi kubwa) Na Allah atakulinda kutokana na watu. Hakika Mwenyezi Mungu hawaongozi watu Makafiri (hawaafiqii kwa kheri wala uongofu”
[Al-Maaidah: 67]
Akawa Rasulullah (s.a.w) anawalingania watu kwa dini ya Allah (swt), akiwa ni mwenye kupambana, anaiamini Haq anayoilingania, na kutangaza vita (mvutano wa kifikra) kwa mwekundu na mweusi; pasi na kupiga hesabu zozote kuhusu mazoea ya watu, dini zao, mila zao ma hata imani zao. Kwani yeye hakujali chochote isipokua Risala ya Uislamu pekee.
Rasulullah (s.a.w) aliwalingania watu kumuabudu Allah (swt) peke yake, kujifunga na Itikadi (Aqqedah) ya Uislamu peke yake na kuzitekeleza hukmu zake katika nyanja zote za kimaisha. Pia alipambana na makafiri na washirikina dhidi ya imani zao na kuzibomoa. Aliyafanya yote hayo ilhali akiwa mtu mmoja peke yake, hana msaidizi wala silaha, isipokua imani yake iliyomakinika ndani juu ya Allah (swt) na kwa Uislamu ambao anaulingania kikamilifu.
Da’wah yake Rasulullah (saw) ilipitia Nukta (Marhala) tatu msingi nazo ni
- Marhala ya Kwanza: kusomesha na kupeana Thaqafa
- Marhala ya Pili: maingiliano na Ummah
- Marhala ya Tatu: Kuchukua uongozi na kusimamisha Dola ya Kiislamu
Itaendelea katika UQAB Toleo la 6; In Shaa Allah