Kuona Mwezi Muandamo na Hesabu za Falaki

بسم الله الرحمن الرحيم

 Silsila ya Maswali Yaliyowasilishwa kwa

Amiri wa Hizb ut Tahrir

Sheikh Ata Bin Khalil Abu Al-Rashtah Katika Ukurasa Wake wa Facebook

Jibu la Swali

(Imetafsiriwa)

Sifa njema zote ni za Mwenyezi Mungu, na swala na salamu zimshukie Mtume wa Mwenyezi Mungu, na jamaa zake, na maswahaba zake, na mwenye kumpenda na kumnusuru, na baada.

Kwa ndugu waliotuma kwenye ukurasa wetu wakiulizia juu ya kuonekana kwa mwezi na hesabu ya falaki …

Assalam alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh,

Nimesoma maswali yenu kuhusu kuona mwezi na hesabu za falaki, na tumetoa majibu mara kwa mara kuhusu suala hili, lakini hakuna neno, nitaongezea ufafanuzi na kukokoteza, nikitarajia kwa maikhwa kuyazingatia kwa maono na ufahamu, nasema wabillahi tawfiq:

1- Hakika sisi enyi ndugu hatujumuishi hesabu ya falaki katika maudhui, kwani andiko (Naswi) linategemea kuuona tu, na tunafunga na kufungua kwa msingi wake, tusipouona jioni ya tarehe 29 katika mwezi wa Ramadhan tunakamilisha idadi ya siku thelathini hata kama mwezi unapatikana kwa hesabu za falaki lakini umefunikwa na wingu au dhurufu za anga, kwa sababu andiko limeegemezwa kwenye uoni na sio kwenye madhihirisho ya ulimwengu.

Tizama Hadith ya Mtume (saw) aliyopokea Al-Bukhari: asema: nimemsikia Abu Huraira (ra) anasema: amesema Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) au akasema: amesema Abul Qasim (saw):

«صُومُوا لِرُؤْيَتِهِ وَأَفْطِرُوا لِرُؤْيَتِهِ فَإِنْ غُبِّيَ عَلَيْكُمْ فَأَكْمِلُوا عِدَّةَ شَعْبَانَ ثَلَاثِينَ»

“Fungeni kwa kuuona mwezi na fungueni kwa kuuona mkifinikwa na wingu kamilisheni idadi ya Shaaban siku thelathini” Kisha Hadith iliyopokewa na Ahmad: asema nimemsikia Abu Huraira akisema: Hakika Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) amesema:

«لَا تَصُومُوا حَتَّى تَرَوْا الْهِلَالَ وَلَا تُفْطِرُوا حَتَّى تَرَوْا الْهِلَالَ، وَقَالَ: صُومُوا لِرُؤْيَتِهِ وَأَفْطِرُوا لِرُؤْيَتِهِ فَإِنْ غَبِيَ عَلَيْكُمْ فَعُدُّوا ثَلَاثِينَ»

“Msifunge hadi muuone mwezi muandamo na wala msifungue mpaka muuone mwezi muandamo, akasema: Fungeni kwa kuonekana mwezi na mufungue kwa kuona mwezi na mkifinikwa na wingu basi hesabuni siku thelathini”.

Kwa mfano mwezi ukifinikwa na mawingu na Waislamu hawakuona pamoja na kwamba upo hakika nyuma ya mawingu kulingana na hesabu ya falaki, basi sisi hatufungui kulingana na hiyo hesabu, bali ni lazima tufunge siku ya thelathini kwa sababu hatukuuona.

Nakariri, tazama Hadith «فَإِنْ غُبِّيَ عَلَيْكُمْ فَأَكْمِلُوا عِدَّةَ شَعْبَانَ ثَلَاثِينَ» “Ikiwa mtafinikwa na mawingu, basi timizeni siku thelathini za Sha’ban”

Ingawa kwenye hesabu za Falaki mwezi upo.

