Natija ya Maridhiano Kati ya Amerika na Ufaransa!

بسم الله الرحمن الرحيم

Jibu la Swali

(Imetafsiriwa)

Raisi wa Amerika Donald Trump amerudi tena siku ya Alhamisi kuzungumzia ziara yake ya hivi karibuni nchini Ufaransa. Trump alisema katika mahojiano na gazeti la The New York Times “Ni mtu mkubwa sana”, akimkusudia Macron. “Ni mwerevu, mwenye nguvu, anaye penda kunishika mkono wangu.” Aliongeza, “Watu hawatambui kuwa anapenda kunishika mkono wangu…” (Al-Arabiya.net-Washington France Press, 20/7/2017). Raisi Trump alizuru Paris mnamo Julai 13, 2017. Raisi wa sasa Macron, alimkaribisha kwa taadhima. Huku raisi wa zamani wa Ufaransa, Hollande, akionyesha kutoridhishwa kwake na raisi huyo wa Amerika, pamoja pia kulikuwa na tuhuma nzito dhidi ya raisi Trump kutoka kwa viongozi wa Ulaya! Maridhiano haya kati ya Amerika na Ufarasa yanaashiria nini na ni yapi malengo ya ziara ya Trump Paris? Na je, kuna natija zozote za ziara hii kwa hali ya Syria, hususan tangu raisi wa Ufaransa Macron kuzungumza kuhusu mkakati mpya wa kifaransa na kiamerika nchini Syria?

Jibu: uzembe wa Trump katika siasa za kimataifa umekuwa na matokeo ya kuchukiza, kwa mfano, taarifa zake za kushtua juu ya uwezo wa NATO, zilipelekea majibizano makali dhidi ya sera ya kiamerika, na miongoni mwa majibizano hayo yaliyojitokeza hadharani yalitolewa kutoka Berlin. Wakati wa kampeni yake ya uchaguzi na baada ya kutawazwa kuwa raisi mnamo 20/1/2017, Trump hakuficha kuchukizwa kwake na Muungano wa Ulaya. Aliipongeza kura ya maoni ya Uingereza ya kutaka kujitoa katika Muungano wa Ulaya (Brexit). Balozi wa Amerika Jijini Brussels alitarajia kuvunjika kwa Muungano wa Ulaya, na Amerika ilisubiri kura za Uholanzi na Ufaransa kwa matarajio ya ushindi kwa wanaopinga Muungano wa Ulaya, ili kuvunjika huku kwa Muungano wa Ulaya kutokee mwaka wa 2017. Hili ndilo ambalo Ulaya ilisimama kidete dhidi ya kutokea kwake; ilifaulu katika kuzuia athari ya maandamano ya Kiingereza kwa Uholanzi na Ufaransa, na hivyo basi kuondoa tishio la kuvunjika kwa Muungano wake. Uzembe wake katika siasa za kimataifa ukaongezeka tena kisha akarudi nyuma kutokana na maamuzi yake. Trump aligeuza maoni yake juu ya NATO kama muungano uliopitwa na wakati, kama alivyo usifu, kisha akarudi nyuma juu ya misimamo hii hadharani. Vile vile alijiondoa kutoka katika makubaliano ya Paris kuhusu hali ya anga, na kuagiza majadiliano yake mapya, kisha akasimama katika ukingo wa vita na Korea Kaskazini, na kurudi nyuma baadaye. Zaidi ya hayo, alibeba mtazamo mbaya juu ya China, baadaye akashirikiana nayo huku akisubiri matokeo yake kutoka katika faili ya Korea Kaskazini, akatoa taarifa nzito juu ya eneo la Syria na baadaye akawaachia mambo yake majirani zake wa Astana na Geneva.

