Kusoma Suratul Faatiha Katika Swala ya Jamaa na Kuchanganyika (Wanawake na Wanaume) Katika Ziyara za Kifamilia

 

بسم الله الرحمن الرحيم

 

 Silsila ya Maswali Yaliyowasilishwa kwa

Amiri wa Hizb ut Tahrir

Sheikh Ata Bin Khalil Abu Al-Rashtah Katika Ukurasa Wake wa Facebook

Jibu la Swali

Kwa: Al-Maqdisi
(Imetafsiriwa)

Swali:

Assalamu Alaikum Wa Rahmatullahi Wa Barakatuh. Allah Awasaidie.

Nina maswali mawili: la kwanza: kuhusu swala na la pili ni kuhusu ziyara za kifamilia.

Ama swali la kwanza: ni ipi hukmu ya kusoma Al-Faatiha katika swala kwa maamuma? Na je kumkuta Imam kwenye rukuu au akiwa karibu na kurukuu kwa hali ambayo maamuma hatoweza kusoma Al-Faatiha nzima, je itahesabika kapata rakaa?

Swali la pili: katika ziyara za kifamili au za kuunga kizazi, katika (siku za) Idd au nyenginezo, hukusanyika mume wa dada pamoja na mke wa kaka au binamu pamoja na binti wa ami, au mke wa kaka pamoja na kaka… n.k pamoja na kuwepo maharimu nyumbani na kwenye mkao mmoja kwenye chakula, au bila ya chakula, ndani ya nyumba ya kifamilia au sehemu nyengine, ni ipi hukmu ya kisheria katika yote hayo?

Tupeni faida na Mwenyezi Mungu awabariki.

Jibu:

Wa Alaikum Salaam Wa Rahmatullahi Wa Barakaatuh.

1- Ama kuhusiana na kumkuta Imam bila kuweza kusoma Al-Faatiha, yaani “swala ya maamuma aliyepitwa” hili tumeliweka wazi kwenye kitabu Hukmu za Swala “Ahkaam ul-Swalaa” katika ukurasa wa 67 tumesema yafuatayo:

(Maamuma akipata kisimamo pamoja na Imam, na akahofia kukosa (mda) wa kusoma Al-Faatiha, basi ataacha (kusoma) dua ya ufunguzi, na (badala yake) atashughulika na kisomo (cha Al-Faatiha). Kwa sababu, hiyo (dua) ni Sunnah na kisomo (cha Al-Faatiha) ni Wajib, hivyo hatoshughulika na Sunnah na kuacha Wajib. Na ikiwa amesoma baadhi ya Al-Faatiha na Imam akarukuu, basi atarukuu naye na kuacha kisomo, kwa sababu kumfuata imamu ni jambo lenye msisitizo zaidi. Na ikiwa atamkuta (Imam) amerukuu, basi atapiga takbiratul ihraam akiwa amesimama wima, kisha atapiga takbira kwa ajili ya kurukuu na arukuu. Ikiwa atapiga takbira na kukusudia kuwa ndio ya ihraam na ya kurukuu kabisa, basi haitomtosheleza na takbira ya faradhi, kwa sababu atakuwa ameshirikisha kwenye niya baina ya faradhi na sunnah, hivyo swala yake itakuwa haikufungika. Na ikiwa atapata pamoja na Imam wake rukuu inayofaa, basi atakuwa ameipata rakaa, na endapo hatoipata hiyo rukuu basi hakuipata rakaa, na ikiwa amepata rakaa basi atakuwa ameipata swala ya jamaa, kutokana na (hadithi) iliyopokewa kutoka kwa Abu Huraira (r.a) akisema: amesema Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw):

«إذا جئتم إلى الصلاة ونحن سجود فاسجدوا ولا تعدوها شيئاً ومن أدرك الركعة فقد أدرك الصلاة»