2 – Tunatambua kwamba kwa hesabu za falaki zinajulikana kwa sekunde wakati mwezi umeunganishwa na wakati unazaliwa na wakati utatoweka na ni dakika ngapi utabakia baada ya jua kutua … Lakini andiko (naswi) la kisheria halikuweka masharti ya madhihirisho ya kiulimwengu bali ni kwa muonekano. Angalia, kwa mfano, kuhusu nyakati za swala, na utaona kwamba andiko (naswi) lilitaja jambo madhihirisho ya ulimwengu na halikuishia kwenye maono: “

 (أَقِمِ ٱلصَّلَوٰةَ لِدُلُوكِ ٱلشَّمۡسِ) “Simamisha swala jua linapo pinduka” [Al-Israa: 78]

«إِذَا زَالَتِ الشَّمْسُ فَصَلُّوا» “wakati jua limepinduka, basi swalini.”

Swala inategemea wakati, kwa hiyo utaswali pindi utakapohakikisha muda kwa mbinu yoyote, ukitazama jua kuona wakati wa kupinduka jua “zawal” au ukitazama kivuli kuona kivuli cha kila kitu mfano wake au mara mbili yake kama ilivyoelezwa katika Hadith za nyakati za swala, ukifanya hivyo na ukathibitisha, swala ni sahihi, na usipofanya hivyo bali ulihesabu kifalaki, na ukajua kuwa wakati wa kupinduka jua “Zawal” ni hivi na hivi, na ukatazama saa yako bila kwenda nje kuona jua au kivuli. Swala yako imeswihi, yaani uhakikishe wakati kwa mbinu yoyote. Kwa nini? Kwa sababu Mwenyezi Mungu (swt), alikutaka uswali kwa kuingia wakati, na akakuachia uhakikishe kuingia kwake bila kubainisha jinsi ya kuhakiki.

Na kama unavyoona, ukitambua kwamba jua limepinduka “Zawal” kwa macho yako utaswali, na ukihesabu kwenye saa yako, utaswali, yaani hapa (kwa maono na hesabu) utaswali kwani andiko (naswi) sio kuona bali ni kwa dhihirisho la ulimwengu… Na hii ni kinyume na andiko (naswi) la kisheria la kufunga na kufungua ambalo linabainisha kuonekana kwa mwezi.

3- Ama hakika shahidi huenda akchanganyikiwa , akatoa ushahidi kwamba aliona hali ya kuwa hakuona mwezi muandamo bali ni kitu kingine, hii ni kazi ya hakimu au mwenye mamlaka ya kutangaza mwanzo na mwisho wa mwezi, hivyo anawachunguza mashahidi na idadi yao, na kadiri idadi inavyoongezeka, ndivyo inavyokaribia uhakikisho, na kuangalia usalama wa macho ya shahidi, sehemu aliyoiona upinde wa mwezi, na muda ambao mwezi ulikaa baada ya kuzama kwa jua, na sehemu aliyouona mwezi, na je ni muislamu, na je ni mtu mchafu fasiki…n.k. Ametupa habari Muhammad bin Abdil Aziz bin Abi Rimzata asema: ametupa habari Fadhlu bin Musa asema: Alikuja mbedui kwa Mtume (saw):

«فَقَالَ رَأَيْتُ الْهِلَالَ فَقَالَ أَتَشْهَدُ أَنْ لَا إِلَهَ إِلَّا اللَّهُ وَأَنَّ مُحَمَّداً عَبْدُهُ وَرَسُولُهُ قَالَ نَعَمْ فَنَادَى النَّبِيُّ ﷺ أن صوموا»

“Akasema nimeuona mwezi muandamo akasema Mtume S.a.w je unasaidia kwamba hapana Mola apasaye kuabudiwa isipokuwa Allah na kwamba Muhammad ni mja wake na Mtume wake akasema ndio Mtume S.a.w akawaita watu na kusema fungeni” [Sunan An-Nasa’i].

