Njia ya Mtume (saw) Kuleta Mageuzi

بسم الله الرحمن الرحيم

Halaqa 5: Kumrai/Kumbembeleza Mtume (saw) awache Da’wah

Hapo awali tulisema kuwa Maquraysh walitumia mbinu nne dhidi ya da’wah ya Mtume (s.a.w). Katika Halaqa hii tutaangazia mbinu ya kwanza nayo ni kumbembeleza Rasulullah (saw) awache da’wah.

Katika harakati za kujaribu kumzuia Mtume (saw) awache da’wah, Maquysh waliamua kumtuma Abal Waleed Utbah bin Rabia kama balozi kwa Mtume (saw) ambembeleze na akawa anamwambia:

“Ewe Muhammad hakika wewe unajua kwetu sisi una nafasi katika  nasaba,na ni wa kati na kati (unaetambulika) katika  jamaa,na hakika watu  wanaona kuwa wewe umekuja na jambo kubwa. Umeutenganisha umoja wao, na ukawafanya wajinga werevu wao, na ukaaibisha miungu yao na dini yao ukawakufurisha waliotangulia katika wazee wao.Hakika wamekusanyika watu watukufu katika jamaa zako, nao wamekubaliana nikuelezee mambo,uyaangalie, huenda ukakubali miongoni  mwayo baadhi yake ama ukapendezwa na yote.”

Mtume (saw) akamwambia Utbah: “Sema ewe Abal Waleed,mimi nasikia.”

Akasema Utbah:

“Ewe mtoto wa ndugu yangu,ikiwa unataka kwa haya uliokuja nayo mali tutakukusanyia mali mpaka uwe mwenye mali nyingi zaidi yetu! Na ikiwa wataka cheo tutakufanya wewe ndiye bwana wetu mpaka tusikate shauri/maamuzi kando na wewe. Na ikiwa wataka ufalme tutakufanya uwe mfalme wetu. Na ikiwa haya yanayokujia ni ndoto za kishetani,huwezi kujikinga nazo nafsi yako tutakutafutia tiba na tutoe mali yetu mpaka tukupoze au tushindwe. ”

Utbah alipomaliza kusema; Rasulullah (saw) akamuuliza: “Ushamaliza ewe Abal Waleed?” Utbah akajibu “ndio”. Mtume (saw) akamwambia: “Basi nisikilize nami.”

Akajibu Abal Waleed: “Nitakusikiliza…”

Rasulullah (saw) akasema yafuatayo:

حَم ، تنزيلٌ مـِنَ الرَّحمَن ِالرَّحيم ِ، كِتابٌ فـُصِّـلـَتْ آيَاتـُهُ قـُرآنا ً عَرَبيَّا ً لِقـَوم ٍ يَعلمُونَ ، بـَشيرا ً وَنذيرا ًفأعْرَضَ أكثرُهُمْ فـَهُمْ لا يَسمَعُونَ ، وَقـَالـُوا قـُلـُوبُنا فِي أكِنـَّةٍ مِمَّا تـَدعُونـَا إليهِ وَفي آذانِنـَا وَقر ٌوَمِنْ بَينـِنـَا وَبَينـِكَ حِجَابٌ فاعمَـلْ إنـَّـنـَا عَامِلـُونَ

H’a Mim. Uteremsho huu umetoka kwa Mwingi wa rehema, Mwenye kurehemu. Hichi ni Kitabu kilicho pambanuliwa Aya zake, cha kusomwa kwa Kiarabu kwa watu wanaojua. Kitoacho khabari njema, na chenye kuonya. Lakini wengi katika wao wamepuuza; kwa hivyo hawasikii. Na wakasema: Nyoyo zetu zimo katika vifuniko kwa hayo unayo tuitia, na masikio yetu yana uziwi. Na baina yetu na wewe lipo pazia. Basi wewe tenda, nasi tunatenda.

[Fussilat: 1 – 5]

Kisha Mtume (saw) akaendelea kumsomea Suratul Fussilat na alipoisikia Utbah alinyamaza kuisikiliza na akaiegemeza mikono yake nyuma akimsikiliza Mtume (saw). Mtume (saw) alikomea katika Aya ya sajdah. Nayo ni kauli yake Allah (swt):

وَمِنْ آياتِهِ الليلُ وَالنـَّهارُ وَالشمسُ وَالقمَرُ لا تـَسجُدُوا لِلشمس ِوَلا لِلقمَر ِوَاسجُدُوا للهِ الذي خـَلقـَهُنَّ إنْ كـُنتـُمْ إيَّاهُ تعبُدُونَ

Na katika Ishara zake ni usiku na mchana, na jua na mwezi. Basi msilisujudie jua wala mwezi, bali msujudieni Mwenyezi Mungu aliye viumba, ikiwa nyinyi mnamuabudu Yeye tu.

[Fussilat: 37]

Mtume (saw) baada ya kusujudu kisha akamwambia: “Umesikia yale uliyoyasikia, basi ni wewe na hayo uliyoyasikia.”