“Pindi mtakapokuja kwenye swala na sisi tumeshasujudu, basi nanyi sujuduni na msihesabu ni chochote, na yeyote atakayepata rakaa basi hakika huyo amepata jamaa”. Na ikiwa (maamuma) atapata pamoja na Imam rakaa ya mwisho, basi hapo ndio mwanzo wa swala yake. Hayo ni kutokana na (hadithi) iliyopokewa kutoka kwa Ali (r.a) kwamba amesema: «ما أدركت فهو أول صلاتك» “Utakapopata (katika swala) basi ndio mwanzo wa swala yako”. Kwa hiyo, Imam atakapopiga salamu (maamuma) atasimama ili kukamilisha kilichobakia katika swala yake. Na ikiwa ni ndani ya swala yenye qunuti, basi atakunuti pamoja na Imam, kisha atarudia qunut tena mwisho wa swala yake.

Na yatakikana maamuma amfuate Imam, na wala asimtangulie katika kitendo chochote. Kutokana na (hadithi) aliyopokea Abu Huraira (r.a) kwamba Mtume (saw) amesema:

«إنما جعل الإمام ليؤتم به فلا تختلفوا عليه، فإذا كبر فكبروا، وإذا ركع فاركعوا، وإذا قال سمع الله لمن حمده فقولوا اللهم ربنا لك الحمد، وإذا سجد فاسجدوا»

“Hakika amewekwa Imam ili afuatwe, basi msitafautiane naye, akipiga takbira nanyi pigeni, akirukuu nanyi rukuuni, akisema: sami`allahu liman hamidah, nyinyi semeni: allahumma rabbanaa lakal hamdu” na akisujudu, nanyi pia sujuduni”. Na pindi Imam akisahau katika swala, ikiwa ni kwenye kisomo (Qur`an) basi (maamuma) atamkubusha. Hiyo ni kutokana na (hadithi) aliyopokea Anas (r.a) akisema:

«كان أصحاب رسول الله ﷺ يلقن بعضهم بعضاً في الصلاة»

“Walikuwa Maswahaba wa Mtume (saw) wakikumbushana katika swala”. Na ikiwa (Imam amenukuu) kisomo tofauti (cha ayah) basi maamuma ataisoma kwa sauti ili Imam asikie, na kama alichosahau Imam ni kitendo, basi atasema “Subhaanallah” ili kumkubusha, na kama maamuma atatia nia ya kuachana na Imam na kukamilisha mwenyewe pia inaruhusiwa, sawa iwe ni kwa udhuru au bila ya udhuru,

«لأن معاذاً أطال القراءة فانفرد عنه أعرابي، وذكر ذلك للنبي ﷺ فلم ينكر عليه» “kwa sababu Mu’adh alirefusha kisomo na Mbedui mmoja akajitenga naye, na akamtajia Mtume (saw) hilo, wala Mtume hakumkemea (Mbedui huyo).

2- Ama kuhusu kuunga kizazi, hili limeelezwa kwenye vitabu vyetu:

  • Kutoka kwenye kitabu cha Nidhamu ya Kijamii – “Kuunga Kizazi”:

“… na kilicho wazi kutokana na hizo hadithi ni ueneaji, kwani zakusanya kuunga kila mmoja katika kizazi, sawa kiwe ni kizazi kinachoharamishwa kuoana (Mahram) au kisichoharamishwa miongoni mwa familia, wote hao ni sawa kuitwa wenye uzao.  Na zimekuja hadithi nyingi kuhusu kuunga kizazi, amesema Mtume (saw): «لا يَدخلُ الجنَّةَ قاطعُ رحِم» “Hatoingia Peponi mkata uzao” (Imepokewa na Muslim kwa njia ya Jubeir bin Mut`im) na imepokewa kutoka kwa Anas bin Malik kwamba Mtume (saw) amesema:

«من أَحبَّ أن يُبْسَطَ له في رِزْقِهِ ويُنْسَأَ له في أَثَرِهِ فَلْيَصِلْ رَحِمَهُ» “Yeyote anayependa kukunjuliwa riziki yake, na kucheleweshewa ajal yake, basi aunge kizazi chake” (Bukhari na Muslim).