Hivi ndivyo unavyomthibitisha shahidi, lakini bila ya kujumuisha hesabu ya falaki katika mada, yaani, humwambii: hesabu ya falaki imepitisha kuwa mwezi upo nyuma ya mawingu, au kuamua kuwa mwezi haupo, kwa sababu kuanzishwa kwa hesabu ya falaki katika suala hilo ni kinyume na kilichokuja katika Hadithi ya Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw): «صُومُوا لِرُؤْيَتِهِ وَأَفْطِرُوا لِرُؤْيَتِهِ فَإِنْ غُبِّيَ عَلَيْكُمْ فَعُدُّوا ثَلَاثِينَ» “Fungeni kwa kuuona, na fungueni kwa kuuona, na ikiwa kuna mawingu kwenu basi hesabuni thelathini”. Andiko liko wazi nalo ni kukamilisha mwezi siku thelathini pamoja na kwamba kwa hesabu ya falaki mwezi upo nyuma ya mawingu, lakini hauonekani.

4- Ama kuhusu swali: (Hakika Mtume ﷺ anasema: «إِنَّا أُمَّةٌ أُمِّيَّةٌ، لاَ نَكْتُبُ وَلاَ نَحْسُبُ، الشَّهْرُ هَكَذَا وَهَكَذَا يَعْنِيمَرَّةً تِسْعَةً وَعِشْرِينَ وَمَرَّةً ثَلَاثِينَ»  “Sisi ni umma usiojua kusoma na kuandika, hatuandiki wala hatuhesabu, mwezi ni kadhaa na kadhaa yaani ishirini na tisa na mara hua ni thelathini”) [Al-Bukhari]. Je, haifahamiki kwa hadithi hii kinyume chake kwamba sisi tunachukua hesabu ya kuona kwa kuwa hatuandiki wala kupiga hesabu lakini tukishajifundisha hesabu basi tunachukua hesabu ya falaki).

Ufahamu huu si sahihi na ni usemi uliokataliwa, kama inavyojulikana katika usuli, ambapo dhana hii inavunjwa, kwa sababu sifa ya (kutojua kusoma na kuandika ) ilitoka kwa wengi “Makhraj ghaalib”, hivyo Waarabu walikuwa katika ujumla wao, ni wasiojua kusoma na kuandika, pamoja na kwamba dhana hii imevurugika kwa mantuq ya Maandiko Mengine. Ikiwa ni pamoja na Hadith: «فَإِنْ غُمَّ عَلَيْكُمْ فَأَكْمِلُوا الْعِدَّةَ ثَلَاثِينَ» “Ikiwa kuna mawingu kwenu, basi timizeni idadi ya siku thelathini” (Bukhari).

Hakuna kizuizi kilichotajwa juu yake, yaani, ikiwa haiwezekani kuonekana mwezi kwa sababu ya mawingu au mvua au sababu yoyote inayozuia kuona, basi hukmu ya kisheria imebainishwa kwa kukamilisha mwezi siku thelathini, hata ikiwa mwezi wa muandamo umetokeza, lakini mawingu yanauficha. Kwa hiyo, usemi “mantuq” wa Hadith hutumika na dhana ya kinyume chake “Mafhum mukhalafa” huatilishwa. Hiyo dhana ya “mafhum mukhalafa” hapa inavunjwa na mambo mawili: inasifia wengi “makhraj ghalib”, na kwa sababu kuna usemi “mantuq” wa andiko jengine linalopingana na dhana hiyo.