Kile ambacho pia chaweza kuonekana ni usumbufu wa hali yake ya ndani hususan upinzani ulioonyeshwa juu ya sera yake katika kadhia ya usaidizi wa Urusi kwake wakati wa uchaguzi.  Natija ya matatizo haya na upinzani huu ni kuwa mawasiliano ya raisi na wanachama wa idara yake kwa Urusi ilikuwa kadhia moto sana nchini Amerika, na hali hii haikumsaidia raisi huyu kufaulu kuunda mkataba baina ya Urusi na Amerika na kwamba ulicheleweshwa, na Trump alifanya mkutano mmoja tu na raisi wa Urusi juu ya ajenda za kongamano la G20 jijini Hamburg, Ujerumani mnamo Julai 7, 2017. Mahusiano baina ya Amerika na Urusi yamezidi kuwa magumu katika wakati ambapo bunge la congress linashinikiza vikwazo vya ziada juu ya Urusi. Hii ikiwa ni ziada ya masaibu ya ongezeko la ripoti za kiamerika juu ya kujiingiza kwa Urusi katika kura za Amerika, hili likiongeza zaidi fedheha kwa raisi ndani ya nchi, bila ya kutaja kuendelea kwa fedheha kupitia kuyarudisha tena mahusiano ya nchi yake na Moscow.

Yote haya yamesababisha kuvurugika kwa siasa ya kimataifa baina ya Amerika na Muungano wa nchi za Ulaya, na kuvurugika huku kumeleta uzuri na ubaya kulingana na maslahi ya nchi hizi na uwezo wao wa kupatiliza hali mpya ya siasa ya kiamerika, tutaiangalia upya misimamo ya nchi hizi kuhusiana na sera ya Trump na kisha kugusia natija ya msimamo wa Ufaransa iliyo pelekea kualikwa kwa Trump kuzuru Paris na kukaribishwa kwa taadhima.

1 – Ama kuhusu Uingereza: ziara ya mapema ya waziri mkuu wa Uingereza Theresa May ya Washington mnamo Januari 20, 2017 na hamu yake ya kutia saini makubaliano ya kibiashara na Washington ni mfano kwa nchi nyengine za Muungano wa Ulaya wa kuzishajiisha kujiondoa katika Muungano huo. Hivyo basi, Uingereza ilirudisha tena mafungamano yake na Amerika na iliipendelea zaidi idara ya Trump, lakini baada ya matarajio ya Amerika ya kuuvunja Muungano wa Ulaya kusambaratika, kama ilivyo shuhudiwa kwa ushindi wa wanaounga mkono muungano huo katika uchaguzi nchini Uholanzi na Ufaransa, mtazamo mzuri aliokuwa nao Trump kwa Uingereza ukabadilika kwani alitaka Uingereza iwe ndio inayoongoza mchakato huo wa kuuvunja Muungano wa Ulaya, na kwa kuwa hali ya kujiondoa London katika Muungano wa Ulaya haikujirudia jijini Paris (Ufaransa) na Amsterdam (Uholanzi), Amerika imerudi tena kuchafua maslahi ya kimataifa ya Uingereza katika hali iliyoishtua London. Amerika inamshinikiza kibaraka wake, Sisi, kuongeza usaidizi wake kwa Hafter (mkuu wa jeshi la Libya) pasi na kutilia maanani maslahi ya Uingereza nchini Libya, na Amerika pia akawasukuma vibaraka wake kutia mshtuko kiasi ili kuishinikiza Qatar, ambayo ni msaada mkubwa kwa Uingereza katika ardhi za kiarabu na kiislamu. Kwa haya na mengineo, sera ya Uingereza ilitingishwa na hivyo kupoteza imani kwa Trump, huku ikijipata katikati ya nyundo ya Amerika upande mmoja, na kinoo cha Ulaya, ambayo ili jadili kuondoka katika muungano wake, kwa upande mwengine. Katika hali ya tashwishi hii pana, waziri mkuu wa Uingereza akatangaza uchaguzi mapema, hili liliwashangaza hata viongozi serikalini, na kwa haya tarehe ya matokeo ya uchaguzi ikapangwa kuwa 8/6/2017, Uingereza ikajikuta kwenye njia panda baina ya kuondoka katika Muungano wa Ulaya au kurudi kwake. Uchaguzi huu ulionyesha kuwa wanaounga mkono kujiondoa katika muungano walizidi kuwa dhaifu, hali iliyo ongeza uwezekano wa kubakia ndani yake ikiwa majadiliano na Brussels (Ubeligiji) hayata zaa makubaliano yanaoiridhisha. Hii inaonyesha jinsi gani siasa mpya ya Amerika ilivyo ichanganya Uingereza.