Na imepokewa kutoka kwa Abu Huraira, kwamba Mtume (saw) amesema:

»إِنَّ اللَّهَ خَلَقَ الْخَلْقَ حَتَّى إِذا فَرَغ مِنْ خَلْقِهِ قَالَتْ الرَّحِمُ هَذَا مَقَامُ الْعَائِذِ بِكَ مِنْ الْقَطِيعَةِ قَالَ نَعَمْ أَمَا تَرْضَيْنَ أَنْ أَصِلَ مَنْ وَصَلَكِ وَأَقْطَعَ مَنْ قَطَعَكِ قَالَتْ بَلَى يَا رَبِّ قَالَ فَهُوَ لَكِ قَالَ رَسُولُ اللَّهِ ﷺ فَاقْرَءُوا إِنْ شِئْتُمْ فَهَلْ عَسَيْتُمْ إِنْ تَوَلَّيْتُمْ أَنْ تُفْسِدُوا فِي الأَرْضِ وَتُقَطِّعُوا أَرْحَامَكُمْ«

“Hakika Mwenyezi Mungu alipomaliza kuumba ulisema uzao: hiki ni kisimamo cha mwenye kutaka ulinzi kwako dhidi ya kukatwa. Akasema (Mwenyezi Mungu) ndio! Hivi huridhii nikimuunga atakayekuunga na nikimkata atakayekukata? Ukajibu: kwanini nisiridhie, ndio ewe Mola wangu! Akasema: basi hilo ni lako… akasema Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw): someni mkitaka: “Basi yanayo tarajiwa kwenu mkitawala ndio mfisidi katika nchi na mwatupe jamaa zenu?” [Muhammad: 22]” (Bukhari na Muslim)

Na amesema tena Mtume (saw):

 «لَيْسَ الواصِلُ بالمُكافئِ ولكنَّ الواصِلَ الذي إذا قَطَعَتْ رَحِمُهُ وَصَلَها»

“Si muungaji uzao yule anayelipa, lakini muungaji ni yule ambaye uzao wake unapokatwa yeye huunga” (Imepokewa na Bukhari kutoka kwa Abdillah bin Amr) na yote hayo yanajulisha uhamasisho juu ya kuunga kizazi, na kuunga kizazi kunajulisha upeo uliowekwa na Mwenyezi Mungu kutokana na muungano na upendo kati ya jamii ya Kiislamu, katika kuungana jamaa za karibu na kusaidiana. Na (pia yanajulisha) ni kwa kiasi gani sheria ilivyojali kupangilia kukutana kwa mwanaume na mwanamke, na kupangilia mahusiano na natija yanayotokana na huko kukutana kwao. Kwa hiyo, sheria ya Kiislamu ikawa nidhamu ya kijamii bora zaidi kwa mwanadamu kutokana na hukmu zake zilizowekwa katika jamii…”

  • kutoka kwenye kitabu cha Nidhamu ya Kijamii – “Maisha ya Kibinafsi”:

“… hizi ni hukmu za kuhifadhi maisha ya binafsi kwenye nyumba dhidi ya wageni wanaotaka kuingia humo, hakuna tofauti katika hilo awe ni mtu wa kando (ajnabi) au maharimu, wa karibu ama wa mbali kwa nasaba au shemegi. Ama hukmu za haya maisha ya ndani, mwanamke anaishi pamoja na wanawake wenzake, au maharimu zake tu. Kwa sababu hao ndio ambao anaruhusiwa (mwanamke) kuwadhihirishia sehemu za mapambo yake katika viungo vyake ambavyo havina budi kudhihiri katika maisha binafsi akiwa ndani ya nyumba. Ama (watu wengine) wasiokuwa wanawake wenzake na maharimu zake, haifai kwa mwanamke kuishi nao, kwa sababu haifai kwake kuwadhihirishia sehemu za mapambo yake katika viungo vyake vinavyodhihirika kwa mwanamke wakati akifanya kazi zake ndani ya nyumba isipokuwa uso na viganja vya mikono. Kwa hiyo, maisha binafsi ni makhsusi kwa wanawake na maharimu tu. na hakuna tafauti kati ya wanawake hao wawe ni Waislamu au wasiokuwa Waislamu, kwa kuwa wote ni wanawake. Kule kwamba mwanamke amekatazwa kudhihirisha viungo vya mapambo yake kwa watu wa kando (ajnabi), na kwamba hakatazwi kuyadhihirisha kwa maharimu zake, hilo ni dalili ya wazi kwamba maisha binafsi ni makhsusi kwa maharimu peke yao. Amesema Mwenyezi Mungu Mtukufu:

(وَقُل لِّلْمُؤْمِنَاتِ يَغْضُضْنَ مِنْ أَبْصَارِهِنَّ وَيَحْفَظْنَ فُرُوجَهُنَّ وَلَا يُبْدِينَ زِينَتَهُنَّ إِلَّا مَا ظَهَرَ مِنْهَا وَلْيَضْرِبْنَ بِخُمُرِهِنَّ عَلَىٰ جُيُوبِهِنَّ وَلَا يُبْدِينَ زِينَتَهُنَّ إِلَّا لِبُعُولَتِهِنَّ أَوْ آبَائِهِنَّ أَوْ آبَاءِ بُعُولَتِهِنَّ أَوْ أَبْنَائِهِنَّ أَوْ أَبْنَاءِ بُعُولَتِهِنَّ أَوْ إِخْوَانِهِنَّ أَوْ بَنِي إِخْوَانِهِنَّ أَوْ بَنِي أَخَوَاتِهِنَّ أَوْ نِسَائِهِنَّ أَوْ مَا مَلَكَتْ أَيْمَانُهُنَّ أَوِ التَّابِعِينَ غَيْرِ أُولِي الْإِرْبَةِ مِنَ الرِّجَالِ أَوِ الطِّفْلِ الَّذِينَ لَمْ يَظْهَرُوا عَلَىٰ عَوْرَاتِ النِّسَاءِ)

“Na waambie Waumini wanawake wainamishe macho yao, na wazilinde tupu zao, wala wasionyeshe uzuri wao isipo kuwa unao dhihirika. Na waangushe shungi zao juu ya vifua vyao, wala wasionyeshe uzuri wao ila kwa waume zao, au baba zao, au baba wa waume zao, au watoto wao, au watoto wa waume zao, au kaka zao, au wana wa kaka zao, au wana wa dada zao, au wanawake wenzao, au iliyo wamiliki mikono yao ya kuume, au wafwasi wanaume wasio na matamanio, au watoto ambao hawajajua mambo yaliyo khusu uke.” [An-Nur: 31]

Na watumwa wanaowamiliki nao wamekutanishwa na maharimu, na vilevile wale wanaume wasiokuwa na hisia kwa wanawake, kama vile wakongwe, matahira, waliovunjwa konde zao, au waliokatwa ala zao, au walio mfano wao miongoni mwa wanaume wasio na haja na wanawake. Hakika, wote hao wanaruhusiwa kuwepo kwenye maisha binafsi, ama wanaume wa kando wote wasokuwa hao (hata kama ni wanafamilia wasio maharimu) haifai kabisa kwao kuwepo kwenye maisha binafsi, kwa sababu haifai kwa mwanamke kuwadhihirishia viungo vyake vya mapambo, ambavyo kawaida huwa wazi akiwa ndani kwake. Kwa hiyo, wanaume wa kando kujumuika na wanawake katika maisha binafsi ni haramu moja kwa moja, isipokuwa katika hali ambazo sheria imezivua, kama vile: katika chakula, na kuunga kizazi, kwa sharti awepo maharimu pamoja na mwanamke, na awe amesitiri uchi wake (mwili wote) …”

  • Pia hayo tumeyaweka wazi mara kadhaa katika majibu yetu. Kama vile:

Kwenye Jibu la Swali la mnamo tarehe 28/2/2010:

“… Hakika uwepo wa wanaume na wanawake katika maisha ya Kiislamu ambayo Mtume (saw) ameyakubali, na dalili za kisheria ambazo zinapangilia miamala ya kisheria kati ya mwanamke na mwanaume… yote hayo yamewekwa wazi kabisa, na tumetoa majibu zaidi ya moja kuhusu hili jambo, na tulikuwa tukitaraji kwamba hili jambo halitakuwa na tatizo!