Na hii ni kweli katika masharti ya kufanya kazi na dhana hii katika hali zaidi ya moja, kwani inasitishwa ikiwa imetoka katika wingi “Makhraj ghaalib”, au ikiwa andiko jengine linaizuia kwa mantuq yake, kama:

((وَلَا تَقۡتُلُوۤا۟ أَوۡلَـٰدَكُمۡ خَشۡیَةَ إِمۡلَـٰقࣲۖ)) “Wala msiwauwe wana wenu kwa kuogopa umasikini.” [Al-Israa: 31]

“Kuogopa umasikini” ni sifa inayofahamika yaani kuogopa ufukara. Kadhalika inasifia wingi “makhraj ghaalib”, walikuwa wakiwauwa kwa kuogopa ufukara, kisha ufahamu huu umetupwa kwa andiko.

((وَمَن یَقۡتُلۡ مُؤۡمِنࣰا مُّتَعَمِّدࣰا فَجَزَاۤؤُهُۥ جَهَنَّمُ)) “Na mwenye kumuuwa Muumini kwa kukusudia, basi malipo yake ni Jahannamu” [An-Nisaa: 93]

Kwa hiyo dhana hii inatupwa, hivyo haisemwi kuwa kilichoharamishwa ni kuua watoto kwa kuhofia umaskini na itakuwa ni halali ikiwa mtu atamuuwa hali ametosheka! Bali imeharamishwa katika hali zote mbili, iwe ni kutokana na ufukara au mali, na vile vile Aya hii:

((لَا تَأۡكُلُوا۟ ٱلرِّبَوٰۤا۟ أَضۡعَـٰفࣰا مُّضَـٰعَفَةࣰۖ)) “Msile riba mkizidisha juu kwa juu” [Aali-Imran: 130]

Kwa hiyo, “kuzidisha juu kwa juu” ni maelezo yanayoeleweka, na hali hiyo hiyo inasifia wingi. Walikula riba maradufu.

Dhana hii ilikatizwa na andiko:

((وَأَحَلَّ اللَّهُ الْبَيْعَ وَحَرَّمَ الرِّبَا)) “Na Mwenyezi Mungu ameiruhusu biashara na akaharamisha riba,” [Al-Baqara: 275]

Kwa hiyo dhana hii imebatilika, kwa hivyo haisemwi kwamba kilichoharamishwa ni riba nyingi, na ama kuhusu riba kidogo inajuzu. Bali riba, licha ya kiwango chake, imeharamishwa kwa sababu dhana ya “maradufu” imekatizwa kama tulivyosema.

Hivyo basi, dhana ya neno (Ummiyah) inavunjwa, kama tulivyoeleza, maana yake ni kwamba kuonekana kwa mwezi ikishindikana kwa sababu ya mvua au mawingu, basi lazima utimizwe muda wa mwezi thelathini, sawa sawa iwe twajua hesabu au hatujui.

5- Kuhusu Eid Al-Fitr mwaka huu, kama mumeona, mara hii tulichelewa kutangaza, na sababu ilikuwa ni kuhakiki jambo hili. Kulikuwa na ushuhuda tofauti tofauti wa muonekano wa mwezi:

A- #Afghanistan, #Mali na #Niger zilitangaza kuonekana mwezi baada ya machweo ya jua Jumamosi 30/4/2022, na kisha kutangaza Eid, Jumapili ya kwanza ya Shawwal 1443 H inayolingana na 1/5/2022 M.

B – Takriban nchi 21 za Kiarabu zilitangaza kuwa muonekano wa mwezi haukuthubutu baada ya kuzama kwa jua Jumamosi, hivyo wakaichukulia Jumapili kuwa ni tamati ya mwezi wa Ramadhan, na kwamba Eid ni Jumatatu tarehe 2/5/2022.

C- Nchi nne zilikuwa na kalenda ya kwamba Jumamosi ni tarehe ishirini na nane Ramadhan, kwa hivyo muandamo haukuchunguzwa Jumamosi jioni, bali ni siku iliyofuata, Jumapili, na hawakuona mwezi muandamo, kwa hivyo wakazingatia kuwa Jumatatu ndio kukamilisha Ramadhan. Na Eid ni siku ya Jumanne tarehe 3/5/2022, na nchi hizi ni India, Bangladesh, Iran, Pakistan.

