Njia ya Mtume (saw) Kuleta Mageuzi

بسم الله الرحمن الرحيم

Halqa 16: Safari ya Mtume (saw) Kwenda Twaif Kutafuta Nusra Na Hifadhi Kutoka Kwa Thaqif

Ndugu watukufu, Tunaendelea na silsila ya halaqat za fiqhi ya sira Nabawiyah, na halqa ya 16 itakuwa kwa anwani: Mtume (saw) kuenda Twaif akitafuta Nusra na hifadhi kutoka kwa Thaqif.

Asema ibn Is’haaq: Alipokufa Abu Twalib, Maqureysh walimuudhi Mtume (saw) maudhi ambayo hakuyapata katika uhai wa Abu Twalib.

Akatoka Mtume (saw) kwenda Twaif kutafuta Nusra na hifadhi, na huku anamatumaini wamkubali na alichowajia nacho kutoka kwa Allah Taa’la, akawaendea akiwa peke yake, wakamjibu majibu mabaya kama utakavyoona mbeleni…!!

Na hapa panahitajika ufahamu mzuri, na tuzingatie mazingatio ya hali ya juu, na tunafahamu kuwa mbeleni tumeyagusia haya katika mazungumzo ya utafutaji wa Nusra, na tunarudia kwa mara ya pili ili iwe mkokotezo, nayo ni kuwa utafutaji wa Nusra inatakiwa iwe katika hali ya usiri mkubwa. Kwa sababu hiyo Rasul (saw) alikuwa anaenda peke yake ama na mmoja katika maswahaba zake ili watafute Nusra, ambayo inamaanisha usiri. Hii kazi haitakiwi mwengine ajue asokuwa katika viongozi…!!

Na alipofika Rasul (saw) ardhi ya Twaif akakusudia kipote miongoni mwa Thaqif ambao ndio mabwana wao na watukufu wao, nao ni ndugu watatu: Abdu Yalayl, na Mas’ud, na Habib, wakiwa na mwanamke mkureysh, akakaa nao na akawalingania kwa Allah, akawaelezea aliowajia nayo ya kumnusuru yeye na Uislamu, na kusimama pamoja naye kwa atakayemkhalifu katika jamaa zake.

Akasema mmoja wao: “Mimi nitaziiba nguo za Kaa’bah iwapo Allah amekutumiliza na jambo lolote…!!” Na akasema mwengine: “Kwani Allah ameshindwa kutuma mwengine asokuwa wewe…!!!?” Akasema wa tatu: “Wallahi sitozungumza na wewe baada ya kikao changu hiki kabisa; ikiwa wewe ni Mtume kama unavyosema, wewe unautukufu mkubwa na haki zaidi kuliko kusemeshwa na mimi!! Na ikiwa unasema uongo dhidi ya Allah, basi wewe ni muovu zaidi kuliko kusemeshwa na mimi!! Na haitakiwi mimi nikuzungumzishe!!” Akasimama Rasul (saw) ilihali amekata tamaa na kheri ya Thaqif, akawaambia: “Ikiwa ndio hivyo mumeamua kufanya basi nifichieni!!”

Basi hawakulifanya hilo, bali waliwatuma wajinga wao na watumwa wao, wamtukane na kumpigia kelele mpaka wakamkusanyikia watu, wanamcheza shere Mtume (saw) wakamkalia safu mbili katika njia wakiwa wamebeba mawe, ikawa Mtume (saw) kila anapo nyanyua mguu wanampiga kwa mawe huku wanamcheza shere na kumdhalilisha…!!

Alipowaondokea (saw), alikwenda katika ukuta wa shamba lao, akaja katika mti wa mzabibu akakaa chini yake ilihali ni mwenye taabu na maumivu, na miguu inachuruzika damu, kumbe katika shamba kuna Utbah na Shaibah watoto wa Rabia’h.

