بسم الله الرحمن الرحيم
Halaqa 2: Nukta ya Kusomesha na Kujenga Thaqafa
Tulisema hapo Awali kuwa Da’wah ya Mtume صلى الله عليه وسلم imegawanyika katika nukta (marhala) tatu. Kuhusu nukta (Marhala) ya kwanza imejumuisha kusomesha na kujenga thaqafa kwa ajili ya kufikia shabaha mbili nazo ni:
- Kujenga Shakhsiya ya Kiislamu
- Kuandaa kundi (chama) litakalobeba Da’wah
Makkah ikawa ndio nukta kianzio ambayo ilipatikana kwayo Halaqa ya kwanza Mtume (saw) akafanya kazi nao kuleta mageuzi. Alianza Mtume (saw) Da’wah yake kwa Jamaa zake wa karibu na watu wake wa nyumbani kisha kwa Qawmu yake. Wakasilimu waliosilimu,
kisha akawa anawapa Thaqafa waumini. Na kuwasomesha kilichoteremka katika Qur’an, akiwa mbali na macho ya mushrikina.
Mtume (saw) alikuwa akikutana na maswahaba zake (ra) kwa siri katika nyumba ya Arqam Ibnu Abi Arqam (ra) au wakati mwingine katika mapango ya Makkah usiku wa kiza ama mchana wakati wa jua kali. Akawa katika Thaqafa anayowapa anachunga mambo mawili msingi:
Kwanza: Kujenga Aqeedah (Itikadi) ya Uislamu katika nafsi zao; ili wapate ufahamu wa ndani katika kuifahamu na kuimakinisha ndani ya nafsi zao misingi ya Aqeedah (Itikadi) ya Uislamu, ili asiweze yoyote kuing’oa.
Pili: Kujenga katika maswahaba zake (ra) Shaksiyyah (Muonekano) ya Kiislamu na kumakinisha ndani yao Aqliyyah na Nafsiyyah ya Kiislamu ili mfumo wa Kiislamu uwe ndio mwili wao, wawe ni majeshi ya Allah (swt) wanaotii Amri zake, wanao wabebea watu risala ya uongofu na nuru ya Uislamu. Hatimaye waweze kuwa na uwezo wa kuwafahamisha na kuwakinaisha wengine. Maanake wao watakua wabebaji Da’wah na ndio wanao uongoza Ummah. Kwa sababu hiyo walihitajika sana wawe ufahamu wa ndani na uweza wa kuwalingania watu kwa dini ya Allah (swt).
Mtume (saw) hakuficha Da’wah japo alificha muundo wa kundi/chama kwani alikua akilingania kwa dini ya Allah (swt) mchana wazi wazi na huku akiwasomea watu wake:
ياأيها الناس إني رسول الله إليكم جميعا)
“Sema: Enyi watu! Hakika mimi ni Mtume kwenu nyinyi nyote, niliye tumwa na Mwenyezi Mungu Mwenye Ufalme wa mbingu na ardhi. Hapana mungu ila Yeye anaye huisha na anye fisha. Basi muaminini Mwenyezi Mungu na Mtume wake asiyejua kusoma na kuandika, ambaye anamuamini Mwenyezi Mungu na maneno yake. Na mfuateni yeye ili mpate kuongoka”
[Al-A’raaf: 158]
Aliendelea na Da’wah yake tokea siku ya Kwanza kama alivyopokea Bukhari kutoka kwa Ibn Abbas (ra) asema; ilipoteremka:
وأنذر عشيرتك الأقربين
“Na uwaonye jamaa zako walio karibu nawe”
[Ash-Shu’araa: 214]
Mtume (saw) alipanda juu ya Swafaa na akawa anaita: “Enyi Baniy Fihri! Enyi Baniy Adiyyi!” mpaka wakakusanyika Maqureysh wakijumuisha Abu Lahab, hata mtu ambaye hakuweza kutoka alituma mjumbe akatizame kuna nini. Kisha Mtume (saw) akawaambia: “Je mwaonaje lau nitawaambia kua nyuma ya hili jabali kuna maadui wamekuja kuwapiga vita, Na wanataka kuwashambulia mtakua ni wenye kunisadikisha?
Wakasema: Ndio, hatujapatapo uongo kutoka kwako! Mtume (saw) akaendelea kuwaambia: Basi mimi bi muonyaji kwenu kwa adhabu kali. Akasema Abu Lahab: Maangamivu yakushukie mchana wote huu! Kwa sababu hii ndio umetukusanya hapa? Ikateremka:
تبت يدا أبي لهب وتب
“Imeangamia mikono ya Abu Lahab, na na yeye pia ameangamia.”
[Al-Masad: 1]
Mtume (saw) akafanya Makkah ndio sehemu kianzilio kwani hakutoka katika nukta (marhala) ya kwanza ambayo iliendelea kwa muda wa miaka mitatu (3). Hatimaye Allah (swt) akamuamrisha kudhihirisha Kundi (Chama) lake na harakati yake kumwambia:
فاصدع بما تؤمر واعرض عن المشركين انا كفيناك المستهزئين الذين يجعلون مع الله الها آخر فسوف يعلمون
“Basi wewe yatangaze uliyoamrishwa, na jitenge na washirikina”
[Al-Hijr: 94]
Kwa maana Mtume (saw) alitoka wazi kwa kudhihirisha Amri ya Mola wake wala hakujali wanayoyasema mushrikina akiwa na hakika Mola wake atamkinga na shari za maadui zake na wanaomcheza shere. Kwa kauli hiyo akatoka Mtume (saw) na maswahaba zake (ra) wakiwa katika safu mbili wakielekea Ka’bah kwa mpangilio ufuatao:
Safu ya Kwanza ikiongozwa na Hamzah bin Abdul Mutwalib (ra) na
Safu ya Pili ikiongozwa na Umar ibn Khatwab (ra).
Wakafika hapo mbele ya macho ya mushrikina na ikawa kitendo cha kutoka wazi kikawa ndio mwanzo wa nukta (marhala) ya pili ambayo ni nukta ya maingiliano (tafaul) na Ummah waziwazi.
Itaendelea katika UQAB Toleo 7…In Shaa Allah.