Kwa Nini Mtume (saw) Hakuomba Nusra (Nguvu za Kimada) kutoka kwa Maquraish

بسم الله الرحمن الرحيم

 Silsila ya Majibu ya Mwanachuoni Mkubwa Ata Bin Khalil Abu Al-Rashtah Amiri wa Hizb ut Tahrir “Juu ya Maswali ya Wanaozuru Ukurasa Wake wa Facebook wa “Kifiqhi”

Jibu la Swali

Kwa: Raid Al-Harsh Abu Muadh

(Imetafsiriwa)

Swali:

Kwa ajili ya ufafanuzi wa swali: Je, Mtume (saw) kutokuomba kwake Nusra kutoka kwa Maquraish ni kwa sababu hawakuwa na vigezo hivyo kabisa, au ni kwa sababu tu waliukataa Uislamu? Na ninaokusudia ni viongozi wa Makkah. Na ikiwa ni hivyo, si Mtume (saw) aliomba Nusra kutoka kwa watu wa Yathrib [Madina] pamoja na kwamba viongozi wa Yathrib walikuwa hawajasilimu na hawakutoa nusra?! Naomba ufafanuzi.

Mwenyezi Mungu akubariki na akulipe kila la kheri.

Jibu:

Kuhusu kutokuomba Nusra kutoka kwa Maquraish wa Makkah, mas`ala ni kama ifuatavyo:

[Mtume (saw) alikuwa akiwalingania wenye nguvu, walio na uwezo wa kubadilisha ujahiliya na kuweka Uislamu, alikuwa kwanza huwalingania kwenye Uislamu … wakisilimu na kukubali, basi huomba Nusra yao baada ya hapo… na viongozi wa Kiquraishi hapo Makkah wenye uwezo wa kubadilisha hawakuubali Uislamu, ndio sababu Mtume (saw) hakuomba Nusra yao, bali Mtume (saw) alikuwa akitosheka tu na kulingania kwenye Uislamu huko Makkah. Na kwa kuwa wenye nguvu miongoni mwao hawakuitikia Uislamu ndio maana hakuomba Nusra kutoka kwao… hapa chini nitakutajia kutoka kwa Seerah ni vipi hayo mambo yalivyokuwa:

Kwanza: kutoka kwenye Seerah ya Ibn Hishaam:

1- [(… na watu wake walikuwa wakali zaidi katika kumkhalifu na kutengana na dini yake isipokuwa wachache tu katika wanyonge waliomuamini. Basi Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) akawa akijionyesha kwa makabila ya Waarabu kwenye misimu [ya hajj], akiwalingania kwa Mwenyezi Mungu, na kuwaeleza kwamba yeye ni nabii aliyetumwa, na akiwaomba wamkubali na wampe ulinzi ili aweze kuwabainishia yale ambayo Mwenyezi Mungu amemtuma nayo…

Amesema Ibn Ishaq: amenihadithia Hussein bin Abdillah bin Ubaidillah bin Abbas: asema, nilimskia Rabia bin Abbaad akimhadithia babangu na kusema: mimi nilikuwa kijana barobaro nikiwa pamoja na babangu huko Minaa, hali ya kuwa Mtume wa Mwenyezi Mungu alikuwa akisimama kwenye mashukio ya makabila ya Waarabu akiwaamba: Enyi bani fulani… hakika mimi ni mjumbe wa Mwenyezi Mungu kwenu, amewaamrisha mumuabudu Mwenyezi Mungu na wala msimshirikishe na chochote, na mvue vyote mnavyoviabudu kutokana na haya masanamu, na muniamini na munikubali, na mnipe ulinzi ili niweze kubainisha kutoka kwa Mwenyezi Mungu yale aliyonituma nayo…)

2- Amesema Ibn Ishaq: na amenihadithia Az-Zuhriy kwamba, [Mtume] aliwaendea Bani Aamir bin Swa`swa`ah akawalingania kwa Mwenyezi Mungu Azza wa Jalla na akajitambulisha kwao. Mtu mmoja kati yao -akiitwa: Baihara bin Firaas. Amesema ibn hIshaam: Firaas bin Abdillah bin Salamat al-Khair, bin Qushair, bin Ka`ab, bin Rabiiaah, bin Aamir bin Swa`swa`ah – akamwambia: “Naapa kwa jina la Mwenyezi Mungu lau nitamchukua huyu kijana wa Kiquraishi basi ningeliwala (ningeliwashinda) Waarabu kupitia kwake”! Kisha akasema: waonaje ikiwa sisi tutakupa bay`ah [kiapo cha utiifu] juu ya jambo lako, kisha Mwenyezi Mungu akupe ushindi dhidi ya waliokukhalifu, je hili jambo [la utawala] litakuwa kwetu baada yako? Akajibu [Mtume]: hilo jambo ni la Mwenyezi Mungu, na huliweka mahali anapotaka. Akamwambia: hivi shingo zetu zilengwe na Waarabu kwa ajili yako, kisha Mwenyezi Mungu akishakupa ushindi hilo jambo [utawala] liwe kwa wengine?! Hatuna haja na jambo lako…