6- Hapa ilikuwa ni lazima kumfuatilia aliyeona, kwani mwenye kuona ni hoja dhidi ya asiyeona, na uthibitisho wa uoni huo ni kama ilivyo katika nusus za kisharia bila ya kuingia hesabu ya Falaki. Kwa sababu Hadith ya Mtume (saw) iko wazi katika hilo kwani Mtume (saw) anasema:

فَإِنْ غَبِيَ عَلَيْكُمْ فَعُدُّوا ثَلَاثِينَ» « “… Ikiwa mtafunikwa na wingu basi hesabu idadi ya siku thelathini”. Na kwa sababu Mali na Niger ziko magharibi mwa Afghanistan, yaani iwapo muono huo utathibitika nchini Afghanistan, basi katika “Babil Awlaa” ni kuthubutu Mali na Niger, na kwa hivyo sisi tulianza kuchunguza na kuhakikisha Afghanistan, na ikawa muonekano wa mwezi ulitangazwa katika hizi nchi tatu:

a – Niger ilitangaza kwamba ilithibitishwa kuwa muandamo wa mwezi wa Shawwal ulithibiti baada ya jua kuzama siku ya Jumamosi katika mikoa ya Diffa, Tawa na Maradi, na pia katika jiji la Zinder.

b- Mahakama ya Juu ya Afghanistan ilitangaza, Jumamosi jioni, kwamba Jumapili, Mei 1, itakuwa siku ya kwanza ya Eid ul-Fitr 2022 nchini humo. Na kama ilivyotajwa kuhusu biladi hizo, muonekano ulifanyika katika majimbo (Ghor, Ghazni, Kandahar, Farah, na ushahidi sahihi wa watu 27 ulithibitishwa na kamati za eneo…).

c- Serikali ya Mali pia ilitangaza kuwa mwezi muandamo wa Shawwal ulionekana Jumamosi jioni katika maeneo mawili na mashahidi 8.

Yamaanisha, muonekano huo ulithibiti kutoka kwa mashahidi wapatao 39 katika maeneo tofauti … na tulifanya kila juhudi kuthibitisha, hasa kutoka Afghanistan, kwa sababu Mali na Niger ziko magharibi ikiwa muonekano ni sahihi Afghanistan basi katika “Baabil awla” muonekano utakuwa sahihi katika Mali na Niger… Hatukutosheka na vyombo vya Habari wala hata kwa yaliyotufikia kutoka wasimamizi (Muutamadina) katika wilayat tukaongeza kwa hilo… Kwa hiyo tuliwasiliana na mtu wa vyombo vya habari nchini Afghanistan, pamoja na baadhi ya ndugu wa Afghanistan walioko Ulaya ili kuwasiliana na baadhi ya watu wanaofahamiana huko Afghanistan ili kuthibitisha suala hilo hadi tulipohakikishiwa kuwa muonekano huo umethibitishwa, kwa hiyo tulitangaza ndani ya saa sita usiku, kwa saa za jiji la Madina.

7- Ama kuhusu swali, kwa nini Waislamu wanatafautiana katika kuona? Jibu ni rahisi na sahali, na ni kama ifuatavyo:

a – Kukhtalifiana huko ni kwa sababu ya kutofuata hukmu ya kishariah, ingawa iko wazi! Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) ametubainishia uwajibu wa kufuata muonekano, na akasisitiza hilo kwa kusema, amani iwe juu yake: فَإِنْ غَبِيَ عَلَيْكُمْ فَعُدُّوا ثَلَاثِينَ “Na ikiwa kuna mawingu kwenu basi hesabuni thelathini”.