2 – Katika upande ulio muhimu zaidi ni upande wa Urusi; testuri za Ulaya zililingana na zile za Amerika baada ya eneo la Crimea kuunganishwa na Urusi mnamo 2014 na kuchochea mashariki mwa Ukraine. Vikwazo vya Kiamerika na Ulaya vya ashiria kukubaliana kimaoni baina yao kuhusiana na hofu ya Ulaya inayo tokana na kulengwa kwa eneo la Ulaya mashariki na Putin, lakini tangu wakati wa kampeni yake ya uchaguzi, Trump amekuwa makini na vikwazo hivi na ameapa kujenga mafungamano ya karibu na Urusi jambo lililo ichanganya Ulaya na kuiacha peke yake katika sura ya kuinuka upya kwa Urusi. Licha ya kuwa viongozi wa Ulaya wametambua kuwa Amerika, wakati wa idara ya Obama, ndio iliyo iruhusu Urusi kuinuka, hususan baada ya kujihusisha katika vita vya Syria, Trump alitishia kusonga mbele zaidi kufanya makubaliano ya pamoja na Urusi katika kadhia za kiulimwengu, jambo litakalo yaondoa matarajio ya Ulaya ya kuwa na dori katika migogoro ya kimataifa.

3 – Ama kuhusu Ujerumani, ilichukua hatua za wazi kuikataa siasa mpya ya kiamerika; ilikataa kashfa za kiamerika dhidi ya nchi za Ulaya za NATO, ikapinga kujiondoa kwa Amerika katika makubaliano ya hali ya anga na kukataa kuwepo kwa majadiliano mapya juu yake. Ili kashifu mkataba wa silaha ambao Trump alitia saini na Saudi Arabia na kuuona kama kutia moto ndani ya mafuta katika eneo ambalo tayari lawaka moto, na kubakia na msimamo huu licha ya Ufaransa kubadilisha msimamo wake. Kulingana na matangazo ya jioni ya shirika la habari la Deutsche Welle: ((Misimamo ya chansela wa Ujerumani Angela Merkel ilikuwa mikali kwa raisi wa Amerika wakati wa kikao cha G20 nchini Ujerumani, lakini raisi wa Ufaransa alikuwa makini kutomuudhi Trump…)), (Deutsch Welle, 14/7/2017).

Kiujumla, yaweza kusemwa kuwa Ujerumani imeongeza pakubwa majaribio ya kuamka tena kama dola kuu yenye nguvu, yote ni kutokana na kuibuka sera mpya za kiamerika.