Baada ya hapo Utbah akasimama na kuelekea kwa watu wake. Watu wake walipomuona Utbah wakawa wanaambiana kuwa tunaapa na Allah hakika amewajieni Abal Waleed kwa uso ambao hakuenda nao. Alipokaa nao wakamuuliza:”Ni kipi kilicho nyuma yako ewe Abal Waleed?  akajibu,”Nyuma yangu hakika nimesikia maneno,WALLAHY sijasikiapo mfano wake.WALLAHY si mashairi,wala uchawi wala ukuhani…!!Enyi mkusanyiko wa Maquraysh,nitiini mimi na munibebeshe mimi jukumu hili na muondoke kati ya huyu mtu na kati ya yale aliyonayo,mwacheni.WALLAHY ,itakua kwa maneno niliyoyasikia kwake, khabari kubwa.Waarabu wakimsibu basi itakua mumetoshelezwa na wengine. Na akiwashinda Waarabu,basi ufalme wake ni ufalme wenu na izza yake ni izza yenu,na mutakua ni wenye saada zaidi kupitia  kwake…”

Baada ya hapo wakaenda Maquraysh kwa ammi yake Mtume (saw), Abu Taalib ili amzuie Rasulullah (saw) na da’wa ili awaridhishe Maquraysh na mabwana wao. Basi haikua kwa Mtume (saw) ila alimpa majibu ambayo kwamba hayakubali maelewano wala suluhisho la kati na kati na kuwajibu:

“Ewe ammi,WALLAHY lau wataeka jua katika mkono wa kulia na mwezi katika mkono wangu wa kushoto ili niwache hili jambo sitoliwacha mpaka Allah alidhihirishe ima nife”.

Kisha Maquraysh wakamtaka Mtume (saw) awawachie mushrikina kwa baadhi ya waliyo nayo naye Mtume (saw) awache baadhi ya aliyo nayo.Ikateremka raddi/jawabu kutoka kwa Allah (swt):

ودوا لو تدهن فيدهنون

Wanatamani lau unge lainisha ili nao wakulainishie.

[Al-Qalam:9]

Wakamtaka Rasulullah (saw) aabudu miungu yao kwa mwaka na wao wamuabudu Mola wake kwa mwaka. Wakajibiwa na Allah (swt):

قل يآ أيهاالكافرون¤لاأعبدماتعبدون

Sema: Enyi makafiri! Siabudu mnachoabudu

[Al-Kaafiroon: 1 – 2]

Allah (swt) akamaliza ubembelezaji wao wa kuchekesha kwa fafanuzi hizo za kukata au moja kwa moja.

Yalipofeli majaribio yote yaliyotangulia ambayo Maquraysh waliazimia ili kumuondosha Mtume (saw) katika da’wah yake. Walikwenda katika mbinu nyengine miongoni mwa mbinu chafu za ubembelezaji (kati na kati)! Wakambembeleza Mtume (saw) wamuamini kwa sharti asiwataje miungu yao kwa uovu akakaribia Rasulullah (saw) kukubali akiwa na tamaa ya kusilimu kwao na akidhani kuwa hili halita dhuru da’wah, lakini usaidizi wa kiungu, upole na uchungaji wa kirabbaaniya kwa hii da’wah ulimpatiliza. Kwani Mtume (saw) hakuamka kutoka kwa kikao hicho cha ubembelezaji mpaka akamjia Jibril (as) kwa kauli yake Allah (swt):

وَإنْ كادُوا لـَيـَفـتِنـُونـَكَ عَن ِالذي أوحَينـَا إليكَ لتفتريَ عَلينـَا غيرَهُ إذا ًلا تـَّخذوكَ خلِيلا ً، وَلـَولا أنْ ثــَبـَّـتـنـَاكَ لقـَدْ كِدْتَ تركـَنُ إليهمْ شَيئا ً قليلا ً ، إذا ً لأذقـْـنـَاكَ ضِعفَ الحَيَاةِ وَضِعْـفَ المَمَاتِ ثـُمَّ لا تـَجـِدُ لكَ عَلينـَا نـَصِيرا ً.

Na hakika walikaribia kukushawishi uache tuliyo kufunulia ili utuzulie mengineyo. Na hapo ndio wangeli kufanya rafiki. Na lau kuwa hatukukuweka imara ungeli karibia kuwaelekea kidogo. Hapo basi bila ya shaka tungeli kuonjesha adhabu mardufu ya uhai, na adhabu mardufu ya kifo kisha usingepata mtu wa kukunusuru nasi.

[Al-Israa: 73-75]

Hakika utetelekaji wowote uwe ni mdogo kwa mbebaji da’wah, hata kama utetelekaji huo ni sehemu katika sehemu za da’wah, basi huwa ni utetelekaji katika da’wah yote. Kwani kila kifungu miongoni mwa vifungu vya ubebaji da’wah huwa ni mfano wa kifungu chengine, nayo ni hukmu ya kisheria miongoni mwa hukmu za twariqa. Inatakikana kusimama nayo wala haijuzu kuteteleka kwayo kabisa.

Itaendelea Katika UQAB Toleo 10…In Shaa Allah.