Ni wazi kutoka kwake kwamba hesabu ya Falaki imeangushwa na haizingatiwi, kwa sababu andiko linalazimisha kukamilisha mwezi thelathini ikiwa mwezi hauonekani kwa sababu mawingu yaliuficha usionekane hata ikiwa uko nyuma ya mawingu. Na hesabu ya falaki inathibitisha uwepo wake nyuma ya mawingu, pamoja na hivyo bado haifai kuifanyia kazi, bali tunakamilisha mwezi wa thelathini kama ilivyokuja katika hadithi za Mtume wa Mwenyezi Mungu ﷺ: «صُومُوا لِرُؤْيَتِهِ، وَأَفْطِرُوا لِرُؤْيَتِهِ، فَإِنْ غُبيَ عَلَيْكُمْ فَعُدُّوا ثَلَاثِينَ» “Fungeni kwa kuonekana kwake, na fungueni kwa kuonekana kwake, ikiwa mtafinikwa na wingu basi hesabuni siku thelathini” na akasema Mtume rehma na amani zimshukie: «لَا تُقَدِّمُوا الشَّهْرَ حَتَّى تَرَوْا الْهِلَالَ أَوْ تُكْمِلُوا الْعِدَّةَ ثُمَّ صُومُوا حَتَّى تَرَوْا الْهِلَالَ أَوْ  تُكْمِلُوا الْعِدَّةَ» “msianze Mwezi hadi muone mwezi muandamo au kukamilisha idadi (ya thalathini) kisha fungeni mpaka muone mwezi muandamo au mukamilishe idadi (ya thalathini)” [Amepokea Abu Dawud]. Na akasema Mtume Rehma na amani zimshukie: «إِذَا رَأَيْتُمْ الْهِلَالَ فَصُومُوا وَإِذَا رَأَيْتُمُوهُ فَأَفْطِرُوا فَإِنْ غُمَّ عَلَيْكُمْ فَصُومُوا ثَلَاثِينَ يَوْماً» “Pindi mkiuona mwezi muandamo fungeni na pindi mkiuona fungueni; ikiwa mtafinikwa na wingu basi fungeni siku thelathini” [Amepokea Muslim].

Na Hadith katika haya ni nyingi, nazo zaonyesha kwamba kinachotambuliwa katika hayo ni kuona mwezi muandamo au kukamilisha idadi, Makusudio ya Hadith hizi ni sio kila mmoja kuona mwezi muandamo yeye mwenyewe, bali kinachokusudiwa hapo ni ushahidi wa bayana wa haki.

Imepokewa kwa usahihi kutoka kwa Ibn Umar (ra) amesema: “Watu walijaribu kuuangalia mwezi mchanga, nikamwambia Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) kuwa nimeuona akafunga na akawaamuru watu wafunge), imepokewa na Abu Dawud.

b- Ama sababu ya pili ni kwamba Waislamu hawakusanywi pamoja na Khilafah, hawana mtawala mmoja anayeondoa mabishano bila kuwafarakanisha, na kwa kuzingatia Hadith ya Mtume (saw) yanabainika hayo.

Amepokea Ahmad katika Musnad yake asema ametuhadithia Hushaym ametupa habari Abu Bishri kutoka kwa Abi Umair bin Anas wamenihadhia maami zangu katika Maanswari katika maswahaba wa Mtume (saw) asema: «غُمَّ عَلَيْنَا هِلَالُ شَوَّالٍ فَأَصْبَحْنَا صِيَاماً فَجَاءَ رَكْبٌ مِنْ آخِرِ النَّهَارِ فَشَهِدُوا عِنْدَ رَسُولِ اللَّهِ ﷺ أَنَّهُمْ رَأَوْا الْهِلَالَ بِالْأَمْسِ فَأَمَرَ رَسُولُ اللَّهِ ﷺ أَنْ يُفْطِرُوا مِنْ يَوْمِهِمْ وَأَنْ يَخْرُجُوا لِعِيدِهِمْ مِنَ الْغَدِ» “Tulizibwa na mawingu katika mwezi muandamo wa Shawwal tukaamka tumefunga ukaja msafara jioni ukatoa ushahidi mbele ya Mtume (saw) kwamba wao waliona mwezi muandamo jana Mtume (saw) akaamrisha wafungue katika ile siku ilobakia na kesho yake watoke kuswali Eid.” Musand ya Ahmad.