4 – Baada ya hayo, tunagusia kuhusu maana ya ziara ya Trump nchini Ufaransa, maridhiano yaliopo sasa katika ya Amerika na Ufaransa, malengo ya Ufaransa ya kumualika raisi Trump kuzuru na kushiriki katika siku ya kitaifa ya Julai 13, 2017, kuangazia kile ambacho Ufaransa anakiita kumbukumbu ya Amerika ya kushiriki katika vita vya kwanza vya dunia, ambayo ni tukio la kale na ambalo ni nadra sana kufanywa kupitia kwa sherehe isipokuwa kwa lengo maalum. Katika wakati ambapo raisi Trump anavutana kimahusiano na Ulaya nzima, Ufaransa ilimualika kushiriki katika sikukuu yake ya kitaifa! ((Macron katika maongezi ya simu mnamo Jumanne alitoa mualiko mpya kwa Trump kuzuru Ufaransa na kushiriki katika sikukuu yake ya kitaifa. Mualiko wa kwanza ulikuwa wakati wa mkutano wa NATO mwishoni mwa mwezi Mei mwaka jana jijini Brussels…)) (Elaph newsite, 28/6/2017). Katika mkutano wa G20, uliofanyika Ujerumani mnamo 7/7/2017, raisi Macron wa Ufaransa alilegeza kamba kwa unyenyekevu ya kutomtenga Trump miongoni mwa viongozi, hususan wa Ulaya, walioshutumu vikali kujiondoa kwa Amerika katika makubaliano ya hali ya anga. Trump mwenyewe alishangazwa na mualiko wa Macron katika mazingira kama haya. ((Trump alisema “ameshangazwa” kupokea ualishi huu baada ya uamuzi wake wa kujiondoa kutoka kwa makubaliano ya hali ya anga ya Paris, yaliotiwa saini na nchi 195 mnamo 2014…))                            (Al Arabiya.net, 20/07/2017)

5 – Ama kuhusu malengo ya muelekeo huu mpya wa Ufaransa, ni lazima isisitizwe kuwa Ufaransa, ambayo ni nguzo muhimu zaidi ya Muungano wa Ulaya, ilikuwa makini kwa Trump na kuhofia natija ya siasa yake juu ya mahusiano kati ya Amerika na Ulaya. Hofu hii haikumsaza pia raisi wa zamani wa Ufaransa Hollande. Raisi wa sasa, Macron, pia amekuwa makini sana kwa Trump tangu kampeni yake ya uchaguzi na mpaka hivi karibuni. Mkengeuko huu wa Ufaransa kwa Amerika umejitokeza tu wiki kadhaa zilizo pita, na umejitokeza wazi wazi kwa ualishi wa raisi wa Amerika Trump kuzuru Ufaransa na kupokewa kwa taadhima na kuzungakwa na heshima kubwa. Udadisi juu ya mkengeuko huu unatoa taswira mbili; na zote ni muhimu:

Taswira ya kwanza ya mkengeuko huo inahusu hali ya Syria. Baada ya Macron kutangaza kuwa: haoni badali halali ya Bashar, na kwamba Ufaransa haioni tena suala la kuondoka Bashar kama sharti la mapatano. (Reuters, Juni 21, 2017). Na akasema baada ya hayo na kabla ya kumpokea raisi wa Amerika: “Tumebadilisha mtazamo wa Ufaransa juu ya Syria ili kufikia suluhisho pana la kisiasa, na hatuweki kuondoka kwa Bashar kama sharti kwa hili…” (Middle East, 13/7/2017), hivyo basi Ufaransa imekuwa karibu sasa na Amerika, inayoshikilia karata ya serikali na makundi mengi ya Syria. Muelekeo huu ni kwa lengo la kuwa na dori nchini Syria ambayo amekuwa na hamu nayo kwa muda sasa. Ufaransa inajua fika kuwa haitaweza kuvuta hata harufu ya dori hiyo bila ya kupata idhini kutoka kwa Amerika.

Kwa hivyo, kukaribisha kwa taadhima na kusisitiza kutoondoka kwa Bashar yote ni kwa sababu Ufaransa inajua kwamba Amerika haitaki kuondoka kwake kwa sasa, isipokuwa baada ya matayarisho ya kupatikana badali ya kibaraka mwengine kuchukua mahali pake, na kwa sasa Amerika bado haijampata. Ufaransa ilianza kubwaga misimamo yake ya mwanzoni kwa sababu ilikuwa ni vizingiti vinavyomzuia yeye kushiriki (katika kadhia ya Syria). Ufaransa ilianza kuimba wimbo wa “vita dhidi ya ugaidi”, kwa kufuata mpangilio sambamba na wa Trump. Raisi wa Ufaransa, Emmanuel Macron, alisema wakati wa mahojiano ya pamoja ya waandishi wa habari na mwenzake wa Amerika Donald Trump: kwamba anakubaliana na raisi Trump juu ya muelekeo wa hali baada ya vita nchini Iraq na Syria. Mnamo Alhamisi katika mji mkuu wa Ufaransa Macron akaongeza kusema kuwa anakubaliana pia na raisi wa Amerika kufanya kila jitihada kupambana na ugaidi… (Russia Today, 13/7/2017).