Alipowaona alichukia kuwaendea kwa kujua uadui wao kwa Allah na Mtume wake, na watoto wa Rabiah walikuwa wakimtizama, na wanaona wanachokifanya wajinga wa Twaif. Alipotulia Rasul (saw), akaanza kumnog’oneza Mola wake na kuomba kwa Dua ambayo inazifungua nyoyo, na kurusha akili:

((EE MOLA NASHTAKI KWAKO WEWE UDHAIFU WA NGUVU ZANGU, NA UCHACHE WA HILA ZANGU, NA UDHALILI WANGU KWA WATU, EE MWENYE SIKITIKO KULIKO WENYE SIKITIKO, WEWE NDIE MOLA WA WANYONGE, NA WEWE NI MOLA WANGU, NI KWA NANI UNANITEGEMEZA MIMI? JE NI KWA ALIYE MBALI AMBAE ATANIKUNJIA USO AMA ADUI ULIYEMTAWALISHIA AMRI YANGU? IKIWA HUKUNIKASIRIKIA BASI MIE SIJALI!! LAKINI AFIA YAKO NDIO KUNDUFU KWANGU, NAJILINDA NA NURU YAKO AMBAYO IMEANGAZA GIZA, NA YAKATENGENEA KWAYO MAMBO YA DUNIA NA AKHERA, KULIKO KUTEREMKIWA NA HASIRA ZAKO AMA KUPATWA NA HASIRA ZAKO, KWAKO WEWE NDIO MAREGEO MPAKA URIDHIE, NA HAMNA PINGAMIZI WALA NGUVU ILA KWAKO))

Mtume (saw) alifanya bidii kwa kila alichoweza, na kwa kila nguvu kutoka kwa Allah, na Mtume (saw) hakubakia na chochote isipokuwa Nguvu za Allah Tabaraka wa Taa’la ambazo hakuna nguvu inayoweza kulinganishwa nayo…!!

ومن يتوكل على الله فهو حسبه

“Na anayemtegemea Allah basi Yeye atamtosheleza” [Twalaq: 3]

Shayba na Utbah vijana wa Rabia’h walipoona yaliompata Rasul (saw) waliguswa na huruma ya uzazi, wakamuita kijana mfanyikazi wao Mnaswara anaitwa: Addas, na wakamwambia: “Chukua hizi zabibu, weka kwa kibakuli, kisha umpelekee yule mtu, umwambie ale”, Addas akafanya alivyoamrishwa. Akaenda na kuweka mbele ya Mtume (saw) kisha akamwambia: “Kula”, Mtume (saw) alipoweka mkono wake alisema: Bismillah, kisha akala. Addas akamwangalia Mtume usoni kisha akasema: “Wallahi haya maneno hawayasemi kwa watu wa mji huu”, Mtume (saw) akamwambia: “Kwani wewe ni wa mji gani ewe Addas?” Akasema: “Mie Mkiristo, na mimi ni mtu wa Ninawa”, Akasema Mtume (saw): “Ni katika mji wa mtu mwema Yunus bin Mattaa” Addas akasema: “Umemjuaje Yunus bin Mattaa?” Akasema Rasul (saw): “Huyu ni ndugu yangu alikuwa Mtume na mimi ni Mtume”. Addas akamwangukia Mtume (saw) huku anakibusu kichwa chake, mikono yake na miguu yake…!!

Akasema mmoja katika watoto wa Rabia’h akimwambia mwenzake: “Ashamharibu kijana wako”, aliporudi Addas walimwambia: “Ole wako ewe Addas! Unanini mbona wambusu huyu bwana kichwa chake, mikono yake na miguu yake…??!!” Akasema, “Ewe bwanangu hakuna katika hii ardhi kitu bora kumliko huyu…!! Amenipa khabari ya jambo hakuna alijuaye isipokuwa nabii…!!” Wakamwambia, “Ole wako ewe Addas, asikuondoe katika dini yako, kwani dini yako ni bora kuliko yake…!!”

Ndugu watukufu tutakomea hapa twataraji kukutana tena katika halqa mpya ya msururu wa halaqaat za njia ya Mtume (saw) kuleta mageuzi. Na tunawakumbusha udharura wa kusambaza hii silsila kwa marafiki zenu na vipenzi vyenu kwani amesema Mtume wenu (saw):

الدال على الخير كفاعله

“Mwenye kujulisha jambo la kheri (kwa ujira) ni sawa na kama aliyelifanya”

Pokeeni maamkuzi yetu Assalam Alaykum

Itaendelea katika UQAB Toleo 20…In Shaa Allah.