Lakini pamoja na hayo, mimi kwenye huu ujumbe nitazidi kulifafanua hili kwa idhni ya Mwenyezi Mungu, nikitaraji utata wowote hautobakia kuhusu hili jambo:

* Kwa hakika, maisha jumla: yanamaanisha uwepo wa wanaume na wanawake katika maeneo jumla ambayo mtu hahitaji ruhusa ili kuingia. Na maisha haya yana hukmu za kisheria zinazopangilia wanaume na wanawake.

Na maisha binafsi: ni sehemu ambazo mtu atahitajika kupewa idhini ili kuingia, kama vile: majumba. Na (maisha) haya nayo yana hukmu za kisheria zinazowapangilia wanaume na wanawake.

* Ama kuhusu maisha binafsi “majumbani” hili liko wazi wala halihitaji ufafanuzi zaidi. Kwa sababu, maisha ya wanawake humo huwa ni pamoja na maharimu zao tu wala sio pamoja na watu wa kando, isipokuwa linapokuja andiko (naswi) katika hali maalumu, kama vile: kuunga kizazi, hapo inaruhusiwa mwanafamilia kumuunga mwanamke anayehusiana naye kidamu hata kama sio maharimu yake. Mfano: binamu kwenda kumsalimia binamu yake siku za Idd, na bila shaka bila kuwa faragha peke yao, na bila ya kufichuka uchi, kama vile akienda pamoja na babake au ami yake na kuunga kizazi chake, hata kama sio katika maharimu zake.

* Ama maisha jumla: pakiwa na haja ambayo sheria imekubali wanaume na wanawake kujumuika kwa ajili yake, basi unaruhusiwa huo mjumuiko “kwa namna yake ya kisheria”. Na tunasema: “kwa namna yake ya kisheria” kwa sababu, kunazo hukmu za kisheria zinazopangilia huo mkusanyiko kwa namna ifuatayo:

1- Ulazima wa kutenganishwa safu za wanaume na wanawake panapokuwa na haja inayokubaliwa na sheria kuwepo wanaume na wanawake kwa ajili yake, ikiwa lengo la wanaojumuika ni moja. Mfano: kuwepo wanaume na wanawake kwa ajili ya swala, au kwa ajili ya kuhudhuria darsa ya kielimu, au muhadhara katika da’wah, au kwa ajili ya kazi jumla ya kida’wah… katika hali hizi inafaa kuwepo wanaume na wanawake pamoja na kutenganishwa safu. Na hii wakati mwengine huitwa “maisha jumla yenye hukmu za maisha binafsi” yaani, kunakuwa na namna maalumu ya kuwepo wanaume na wanawake.

2- Kutokuwa na ulazima wa kutenganishwa safu katika maisha jumla, pindi ikiwa haja inayokubaliwa na sheria kuwepo kwa wanaume na wanawake, ikiwa malengo ya wanaokusanyika ni tafauti. Mfano: kuwepo wanaume na wawake sokoni, au barabarani, au kwenye bustani la jumla, au wakati wa kupanda mabasi ya uma… maisha haya yako aina mbili:

A- Malengo yao hayawezi kutekelezwa ila kwa mchanganyiko, yaani mchanganyiko wa kukaribiana na bila maongezi. Mfano: kwenye kuuza na kukununua sokoni, katika aina hii yaruhusiwa mchanganyiko.