Pamoja na ugumu wa mawasiliano baina ya vijiji na miji wakati huo, lakini tatizo lilitatuliwa na Mtume (saw), akawaamrisha Waislamu wa Madina wafungue saumu kwa sababu mwezi mchanga ulionekana jangwani, kisha aliwaamrisha Waislamu kuswali Eid kesho kwa sababu ujumbe wa Badia ulifika Madina baada ya muda wa swala ya Idi kupita siku hiyo, huu ni wakati ambao ulikuwa ndani yake uwasilishaji wa habari kutoka nchi moja hadi nyengine huchukua muda mrefu, basi vipi leo ambapo habari zinaweza kusafiri haraka? Lau Waislamu wangekuwa na khalifa na dola moja, wangekuwa waja wa Mwenyezi Mungu kama ndugu, hasa kwa vile tabanni katika kila jambo linalowaunganisha Waislamu na umoja wao imeamrishwa na Uislamu kwa dola, chama na mtu binafsi kwa mujibu wa hukmu ya kisheria. Hivyo kutabanni rai ya kisheria inayowaunganisha Waislamu ni jambo la daraja kubwa katika Uislamu.

Mambo haya mawili ndiyo yanaondoa hitilafu, na Waislamu wanapaswa kufanya kila juhudi kuyafanikisha ili Waislamu warudi kwenye Umma bora uliotolewa kwa ajili ya watu, kama Mwenyezi Mungu alivyoteremsha katika kitabu chenye maamuzi:

((كُنتُمۡ خَیۡرَ أُمَّةٍ أُخۡرِجَتۡ لِلنَّاسِ تَأۡمُرُونَ بِٱلۡمَعۡرُوفِ وَتَنۡهَوۡنَ عَنِ ٱلۡمُنكَرِ وَتُؤۡمِنُونَ بِٱللَّهِ)) “Nyinyi mmekuwa bora ya umma walio tolewa watu, kwa kuwa mnaamrisha mema na mnakataza maovu, na mnamuamini Mwenyezi Mungu” [Aali-Imran: 110].

Kwa kumalizia, namuomba Mwenyezi Mungu (swt) awaongoze Waislamu wote katika mambo yao yenye uongofu zaidi, awape utukufu kwa izza ya Uislamu, na wasimamishe dola yao baada ya kutokuwepo kwa muda mrefu, kisha wasihitilafiane katika kumtii Mola wao Mlezi, bali wawe kama alivyosema Mwenyezi Mungu:

((فَٱنقَلَبُوا۟ بِنِعۡمَةࣲ مِّنَ ٱللَّهِ وَفَضۡلࣲ لَّمۡ یَمۡسَسۡهُمۡ سُوۤءࣱ وَٱتَّبَعُوا۟ رِضۡوَ ٰنَ ٱللَّهِۗ وَٱللَّهُ ذُو فَضۡلٍ عَظِیمٍ)) “Basi wakarudi na neema na fadhila za Mwenyezi Mungu. Hapana baya lilio wagusa, na wakafuata yanayo mridhi Mwenyezi Mungu. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye fadhila kuu.” [Aali-Imran: 174].

Mwenyezi Mungu ayakubali matendo yenu ya utiifu, Wassalam Alaikum Wa Rahmatullah Wa Barakatuh.

Ndugu Yenu,

Ata Bin Khalil Abu Al-Rashtah

10 Shawwal 1443 H

10/05/2022 M

Link ya jibu hili kutoka ukurasa wa Amiri wa Facebook.