3- Amesema tena Ibn Ishaq: “Akawa Mtume wa Mwenyezi Mungu ni mwenye kuendelea na jambo lake hilo kila anapokusanyika na watu katika misimu, huwaendea na kuyalingania makabila kwa Mwenyezi Mungu na kwenye Uislamu, na huionyesha nafsi yake kwao [hujitambulisha] na yale aliyo kuja nayo kutoka kwa Mwenyezi Mungu: uongofu na huruma. naye hasikii kuna mtu yeyote amekuja Makkah katika Waarabu na akawa ni mwenye jina [mtambulika] na ubora, isipokuwa humfuata na kumlingania kwa Mwenyezi Mungu, na kumuonyesha aliyo nayo”.

Na kama unavyoona, Mtume (saw) alikuwa akimlingania kwenye Uislamu kwanza mwenye nguvu, akikubali ndipo huomba Nusra yake.

Pili: kutoka kwenye Seerah ya Ibn Kathir:

1- [… amesema: kisha tukaishia kwenye mkao wenye utulivu na heshima. Mara [tukakutana na] wazee wenye vyeo, Abubakar akatangulia, akasalimia – amesema Ali: “Na Abubakar alikuwa wa mbele katika kila jambo la kheri” – akawaambia: mwatokana na nani? Wakasema: twatokana na Banu Shaibaan bin Thaalaba. Abubakar akamgeukia Mtume wa Mwenyezi Mungu na kumwambia: nakufidia kwa babangu na mamangu! Baada ya hawa hakuna watu wengine wenye utukufu kuwaliko. Na katika mapokezi mengine: nyuma ya hawa udhuru wowote katika watu wao, na hawa ni wa mbele katika watu wao, hawa ni viongozi wa watu! Na kati yao walikuwepo Mafruq bin Amr, Hani`i bin Qubaiswa, Muthanna bin Haritha, na Nu`maan bin Harik… na aliyekuwa karibu zaidi kwa Abubakar ni Mafruq bin Amr. Na alikuwa huyu Mafruuq bin Amr amewashinda kwa ufasaha, na alikuwa na misuko miwili ya nywele iliyoangukia kifuani kwake, na ndiye aliyekuwa karibu sana kwa Abubakar katika mkao. Abubakar akamuuliza: idadi yenu iko vipi? Akajibu: hakika sisi twazidi elfu moja, na hawatoshindwa watu elfu kutokana na uchache. Akamuuliza tena: na nguvu yenu ikoje? Akajibu: ni juu yetu kujitahidi, na kila watu hujikakamua. Abubakar akamuuliza: na vita kati yenu na maadui zenu huwa vipi? Mafruq akajibu: sisi huwa wakali zaidi pale tunapokasirika, na hakika sisi hufadhilisha farasi kuliko watoto, na silaha kuliko mashamba, na ushindi hutoka kwa Mwenyezi Mungu, mara nyengine hutupa ushindi na mara nyengine huwapa ushindi wengine dhidi yetu… huenda wewe ni ndugu wa Maquraish? Akasema Abubakar: ikiwa mumefikiwa na habari kuwa kuna Mtume wa Mwenyezi Mungu basi huyu hapa ndiye. Akasema Mafruq: imetufikia kwamba anasema hivyo. Kisha akamgeukia Mjumbe wa Mwenyezi Mungu na kumuuliza: walingania nini ewe ndugu wa Maquraish? Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) akatangulia mbele, akaketi, na Abubakar akasima na kumuekea kivuli kwa nguo yake. Akasema Mtume (saw):

«أدعو إلى شهادة أن لا إله إلا الله وحده لا شريك له وأني رسول الله وأن تؤووني وتنصروني فإن قريشا قد تظاهرت على أمر الله وكذبت رسله واستغنت بالباطل عن الحق والله هو الغنى الحميد»