B- Malengo yao yaweza kutekelezwa bila ya mchanganyiko, yaani, pasipo mchanganyiko wa kukaribiana na maongezi. Mfano: kupanda usafiri wa uma, katika mabustani jumla, na kwenye kutembea barabarani. Katika aina hii yaruhusiwa kuwepo wanaume na wawake bila mchanganyiko, yaani bila ya kukaribiana na bila maongezi. Bali yawezekana kuwa jirani na kila mmoja akiwa na lengo lake bila ya kuongea pamoja, kama vile: wakitembea njiani, au wakiwa kwenye mabustani jumla, au katika kupanda usafiri wa uma…

* Kama unavyoona, hukmu za kuwepo wanaume na wawake ziko wazi na zimeainishwa katika maisha binafsi na maisha jumla:

Maisha binafsi (ndani ya nyumba) ndio yanayohitaji idhini ili mtu kuingia. Na maisha jumla: ni yale ambayo mtu hahitaji idhini ya kuingia, na katika maisha haya jumla kuna hali inayohitajika safu kutenganishwa, na kuna hali nyengine isiyohitajika kufanya hivyo, pia katika maisha hayo kuna hali inayoruhusiwa mchanganyiko wa ujirani na maongezi, na kuna hali isiyofaa kuchanganyika bali ujirani tu bila ya maongezi…” mwisho wa nukuu.

na nataraji hayo yanatosheleza) Mwisho

Na katika jibu la swali la mnamo tarehe 6/6/2016 yamekuja haya ndani yake:

(A- Mchanganyiko (ikhtilaatw): yaani wanaume wa kando na wawake kukusanyika ni haramu ikiwa ni bila ya haja inayokubaliwa na sheria kukusanyika kwa ajili yake…. ama ikiwa ni kwa ajili ya haja inayokubaliwa na sheria (watu) kukusanyika kwa ajili yake kwa namna ambayo haiwezekani hiyo haja kukidhiwa ila kwa kukusanyika: basi hapo itaruhusiwa.

B- Zimekuja dalili zinazokubali kukusanyika kwa ajili ya haja ambazo sheria imezibainisha, sawa iwe ni katika maisha binafsi ama maisha jumla. Kwa mfano: katika maisha binafsi (ndani ya nyumba) kukusanyika wanafamilia, zimekuja dalili za kisheria kuruhusu kuunga kizazi, na (kukusanyika) kwa ajili ya chakula, na kumtembelea mgonjwa… na katika maisha jumla: kuwatibu majeruhi vitani… kukusanyika masokoni, kuswali misikitini, kuhudhuria vikao vya elimu, hijjah… n.k yote hayo yawe kwa mujibu wa hukmu za kisheria, kwa namna ya kutenganishwa safu kama vile misikitini na kwenye mihadhara ya uma, au bila ya kutenganishwa safu kama vile: masokoni na hijjah…

C. Na kuunga kizazi sio kwa wanafamilia walio maharimu peke yao, bali pia kwa wanafamilia wasio maharimu, kama bint wa ami… “rudi kwenye kitabu cha Nidhamu ya Kijamii – “kuunga kizazi” … hili laruhusiwa kwa wanafamilia kuungana na kukaa pamoja katika Idd au minasaba mengine, lakini kwa ajili ya kuunga kizazi tu, yaani: kujuliana hali ya afya, kumtembelea mgonjwa wao, na kukidhi mahitaji yao, na mfano wa hayo. Lakini (ruhusa) sio ya wao kukaa pamoja na kucheza kwa mfano, au wao kutoka pamoja kwa ajili ya matembezi, au kukaa pamoja katika bustani na kupiga gumzo… hayo hayafai…) mwisho wa nukuu.

Nataraji majibu haya kwa maswali yako yanatosheleza, na Mwenyezi Mungu ndiye Mjuzi na Mwenye hekima zaidi.

Ndugu Yenu,

Ata Bin Khalil Abu Al-Rashtah

16 Ramadhan 1443 H

17/4/2022 M

Link ya jibu hili kutoka kwa ukurasa wa Amiri wa Facebook