Taswira ya pili ni hofu ya Ufaransa juu ya kukua kwa dori ya Ujerumani; hofu hii imeifanya Ufaransa kuipinga Ujerumani. Huku tuhuma za Ujerumani dhidi ya Trump zikiongezeka, Ufaransa inajikaribisha zaidi (kwa Trump)! Punde tu baada ya ziara raisi wa Amerika jijini Paris, balozi wa Ufaransa katika Umoja wa Mataifa, Francois Delattre, alisema kuwa: “Kundi la kimawasiliano nchini Syria ambalo Paris inapendekeza kubuniwa, linapaswa kuhusisha wanachama wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na washirika wa kieneo. Balozi huyu aliwaambia wanahabari katika kikao cha faragha cha Baraza la Usalama, mnamo Ijumaa jioni, kwamba timu hiyo iliotajwa hapo juu ni lazima itekeleze “uenezaji wa amani na kutayatisha ramani ya muelekeo”. Mjumbe huyu wa Ufaransa aliongeza kuwa jambo muhimu zaidi kwa sasa ni kuunganisha jamii ya kimataifa na kuanzisha miradi mipya itakayo saidia jitihada za balozi maalum wa Ufaransa nchini Syria, Stefan de Mistura… (Russia Today, 14/7/2017). Hivyo basi, Ufaransa inatoa wito wa kubuniwa kwa “kundi la kimawasiliano chini Syria lijumuishe nchi wanachama wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na washirika wa kieneo” na “kuzalisha mradi imara kwa nchi tano zitakazo jihusisha (na Syria)” yaani kutengwa kwa Ujerumani kutokana na dori hii kwa kule kuwa si mwanachama wa Baraza la Usalama, ni jambo linalo fichua wasiwasi wa Ufaransa juu ya kuinuka kwa Ujerumani; kamwe haitaki iwe na dori ya kimataifa.

6 – Hivyo basi, kuvurugika kwa sera ya Trump, hususan ziara yake nchini Ufaransa, imesababisha mabadiliko katika siasa ya kimataifa baina ya Amerika na Muungano wa Ulaya kiasi cha kuwa baadhi ya vyombo vya habari vinaichukulia ziara hiyo ya raisi wa Amerika Donald Trump jijini Paris, kuwa ndio mwanzo wa mpangilio mpya wa kiulimwengu, ambapo raisi wa Ufaransa Emmanuel Macron anaongoza nchi yake katika mahusiano mapya ya Amerika na Ujerumani. Gazeti lilisema kuwa Macron anajiwasilisha kama kiongozi mwenye akili katika Muungano wa Ulaya baada ya Uingereza kujiondoa kutoka kwa Muungano huo. Karata za Ulaya zitagawanywa baada ya Uingereza kujiondoa, kwa mujibu wa gazeti. Tahariri ya gazeti hili ilitamatisha kwa kusema kuwa Muungano wa Ulaya umeundwa katika hali isiyo iwezesha Ujerumani wala Ufaransa kusimama kama dola iliyo na nguvu kipekee na kwamba nchi mbili hizi ziliweza kumaliza uhasama wa makarne baina yazo na hatimaye kufanya kazi pamoja katika kuliongoza Bara Ulaya Uingereza ikiweko au bila ya Uingereza. Lakini kwa sasa zinaogelea katika mawimbi tofauti; Ufaransa iko chini ya uongozi wa Macron, iliyo na ari ya kuongoza Ulaya, na Ujerumani chini ya uongozi wa Merkel, ina angazia namna ya kudumisha Ulaya yenye uwezo kamilifu. (Al-Wafd website, 14/7/2017).