 “Nawalingania kwenye kushuhudia kwamba, hapana Mola apasaye kuabudiwa kwa haki isipokuwa Mwenyezi Mungu, peke yake na hana mshirika, na kwamba mimi ni Mjumbe wa Mwenyezi Mungu, na munihifadhi na muninusuru ili niweze kufikisha [ujumbe] wa Mwenyezi Mungu alioniamrisha, kwani Maquraish wameshirikiana dhidi ya amri za Mwenyezi Mungu, na wakamkadhibisha Mjumbe wake, na wakatosheka na batili badala ya haki, na Mwenyezi Mungu ndiye Mkwasi na Mwenye kusifiwa”. Akamuuliza tena: na walingania nini tena, ewe ndugu wa Maquraish? Mtume wa Mwenyezi Mungu akawasomea:

(قل تعالوا أتل ما حرم ربكم عليكم: ألا تشركوا به شيئا وبالوالدين إحسانا)

“Sema: Njooni nikusomeeni aliyo kuharimishieni Mola wenu Mlezi. Nayo ni kuwa, msimshirikishe Yeye na chochote. Na wazazi wenu wafanyieni wema.” Mpaka neno lake: (ذلكم وصاكم به لعلكم تتقون) “Hayo amekuusieni ili myatie akilini.” [Al-An’am: 151]

Mafruq akasema: “Na walingania nini tena, ewe ndugu wa Maquraish? Naapa kwa jina la Mwenyezi Mungu haya si maneno ya watu wa ardhini, na lau ingekuwa ni katika maneno yao basi tungelijua!” Mtume akamsomea:

(إن الله يأمر بالعدل والإحسان وإيتاء ذى القربى وينهى عن الفحشاء والمنكر والبغى، يعظكم لعلكم تذكرون)

“Hakika Mwenyezi Mungu anaamrisha kufanya uadilifu, na hisani,na kuwapa jamaa; na anakataza uchafu, na uovu, na dhulma. Anakuwaidhini ili mpate kukumbuka.” [An-Nahl: 90]

Mafruuq akamwambia: “Wallahi umelingania -ewe ndugu wa Maquraish – kwenye tabia njema na matendo mazuri, na kwa hakika wamezua uongo watu ambao wamekukadhibisha na wakaungana dhidi yako”!

Na ni kana kwamba alipenda Hani`i bin Qubaiswa ashirikiane naye katika mazungumzo, akasema: “na huyu ni Qubaiswa bin Hani`i mzee wetu na mwenye dini yetu. Hani`i akasema: “Hakika nimesikia maneno yako, ewe ndugu wa Maquraish, na nimeyakubali, na mimi naona suala la sisi kuacha dini yetu na kufuata dini yako kwa kikao kimoja tu ulichokaa na sisi ambacho hakina mwanzo wala mwisho, na bado hatujafikiria kuhusu jambo lako na kuangalia mwisho wa unayotulingania, [kufanya hivyo] ni kuteleza katika rai, na ni ukurupukaji katika akili, na pia ni uchache wa kuangalia mwisho wa mambo, na hakika si vyengine kuteleza hutokana na uharaka. Na nyuma yetu kuna watu ambao twachukia kuwaamulia jambo, lakini wewe rudi na sisi tutarudi, wewe kayaangalie na sisi tuyaangalie”.

Naye ni kama alipenda Muthanna ashirikiane naye katika mazungumzo, akasema: “na huyu ni Muthanna, mzee wetu na mwenye kuhusika na vita vyetu”. Muthanna akasema: “Bila shaka nimeskia maneno yako na nimeyaona ni mazuri ewe ndugu wa Maquraish, na nimeyapenda uliyozungumza, na jibu ni lile lile jibu la Hani`i bin Qubaiswa, na sisi kuachana na dini yetu na kukufuata kwa kikao kimoja tu ulichokaa na sisi… na hakika sisi tumeshukia katika sehemu mbili za maji: moja wapo ni “Yamama”, na nyengine ni “Samaawa”. Mtume (saw) akamuuliza: ni zipi hizo sehemu mbili? Akasema: “moja wapo ni … nchi kavu na ardhi ya Waarabu, na nyengine ni ardhi ya Fursi na mito ya Kisra. Na sisi tumeshukia kwa ahadi aliyochukua kwetu Kisra kwamba tusizushe jambo, wala tusimhifadhi mzushi, na huenda hili jambo ambalo watulingania ni miongoni mwa mambo yanayochukiwa na wafalme, ama [sisi kukupa ulinzi] sehemu zinazokaribiana na miji ya Waarabu, hilo ni kosa ambalo mwenyewe aweza kusamehewa, na udhuru wake utakubalika, ama zile sehemu zinazokaribiana na miji ya Wafursi, basi ni kosa lisilosamehewa, na udhuru wake haukubaliki. Kwa hiyo, kama utataka tukunusuru na tukulinde kwa sehemu za Waarabu basi tutafanya hivyo”.

Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) akasema:

«ما أسأتم في الرد إذ فصحتم في الصدق وإن دين الله لن ينصره إلا من حاطه من جميع جوانبه»

“Hamjatoa jibu baya, kwa sababu mumesema ukweli kwa ufasaha, [lakini] hatoisimamia dini ya Mwenyezi Mungu isipokuwa yule atakayeizunguka kwa pande zake zote”…]

2- Asema: [kisha tukaondoka na kwenda kwenye mkao wa Aus na Khazraj, basi hatukuenuka hapo mpaka wakampa Bay`ah Mtume (saw).

Ali (ra) alisema: “Na walikuwa wakweli na wenye subra, basi Mtume (saw) akafurahishwa sana kutokana na Abubakar kujua nasaba zao”.

Asema: “Basi Mtume (saw) hakukaa isipokuwa kidogo tu mpaka akawatokea maswahaba zake na akawaambia:

«احمدوا الله كثيرا، فقد ظفرت اليوم أبناء ربيعة بأهل فارس، قتلوا ملوكهم واستباحوا عسكرهم وبي نُصروا»

 “Msifuni Mwenyezi Mungu kwa wingi, kwani kwa hakika leo wana wa Rabiiah wamewashinda watu wa Fursi, wamewaua wafalme wao na wakachukua kambi zao, na ni kwa ajili yangu ndio wamenusuriwa.”

Akasema: “na hilo tukio [la vita] lilikuja kutokea huko “Qaraqir” pambizoni mwa “Dhii Qaar”… na hii ni hadith “Gharib jidda” [geni sana] tumeiandika kwa kuwa ndani yake kuna dalili za utume, tabia njema, na ufasaha wa Waarabu. Na hii [hadith] imekuja kwa njia nyengine, na ndani yake imekuja: kwamba wao [Waislamu] walipopigana na Wafursi na kukutana nao huko “Qaraqir” ambapo ni karibu na “Furaat” walifanya kauli mbiu yao ni jina la Muhammad (saw) ,wakapewa ushindi dhidi ya Wafursi kwa hilo. Na baada ya hilo [Wafursi]  waliingia katika Uislamu.

Na imam Muhammad bin Umar Al-Waqidiy amefuatilia kwa undani akasimulia yale makabila moja baada ya nyengine, akataja kujitambulisha kwake (saw) kwa: Bani Aamir, na Ghassaan, Bani Fazaarah, Bani Murra, Bani Hanifa, Bani Sulaim, Bani Abasa, Bani Nadhr bin Hawaazin, Bani Thaalaba bin Ukaba, Kinda, Kalb, Bani Al-Haarith bin Kaab, Bani Udhra, Qais bin Al-Hatwim, na makabila mengine. Na mtiririko wa habari zao ni mrefu, tumetaja miongoni mwa hizo habari kiasi kinachofaa, sifa njema na wema zote ni za Mwenyezi Mungu.

Na amesema Imam Ahmad: ametuhadithia As`wad bin Aamir, [akisema] alitueleza Israil, kutoka kwa Uthmaan -yaani – bin Al-Mughirah, kutoka kwa Salim bin Ja`ad, kutoka kwa Jaabir bin Abdillah, akisema: “alikuwa Mtume (saw) akijionyesha nafsi yake [akijitambulisha] kwa watu kwenye kisimamo cha Arafah, kwa kusema:

«هل من رجل يحملني إلى قومه فإن قريشا قد منعوني أن أبلغ كلام ربى عز وجل؟»

 “Je, kuna mtu ambaye atanichukua mimi na kunipeleka kwa watu wake? Kwani Maquraish kwa hakika wamenizuia kufikisha maneno ya Mola wangu Mtukufu?”]

Ni wazi kutokana na [nukuu zote hizo] kwamba, Mtume (saw) alikuwa haombi Nusra kutoka kwa yeyote isipokuwa baada ya kumlingania kwenye Uislamu, na ikiwa hakuitikia Uislamu basi hakuomba Nusra yao.

Ndugu Yenu,

Ata Bin Khalil Abu Al-Rashtah

 26 Jumada Al-Awwal 1443 H

30/12/2021 M

 Link ya jibu hili kutoka kwa ukurasa wa Amiri wa Facebook