7 – Tunachotaka kutamatisha katika jibu hili ni kuwa ndoto za Ufaransa za kuingia eneo la Syria hazitakuwa za muda mrefu, hatimaye zitagongana na uhakika wa msimamo wa Amerika ambayo inakubali tu kuwepo na usimamizi mmoja juu ya mgogoro wa Syria, na baadhi ya upole ambao Amerika ina uonyesha kwa harakati za kifaransa nchini Syria ni tu kwa ajili ya kuchochea ugomvi kati ya Ufaransa na Ujerumani ndani ya Muungano wa Ulaya ili kuuvunja.

Ama kuhusu hofu ya Ufaransa ya kuinuka kwa Ujerumani, ni hofu ya kihakika; msingi wa muundo wa serikali ya Kijerumani unaupiku msingi wa muundo wa serikali ya Kifaransa. Hili linajulikana kihistoria na kijografia. Katika wakati ambapo kwa sasa Ujerumani kimaadili ina achana na kujifunga na makubaliano ya vita vya pili vya dunia yanayo inyima dori ya athari ya kijeshi ya kiulimwengu, kwa kuyatupilia mbali, ni wazi kuwa itaibuka tena barani Ulaya, ikiwa na nguvu kushinda Ufaransa, hata kama itajikaribisha na Amerika kiasi gani.

Twamuomba Allah (swt) aukoleze zaidi ugomvi kati yao na hatimaye jengo lao liporomoke:

فَأَتَى اللَّهُ بُنْيَانَهُم مِّنَ الْقَوَاعِدِ فَخَرَّ عَلَيْهِمُ السَّقْفُ مِن فَوْقِهِمْ وَأَتَاهُمُ الْعَذَابُ مِنْ حَيْثُ لَا يَشْعُرُونَ﴿

((… Allah akayang’oa majengo yao kutoka kwenye misingi, dari zikawaporomokea juu yao, na adhabu ikiwajia kutoka wasiko kujua)) [An-Nahl: 26]

na serikali ya kiislamu kuchukua mahali pao na kueneza kheri ulimwenguni, na maneno ya Mtume (saw) katika hadith yake yadhihiri. Katika Musnad ya Imam Ahmad kutoka kwa Tamim Ad-Dari ambaye amesema: Nimemsikia Mtume wa Allah (saw) akisema:

«لَيَبْلُغَنَّ هَذَا الْأَمْرُ مَا بَلَغَ اللَّيْلُ وَالنَّهَارُ وَلَا يَتْرُكُ اللَّهُ بَيْتَ مَدَرٍ وَلَا وَبَرٍ إِلَّا أَدْخَلَهُ اللَّهُ هَذَا الدِّينَ بِعِزِّ عَزِيزٍ أَوْ بِذُلِّ ذَلِيلٍ عِزًّا يُعِزُّ اللَّهُ بِهِ الْإِسْلَامَ وَذُلًّا يُذِلُّ اللَّهُ بِهِ الْكُفْرَ..»

“Hakika jambo hili litafika kila sehemu yenye kufikiwa na usiku na mchana wala Allah hataiwacha nyumba yoyote isipokuwa ataingiza dini hii kwa izza kubwa au udhalilifu mkubwa – kwa izza atayo upa Uislamu na udhalilifu atakao udhalilisha kwayo ukafiri.”  

Al-Bayhaqi pia amepokea hadith sawa na hii katika Sunan Al-Kubra vile vile katika Mustadrak ya Hakim. Na hili litapatikana kwa uwezo na usaidizi wa Allah, na hilo sio gumu kwa Allah.

29 Shawwal 1438 H

23/7/2017 M